Home Makala UCHAGUZI KENYA 2017: UPINZANI KUWEKA MAWAKALA 450,000 KUHAKIKI HESABU ZA KURA

UCHAGUZI KENYA 2017: UPINZANI KUWEKA MAWAKALA 450,000 KUHAKIKI HESABU ZA KURA

519
0
SHARE

NAIROBI, KENYA


Mapema wiki hii kiongozi wa upinzani Raila Odinga ametangaza kwamba chama chake cha ODM kitahamasisha mawakala 450,000 watakaowekwa karibu na vituo vya kupiga kura nchi nzima kufanya hesabu za kura sambamba na IEBC ili kuzuia wizi wa kura.

Alisema: “Katika uchaguzi wa mwaka 2013 nilishinda uchaguzi lakini (Tume ya Uchaguzi) ilipindua matokeo na kumpa Uhuru Kenyatta. Tuna uwezo wa kuuondoa utawala wa Jubilee iwapo kura zote zitahesabiwa bila wizi.”

Alisema katika vituo vyote vya kuhesabu kura wataweka kamati za watu 50 kila moja, na kuongeza: “Baada ya IEBC kutangaza matokeo yake, sisi upande wa upinzani tutatangaza matokeo yetu kwa ajili ya kulinganisha.”

Hata hivyo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (Independent Electoral and Boundaries Commission – IEBC) imesema  mpango wa upinzani wa kufanya majumuisho ya hesabu za kura wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti 8 mwaka huu sambamba na majumuisho ya Tume hiyo ni ukiukwaji wa sheria.

Katika taarifa yake iliyotumwa kwa vyombo vya habari Jumatatu wiki hii Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chekubati aliushutumu mpango huo wa upinzani, akisema ulikuwa unakiuka sheria inayosimamia vyama vya siasa, ambayo inakataza chombo kisichohusika kufanya majumuisho ya kura kivyake.

Chebukati aliongeza: “Ili kuondoa utata wa tafsiri, ni Tume tu ndiyo inaruhusiwa chini ya sheria kuhesabu, kufanya majumuisho, kuthibitisha na kutangaza matokeo.”

Alisema wadau wengine vikiwemo vyama vya siasa watapata matokeo ya hesabu za kura kwa mujibu wa mfumo uliowekwa na Tume.

Aliongeza: “Tunawaomba wadau wote waiachie tume kutimiza kazi yake kama ilivyowekwa kisheria.”

Mwenyekiti huyo alisisitiza kwamba Tume yake itaendesha uchaguzi ulio huru na haki na kwamba askari polisi zaidi ya 85,000 wanapata mafunzo kwa ajili ya kulinda amani na utulivu kuhakikisha uchaguzi wa Agost 8 unaendeshwa bila ya mushkeli wowote.

Aidha kauli ya Raila imewachukiza Wakenya ambao wengi waliingia katika mitandao ya jamii kutoa mawazo yao wakisema mpango wake unaweza kurejesha tena ghasia za baada ya uchaguzi kama ilivyotokea nchini humo baada ya uchaguzi wa 2007 ambako vurugu zilisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,500 na wengi wengine kujeruhiwa na kupoteza makazi yake.

Vurugu hizo zilikuja mara tu baada ya kutangazwa kwa matokeo ambayo yalimuonyesha Mwai Kibaki, aliyekuwa rais madarakani  (incumbent) wa chama cha PNU kumshinda Raila Odinga wa ODM.

Mwenyekiti wa Tume wakati huo Samuel Kivuitu alitangaza matokeo yale chini ya ulinzi mkali wa polisi, na siyo katika ukumbi wa mikutano uliokuwa umepangwa kutangaza matokeo.

Isitoshe mshindi, Mwai Kibaki aliapishwa majira ya magharibi ya siku hiyo hiyo kinyume cha utaratibu na mazoea ya kuwepo wageni waalikwa wakiwemo mabalozi wa nchi za nje na wageni wengine.

Ghasia hizo ziliitia sana doa nchi ya Kenya ambayo kwa kipindi kirefu ilikuwa inaonekana kama tulivu katika sehemu ya machafuko.

Hata hivyo juhudi za mapatano chini ya AU zilizaa serikali ya mpito chini ya Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga na juhudi zikafanywa kuandika katiba mpya ambayo ilitangazwa rasmi mwaka 2011 na uchaguzi wa 2013 ulifanyika chini ya Katiba hiyo.

Hata hivyo matokea ya uchaguzi huo yaliompa ushindi Uhuru Kenyatta kutoka Muungano wa vyama vya Jubilee dhidi ya Raila Odinga wa Muungano wa CORD yalipingwa mahakamani na Muungano wa CORD lakini mahakama ilithibitisha ushindi wa Kenyatta.