Home Habari BAJETI YAWALIZA MADIWANI

BAJETI YAWALIZA MADIWANI

557
0
SHARE
Diwani wa Kata ya Mvumi, Misheni Matalamuna Masaka (aliyesismama), akifafanua jambo wakati wa mafunzo ya Ufuatiliaji wa bajeti ya kilimo na utetezi mjini Dodoma

NA SIDI MGUMIA, ALIYEKUWA DODOMA

WAKATI Serikali ikitangaza ukomo wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/18 kuwa ni Sh trilioni 31.69, huku kipaumbele kikiwekwa kwenye miradi mingi ya ujenzi, baadhi ya madiwani wanaonekana kulia na bajeti hizo kwa hoja kuwa hazikidhi matakwa ya wananchi.

Wakizungumza na RAI kwa nyakati tofauti baadhi ya madiwani walisema kwa muda mrefu sasa wamekuwa wanapata changamoto kubwa juu ya bajeti zinazopangwa na Serikali hasa kwenye fedha zinazoelekezwa kwenye sekta ya kilimo.

Diwani wa kata ya Bigiri, Chamwino, mkoani Dodoma,  Kenneth Yindi, anasema pamoja na kuwa kilimo ndio uti wa mgongo wa nchi, bado wakulima hasa wadogo  wanalima kwa zana duni.

“Wakulima wengi hawalimi kilimo cha tija na hii ikiwa na maana ya kufanya kilimo bila utaratibu maalum. Ipo haja kwa bajeti kuliangalia eneo hili, ambalo linajumuisha idadi kubwa ya watu.

Yindi anaongeza kuwa miundombinu mibovu inawanyima maafisa ugani fursa ya kuwahudumia wananchi kwa karibu zaidi.

“Haya yote yangeweza kuwa tofauti kama bajeti ingeanzia chini kwenda juu ili kuwe na nafasi ya wananchi wa kawaida kutoa mapendekezo katika mahitaji yao yalenge mahitaji ama matakwa ya kilimo,” aliongeza Yindi.

Alisema takriban asilimia 90 ya bajeti inayoelekezwa kwenye wizara inayohusika na kilimo, haiwafikii kabisa walengwa.

Anasema na kwakuwa wao ni Madiwani wawakilishi wa wananchi huwa wanawaambia watu wao kuwa pesa zinakuja kwa ajili yakuwasaida katika masuala ya kilimo na zisipokuja huwa inawaharibia sifa.

“Lakini kama hiyo haitoshi, suala la kubadilishwa kwa bajeti na kupelekwa kwenye kipaumbele kingine zaidi ya kilimo huwa inatugharimu sana,” aliongeza Yindi

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mvumi, Misheni, Matalamuna Masaka, anasema kuwa kilimo kina gharama kubwa sana na pembejeo ziko juu kwa bei.

“Kwa hili, bajeti inabidi iongezwe kwa kiasi kikubwa ili kuwasaidia katika kilimo na Serikali ipunguze kodi kwenye pembejeo,” alisema Diwani Masaka

Diwani Masaka anasema kuwa katika kata zao ukomo wa bajeti ni tatizo na unafanya mambo kwenda ndivyo, sivyo.

Naye Diwani wa Kata ya Msamalo, Chamwino,  Elias Kawea, anasema changamoto zipo ambapo huwa wanapata shida sana kwenye Serikali za Mitaa na kwa ufumbuzi wa hilo ni vema Serikali kupeleka fedha kwa wakati.

“Kuna changamoto ya watu kutokujua bajeti inasemaje. Bajeti haishuki kwa watu wa chini, viongozi wa serikali ya kijiji wapewe elimu ili waweke vipaumbele ili kuwe na mfumo unaofanya kazi kikamilifu. Pesa ndio mawasiliano makuu na bila zenyewe mambo hayatekelezeki,” alisisitiza Kawea

Diwani Viti maalum tarafa ya Ilongero, Halmshauri ya wilaya ya Singida,  Salima Kundya, anasema changamoto zipo kwenye masuala ya ufuatiliajai wa bajeti na kwamba bajeti wanazitengeneza lakini hazina ratiba (kalenda), tunafanya tu kwa uzoefu ama kwa mazoea tuliyonayo.

“Changamoto nyingine ni kuwa bajeti yetu ni kikwazo katika halmashauri kwasababu ni ndogo na haizingatii kipaumbele cha mkulima.

Diwani wa Singida, Emanuel Sima, anasema kuwa changamoto kubwa ni uelewa mdogo wa masuala ya bajeti kwa wananchi hasa vijijini lakini kwakua sasa wamepata elimu kupitia ActioAid watahakikisha wanasimama kidete.

“Tukiwa sambamba kati ya Madiwani na wakulima itatusaidia kuwa tunapata taarifa kwa wakati na kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili wakulima wote kwa ujumla,” alisema Sima

Shirika la Kimataifa la ActionAid lilitoa mafunzo ya ufuatiliaji wa bajeti ya kilimo na utetezi mjini Dodoma kwa baadhi ya Madiwani wa Dar es Salaam, Dodoma na Singida, wakulima na waandishi wa habari.

Malalamiko hayo ya madiwani yalipata majibu kutoka kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alipowasilisha mapendekezo ya Serikali ya mpango wa maendeleo wa taifa na ukomo wa bajeti ya 2017/18, kwa kusema kuwa bajeti ya 2016/17 iliyokuwa ya Sh trilioni 29.5, haijatekelezeka kwa asilimia 100 kutokana na mambo mbalimbali.

Aliyataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni mwamko mdogo wa kulipa kodi, matumizi hafifu ya mashine za risisti za kielektroniki (EFDs) na kuchelewa kupatikana kwa mikopo yenye masharti nafuu na ya kibiashara kutoka nje.