Home Latest News VIONGOZI WASIWADHARAU MACHINGA

VIONGOZI WASIWADHARAU MACHINGA

562
0
SHARE
Wamachinga wakiendelea na biashara zao katika mji wa Moshi

NA JAPHARY MICHAEL,

SUALA la wamachinga katika nchi yetu linatakiwa lipate mtazamo mpya kutoka kwa viongozi wetu wakuu wa nchi.

Kutokana na kukosekana kwa ajira rasmi watu wengi wanawake kwa wanaume wameamua kujiajiri wenyewe kwenye biashara ndogo ndogo ili waweze kukidhi mahitaji yao ikiwemo chakula, malazi, mavazi, elimu, matibabu, n.k.

Utashi huo wa wananchi kujishughulisha na biashara ndogo ndogo unasaidia sana kundi kubwa hasa la vijana kutojihusisha na vitendo vya uhalifu kama wizi, uzuzuraji, n.k. Vitendo vya uhalifu vinapopungua inakuwa ni faraja kwa kundi la matajiri, watu wa kipato cha kati na hata viongozi wetu. Pia linasaidia utulivu wa nchi hivyo vyombo vya ulinzi na usalama navyo vinakuwa na kazi ndogo ya kupambana na uhalifu.

Jambo muhimu sana ambalo viongozi mbalimbali wanapaswa kulifahamu ni kwamba kundi hili ndilo ambalo baadaye linazalisha watu wanaopata mafanikio makubwa kimitaji na hatimaye kuwa wawekezaji mashuhuri na muhimu katika uchumi wa nchi. Mifano ipo mingi nje na ndani ya nchi ambapo wajasiriamali wa sekta isiyo rasmi ndio baadhi yao walirasimishwa kutokana na kukua kwa mitaji yao na leo ni matajiri wakubwa sana katika nchi zao wakiwa wanamiliki mitaji mikubwa sana.

Maoni yangu siku zote kama mtu mwenye uzoefu wa kivitendo katika biashara dogondogo zisizo rasmi hadi kuwa rasmi ni kuwashauri viongozi wenzangu kubadili mitazamo yao juu ya wamachinga ili wawatengenezee mazingira rafiki kwa biashara zao badala ya kuwa kikwazo kwao.

Wakati fulani nikiwa Sweden na Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi tulikuta wenzetu wa Halmashauri-Swedeni wanatenga eneo ndani ya eneo la Manispaa kuanzia siku ya Ijumaa mpaka Jumapili ili wafanye biashara zao.

Hatua hiyo ilimfanya Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi akubaliane na wazo langu la kufanya Manyema kuwa eneo la wamachinga wa bidhaa za shambani. Leo Manyema imesaidia wajasiriamali wadogo wadogo na wengine wamepata mitaji ya kutosha. Lakini watu wameweza kupata vipato vya kujikimu mahitaji yao muhimu.

Baraza la madiwani wa Manispaa ya Moshi limekuwa likiagiza baadhi ya barabara zifungwe siku za Jumamosi na Jumapili na hata Soko kuu na soko la Kiusa, eneo la wazi chini ya barabara ya kahawa, eneo katikati ya stendi kuu na police mess na maeneo kadha wa kadha yaruhusiwe kwa ajili ya wamachinga.

Nyakati za jioni kuanzia saa tisa waruhusiwe kuwa kwenye maeneo ambayo wanakutana na wanunuzi wa mali zao kwa dhana kwamba wamachinga wanatakiwa wakutane na wateja kwa kuwapelekea mali wanazotembeza.

Baraza la madiwani pia limeagiza masoko yote kwenye kata mbalimbali yaboreshwe ili yafanye kazi kiasi kwamba wamachinga wengine wanaweza wakatamani kufanya shughuli zao katika masoko hayo.

Jambo kubwa ambalo ndio najaribu kulichanganua kuhusu utashi wa viongozi wetu hasa kwenye serikali kuu, wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri ni kubadili mitazamo yao ya kuwaona wamachinga kama watu wanaovunja sheria za mipango miji hivyo kila wakati kutoa maagizo ya kuwakamata na kuwasumbua tena kwa kuwanyanganya mali zao.

Baada ya Rais John Magufuli kutoa agizo la kuwatetea Wamachinga mimi nilifarijika sana na nilidhani wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri watajiongeza kwa kuona namna bora ya kujenga mazingira rafiki kwa wamachinga yatakayowafanya wawe na uhuru, amani na utulivu katika biashara zao lakini bado hali imekuwa ni ile ile ya kuwatesa wamachinga na kuwafanya wasiwe na uhakika na maisha yao ya kila siku.

Mara kwa mara nimekuwa nikipaza sauti juu ya umuhimu na ulazima wa kuwalinda watu waliopo katika soko la mitumba la uwanja wa memorial kwa vile najua wafanyabiashara wa mitumba wamekuwa msaada mkubwa kwa mzunguko wa uchumi wa Moshi na Kilimanjaro kwa ujumla hivyo kuwahamisha pale bila kuwa na mahala sahihi na pa uhakika pa kuwahamishia ni kutikisa uchumi wa mji wa Moshi kwa kiwango kikubwa.

Aidha, ni vema tukawalinda wafanyabiashara wadogo wadogo katika soko la Mbuyuni na Manyema katika manispaa ya Moshi kwavile wana mchango mkubwa sana kwa mzunguko wa uchumi wa Moshi.

Vilevile vile ni lazima tujenge mazingira rafiki kwa wamachinga wote, waendesha bodaboda, na wajasiriamali wengine wadogo katika manispaa ya Moshi ili wawe na uhakika wa ajira zao ili kuweza kusukuma ustawi wa uchumi wa Moshi.

Zoezi lolote la kuwabughudhi Wamachinga kwa kutumia nguvu nyingi ni unyanyasaji usiozingatia haki
na utu wa watu wanaojitafutia riziki yao halali hasa katika nchi ambayo kuna upungufu wa ajira za uhakika kutokana na upungufu wa viwanda na uwekezaji mwingine.

Naamini tukiwawezesha wamachinga kuwa na mazingira mazuri ya kufanya kazi zao baada ya muda fulani tutatengeneza watu wenye mitaji ya kati hivyo kuimarisha uwekezaji na ukusanyaji wa mapato katika Taifa letu.

Mwandishi wa makala hii ni Mbunge wa Moshi Mjini (Chadema)