Home Habari kuu TAIFA NJIA PANDA

TAIFA NJIA PANDA

704
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI,

MFULULIZO wa matukio yenye sura ya utekaji,  utesaji, uvamizi na matumizi ya silaha za moto hadharani  kwa baadhi ya wasanii,wanahabari na wanasiasa, yanatajwa kuliweka Taifa njia panda, RAI linachambua.

Matukio hayo yanayowakuta raia wasio na hatia yameanza kuonekana miaka mingi iliyopita, hata hivyo kwa mwaka huu yanaonekana kushamiri hadi kufikia hatua ya kujadiliwa ndani ya vikao vya Bunge.

Mwanzoni mwa wiki hii Bunge lilipuka baada ya baadhi ya wabunge bila kujali itikadi zao za vyama kuungana na kupaza sauti zao wakitaka shughuli zote zisitishwe ili kujadili jambo hilo, ambalo lilikolezwa zaidi na hatua ya kutekwa kwa Mwanamuziki Ibrahimn Musa ‘Roma Mkatoliki’.

Roma ambaye anadaiwa kutekwa na watu wasiojulikana kwa zaidi ya siku mbili, juzi aliwaambia waandishi wa habari kuwa alitekwa na watu wasiojulikana akiwa na wanamuziki wenzake na kufichwa mahali ambako hawakujui huku wakiteswa na kuhojiwa kwa siku zote hizo.

Mkutano huo wa Roma na waandishi wa habari pia ulihudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, hatua ambayo ilionesha kuibua maswali nje na ndani ya Bunge.

Mbunge wa Chemba,(CCM) Juma Nkamia ni miongoni mwa watu waliohoji uwapo wa Dk. Mwakyembe kwenye mkutano huo wa Roma huku akihoji kuwa ni kwa namna gani Serikali itakataa kuhusishwa na kadhia hiyo.

Nkamia alimshangaa Dk Mwakyembe kuonekana kwenye mkutano wa Roma akisema, wakati mwingine viongozi wa serikali wanamchonganisha Rais na wananchi bila sababu.

“Serikali lazima iwe active (imara) lakini siyo kuwa active kwa kukosea, nitoe mfano samahani sana, jana (juzi) nilikuwa naangalia mkutano wa waandishi wa habari, wa yule bwana anaitwa Roma Mkatoliki, hivi Waziri wa Habari alienda kufanya nini?

“Unajua wakati mwingine unaweza kuambiwa ukweli ukachukia lakini ni afadhali uambiwe  ukweli, Waziri wa Habari alikwenda kwenye mkutano wa Roma Mkatolini, anampisha na kiti, anayeongoza mkutano ule wa Press Conference ile Zamaradi Kawawa, Ofisa wa Serikali.

“Hivi kesho mtu akikwambia wewe ndiye ulimteka Roma utakataaje? Ni vizuri uchukue ukweli hata kama unauma, lakini you take it, at the end of day (unauchukua na mwisho wa siku) unaweza ukafanya marekebisho.

“Ebu liangalieni hili ilitokea wapi mpaka waziri akakosa kiti, alafu huyu mtu binafsi anafanya Press Conference wewe naenda kufanya nini? What are doing there, alafu leo kina Nkamia wakisema ukweli huku kuna watu wanasema, unajua ni kwa sababu  alikosa uwaziri sijui nini (Nkamia),    this is principle, we have to tell you the truth,” alisema.

Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph  Mbilinyi ‘Sugu’, alisema Taifa limekuwa gizani kwa utamaduni mpya uliozuka wa kuteka watu, utamaduni ambao si wa nchi bali ni wa kimafia.

Alisema utamaduni huo kwa mara ya mwisho ulikuwapo katika mipaka ya Bara na Zanzibar kwa kupotezwa Mzee Kassim Hanga.

“Lakini tangu kipindi hicho haujakuwapo tena. Toka operesheni hii ya kuteka watu nyara ianze, kila anayehusika na usalama likiwamo Jeshi la Polisi, always (kila wakati) wanasema ‘hatujui, hatujawaona kwenye vituo vyote” alisema Sugu.

Kwa upande wake Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwani Kikwete nae alionesha hofu yake dhidi ya hali inayoendelea nchini kwa kusema kuwa hakuna sababu kwa serikali kukaa kimya huku wananchi wakiishi kwa wasiwasi.

“Hakuna sababu ya Mwigulu Nchemba (Waziri wa Mambo ya Ndani) kuendelea kukaa kimya wakati wananchi wanaishi kwa wasiwasi juu ya usalama wao. Kutoa kauli kunasaidia kutoa hofu,”alisema Kikwete.

Mbunge wa Sumbawanga Mjini kwa tiketi ya CCM, Aeshi Hilal (CCM) ni miongoni mwa wabunge wanaoliona Taifa liko njia panda.

Katika maelezo Hilal, akichangia hotuba ya Waziri Mkuu, pamoja na mambo mengine alisema “Nilikuwa sitaki kusema lakini ngoja hili niseme, tena mimi sikutishwa kwa maneno, yeye mwenyewe nilikutana naye ana kwa ana akiniambia, ‘nyie wabunge mmezidi unafiki’ kwa bahati mbaya zaidi maneno haya ameyatamka mbele ya Mkuu wa Wilaya wa Kinondoni (Ally Hapi), akasema ‘Wabunge mmezidi unafiki, na nita-deal na nyie nikianza na wewe’.

“Mimi leo Mheshimiwa, Dar es Salaam sikanyagi, na ninaiogopa, yaani nilikuwa nimei-miss mno, baada ya kutishwa nimeogopa inabidi nikae Dodoma na Sumbawanga,  kwa hiyo nilitaka tu nisema kwamba naliarifu Bunge na familia yangu ijue kwamba Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, miongoni mwa watu aliowatisha ni pamoja na mimi.

“Mengine mabaya siyasemi, wala mazuri yake siyasemi, nasemea hili kwa usalama wa nafsi yangu, najua yapo mazuri aliyoyafanya, yapo mabaya aliyoyafanya, lakini mimi naomba niseme hilo moja tu kwamba, ni bora tukaliangalia kwa makini niko tayari kuhojiwa, nipo tayari kuja kusema, na nikatoe ushahidi kwa sababu nilikuwa hoteli inayoitwa Colosseum hoteli, niliitwa mbele ya Mkuu wa Wilaya na akanitisha,” alisema Aeshi.

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe alionekana kukerwa zaidi na mwenendo wa mambo nchini baada ya kuamua kutupa lawama zake moja kwa moja kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama, akidai kuwa hata yeye alishawahi kukumbana na kadhia hiyo.

Bashe alibainisha kuwa ameambiwa na baadhi ya mawaziri kuwa yeye ni kati ya wabunge 11 ambao wakikaa vibaya wanaweza kupoteza maisha.

Bashe ambaye aliomba mwongozo kwa Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, kuhusu kuahirisha hoja zinazojadiliwa ili kujadili matukio hayo ya utekaji nchini alisema. “Kumekuwa kukitokea matukio ya sintofahamu na si tu kuhusu wabunge, hata raia, kumekuwa na kikundi ambacho kimekuwa kikiteka watu.

“Miongoni mwa watu waliowahi kutekwa ni Mheshimiwa Msukuma (Joseph Msukuma, Mbunge wa Geita Vijijini) Mheshimiwa Bashe (Hussein Bashe), kwenye Mkutano Mkuu wa CCM, ndugu Malima (Adam Malima, aliyekuwa Mbunge wa Mkuranga).

“Ben Saanane (Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema) amepotea, juzi ametekwa ndugu Roma Mkatoliki (Msanii Ibrahim Mussa), Mheshimiwa Naibu Spika, nasema ni jambo la dharura kwa sababu hawa ni wale ambao wanafahamika, hatujui ni Watanzania wangapi hawafahamiki katika ngazi za chini.

“Zipo taarifa ambazo binafsi nimezipokea kutoka kwa baadhi ya mawaziri wakinitahadharisha mimi binafsi kwamba, Bashe kuwa makini wewe ni mmoja kati ya wabunge 11 ambao wamewekwa katika list (orodha), mkikaa barabarani vibaya, mnaweza kupoteza maisha yenu.

“Mheshimiwa Naibu Spika jambo hili ni dharura kwa sababu, kikundi hiki kilichomo ndani ya (anataja moja ya taasisi ya mambo ya usalama), ambacho kimeamua kuchukua mamlaka haya ya kuteka watu, kinaharibu heshima ya Serikali yetu, kinaharibu heshima ya chama changu, ambacho mimi na wabunge wenzangu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tuliomba ridhaa ya kutaka kuwaongoza Watanzania na si kuwahatarishia maisha yao.

“Kwa hiyo naomba mheshimiwa Naibu Spika, uruhusu jambo  hili tulijadili kama Bunge na ikikupendeza Bunge hili liunde Committee (kamati) maalumu ya kuweza kuchunguza jambo hili linaloendelea katika nchi yetu.

“Ama kuiagiza Kamati ya Usalama na Mambo ya Nje ya Bunge hili,  iweze kufanya kazi yake na kutuletea taarifa kwa ajili ua usalama wa wananchi wa nchi hii, hali ya nchi siyo salama, Watanzania wana taharuki, Watanzania wanajadili mambo haya katika mitandao, na there is no statement ya hope (hakuna kauli ya matumaini) kutoka serikalini,” alisema Bashe.

Bashe ahakuishia hapo, siku iliyofuata aliibua hoja jingine nzito kwa kuwataka Mawaziri kuacha unafiki kwa kile alichokiita kukamatwa na usalama wa Taifa.

,“Kwamba mimi Hussein Mohamed Bashe, nilikamatwa na maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa, acheni unafiki, acheni unafiki, we are all Tanzanian (wote ni Watanzania) hamjawahi kunyanyaswa ninyi, acheni mimi ni mwana CCM, I don’t care (sijali).

“Mimi nimekamatwa na usalama, nimeonewa in this country acheni unafiki, tunavumilia mambo mengi, acheni, hamjawahi kuwa  humiliated,” alisema Bashe.

Bashe aliyasema hayo baada ya  kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Hassa ‘Zungu’ akipinga kile utaratibu ulioombwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, George Simbachawene akipinga hatua ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) kudai Idara ya Usalama wa Taifa inahusika kwenye kukamata watu.

Akizungumzia suala hilo alisema ni vyema sasa ikaundwa kamati maalumu ya kuchunguza vitendo vya utekaji.

“Mtanzania aliyepotea Ben Saanane ni suala ambalo linapaswa kuchukuliwa kwa uzito wa juu, sio suala linalopaswa kuchukuliwa kisiasa.

“Usalama wa Taifa hawana mamlaka ya kukamata hata wakimuona mwizi hivi, sheria inakataa kwa sababu ya kuepuka haya mambo ambayo tunayaona sasa hivi kumekuwa na matatizo, hatuyapatii ufumbuzi nyinyi mnafahamu.

“Aliyekuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Kibanda (Absalom) alikamatwa, akateswa, akaumizwa na leo jicho lake moja halioni, lakini hadi leo hakuna hata mtu mmoja aliyekamatwa.

“Kulingana na tukio kama hilo katika mazingira kama haya, hatuna namna na katika historia nyinyi wenyewe ni mashahidi ambao mmekaa bungeni muda mrefu, haijatokea Bunge hili kujadili usalama wa taifa kwa mara ya kwanza tunaivuka hiyo ‘taboo’ (miiko).

“Watu wamechoka na naomba kwa mujibu wa kanuni ya 120 ya Bunge, natoa taarifa rasmi kwamba nitaleta hoja binafsi ndani ya Bunge ili  liunde Kamati Teule ya kufanya uchunguzi wa matukio yote ya upoteaji matukio yote ya mauaji na matukio yote ambayo yanaweza kujenga taswira hasi dhidi ya ya usalama wa taifa katika nchi yetu,” alisema

“Tuanze kujianika, niliwaeleza ‘its taboo’ kuongelea usalama wa taifa ndani ya Bunge, lakini leo tunaongelea kwasababu ya utaratibu unaoendelea,” alisema.

PROF. LIPUMBA, BAREGU WAONYA

Wakizungumza na RAI kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahimu Lipumba na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu wameionya Serikali na kuhoji ukimya wake licha ya Rais John Magufuli kujitokeza mara kwa mara kuzungumzia matukio ya kawaida huku hili la utekaji akiendelea kudumisha ukimya.

Profesa Lipumba alisema licha ya kushtushwa na taarifa za Bashe ni muhimu kwa serikali kurudisha imani ndani ya jamii na kulitolea kauli suala hilo.

“Serikali inatakiwa kukiri kuwa mambo haya ni mambo ambayo hayakubaliki na wahusika watachukuliwa hatua za kisheria, hivyo ni muhimu sana kuwajengea imani watanzania, kwani ni jambo ambalo halina msaada kama mtu ana makosa polisi wafanye kazi zao kwa uwazi na kufuata sheria.

“Mwigulu amesema hilo ndilo linatekelezwa na watu wataenda kuhojiwa kwa kufuata taratibu lakini hili suala la watu kukamatwa haifahamiki wamekatwa na nani inatujengea taswira mbaya na utawala wa sheria unapoteza imani ya wawekezaji… inabidi kujenga imani haraka kwa jamii, ni jambo ambalo serikali inatakiwa kujitahidi kujenga uaminifu kwa jamii kuhakikisha mambo haya yanashughulikiwa mapema,” alisema Prof. Lipumba.

Hoja ya Profesa Lipumba iliungwa mkono pia na Profesa Baregu ambaye alisema ni maajabu sana kwamba matukio ya namna hii kama hili la Roma badala ya kufuatiliwa kwa karibu na waziri wa mambo ya ndani Mwigulu Nchemba linafuatiliwa na waziri wa habari, sanaa, utamaduni na michezo. Dk. Harrison Mwakyembe.

“Na kimya cha Rais kinapeleka ujumbe kwa wanaoelewa kuwa nini kinatokea kwa sababu rais angezungumzia angewaambia wananchi kuwa waangalifu na kutoa taarifa namna anafanya haya mambo, ila ukimya wake inaleta picha kwamba wanajua hivi vitendo, na mimi kama mwanasayansi wa siasa  hivi ni vitendo vinaendana na utawala kandamizi, au udikteta kutengena uoga.

“Kwa sababu tangu kipindi cha Dk. Ulimboka hakuna hata mmoja aliyetoa taarifa inayoelewekakwa sababu wametishwa hawawezi kufungua mdomo wanaogopa labda kuuawa. Kina Roma hawawezi kusema kuhusu maswali waliyoulizwa yaani inatisha sana, inakumbusha matukio ya Amerika ya kusini, nilipokwenda huko katika nchi za Argentina na Chile miaka 20 kulikuwa na akina mama bado wanawatafuta watoto wao.

“Tunatakiwa tuwe macho sana na kama wanataka watanzania warudishe imani watoe taarifa za kuridhisha, basi kama wameshindwa waombe msaada wa vyombo vya uchunguzi vya nje kama interpoll vitusadie kama tumeshindwa kiasi hicho,” alisema Profesa Baregu.

Aidha, kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima naye katika ibada yake Jumapili hii alionya kuwa Tanzania imeanza kuwa mahala pa hatari, huku akitaka vyombo vya dola vichukue hatua kuyakomesha.

Gwajima pia alimtaja  mdogo wake, Mchungaji Samson Gwajima ambaye alidai alitekwa wiki iliyopita mkoani Mwanza.

“Tanzania inaanza kuwa nchi ya watu kupotea kama mzuka, Ben Saanane hajaonekana hadi leo, Meneja wa Diamond alisema wa kuulizwa aliko Roma ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, wakaenda akasema atapatikana kabla ya Jumapili.

“Aliyesema atapatikana Jumapili ama alijua, ana jeshi la kumfuatilia alipo, amemficha, amempa kazi maalumu ama alikuwa naye.

“Nazungumza haya kwa sababu hata mdogo wangu (Mchungaji Samson Gwajima) naye alitekwa, lakini alifanikiwa kujinasua, hivyo naunganisha watekaji wa Dar es Salaam na Mwanza,” alisema.

MWIGULU ATOA NENO

Akizungumza nje ya ukumbi wa Bunge mapema wiki hii, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, alisema inabidi watu watofautishe kati ya kutekwa na kukamatwa ingawa hata wanaokamata watu, inapaswa kuwaeleza wanawakamata kwa kosa gani.

“Serikali ina mkakati wa kuhakikisha wananchi wanakuwa katika usalama wao wenyewe na mali zao na wananchi tunawaomba sana kuendelea kutoa ushirikiano ili kuwabaini watu wanaotenda mauvu,” alisema.

Kuhusu masuala ya utekwaji kwa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Roma aliyeonekana na Saanane ambaye ukimya umetawala alisema hayo ni masuala  ambayo yako katika ngazi ya kiuchunguzi, hawezi kuyazungumzia.