Home Uchambuzi Afrika UCHAGUZI MKUU KENYA 2017: MMAREKANI AJITOSA KUGOMBEA URAIS

UCHAGUZI MKUU KENYA 2017: MMAREKANI AJITOSA KUGOMBEA URAIS

396
0
SHARE
Amram Musungu

SALT LAKE CITY, USA

Amram Musungu (39) mwenye uraia wa nchi mbili (Marekani na Kenya) ambaye anaishi Marekani, ametangaza kugombea urais wa Kenya katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti 8 mwaka huu.

Musungu ni muumini wa madhehebu ya Mormon Kanisa la “Church of Jesus Christ of Latter-day Saints” na mhitimu wa Shahada ya juu (Masters) katika masuala ya  Uhasibu kutoka chuo cha Westminister College, kilichopo mji wa Salt Lake Jimbo la Utah.

Katika mahojiano na gazeti moja la mji huo wa Salt Lake alisema wiki iliyopita kwamba mwaka mmoja uliopita alifuatwa na wanasiasa kutoka Kenya kuwawakilisha kama mgombea wao wa urais katika uchaguzi wa mwaka huu.

Anasema kwamba walipenda kumteua yeye kama mgombea kutokana na uwezo wake mkubwa alio nao kiuongozi, na pia hadhi yake na maono yake kwa wananchi ambayo ameyaonyesha kwa watu anaoishi nao huko Marekani.

Amram mwenye mke na watoto wawili wa umri wa miaka 4 na 8 alisema wakati anaondoka Kenya na kwenda kuishi Marekani alikuwa ameahidi kwamba akiwa Marekani atafukuzia elimu bora na kupata mafunzo mengine mbali mbali na baadaye arudi nyumbani kutoa uongozi bora kwa wananchi.

Alisema sasa ameamua kutimiza ndoto hiyo, kwa kukubali kugombea urais kwani mimi na familia yangu tunaamini kwa nguvu kwamba “baba yetu aliye mbinguni ndiyo ameamua iwe hivyo.”

Anasema vizheni yake ni kuwapa wananchi wa Kenya maisha bora ya baadaye na kuwajaza matumaini makubwa na kuongeza kwamba anatarajia kuunda serikali ya uwazi ambayo itaruhusu mijadala ya wazi baina ya serikali na wananchi kitu anachsema kwamba litasukuma maendeleo. Aidha amesema serikali yake itakuwa na uhusiano mzuri na majirani zake.

Anaeleza historia ya maisha yake kwamba alizaliwa katika kijiji cha Hamuyundi, County ya Vihiga magharaibi mwa Kenya na kupata elimu yake ya awali katika shule ya eneo hilo ambayo ilibidi atembee kilomita 8 kila siku kwenda na kurudi shule.

Anahadithia kwamba hakuwahi kuwa na pea ya viatu hadi alipofikisha umri wa miaka 15. Lakini sasa anasema kwa jitihada zake ameweza kujielimisha na kujipa maendeleo makubwa binafsi na kwamba umefika wakati wa kuwainua wananchi wa Kenya kwani ana uhakika atakuwa rais bora kuliko wote waliowahi kutokea nchini Kenya kwani katika maisha yake yote amekuwa amejitayarisha kwa hilo.

Anaongeza: “Nimo katika kinyang’anyiro hiki ili nishinde,” na kuongezea kwamba inaweza kuwa rahisi kwake kutimiza ndoto yake akiwa huko huko Marekani.

Alisema wazo la kugombea urais wa nchi kama Kenya halikumjia hivi hivi tu kwani alitumia masaa mengi kuliwaza – hasa akifikira ufisadi uliokithiri na vurugu za kisiasa katika nchini Kenya.

Amesema kila siku alikuwa anawaza hali ya usalama wa nchi ambayo imekuwa isiyoridhisha, asilimia kubwa ya watu wasiokuwa na ajira na uchumi uliodorora – na hivyo anasema ana mpango kabamne wa kuyarekebisha yote hayo.

Pia ameeleza kwamba kampeni yake imeshaanza katika kiwango cha mashina na kupitia ujumbe katika mitandao ya jamii ili iwafikie wananchi wengi na zaidi walengwa ni makundi yaliyo katika hali ngumu, wanawake na watoto ambao anasema ndiyo watafaidika sana na sera zake akiwa rais.

Amesema hivi karibuni atateua mgombea mwenza wake ambaye atakuwa wa kike, hatua ambayo itathibitisha kwamba hama mzaha katika harakati zaje kwani mgombea mwenza wa kike atawasaidia wanawake nchini humo kuwa na sauti katika masuala yao.