Home Makala MFALME WA SWAZILAND APIGA MARUFUKU WANANDOA KUTALIKIANA  

MFALME WA SWAZILAND APIGA MARUFUKU WANANDOA KUTALIKIANA  

312
0
SHARE

MBABANE, SWAZILAND


Mfalme Mswati III wa nchi ndogo ya Swaziland kusini mwa Afrika amepiga marufuku kutalikiana nchini mwake.

Ametoa marufuku hiyo kupitia agizo (decree) ya Mfalme katika mkutano wake na viongozi wa dini ya Kikristo ulifanyika katika Jumba la Mfalme la Engabezweni siku ya Jumapili iliyopita.

Gazeti la The Times of Swaziland la nchi hiyo wiki iliyopita limemnukuu Mfalme Mswati akiwaambia makasisi hao kuwaarifu wananchi kwamba hakuna kuachana kabisa baada ya ndoa kufungwa.

Alisema: “Katika mila zetu baada tu ya “kutiana pingu za maisha” basi zinakuwa hivyo hivyo – pingu za maisha na katu hakuna kurudi nyuma.”

Katazo hilo la Mfalme limekuja wakati Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo inatayarisha Muswada mpya wa Sheria Ndoa ya 2017 ambayo itaorodhesha maeneo matano ambapo wanandoa wanaweza kutalikiana.

Sheria ya sasa ya ndoa iliyotungwa mwaka 1964 hairuhusu talaka. Kwa maana nyingine ni kwamba Mfalme huyo anapingana na mwanasheria wake mkuu.

Wachunguzi wa mambo wanasema kauli yake ya katazo ni kumwambia asiendelee na mpamgo wake wa kupitisha muswada mpya wa ndoa, na iwapo utapitishwa Bungeni basi kuna uwezekano mkubwa hatautia saini.

Aidha gazeti hilo limemnukuu Mfalme Mswati akiifaninisha ndoa kama ni mkataba na Mwenyezi Mungu, akisema si sahihi kwa watu kuvunja mikataba wanayowekeana na muumba wao.

Swaziland ni ni miongoni mwa nchi zilizobakia zenye ufalme wa madaraka makubwa.

Kufuatana na ripoti za Umoja wa Mataifa, nchi hiyo ina ina viwango vya juu kabisa vya maambukizi ya ukimwi duniani. Kati wa Waswazi 1.2 milioni, laki mbili na elfu kumi wana maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Mfalme Mswati alitawazwa mwaka 1986 akiwa na umri wa miaka 18 akirithi kiti cha baba yake aliyetawala muda mrefu, Mfalme Sobhuza II ambaye alikufa akiwa na umri wa miaka 82.

Mfalme Mswati mwenye unri wa miaka 49 anajulikana kama ‘Ngweyama’ – yaani simba. Alama hii pia inatumika katika nembo ya taifa (coat of arms). Kwa upande mwingine  “indlovukazi” – yaani tembo ndiyo alama inayomtambulisha Mama wa Mfalme na imo katika nembo hiyo ya taifa.

Kwa sasa Mfalme Mswati ana wake 15 na watoto 24. Chini ya sheria za nchi hiyo, wake zake wawili wa kwanza huchaguliwa na wajumbe wa baraza la wazee.

Aidha huchagua mchumba mpya katika sherehe za kijadi za kila na huwao pindi watakapobeba mimba kuhakikisha kwamba wana uwezo wa kuzalisha warithi wa mfalme.