Home Makala TANZANIA HAKUNA MFUMO WA VYAMA VINGI

TANZANIA HAKUNA MFUMO WA VYAMA VINGI

493
0
SHARE

Na YAHYA MSANGI


KWA wale ambao walichelewa kuzaliwa niwape historia kidogo ili twende pamoja. Tanganyika iliwahi kupitia mfumo wa vyama vingi hasa kabla ya uhuru.

Msije mkadhani ulianza 1985 baada ya ile kura. Wengine tuliuishi kabla ya hapo. Wakati ule mtu ungeweza kudai kuwa kweli kuna mfumo wa vyama vingi. Kwa nini?
Ni kwa kuwa kulikuwa na sera, itikadi na mikakati tofauti baina ya vyama. Ulikuwa unaweza kuona hawa wanatetea ubepari, wale wanatetea ujamaa na wale wako kati kwa kati.
Baada ya uhuru Tanganyika ikaamua kufuata mfumo wa chama kimoja na mwaka 1964 nchi ikarudi mfumo wa vyama vingi baada ya kujiunga na Zanzibar.

Bara kukawa na TANU Zanzibar ikawepo ASP. Kipindi hicho mtu pia unaweza kudai kulikuwa na vyama viwili (si vingi) Sera, itikadi na mikakati ikawa inatofautiana. Ilipofika 1977 nchi ikarudi kwenye mfumo wa chama kimoja.
Sasa nijibu swali la kwanza, je Tanzania ya leo ina mfumo wa vyama vingi? Jibu langu ni hapana! Ili mfumo wa vyama vingi uwepo kuna kanuni lazima zisimame.
Mosi: Utofauti bayana wa sera, itikadi na mikakati ya kujenga nchi. Nikitizama vyama vya upinzani na nikalinganisha sera, itikadi na mikakati kati yao na CCM sioni tofauti iliyo wazi.

Ni kama vile vyama vya upinzani ni mwanafunzi aliyeiba daftari la mwanafunzi mwenzao na kunakili bila kubadili hata nukta. Mbaya zaidi ni kama katika kiwewe na harakati za kunakili kuna majibu mazuri wameruka.

Kutokuwepo kwa tofauti iliyo bayana ya kisera, kiitikadi na kimkakati kunaua kabisa dhana ya uwepo wa vyama vingi. Mfumo wa vyama vingi haimaainishi idadi tu ya vyama! Ingekuwa hivyo mbona nchi kama China ingekuwa kinara wa vyama vingi? Maana kwenye vitabu majina mengi lakini uwanjani timu ni moja!

Pili: Ili vyama vingi viwepo lazima miundo ya kiutendaji au kitaasisi itofautiane. Lakini ukitizama miundo na mfumo wa kutoa maamuzi wa vyama vya upinzani hauna tofauti kubwa iliyo wazi na ya CCM! Sawa kijijini umpinge mganga wa kienyeji lakini utumie tunguri na manyanga yake kuongoza nyumba yako na kutolea maamuzi! Walio pembeni hawataona tofauti yako wewe na huyo mganga hata kama utadai wewe ni Paroko au Shehe!

Tatu: Ili mfumo wa vyama vingi usimame inabidi vyama hasa vya upinzani vionyeshe kwa matendo kuwa vinathamini na kuheshimu mfumo wa vyama vingi.

Haiwezekani vijiendeshe kwa mfumo wa chama kimoja halafu vidai vinashiriki au vinataka mfumo wa vyama vingi! Kwa nini nasema hivi? Niwapeleke moja kwa moja hadi ngome ya UKAWA kupata majibu! Ndani ya UKAWA kuna mfumo wa chama kimoja!

Ni zuzu tu ambae hataona kuwa ndani ya UKAWA kuna chama kimoja! Wengine wapambe nuksi! Na ndio maana katika kuachiana majimbo tuliona chama kimoja kikivamia wanyonge! Na baada ya uchaguzi tumeona wanyonge walivyodhoofika! Iko wapi ile CUF ngangari? Iko wapi NCCR ya Mrema na Marando?

Nini kimeisibu NLD? Ni kwa kuwa kuna mfumo wa chama kimoja ndani ya UKAWA! Kuna chama ni sawa na shehe anayehubiri uharamu wa kitimoto lakini anajichana mishikaki ya kitimoto chumbani yeye na mkewe! Ni sawa na Padri anahubiri ubaya wa pombe lakini nyumbani kwake anakunywa hadi anakuwa mbwiii!
Na uchama kimoja wa kambi ya upinzani hauko ndani ya UKAWA pekee, umeenea hadi nje! Kina TLP, ACT, CHAUMA na wenzao hawafurukuti ndani ya kambi maana kuna chama kimoja! Ndio maana saa nyingine ukisikiza maneno kama ya Zitto Kabwe utatambua huko kuna mfumo wa chama kimoja!

Hebu jiulize Mbowe alipotajwa kuhusu kuhusika na biashara ya unga! Ni Zitto aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kudai eti kama Mbowe angekuwa zungu basi yeye angejua maana amemlea na wamefanya naye kazi pamoja!

Ni Zitto yuleyule aliyetaka kugombea nafasi ya huyo aliyemlea na ni Zitto huyohuyo aliyefurushwa na huyo aliyemlea! Ni dalili kuwa kuna chama kimoja tena supreme! Yaani kwenye kambi ya upinzani kina ACT, CUF, TLP, NCCR, NLD, CHAUMA na wenzao ni sawa na nyasi kwenye tenga la nyanya! Kazi yao ni kuzuia nyanya zisisagane! They don’t count! Nyanya zikifika sokoni nyasi hutupwa au huchomwa moto maana zinageuka uchafu!
Sasa nchi itakuwaje na mfumo wa vyama vingi ilhali upinzani unaendeshwa kwa mfumo wa chama kimoja?

Nne: Ili mfumo wa vyama vingi usimame lazima pasiwe na tofauti kuubwa ya nguvu kati ya vyama. Ni mjinga tu asiyeona kuwa CCM ina maguvu makubwa kuliko wapinzani mmojammoja au hata wakiwekwa kwenye tenga moja! Yaani CCM sawa na Tyson apigane na kina Power Ngaramtoni! Lazima Power auawe hata akijifanya ngangari vipi! Na si kosa la CCM hata kidogo! Chama chochote kinachojitambua hukusanya maguvu hasa kwa kutumia udhaifu wa vyama vilivyojisahau!

Hivi kwa nini CCM isiwe na maguvu kama wapinzani wake nguvu kidogo walizonazo wanazitumia kuomba cheti cha mtu ambae hawajamwajiri, kuitisha press na kutangaza wameota rais atakufa, kudai ripoti ya faru john, kujenga ukuta hewa, kuandaa operesheni hewa ya katafunua, kukamatwa na kuswekwa rumande kwa kusema rais ni rais uchwara halafu baade kuomba kukutana nae kubadilishana mawazo na upuuzi mwingine kama huo? Kuna ubaya gani CCM kutumia fursa hii kujikusanyia maguvu?
Ukitizama kwa wenzetu waliobobea kwenye mfumo wa vyama vingi hakuna tofauti kubwa sana ya maguvu baina yao mfano democrats na republicans au labour na conservatives.

Tofauti ikishakuwa kuubwa mno ni mzaha kudai kuna mfumo wa vyama vingi. Sawa ukute kuna mabondia kibao sehemu lakini mmoja ana afya njema wengine wana utapiamlo halafu udai hapa kuna mpambano kabambe wa ngumi za kulipwa! Utakuwa unawatakia kifo wagonjwa!
Itoshe kwa leo kuonyesha kwa nini Tanzania hakuna mfumo wa vyama vingi bali ni illusion tu!
Sasa nijibu swali la pili, je ni lazima kuufutwa mfumo wa vyama vingi?
Jibu langu la dhati kabisa ni kuwa hakuna ulazima na huenda tumepanda basi hatulijui vizuri dereva nani, linaenda wapi na tutashuka kituo gani!
Ngoja nitoe sababu mbili tatu hivi ili hata zuzu aweze kuwaza!
Kwanza nijuavyo mimi ukiniambia vitu ni vingi mawazo hayatanipelekea kudhani ni viwili! Wala sitawaza kuwa nyingi ni zaidi ya moja maana nitakuwa nyumbu! Ni nyumbu tu inadhani mamba kula mmoja au wa wawili ni kula nyumbu nyingi! Kama binadamu mwenye ufahamu ukiambia kuna vyama vingi nitafikiria kuanzia labda 10 na kuendelea: Au basi walau vyama vitano! Sasa hebu angalia vituko vya vyama vingi huko ambapo tunaambiwa ni waasisi wa vyama vingi.

Utazaliwa hadi utakufa Marekani ataingia White House kama si Republicans ni Democrats! Utazaliwa hadi utazeeka Uingereza ataingia aidha Labour au Conservatives! Na tunaaminishwa huu ndio mfumo wa vyama vingi ilhali tunajua wengine ni wasindikizaji tu! Sasa huu wingi unakujaje hapo? Maana tofauti yao na wa chama kimoja ni chama kimoja tu! Si tofauti kubwa hata kidogo!.

Kama katika mfumo wa chama kimoja kuna hadaa ya chama kimoja basi kwenye mfumo wa vyama vingi kuna hadaa ya vyama viwili tu! Kutokana na hadaa hii ya kutuaminisha kuwa mfumo wa vyama vingi unatoa fursa kwa vyama ‘vingi’ kuongoza nchi sioni haja ya kuupa kipaumbele zaidi ya mifumo mingine.
Pili naona si lazima tuukumbatie mfumo wa vyama vingi kwa kuwa dunia sasa inaongozwa kiuchumi, kidiplomasia na kijeshi na magwiji wa mfumo wa chama kimoja! Kina China, Russia, Korea, Cuba, Iran! Tena hata baada ya vyama vingi kuleta hila ya vikwazo kila kukicha! Bado wa chama kimoja wameibuka kidedea! Leo kina Marekani na Ulaya wanahaha kudhibiti nguvu za China duniani! Leo hii Iran inasumbua wakubwa na vibaraka wao mashariki ya kati! Iran peke yake anakabiliana na wa vyama vingi kule Iraq, Syria, Lebanon na Yemen!
Sasa hivi kweli sisi si wajinga? Tuache kumuiga China, Cuba, Russia, Iran na North Korea tuige walioshindwa? Hakika tukitaka sasa tuendelee tuige mfumo wao si huu upuuzi wa vyama utitiri na utandawizi! Toka tumeruhusu vyama utitiri tumepata nini? Kila siku tunakalia kutukanana, kupigana, kukwamishana na kukamatana!

Anatoka mtu na wazo zuri la kupinga biashara ya madawa ya kulevya anapingwa, anatukanwa kwa kuwa tu tuna vyama vingi! Nenda uchina utetee mihadharati ukione cha nyeti za kuku! Ni sie tunaelea ujinga tukidhani kwa mwamvuli wa vyama vingi! Nenda Moscow utoke barabarani udai umeota Putin atakufa uone! Hutaota tena maishani mwako!
Tatu, nikitizama maendeleo nchi ilipita chini ya mfumo wa chama kimoja na hasara nchi imeingia toka tunakili mfumo wa vyama vingi ni heri turudi chama kimoja! Chini ya chama kimoja shule zilijengwa, viwanda hadi vya gari linaitwa nyumbu vilijengwa, matrekta ya valmet tu ku-assemble, hospitali za rufaa hadi zahanati kila kona ya nchi, n.k. Toka tukopi vyama vingi ni kuuza kila kitu!

Sasa cha ajabu hata wanaokoroma kuhusu ufisadi wanasahau umeletwa baada ya mfumo wa vyama vingi kunakiliwa kama hatuna vichwa! Nyerere alisema ubepari ni unyama! Watu wanashabikia mfumo wa wanyama wakiliwa wanakoroma! Mazuzu! Mfumo huu ambao msingi wake ni ubepari umeanguka mno hasa Ulaya! Tazama yanayotokea Greece, Hispania, Italy na nchi kadhaa utajua mfumo huu umefeli! It is moribund! Will die soon.

Hata magwiji Uingereza wanasepa soko la pamoja kupitia brexit! Ufaransa mama Lapen anataka akipita naye asepe kupitia frexit! Uholanzi jamaa wa siasa kali anadai akipita tu anaanza na nexit! Meli inazama watu wanaruka! Mijinga yetu ndio kwanza wanadai tuwe mabepari zaidi na zaidi!
Nihitimishe kwa kusema Tanzania hakuna mfumo wa vyama vingi bali ni udanganyifu tu kuwa upo! Hata wanaodai ni waumini wa mfumo huo wao wenyewe ndani wanaendesha mfumo wa chama kimoja.
Pia nishauri wenye serikali wasione aibu kujifunza na kunakili waliofanikiwa kama China, Urusi, North Korea au Iran. Tusione haya kunakili mafanikio. Uzuzu ni kugangamala na mfumo uliotuletea maumivu utadhani sie ni kiazi ndani ya pilau inayoyokota! Tunaungulia ndani kwa ndani kwa faida ya nani?
Wasalaam,