Home Makala TANZANIA YA VIWANDA WATAALAMU HAWAMSAIDII JPM

TANZANIA YA VIWANDA WATAALAMU HAWAMSAIDII JPM

415
0
SHARE
Mojawapo ya kiwanda cha vinywaji nchini

NA NASHON KENNEDY,

TANGU aingie madarakani, tumemuona Rais John Magufuli akiwa na dhamira ya dhati ya kuanzisha viwanda ili kukuza uchumi wa nchi yetu, akisisitiza kuwa Tanzania ni kati ya nchi tajiri na kwamba hakuna sababu ya watu wake kuwa maskini.

Ni kutokana na dhamira yake hiyo, tumeona mambo kadhaa ambayo yanashabihiana na azma yake ya kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya viwanda yakifanyika kwa haraka na kwa ustadi mkubwa.

Kwanza, Rais ameimarisha kasi ya ukusanyaji wa mapato ya nchi, ambayo kwa sasa serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania inakusanya karibu trillioni moja kwa mwezi kutoka makusanyo ya awali ya Sh bilioni 900 kwa mwezi.

Hili ni jambo jema, maana kama Taifa hatuwezi kuanza safari ya viwanda, kama hatuna uwezo wa kukusanya kodi kutoka hasa kwa wafanyabiashara wakubwa watakaokuwa kuja kuwekeza, katika hilo kama hatayumbishwa, Rais ameliweza na naamini hawezi kuwekwa mfukoni!

Matumani ya wengi ni kwamba, ataendelea kudhibiti mapato kwa kukusanya kodi na kuacha kukimbizana na wafanyabiashara wadogo barabarani, kwa kuwamwagia wali na chai zao, kodi siku zote hata kwa nchi zilizoendelea duniani zinakusanywa kwa wafanyabiashara wakubwa na wenye uwezo ambao kimsingi ndio wanawezesha ukuaji wa uchumi.

Na hata katika mataifa hayo makubwa, wafanyabiashara wakubwa hutumia uzalendo wao na kudhibitiana wao kwa wao katika kukusanya kodi. Kwa kifupi wafanyabiashara hao huona fahari kulipa kodi!

Tofauti na hapa nchini, isipokuwa kwa Serikali ya awamu hii ya tano, huko nyuma baadhi ya wafanyabiashara wachache wa hapa nchini walikuwa wanaona ni fahari kukwepa kulipa kodi!

Pili Rais amefungua milango ya wawekezaji kuja kuwekeza hapa nchini kutoka nchi mbalimbali duniani akiwa na matamanio kwa kufanya hivyo itakuwa ni moja ya hatua ya kutekeleza azma ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Baadhi ya nchi hizo kati ya nyingi ambazo ni moja ya juhudi kubwa iliyofanywa na Rais Magufuli ni pamoja na nchi ya Uturuki. Kutokana na juhudi yake, Rais alimwalika Rais wa Jamhuri ya Uturuki, Recep Erdogan ambayo walijadiliana mambo ya msingi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.

Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na kutiliana mikataba tisa ya ushirikiano inayolenga kukuza uchumi wa nchi ili kuiwezesha nchi yetu kuingia kwenye Tanzania ya viwanda, ambapo hadi sasa tayari kampuni zaidi ya 30 kutoka Uturuki zimefanya uwekezaji nchini wenye dola za kimarekani milioni 305.08 ambazo zinatarajia kuteng’eneza ajira 2959.

Biashara kati ya Uturuki kwa mujibu wa takwimu, imeongezeka kutoka dola za Marekani milioni 66 hadi kufikia mwezi Februari mwaka jana, ikiwa ni sawa na Sh bilioni 145.2.

Rais amenunua ndege mbili za serikali ambazo zinaleta heshima kwa nchi kwa kuifanya nchi kuaminiwa na mataifa makubwa ya nje. Kwa wasiofahamu ni kuwa katika nyanja za kimataifa na kidiplomasia kama nchi haina ndege zake za Serikali au ndege binafsi ilizoingia nazo ubia kwa kupata gawio huleta mashaka kwa wawekezaji kutoka mataifa makubwa duniani kutoiamini nchi hiyo kwa nyanja za kiuchumi.

Yapo baadhi ya mataifa kwa hulka na mwenendo,  yanaheshimu na kuthamini baadhi ya vitu muhimu vya nchi ambavyo kwao  huamini kuwa ni utambulisho halisi wa nchi husika, ambavyo pia huwafanya watu hao kuamini kuwa uchumi wa nchi wanayokwenda kuwekeza uko imara ili kila mtu aweze kupata alichokitarajia.

Yote hayo ameyafanya Rais kwa azma ile ile ya kuipeleka Tanzania kwenye viwanda, lakini labda niseme watalaam wetu hawamsaidii mheshimiwa Rais katika kufikia azma hiyo ama bado wanahitaji kuelimishwa! Maana Rais hawezi kufanya kila kitu.

SAFARI YA VIWANDA NA MAGUFULI

Kama nilivyosema, tangu Rais atangaze azma yake hiyo, bado sijaona mipango madhubuti kutoka kwa watalaam wetu kutoka Wizara mama inayoonyesha kuitekeleza dhamira hiyo njema ya Rais ili kuiwezesha Tanzania kuwa ya viwanda.

Wizara mama ni Wizara ya Kilimo na Ushirika, Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Nishati na Madini ambazo kwa pamoja wizara hizi ndio ufunguo muhimu wa kuifanya nchi yetu kuwa ya viwanda kwa kutumia watalaam walio kwenye wizara hiyo.

Kwa mfano mpaka sasa kama Taifa, bado hatujaambiwa na watalaam, ni aina gani ya viwanda vitakavyoanzishwa au kufufuliwa ili viwe ndio dira ya nchi kuingia kwenye uchumi wa viwanda.

Tunachokiona na kukishuhudia kwa sasa ni maelezo ya jumla ya zima moto kuhusu kuelekea kwenye Tanzania ya viwanda kutoka kwa watalaam wetu karibu kila sekta, huku mkazo wa watalaam ukijikita katika kutenga na kubainisha maeneo ya watu kuja kuwekeza hapa nchini wakiamini watakuja kujenga viwanda.

Huwezi kuandaa eneo la ujenzi wa kiwanda kabla haujawa na uhakika wa malighafi zinazotumika kwenye viwanda ili ziweze kutoa ajira na kukuza uchumi.

Kuna aina nyingi za viwanda, kuna viwanda vya vipuri vinavyotokana na madini, kuna viwanda vinavyotokana na malighafi za mazao kama vile pamba vinavyozalisha nguo na vifaa tiba, lakini pia viwanda vinavyotokana na mazao ya mifugo, viwanda vya nyama na gundi.

Kwa mujibu wa takwimu, idadi ya viwanda hapa imeendelea kuongezeka kutoka viwanda 125 mwaka 1961 hadi kufikia viwanda 49,243 mwaka 2013. Aidha kati ya hivyo viwanda vikubwa vinavyoajiri kuanzia watu 100 ni 247, viwanda vya kati vinavyoajiri kati ya watu 50 na 99 ni 170 na vinavyoajiri kati ya watu watano na 49 ni viwanda 6,907 na vile vinavyoajiri chini ya watu watano ni 41, 919.

Kwa mujibu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, kati ya viwanda 106 vilivyofanyiwa utafiti kwa mwaka jana, viwanda 45 vinafanya kazi vizuri, viwili vinafanya kazi kwa kusuasua na viwanda 37 vimefungwa.

Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Charles Mwijage alikaririwa bungeni mjini Dodoma mwaka jana alisema kuwa mpango wa wizara ni kuhakikisha kuwa viwanda 35 vilivyobakia vitafanyiwa tathmini na kwamba hadi mwezi Julai, 2016 hatima ya viwanda ambavyo vilikuwa havifanyi kazi ingekuwa imejulikana, hadi naandika makala hii taarifa hiyo ilikuwa bado ni mbichi.

Tunapozungumzia ujenzi wa kiwanda kipya, kwanza tunazungumzia kwanza uwepo wa malighafi zinazosababisha kujengwa kwa kiwanda. Ndio maana baadhi ya wawekezaji wanapokuja hapa nchini kwa ajili ya kuwekeza wanachokifanya kwanza hujikita katika kutafuta malighafi zitakazowafanya wawekeze.

Sisi watalaam wetu kutoka wizara mama hizo nilizozitaja ambazo kimsingi katika kuelekea Tanzania ya viwanda zinategemeana bado hatujaona mpango yao ya kufanya tafiti za kubaini malighafi zitakazotuwezesha kuwa na viwanda.

Mikutano mingi inayofanyika kwenye halmashauri na sekretarieti za mikoa hapa nchini imejikita katika kubainisha  maeneo ya uwekezaji (viwanda) bila ya kufanya tafiti za kugundua ni wapi kuna madini yanayofaa kutumika kwa ajili ya ujenzi wa  kujengwa viwanda au mipango ya kuboresha kilimo chenye tija kitachozalisha malighafi za ubora kwa ajili ya kiwanda cha mazao ya aina hiyo.

Kibaya zaidi tumeruhusu wawekezaji wanaotoka nje ya nchi kufanya tafiti kwenye maeneo wanayotaka kuja kuwekeza. Unapomruhusu mtu kutoka nje akafanya tafiti zake mwenyewe kwa ajili ya kuwekeza bila shaka baada ya tafiti atafanya uwekezaji unaoendana na matakwa yake sio matakwa ya nchi husika.

Hili nalo la utafiti watalaamu wetu hawalioni wanasubiri Rais alisemee au afanye utafiti yeye ili agundue ni mambo gani muhimu yanayotakiwa katika kuanzisha viwanda.

Viwanda alivyoahidi kuvijenga Rais Magufuli wakati wa kampeni yake ni pamoja na kiwanda cha saruji Kigoma, cha kahawa-Bukoba, viwanda vya samaki vya mwambao wa Mtwara- Tanga ambavyo sina hakika kama mchakato wake au utafiti wake umeishaanza.

Lazima kama Taifa tuchukue fursa ya kufanya tafiti hizi hasa kwa uwekezaji muhimu wa viwanda badala ya kuwaacha wageni wanakuja wanafanya tafiti na kutuvua nguo, na katika hili namshukuru Rais Magufuli kwa kuteua timu tatu za wasomi wazalendo kufanya uchunguzi wa mchanga wa dhahabu ili kujua kama taifa tunapata hasara kiasi gani.

Tukifanya utafiti kwa mfano wa madini ya chuma, shaba, alminium na madini mengine tutajua mahitaji yetu kwa mwekezaji atakayekuja kuwekeza kwa ajili ya kujenga kiwanda cha chuma.

Sisi mbali na kuingia mkataba naye, tutampatia taarifa muhimu kuhusu kile anachotarajia kuwekeza na sio wao  wafanye halafu tuingie nao kwenye mazungumzo, haiwezekani!

Ni vigumu kumtoa mtu ambaye tayari ameishaingia chumbani kwako kumleta sebuleni ni lazima atatafuta namna ya kujihami ili aendelee kufaini ya chumbani!  Kwa viwanda vinavyotumia malighafi za kilimo na mifugo, lazima napo tufanye tafiti za kutosha ili tuwe na taarifa sahihi kwa watu wanaotaka kujenga viwanda au kuwekeza katika eneo hilo, je tuna mifugo ya kutosha katika kuanzisha kiwanda cha aina hiyo? Je, kilimo chetu kina tija, mazao tunayozalisha yana ubora na yanakidhi mahitaji ya kuanzisha viwanda husika?

Kwa mfano, katika msimu wa kilimo wa mwaka 2015/16 licha ya nchi kuzalisha tani 12, 946,103, tani 8,190, 573 zikiwa za nafaka na tani 4, 755, 530 zikiwa ni za mazao yasiyo ya nafaka na kuwa na ziada ya tani 2, 582, 717 za chakula, bado kilimo chetu kinakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za kutegemea mvua za msimu na kusababisha nchi kutofikia malengo iliyojiwekea ya uzalishaji wa mazao ya kilimo na biashara.

Tanzania yenye km. za mraba 945, 203.  Mchanganuo wa matumizi yake ya ardhi katika kilomita ni , km Milioni 22 zimetengwa kwa ajili ya hifadhi, hekta milioni 4.2 kwa ajili ya hifadhi za taifa, hekta milioni 7.7 kwa ajili ya hifadhi za wanyama, na hekta milioni 10.1 zimetengwa kwa ajili ya uhifadhi wa mistu, lakini ni hekta milioni 5.1 tu zilizotengwa kwa ajili ya kilimo na ufugaji sawa na asilimia 5 ya eneo lote la nchi.

Idadi ya watanzania wanaojihusisha na shughuli za ufugaji kwa mujibu wa Sensa ya 2012  ni asilimia 80 ya watanzania wote sawa na milioni 44, ambapo watu wanaojihusisha na  kilimo ni milioni 15.

Idadi ya mifugo iliyopo nchini kwa sasa ni ng’ombe milioni 23, mbuzi milioni 15.6, kondoo milioni 7 na ina kuku wa asili milioni 35.5, kuku wa kisasa milioni 24.5 na nguruwe milioni 5. Kwa takwimu hizo tukianzisha viwanda makini, malighafi hizo zitatosheleza?

Je, tuna mipango ya kuanzisha ufugaji wa kisasa kwa ngombe  wa nyama na maziwa na  tukatosheleza mahitaji ya nchi na idadi ya watu tuliyo nayo na kuuza nje ya nchi?  Je eneo la uwekezaji wa viwanda na kilimo  kwa takwimu hizo utakidhi mahitaji yetu ya kuwa nchi ya viwanda? Hii siyo kazi ya Rais ya kujibu hoja hizi ni kazi ya watalaam wetu kufanya tathimini ya kina juu ya jambo hili.

Watalaam wetu wakiyajibu maswali haya watakuwa wametengeneza dira ya kuelekea Tanzania ya viwanda na niwaombe sasa watalaam wetu kutoka Wizara mama hizo nilizozitaja wawe wachachamuzi ili tufikie azma hiyo ya Rais ya kuifanya nchi kuwa ya viwanda

Ila ninachokiona kwa sasa bado hawajamsaidia Rais Magufuli kutimiza ndoto yake hiyo  kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda, hapa  haihitajiki  elimu ya Chuo Kikuu kubaini udhaifu wao huo.