Home Makala Kimataifa UTAWALA WA TRUMP NI KAMA WA BUSH

UTAWALA WA TRUMP NI KAMA WA BUSH

387
0
SHARE

NA HILAL K SUED,

Yapo matukio mengi nje ya mipaka yetu yanayofaa kufahamika kwani mengi huelezea namna baadhi ya mataifa machache yanayojifanya “mataifa teule” yanavyojitahidi kuyashawishi au hata kuyalazimisha mataifa mengine kufuata mwenendo au tabia ambazo wao wanaziona ni njema zinazotakiwa kufuatwa.

Wanafanya hivi wakati mataifa yao yanalea hali ya uchafu mkubwa – kama tukitaja hizo tabia wanazosisitiza kwa wengine.

Wiki iliyopita zilitimia siku 100 tangu Donald Trump aapishwe kuwa Rais wa 45 wa Marekani – na tayari dunia imekuwa katika hali ya kuvuta pumzi kwa hofu ya kutokea vita – wengine hata wanasema kuna uwezekano wa kutokea Vita ya tatu ya Dunia.

Hali hii inatokana na vita vya maneno baina ya taifa dogo la Korea ya Kaskazini linalodaiwa kumiliki zana kali za nyuklia kwa upande mmoja – na Marekani pamoja na washiriki wake wa mataifa ya magharibi kwa upande mwingine.

Wengi hawaelewi kwa nini Korea ya Kaskazini inajitutumua namna hiyo kijeshi. Kuna askari wa Marekani takriban 30,000 huko Korea ya Kusini kwa madai ya kuilinda nchi hiyo isivamiwe na Korea ya Kaskazini – askari ambao wako mpakani baina ya nchi hizo mbili za mashariki ya Asia.

Lakini pengine Trump anajua hatari ya kuicheza vibaya karata yake katika eneo hilo, ukilinganisha na mtangulizi wake kutoka chama chake (Republican) miaka 14 iliyopita – George W Bush.

Mapema 2009 wakati George W Bush anaondoka Ikulu ya nchi na hivyo kuondoka kutoka medani nzima ya dunia aliyokuwa akitamba nayo baada ya miaka minane tangu aukwae urais – aliushangaza ulimwengu alipokiri kwamba ile vita yake ya “kushtua na kupumbaza” (shock anda awe) dhidi ya Iraq ilikuwa ya kimakosa.

Ikumbukwe kwamba kiongozi huyo alipata urais kwa namna tofauti kabisa na watangulizi wake – kwa maamuzi ya 5-4 ya kura za majaji wa Mahakama Kuu (US Supreme Court) kutokana na sintofahamu kubwa iliyoibuka kuhusu matokeo ya kura ya uchaguzi wa mwaka 2000.

Lakini hivyo ndivyo alivyokiri bila aibu yoyote katika mahojiano na chaneli ya ABC, mwezi mmoja tu kabla ya mrithi wake, Barack Obama kuapishwa kuwa rais wa 44 wa nchi hiyo. Alianzisha vita dhidi ya saddam Hussein baada ya kuyapuuza maoni ya Umoja wa Mataifa na ya dunia nzima kwa kuzikubali ripoti za kintellijensia zisizokuwa sahihi – kwamba nchi hiyo ya Mashariki ya Kati ilikuwa inamiliki silaha za kimaangamizi.

Kwa maneno mengine alikumbatia tetesi tu kupeleka askari wake Iraq ambako kati yao zaidi ya 4,000 waliuawa pamoja na malaki ya Wairaq. Hata mtoto wa miaka 11 anaweza kusema sasa kwamba Bush hakustahili kuwa Rais wa Marekani – nchi tajiri yenye ushawishi mkubwa duniani.

Na alichoanzisha kule Iraq hadi leo kinaendelea, maelfu ya watu wanateketea katika vita ya wenyewe kwa wenyewe, pamoja na kusababisha kuibuka kwa makundi mengine ya kigaidi hususan lile la Kiisilamu la ISIS ambalo nalo limesababisha mauaji makubwa – si ndani ya Iraq pekee, lakini sehemu nyingine pia na linaendelea kufanya hivyo. Umwagaji damu ambao chimbuko lake ni hatua ya Bush kuivamia Iraq pia yanaendelea Yemen, Syria, Mali na Nigeria.

Na kwa sababu bado hazijaeleweka, Mahakama ya Kimataifa ya Kesi za Jinai (ICC) bado inaamini kwamba mikono ya rais Hassan Al-Bashir wa Sudan ndiyo imetapakaa damu nyingi za binadamu kuliko mikono ya Bush. Mahakama hiyo bado inamtaka kumtia mbaroni Al-Bashir lakini iko kimya kwa yule ambaye mwenyewe amekiri kusababisha vifo – Bush.

Lakini yote hayo yalianzia miaka 14 iliyopita, lakini sasa hivi, ugaidi, kwa tafsiri ya nchi za Magharibi bado unaitesa dunia na kuuangamiza ustaarabu wake ukitazama kilichowapata watu wa Iraq, Syria na Yemen.

Ni ushahidi tosha kwamba hakuna hapa duniani kitu kisichokuwa na tija katika kuendeleza uchumi wa nchi kama bunduki, na hakuna kitu kinachozuia maendeleo ya jamii kama fedha zinazogharamia vita. Vita ni adui mkubwa wa maendeleo ya nchi na ni kihunzi kikubwa cha ustaarabu.

Na hivi ndivyo dunia inavyoeanda – yaani kwa kurudi kinyumenyume katika karne za zamani. Lakini ni sehemu ya dunia ile masikini ndiyo inayorudi kinyumenyume, siyo ile tajiri, zikiwemo nchi zenye nguvu kubwa (superpowers), ambazo baadhi yao zimejiamulia kuwa polisi wa dunia. Zinaamua tawala zipi zing’olewe, na zipi zimiliki zana za nyuklia na zipi ambazo viongozi wao ndiyo wasimame kwenye vizimba vya Mhakama ya The Hague.

Lakini hata hayo mara nyingine huwa yanawarudia wenyewe. Mwaka 2011 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa – ambalo nchi za magharibi lina ushawishi mkubwa – liliweka amri kwa ndege za aliyekuwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi kutoruka juu ya anga za nchi hiyo – yaani “No Fly Zone.” Hatua hiyo ndiyo ulikuwa mwisho wa Gaddaffi kwani ilimfunga kwa nyuma mikono yake na kuitundika shingo yake kwenye kamba.

Sasa hivi nchi hiyo inatawaliwa na magenge ya watu wenye silaha na bila shaka wananchi wanajuta kwa nini walishrehekea kung’olewa kwa Gaddafi. Italia, Ufaransa na Ujerumani –  nchi za Umoja wa Ulaya (EU) ambazo ndizo ziliongoza mashambulizi ya anga dhidi ya Libya ambayo hatimaye yaliuondoa utawala wa Gaddafi baadaye ziligundua upumbavu wa walichokifanya. Kwa miaka kadha sasa zimekuwa zikilazimika kumeza mawimbi ya wakimbizi kutoka nchi hiyo wanaokimbia vita, pamoja na wengine kutoka Syria, Iraq, Yemen n.k.

Lakini pia kuna hili: Marekani nchi ambayo huwa inakuwa na kasi kwa tabia yake ya kuweka kwenye ‘orodha’ zake watu ambao huwaainisha kama magaidi katika nchi za nje, sasa hivi yenyewe inao ndani ya mipaka yake mamia, kama siyo maelfu ya “magaidi” wake ambao ni raia wake.

Lakini nchi hiyo huwa angalifu – hukwepa kuwaita hawa ‘magaidi’ kwani gaidi wa mwisho raia wa Marekani alihukumiwa na kunyongwa zaidi ya miongo miwili iliyopita. Huyo alikuwa Tim McVeigh aliyelipua jengo la serikali katika mji wa Oklahoma City mwaka 1995 na kuua watu 168 na kujeruhi wengine 600.

Alihukumiwa kunyongwa, na kitanzi kilimkuta Juni 11 2001 katika gereza la Terre Haute, Jimbo la Indiana, miezi mitatu kamili kabla ya kulipuliwa kwa jengo la Twin Towers jijini New York na magaidi waliodaiwa kutoka kikundi cha Al-Qaeda.

Lakini ‘magaidi’ wa ndani ya Marekani bado wanaitesa nchi hiyo. Hawa huvamia shule, vyuo vikuu na sehemu za maduka (malls) wakiwamiminia wahanga wao risasi – hakuna tofauti na wale wa kikundi cha Al-Shabab walivyofanya katika jengo la maduka la Westgate mjini Nairobi mwaka 2013 huku wakielezea sababu zao za kufanya hivyo kupitia mitandao ya jamii.

Mara kadha mamlaka za nchi hiyo huwaanisha ‘magaidi’ kama ni watu punguani wa akili, au wanasumbuliwa na maradhi haya au yale. Lakini ukweli ni kwamba wengi ni magaidi tu wa ndani ya nchi hiyo. Kwa jumla wamesababisha vifo vingi kuliko wale wa September 11.

Chukulia mfano wa mauaji ya watu tisa wa asili ya Afrika takriban miaka miwili iliyopita ndani ya kanisa moja katika mji wa Chareston, Jimbo la South Carolina.

Muuaji Dylan Roof Storm, mwenye asili ya Kizungu aliingia kanisani na kuwamiminia risasi waumini waliokuwamo wakifanya ibada. Hata hivyo mamlaka za nchi hiyo ziliwia vigumu kumuainisha mtu huyo kama gaidi – watu walisema wangelifanya hivyo kama jina lake lingelikuwa Abdul Al-Muttajib.

Lakini tukio hili ni moja tu miongoni mwa mengi nchini humo yanayotokana na chuki zinazohusishwa na ubaguzi wa rangi na dini. Matukio kama haya yamesababisha vifo vya maafisa wa polisi, viongozi wa dini na makundi ya jamii nyingine ndogo ndogo (minorities).

Inaelezwa kwamba magaidi ambao siyo Waisilamu wamehusika na matukio 21 ya kigaidi nchini Marekani tangu September 11, kutokana na takwimu rasmi za FBI. Kwa ulinganisho, katika kipindi hicho magaidi wa Kiisilamu wamehusika na matukio tisa tu ya kigaidi.