Home Makala WATANZANIA WENGI TUMEPITA SHULE BILA KUELIMIKA (3)

WATANZANIA WENGI TUMEPITA SHULE BILA KUELIMIKA (3)

250
0
SHARE
Wanafunzi wakiwa darasani

NA GERARD M. CHUCHUBA,

Makala mbili zilizoitangulia hii, zimefafanua kwa kiasi kikubwa na kuonesha kuwa Watanzania wengi tumepitia shule bila kuelimika. Hii haijalishi ni msomi yupi wa Biblia au mwingine awaye msomi wa vyote.

Kwa leo nataka niwatoe katika kundi hili la hao wanaojiita ‘Mawakili’ na hata sisi tunawaita hivyo. Mawakili wamesoma kwelikweli, kila mmoja kwa kiwango chake.

Wakili anayewasaidia wateja wake wengi kushinda kesi, anakuwa maarufu kweli kweli. Na mhalifu hawezi kuishinda kesi bila kumweleza wakili mazingira ya kesi na ukweli wote kulihusu kosa lake liwe ni la jinai au madai.

Mawakili wamesoma, wamehitimu na nadhani wanafanya marejeo ya mara kwa mara ya tawi la falsafa liitwalo ‘Sophism’ – False reasoning intended to deceive. (Advanced learner’s Dictionary of current English by A.S. Hornby, kwa tafsiri yangu, mjadala wa kupotosha kwa lengo la kudanganya au kuhadaa. Anayefanya hivyo Waingereza wanamwita ‘Sophist’, mtu anayetumia hoja za ujanja kwa lengo la kupotosha ukweli.

Wakili akishakuyaelewa mazingira na jinsi kosa lilivyofanyika, atazungusha maneno mahakamani kwa lengo la kumpotosha hakimu na pia wakili wa mhalifu kwa lengo la kumtoa mteja wake au kumshawishi hakimu ampunguzie adhabu. Hili linathibitishwa  na malalamiko ya wengi kwamba wengi wa wafungwa si wahalifu bali ni watu walioshindwa kujieleza, wala si kujitetea mbele ya mahakama.

Kwa lugha nyingine, mawakili hutafuta kitu kiitwacho…’loop – hole in the law’ sheria nyingi nazo zinaachiwa kipenyo cha kumtolea mhalifu. Kinaachwa ama kwa makusudi au kwa uzembe wa hao wanaoitwa ‘Legal draftsmen’. Wataalamu wa kuandaa miswaada ya sheria.

Miswaada nayo ikifika bungeni, kwa sababu kuu tatu hupitishwa ikiwa na vipenyo hivyo vya kuwatoa wahalifu bila kuadhibiwa kulingana na makosa yao.

Wabunge hupitisha miswada kwa kutozingatia wajibu kutokana na uchovu utokanao na kutopumzika ipasavyo usiku kwa sababu kadha wa kadha.

Pili kwa kutafuta umaarufu wa Mbunge binafsi na chama chake badala ya manufaa ya umma. Tatu kwa tatizo kuu la kupitia shuleni na kutoka bila kitu kichwani.

Ukiona kuwa hapa mwandishi ninabwabwaja tu, utuambie ilikuwaje mahakimu 28 wafikishwe mahakamani kwa kosa la kula rushwa na wote waonekane hawana hatia?.

Kwa vipi likamuumiza Rais Magufuli wa Jamhuri ya Tanzania hivi sasa hata aseme kwa uchungu kulihusu hili hata akapendekeza kuwa ikiwezekana, hao wanaowatetea na kuwatoa wahalifu nao waunganishwe wote waende huko. Basi tukubaliane na usemi uliozoeleka kwamba mla rushwa anafungwa kwa kushindwa kula na watu? Na vivyo hivyo mwizi anafungwa kwa kutokula na watu au kwa kuiba kwa kiasi kidogo mno kisichowatosha wote?

Ni vizuri Watanzania tufahamu kwa kujua kuwa si kila king’aacho ni dhahabu na kinyume chake. Hawa wanaojiita na kuitwa watetezi wa haki za binadamu, wangekuwa hivyo ndivyo walivyo, wasingepuuza usemi huo kwamba wengi wa wafungwa hawana hatia. Kinyume chake tutawadhania kuwa wengi wao ni wasaka tonge maana mkono mtupu haurambwi.

Yawezekana wapo mawakili waaminifu wanaofanya kazi kwa kutetea haki kulingana na sheria kwamba anayestahili adhabu aadhibiwe na mwenye haki apewe haki yake na awe huru. Hawa nao watakwazwa na vipenyo vya makusudi vilivyoachwa na waandaa miswaada.

Nidokeze kwamba umekuwapo mtindo wa kusomea KAZI. Mtindo au utaratibu huu umeanza kufifia na polepole utatoweka.

Utaratibu huu wa kusomea kazi uliidumaza akili ya mwanachuo. Kazi zinasomewa vyuoni. Katika chuo kikuu cha kwanza Tanzania, Mlimani au Chuo Kikuu cha Dar es Saalam, mtu aliyekuwa anachukua Shahada ya kwanza waliyokuwa wakiita B.A. general, alikuwa anaonekana bwege tu. Huyu angeweza kuajiriwa kwa bahati bahati tu. Aliyesomea kazi alikuwa ana hakika ya ajira, awe ana Cheti, Diploma au Shahada ya kwanza.

Mtanzania aliyesomea kazi akishaipata, vitabu alivyovitumia anagawa au anavifungia sandukuni. Hana habari navyo tena ili mradi cheti kinaning’inia ukutani na akihama ni cha kwanza kufungashwa. Magazeti hasomi, vitabu vya riwaya au vinginevyo hasomi isipokuwa wachache tuliowaona wanajitia uzungu..

Wanaojua mambo wanatuambia: “Unaposema unajua kiasi cha kutosha na hivyo huhitaji kujifunza zaidi”, siku hiyo unaanza safari ya kuwa mjinga. Aidha, unavunja ukweli unaosemwa ‘revision is the mother of study’ marudio ndiyo mama wa kujifunza.

Tumekuwa wepesi sana kuiga uzungu bila hata kuchuja. Wazungu wanajifunza somo moja tu. Enzi hizo ukiwa Uingereza, ukasema unatoka Tanzania, baadhi ya Waingereza wajinga wangeweza kudakia ‘ile nchi karibu na Nigeria?’ mpaka uwaambie ile nchi ya Nyerere napo tena mmoja anadakiza, ‘Yule Rais wa Afrika’.

Pamoja na ujinga huo, wao ni wasomaji wazuri wa vitabu na magazeti. Mzungu akiwa stendi au stesheni anasubiri usafiri, huku anasoma. Akiwa maliwato, nako kuna vitabu na magazeti ya kusoma. Waingereza huko wakipaita ‘Resting room’ yaani chumba cha mapumziko.

Sisi tuliofundishwa ‘Uzuzu’ kwa maneno ya Jenerali Ulimwengu, tukihitimu chuo, vitabu vimekuwa mama au baba mkwe. Tusipobadilika, tutaendelea kutawaliwa kisiasa na kiuchumi pia.

Kama unapinga, basi na usemi,   ‘Information is power’ kumaanisha kuwa ujuzi ni nguvu. Asiye na nguvu hushindwa na akishindwa vitani, anakuwa mateka. Mateka hana haki, mtumwa ana nafuu!

Vijana someni kutafuta ujuzi, uwezo wa kuikabili dunia ya utandawazi na mshindane na mataifa mengine au vijana wa mataifa mengine kwa usawa.

Tafadhali zingatia.

0768462511