Home Makala CATHERINE RUGE: NITALITUMIA BUNGE KUTETEA HAKI ZA WANAWAKE

CATHERINE RUGE: NITALITUMIA BUNGE KUTETEA HAKI ZA WANAWAKE

277
0
SHARE

HARRIETH MANDARI

MAPEMA wiki iliyopita Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imemteua Catherine Ruge kuwa Mbunge wa Viti Maalumu katika Bunge la Jamhuri kwa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Elly Macha aliyefariki dunia Machi 31 mwaka huu.

Uteuzi wake ulifanyika katika kikao cha tume hiyo kilichofanyika Mei 4 mwaka huu jijini Dar es salaam kwa mujibu wa Ibara ya 78 (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa pamoja na kifungu cha 86 A (8) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343, Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

NEC ilichukua jukumu hilo la kumteua Catherine baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye kwa mujibu wa kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 aliitarifu Tume juu kuwepo kwa nafasi wazi ya Mbunge wa Viti Maalum Dk. Elly Macha.

Kutokana na hatu hiyo, RAI wiki hii lilifanikiwa kufanya mahojiano na mbunge huyo mpya wa viti maalumu ambapo pamoja na mambo mengine anasema yuko imara na atajitahidi kuwa mwakilishi mchapakazi wa wananchi.

Jina lake kamili ni Catherine Nyakao Ruge ni mwanamke Mtanzania aliyezaliwa wilayani Serengeti Mkoa wa Mara miaka 34 iliyopita. Akiwa ametoka kwenye familia ya kifugaji ambako elimu kwa mtoto wa kike si jambo linalotiliwa mkazo, Catherine aliweza kuvuka vikwazo hivyo na kufikia kiwango cha elimu aliyonayo sasa.

Kwa sasa Catherine ni mwanafunzi wa shahada ya uzamivu (Phd) akiwa ameegemea eneo la jinsia na utunzaji wa mahesabu. Hii ni baada ya kumaliza shahada ya uzamili katika Usimamizi wa Biashara (MBA) mwaka 2015 katika Chuo cha ESAMI iliyokuwa imetanguliwa na shahada ya kwanza ya biashara na uhasibu yaani (B.Com) Accounting aliyoipata Chuo kikuu cha Dar es salaam (UDSM) mwaka 2007. Pia Catherine ana cheti cha juu cha ukaguzi wa mahesabu (CPA) kilichotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Mahesabu Tanzania (NBAA)

Mwaka 2014, Catherine alianza rasmi harakati za kumkomboa mwanamke dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kama moja ya ndoto zake kubwa katika maisha. Catherine amekuwa akifanya harakati hizo kupitia asasi isiyo ya kiraia inayojulikana kama GESI (Girls Education Support Initiative) ambayo ina malengo ya kuwasaidia watoto wa kike walioko mashuleni kufikia malengo yao ya kielimu na ndoto zao za kimaisha.

Catherine ni miongoni mwa mabalozi wa dunia wa umoja wa mataifa katika kuwawezesha wanawake kufikia malengo yao ya kiuchumi (UN-Empower Women Champion) pia ni balozi wa kupinga ukeketaji kutoka wilaya ya Serengeti. Mwaka 2015 aliamua kuacha kazi za kuajiriwa ili aweze kutekeleza majukumu yake ya kutetea haki za wanawake na wasichana kwa uwanda mkubwa.

Pamoja na kuwa mwanaharakati kwenye masuala mbalimbali, Catherine ni mwanasiasa aliyeweza kujijengea jina katika uchaguzi wa mwaka 2015 ambapo alikuwa kwenye timu ya kampeni ya mkoa wa Mara na kanda nzima ya Serengeti wakati huo huo akiwa mgombea ubunge wa viti maalum kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Catherine pia anatumikia nafasi ya mweka hazina wa chama kanda ya Serengeti.

Pamoja na mambo mengine anaongeza kuwa ni mwanamke mchapakazi, msomi, mwanaharakati na mwanasiasa mwenye kiu ya kuona Taifa linasonga mbele kwa kuhakikisha anakuwa sehemu ya utunzi wa sera na sheria mbalimbali wezeshi hasa kwa wanawake ili kufikia dira ya maendeleo ya Taifa.

Katika muda wake wa ziada Catherine anapenda kusoma vitabu na kusafiri ili kuongeza uelewa na kujifunza mambo mbalimbali yatakayoweza kumjenga ili kufanya maamuzi sahihi katika yale anayoyaamini na kuyasimamia.

RAI: Ni nini kilikuvuta kuingia kwenye siasa?

CATHERINE: Bunge ndicho chombo kikuu cha kutunga sheria hapa nchini, hivyo niliona nikiwa ndani ya Bunge nitakuwa na uwezo wa kuchangia sera na sheria mbalimbali hususan zinazohusu wanawake na wasichana zitakazoweza kusaidia maendeleo ya nchi yetu.

RAI: Ni changamoto zipi ambazo umekumbana nazo kwenye siasa?

CATHERINE: Bado kuna mtazamo hasi juu ya wanawake na uwezo wao wa kuongoza, wananchi wengi hasa vijijini wanaamini wanaume wana uwezo zaidi wa kuongoza kuliko wanawake. Hii ni changamoto ambayo naamini wabunge wengi wanawake wamepitia au hata wale ambao hawakufanikiwa kushinda kuna uwezekana changamoto hii ikawa chanzo cha kushindwa kwao.

RAI: Utakapoanza kutumikia watanzania unategema kuwafanyia nini hasa wanawake vijana kama wewe?

CATHERINE: Nashukuru sasa nimeweza kupata jukwaa kubwa zaidi ili niweze kutumia weledi wangu kuchangia sheria mbalimbali zitakazokuwa na mlengo wa kuwainua vijana (hasa kwenye eneo la ajira), wanawake hasa kwenye sheria zinazokumbatia mila kandamizi kwa wanawake na wasichana. Pia nitapaza sauti yangu kuhakikisha mtoto wa kike anapata fursa ya kupata elimu ili aweze kujikwamua yeye na familia yake pamoja na Taifa zima kwa ujumla.

RAI: Unazungumziaje utendaji wa serikali hii ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli?

CATHERINE: Kuna maeneo ambayo naamini nia ni njema lakini utekelezaji hauko sawa. Kwa mfano eneo la uadilifu na matumizi mabaya ya mali ya umma, nia inaweza kuwa njema lakini utekelezaji wake umekuwa unaangalia sana sura za nani anaguswa na nani haguswi (Double Standard). Pia kuna maeneo ambayo nadhani mpaka sasa serikali ya awamu ya tano haijafanya vyema hasa eneo la demokrasia. Kumekuwa na kuminywa sana kwa demokrasia kwenye awamu hii kiasi cha kuogofya watu kuelezea hisia zao pale wanapokuwa hawakubaliani na jambo fulani.

Pia serikali awamu ya tano haijawapa nafasi ya kutosha wanawake hasa kwenye nafasi za uteuzi kulinganisha na awamu iliyopita

RAI: Wito wako ni nini kwa wanawake nchini hasa linapokuja suala la kuwa na uthubutu wanapotaka kufanya shughuli zozote za kimaendeleo hasa ukizingatia kuwa wanawake wengi bado tunakosa kujiamini?

CATHERINE: Natoa wito kwa wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, wale waliofanikiwa kupata nafasi maeneo mbalimbali kuwajengea uwezo wanawake wenzao ili kuwafanya wawe na hamasa ya kufikia malengo yao. Wanawake ni lazima tufanye vyema kwenye shughuli zetu tunazozifanya na kwa wale walioko mashuleni basi wasome kwa bidii. Hii ndio njia pekee itakayofanya tuheshimike, kuaminiwa na jamii nzima. Lazima tuwe na uthubutu.

RAI: Ukiwa umepumzika unapenda kufanya nini?

CATHERINE: Napenda kusoma vitabu na kusafiri ili kuongeza uelewa na kujifunza mambo mbalimbali yatakayoweza kunijenga ili kufanya maamuzi sahihi katika yale anayoyaamini na kuyasimamia.