Home Makala HUZUNI YETU IKAGUE BARABARA ZETU

HUZUNI YETU IKAGUE BARABARA ZETU

180
0
SHARE

NA MARKUS MPANGALA,

Taifa limekumbwa na huzuni kubwa kutokana na ajali mbaya ya Toyota Coaster iliyosababisha vifo vya wanafunzi 32 wa Shule ya Msingi ya Luck Vincent iliyopo wilayani Karatu mkoani Arusha.

Ajali hii imechukua maisha ya watoto ambao walikuwa na ndoto mbalimbali maishani mwao. Ajali hiyo imeushtua ulimwengu, kuanzia Xinhua ya China, hadi The Guardian ya Uingereza, na AFP na AP huko ughaibuni.

Ni ajali ambayo imesababisha matatizo makubwa kama ilivyowahi kutokea ajali za Mv Bukoba, Mv Spice Islanders, City Boys, Newforce na kadhalika. Kifupi nchi yetu imezingirwa na ajali za kizembe, kishenzi, ujinga, upuuzi na yale ambayo tunaweza kusema mapenzi ya mwenyezi Mungu.

Katika ajali hii ya Karatu, nina hakika tumepoteza wahandisi, matabibu, wauguzi, walimu, wavumbuzi, wakutubi, waandishi, wakulima, wafanyabiashara, wahunzi, wavuvi na kadhalika, ambao wangekuja kulitumikia taifa miaka ijayo. Ni huzuni mno.

Suala la usalama wa raia wetu ni pamoja na kuhakikisha mazingira wanayotumia kwa safari au vyombo vinavyotumiwa ni salama wakati wowote.

Tunaungana na watanzania wenzetu. Tunasikitika pamoja. Tunalia pamoja. Tunaungana na wanafamilia katika janga hili baya. Tunajua tumepoteza wapendwa wetu, ndugu zetu, watoto wetu na wataalamu wa fani mbalimbali wa miaka ijayo katika taifa letu. Kwa jina la baba, mama, na roho mtakatifu! Amina.

Baada ya kusema hayo sasa tugeukia upande wa pili wa mazingira yetu ya usafiri barabarani. Tunajua kuwa katika Mabasi yetu tunayotumia kusafiria yamekuwa na kero kadhaa. Tumeshuhudia namna madereva wanavyojaza abiria huku abiria mwenyewe asijali usalama wake kwani anakuwa sehemu ya kero.

Abiria tumekuwa tukitumiwa vibaya kwenye mabasi ya mikoani. Tumeshuhudia maasi mengi lakini siku zote tunasema kuwa yanapotokea maafa ni mapenzi ya Mungu.

Sisi kama abiria hatupaswi kutumika kwa kuhamishwa siti za nyuma ili tuchuchumae katikati Basi kupunguza uzito wa gari husika.

Sisi abiria hatutakiwi kuwa chanzo cha maovu yanayotokea kwenye ajali mbalimbali hapa nchini. Abiria makini anatambua kuwa endapo Basi limejaa kiasi kwamba hawezi kupata nafasi ya kukaa (sio kukaa kwenye korido) anatakiwa kutafuta usafiri mwingine.

Tunafahamu kuwa sisi abiria ni wateja na watu muhimu kwenye biashara ya usafirishaji. Tunatakiwa kutambua haki zetu ni pamoja na kujilinda dhidi ya dalili au mwelekeo wowote wa kuhatarisha usalama wetu.

Tangu nilipojitokeza kwenye tasnia ya habari miaka 7 iliyopita nimekuwa nikipigia sana kelele suala la barabara zetu. Aghalabu nimesema kuwa barabara ya Morogoro ni nyembamba mno na haitoshi mahitaji ya usafirishaji.

Katika kipindi chote nimesema nikiwa na ushahidi wa kutosha (licha ya kwamba mimi si mhandisi wa barabara). Ninasema kuwa barabara hii kabla ya uamuzi wa kupanuliwa bado ni nyembamba mno, haotoi fursa ya kutosha kujilinda dhidi ya ajali.

Aidha, tumekuwa na madereva ambao wanalelewa na wamiliki wao pamoja na serikali, kwakuwa ni ndugu,washkaji,binamu,kaka, dada,mjomba, shangazi, na kadhalika. Ujinga mtupu!

Kuwahisha abiria katika mkoa mwingine ni jambo muhimu. Lakini kuhakikisha wanawahishwa mwisho safari katika mazingira salama ni jambo bora zaidi maishani mwetu.

Ni sababu hiyo mara baada ya kuzinduliwa barabara ya inayounganisha safari za kwenda Songea kuanzia Dar es salaam kupitia Lindi-Masasi (Mtwara) kwenda Ruvuma sijawahi kukanyaga tena barabara ya Morogoro-Iringa-Njombe hadi Songea.

Ninaifahamu barabara ya kutoka Dar es salaam kwenda Songea kupitia Morogoro-Iringa na Njombe. Ni barabara iliyo na mrundikano wa magari, barabara nyembamba, ajali zisizo na kikomo, usimamizi mbovu wa Askari wa barabarani, na ulaji rushwa mkongwe umechangia uamuzi huo.

Mimi si muumini wa kusema ajali zetu ni mapenzi ya Mungu, ingawaje sikatai nafasi ya Mungu katika maisha yetu. Lakini kwa hali ilivyo barabara zingine zinatokana na matatizo yetu tunayojitakia.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano mkuu wa baraza la Taifa la usalama barabarani uliofanyika mkoani Dodoma, Agosti 14, 2009 aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema, “Takwimu za Ajali Barabarani: Ndugu Wajumbe, Suala la Ajali Barabarani ni suala ambalo ni kero na lenye athari kubwa kiuchumi na kijamii. Takwimu zinaonyesha kuwa kwa mwaka 2007 kulikuwa na Ajali 18,894 ambapo katika ajali hizo Watu 2,586 walipoteza maisha na Watu 16,308 walijeruhiwa. Idadi hiyo ya ajali ni sawa na wastani wa Ajali 52 kwa siku au Ajali 1,583 kwa mwezi,”

“Kwa mwaka 2008 kulikuwa na Ajali za Barabarani 20,148. Ajali hizo zilisababisha jumla ya Vifo 2,924 na kujeruhi wengine 17,825. Idadi hii kwa mwaka 2008 ni wastani wa Ajali 55 kwa siku au Ajali 1,679 kwa mwezi. Takwimu za kipindi cha Januari hadi Juni 2009 zinaonyesha kuwa jumla ya Watu 1,460 walifariki na wengine wengi kujeruhiwa. Idadi hii ni kubwa mno, lakini cha kusikitisha zaidi hizi ni ajali na vifo ambavyo vingeweza kuepukika kama Madereva, Abiria, Watembea kwa Miguu na Askari wa Usalama Barabarani wangetimiza wajibu wao ipasavyo,”

Waziri Mkuu Mizengo Pinda alimaliza kwa sentesi hii, “vifo ambavyo vingeweza kuepukika kama watembea kwa miguu na askari wa usalama barabarani wangetimiza wajibu wao ipasavyo,”.

Ni jawabu kwamba serikali inafahamu upuuzi mwingine unaofanywa na askari wa barabarani na madereva. Wananchi wanafahamu upuuzi mwingine vilevile. Sisi ni jamii ambayo yenyewe ni kero kwanza kabla ya kero husika.

Kuanzia mwaka 2009 hadi leo kuna ajali ngapi zimetokea? Huwa tunajifunza chochote? Hatua gani zimechukuliwa? Je magari yaliyoko barabarani ni mazima? Ni mara ngapi umeshuhudia Breakdown mbovu zinakokota magari mabovu?

Ni mara ngapi tumeshuhudi madereva wanazungumza na abiria ili kumzidi ujanja askari wa barabarani? Ni mara ngapi tumeona makorongo katikati ya barabara za lami?

Ndugu zangu, usalama wetu uko mikononi mwetu kwanza kabla ya kuvidai vyombo vya usalama vituhakikishie usalama. Ubovu wa vyombo vya usalama si kigezo cha wewe kuacha kujilinda.

Ni wakati ambao tunatakiwa kuzitazama barabara zetu mitaani na kujiuliza je zinaturidhisha? Je tunaposhirikiana na dereva kumzidi maarifa askari inatusaidiaje kuepuka ajali? Tunapowaona askari wanavuruga ama kupindisha sheria tunachukua hatua gani? Tukilea upuuzi tusilalamikie matokeo ya kipuuzi yanapofanywa na wapuuzi.

Niandikie; mawazoni15@gmail.com