Home Habari kuu MEYA WA JIJI AKIRI MAKOSA, NI BAADA YA KAULI YA JPM

MEYA WA JIJI AKIRI MAKOSA, NI BAADA YA KAULI YA JPM

949
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI,

MEYA wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita amekiri kuwapo kwa makosa katika  kutangaza zabuni ya ukusanyaji ushuru wa maegesho ya magari jijini humo. RAI linaripoti.

Kauli hiyo ya Meya wa jiji la Dar es Salaam, imekuja baada ya Rais Dk. John Magufuli kuonekana kutofurahishwa na hatua ya Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, kutoa zabuni hiyo kwa kampuni ya Kenya Airport Parking Service (KAPS) ya nchini Kenya.

Akiwa mkoani Kilimanjaro katika ziara ya kikazi ya siku tatu, iliyoanza Aprili 29 hadi Mei Mosi, pamoja na mambo mengine Rais alioneshwa kukerwa na zabuni zenye harufu ya ufisadi pamoja na zile ambazo zinaweza kufanywa na wazawa, lakini zimegaiwa wageni na kudai kitendo hicho ni sawa na uroho wa pesa usiojali masilahi ya Watanzania.

“Kitendo cha kuweka makampuni ya nje kukusanya fedha za parking ni uroho wa pesa usiojali utu na masilahi ya Watanzania,” alisema.

Alikwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa kampuni hizo za nje zimekuwa haziheshimu wakubwa na nafasi za watu kwani hata Masheikhi na Wachungaji wamekuwa wakifungiwa magari yao.

Msingi wa kauli hizo za Rais Magufuli ulikuwa ni kampuni zabuni iliyopewa kampuni ya ukusanyaji wa ushuru wa maegesho ya magari katika mji wa Moshi, ambao alionesha shaka na zabuni hiyo hali iliyomsukuma kuiagiza Tume ya kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi.

“Hizi Parking System wanajisahau, wanashindwa kuheshimu watu wa umri mkubwa, utakuta hata sheikh au mchungaji au mzee anasimama kidogo wanakuja kufunga gari yake bila kuwa na utaratibu, huo ni ushetani, wanashindwa kuheshimu utu wa Watanzania,” alisema.

Akitoa ufafanuzi wa zabuni ya jiji la Dar es Salaam, Meya Mwita alisema hakukuwa na aina yoyote ya rushwa kwenye zabuni yao, badala yake anachokiona yeye makosa waliyoyafanya ni kutoa mkataba kwa wageni.

“Hatujaingia mikataba ya kibadhirifu, nimemsikia  Rais anasema tumewapa wageni jambo ambalo ni kweli tumelifanya, sisi tunachoangalia ni kukusanya fedha, suala la ubadhirifu halipo kwetu, bali linawahusu wenzetu wa Moshi.”

KWANINI KAPS?

Akitoa ufafanuzi wa uamuzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kutoa zabuni kwa kampuni ya KAPS, Mwita alisema, kilichosababisha kuwapo kwa kampuni hiyo ni hatua yao ya kutangaza zabuni iliyofungua milango kwa wageni pia.

“Tatizo lililotukumba sisi ni kuwapa wageni mkataba, bahati mbaya huko nyuma tulitangaza ‘international tender’,(zabuni za kimataifa). Ukweli ni kwamba hatufungwi na sheria ya zabuni, lakini pengine tulipaswa kuzipa kipaumbele kampuni za ndani, tulifanya hivyo tukijua kwamba huenda tungeongeza mapato na kweli tumeongeza mapato.”

Alisema katika zabuni waliyotangaza, kampuni nyingi za ndani na nje zilijitokeza, lakini KAPS ndio walionesha kuwa na sifa walizozihitaji, ambazo ni kuongeza makusanyo kwa siku, wiki, mwezi na hata mwaka.

Alisema, awali kampuni ya National Parking Solutions (NPS)  iliyokuwa ikiongozwa na Watanzania ilikuwa ikikusanya kiasi cha Sh. 100 milioni kwa mwezi, hali iliyokuwa ikisababisha kila wilaya kupata mgawo wa sh. 17 milioni.

Alisema KAPS iliahidi kukusanya fedha zaidi, ahadi ambayo wameitekeleza kwani sasa wanakusanya  Sh. 827 milioni kwa mwezi ikiwa ni mara nane zaidi ya ile ya NPS.

Mwita, alieleza kuwa fedha hizo si kidogo kwani inawapa jeuri ya kugawa kiasi cha zaidi ya Sh. 100 milioni kwa mwezi kwa kila wilaya ya mkoa wa Dar es Salaam.

“Fedha tulizopata tumewasaidia  halmashauri, kwa mfano kila mwaka tunagawa kwa kila Halmashauri kiasi cha Sh 1.5  bilioni  kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kujenga barabara na shule. Makusanyo yakiongezeka tutaendeleza miradi. Ukusanyaji wa pesa ukiwa mzuri tutaongezea zaidi kwa halmashauri na kusaidia kutoa mikopo.

Alisema vigezo walivyotumia kuipa zabuni kampuni hiyo ya KAPS ndio vigezo vinavyotumiwa na bodi ya zabuni nchini, kwa kuangalia urahisi wa makato yao, ukubwa wa mapato na utendaji kazi sahihi.

KUTEKELEZA AGIZO LA RAIS

Mwita alisema  kwakuwa lengo lao la awali lilikuwa ni kutaka kuona mapato  katika makusanyo yanaongezeka, wameshaanza kuchukua hatua za awali za kuandaa zabuni mpya itakayowapa kipaumbele wazawa.

“Katika kuzingatia kauli ya Rais ambayo ni sawa na agizo, tayari hatua za awali zimeshaanza kuchukuliwa, tupo kwenye mchakato wa kuandaa zabuni mpya, mkataba wa ukusanyaji ushuru wa maegesho ni wa kila mwaka.

“Kwa kuwa tunaelekea mwishoni mwa mwaka, nitumie fursa hii kualika Watanzania wale ambao wanahamu ya kuendesha shughuli hizi waje wafanye kazi, ila pia wajifunze kupitia KAPS kwani tumeshaona makusanyo yalivyo, mfano huyu mzabuni mmoja tu anakusanya zaidi ya Sh milioni 600. Hatutegemei kuambiwa kampuni imekusanya milioni 200 au 300.

“Tukitangaza hii zabuni Watanzania watapewa kipaumbele, tumekuwa tukitangaza zabuni mwezi Julai na kutoa mkataba Septemba, hii inamaanisha tuko mbioni kutangza zabuni, tujiandae,” alisema.

Alisema kwa sasa bado jiji lipo kwenye kutafuta vyanzo sahihi vya kukusanya fedha na tayari mwanga umeonekana na Halmashauri zimeanza kufaidika.

MALALAMIKO

Kutokana na kuwapo kwa malalamiko kutoka kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam, juu ya ongezeko la ushuru wa maegesho kutoka Sh. 300 hadi 500 na ubabe unaofanywa na wakusanyaji hao.

Meya Mwita alisema malalamiko hayo wameyapokea na wanaanza kuyafanyia kazi.

“Tumeona, tumeshaanza kufanyia mapitio sheria ndogo ndogo, kwa sababu maisha yamekuwa magumu, kwa siku Sh 5000 kwa saa 10 kweli ni gharama tunaangalia namna gani ya kupunguza, hii sheria ilitungwa mwaka 2014 tumeirudisha kwenye baraza ili hizo tozo zipunguzwe,” alisema.

Alisema jiji liliamua kuipa KAPS zabuni ya kukusanya ushuru huo kwa kuwa sheria haizuii jiji kugawa tenda kwa kampuni za nje.

“Lakini tumeshapata kitu cha kujifunza, hivyo tumeona kiasi gani alikuwa anakusanya,” alisema Mwita.

Kampuni ya KAPS inakusanya ushuru ndani ya Halmashauri ya Ilala, ambako kunatajwa kuwa kitovu cha biashara na shughuli nyingi za maisha ya kila siku za wakazi wa jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza na RAI, Naibu Meya wa Ilala, Omary Kumbilamoto, alionekana kutoridhishwa na kiwango cha Sh. 500 kinachokusanywa na kampuni hiyo ya KAPS.

Kumbilamoto ambaye pia ni Diwani wa kata ya Vingunguti (CUF) alisema hivi sasa asilimia kubwa ya wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kariakoo huegesha magari yao katika uwanja wa Shule ya Benjamini Mkapa ambako hutozwa Sh. 3000 badala ya 5000 wanazotozwa kwenye maegesho ya barabara za jiji kwa saa 10.

“Kweli mradi huu unaliletea jiji pesa,  ila wananchi wa kawaida wanaumia, ni bora wasingeingia ule mkataba. Hakuna mtu mwenye uwezo wa kulipa 5,000 kila siku, si watu wote wenye uwezo ,” alisema.

Alisema suala hilo wameshindwa kulitatua ndani ya Baraza la madiwani kwa kuwa hakuna mtu yeyote mwenye majibu nalo.

“Hatuwezi kuzungumzia kwa sababu hakuna mwenye majibu, bahati mbaya mimi si mjumbe kwenye vikao vya jiji, ningeingia lazima ningehakikisha suala hili linajadiliwa. Hili suala linasikitisha,” alisema.

Mapema Novemba mwaka jana uongozi wa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam ulitangaza kampuni tatu zilizoshinda zabuni za ukusanyaji ushuru wa maegesho katika Halmashauri zake.

Naibu Meya wa Jiji hilo, Mussa Kafana alizitaja kampuni zilizoshinda zabuni hiyo kuwa ni, Kenya Airport Parking Services iliyokabidhiwa kazi ya kukusanya ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Ubapa ilipewa Manispaa ya Kinondoni na  Temeke ilishinda kampuni ya Upauka.