Home Habari MGOGORO WA CUF, MUTUNGI ASITOLEWE KAFARA!

MGOGORO WA CUF, MUTUNGI ASITOLEWE KAFARA!

351
0
SHARE

NA NASHON KENNEDY,

HIVI karibuni jijini Dar es Salaam kulitokea vurugu zilizohusisha makundi mawili ya Chama cha Wananchi- CUF zilizosababisha baadhi ya wanachama wa chama hicho pamoja na  wandishi wa habari kujeruhiwa.

Tukio hilo sio tu lilileta taharuki hapa nchini, bali pia liliitia doa nchi yetu mbele ya Jumuiya ya kimataifa kutokana na ukweli kuwa nchi yetu mbali na kuridhia baadhi ya mikataba mbalimbali ya kimataifa ihusuyo haki za binadamu, iliafiki na kuingia rasmi kwenye mfumo wa vyama vingi kisheria mwaka 1992.

Kwa watu wenye busara na hekima, siasa za aina hiyo tuliyoishuhudia kama nchi siyo za kujivunia hata kidogo, ni siasa za kihuni ambazo hazina mashiko katika nchi kama yetu licha ya ukweli wa dhana iliyozoeleka kuwa siasa inahusisha pia maisha ya jamii.

Kwa chama kikongwe cha Siasa, kilichoshiriki katika kuleta demokrasia hapa nchini, kinachoongozwa na viongozi wenye weledi wa kitaaluma na kisiasa, niseme wazi vurugu hizo sio stahili yake, ni vurugu zinazolenga kuua demokrasia hapa nchini.

HALI ILIVYO SASA

Kimsingi vurugu hizo ni za  muda sasa,  baina ya makundi mawili ya wanachama yanayoongozwa na viongozi wa CUF. Mwenyekiti wa CUF Prof Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.

 Chokochoko za vurugu  hizo zilianzia kwa Maalim Seif mwaka jana jijini Dar es Salaam, pale alipotoa tuhuma nzito kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi na Jeshi la Polisi kuwa wamekuwa wakishirikiana kwa ajili ya kukihujumu CUF.

“Kama mnavyofahamu, CUF kinapitia wakati mgumu kutokana na mambo yanayofanywa na Msajili wa Vyama pamoja na Lipumba. Lipumba na Jeshi la Polisi wamekuwa wakishirikiana kufanya hujuma dhidi yetu”, alikaririwa Maalim Seif alipozungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwaka jana.

Maalim Seif alifafanua kuwa Jeshi la Polisi limekua likivamia aliyoita mikutano halali ya CUF kwa kushirikiana na msajili wa vyama vya siasa, huku Prof Lipumba akiwa na kundi lake aliloliita la wahuni, ambapo alikiri kuwa waliwavamia kwenye mkutano wao uliofanyika katika hoteli ya Blue Pearl na kuvuruga mkutano huku polisi walishuhudia.

Maalim alikwenda mbali zaidi kwa kumuandikia msajili wa vyama barua Septemba 27 mwaka jana ya kupinga kumtambua Prof. Ibrahimu Lipumba kama Mwenyekiti halali wa CUF akidai kuwa Ofisi ya Msajili haina mamlaka ya kisheria ya kutoa ‘ Msimamo na Muongozo” kwa chama cha siasa kilichosajiliwa hapa nchini, na badala yake amepewa mamlaka ya kuhifadhi kumbukumbu na taarifa za vyama vya siasa peke yake.

Prof Ibrahim Lipumba aliandika barua ya ‘kusudio” lake la kujiuzulu yaani intention to resgn Agosti 5, 2015 kwa kutangaza kusudio lake hilo mbele ya wandishi wa habari.  Kwa mujibu wa Katiba ya CUF, Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu na Katibu Mkuu Msaidizi uamuzi wao wa kujiuzulu unapitishwa na Mkutano Mkuu wa CUF baada ya mtu anayekusudia kujiuzulu kuandika barua kwa Katibu Mkuu wa Chama, hata kama Katibu Mkuu asingekuwepo angeandika barua.

Ni jukumu la ofisi ya Katibu Mkuu kuitisha kikao cha Baraza Kuu ili kuandaa mkutano mkuu maalum kwa ajili ya kujadili jambo nyeti la aina hiyo. Endapo jambo hilo litatokea kipindi ambacho mkutano mkuu wa kawaida haujaitishwa kwa mujibu wa katiba, mkutano huo utajadili sababu za anayetaka kujiuzulu kwa kuziafiki au kuzipinga kabla ya mkutano huo haujaitishwa ndani ya muda unaokubalika kwa mujibu wa katiba ya CUF.

Kabla ya kuitishwa kwa vikao hivyo ndani ya muda unaokubalika, Kiongozi anayetaka kujiuzulu, anaweza kuandika barua ya kutengua nia yake ya kusudio lake la kujiuzulu, wakimukubalia atajiuzulu, wakimkatalia ataendelea na nafasi yake ya uongozi.

Kama ataandika barua ya kufuta kusudio lake la kujiuzulu( intention to resgn), kama alivyofanya Prof Lipumba, mkutano mkuu hautaitishwa kwa sababu anarudi kwenye nafasi yake ya awali. Kilichotokea ndani ya makundi mawili ya CUF, ambacho kwa sasa kinapotoshwa ni kwamba Prof Lipumba aliandika barua ya ‘kukusudia”  kujiuzulu na Maalim Seif alikabidhiwa barua ile lakini hakuitisha mkutano wa kumjadili kwa mujibu wa katiba ya CUF.

Matokeo yake, muda wa uliokusudiwa wa kuitisha mkutano ulikwisha, hivyo Prof Lipumba akaamua kuandika barua ya kufuta kusudio lake la kujiuzulu, ambapo Maalim Seif alikiri kuipokea barua hiyo ambayo haikuwa ya kujiuzulu bali ya kukusudia kujiuzulu!

Maalim Seif aliitisha mkutano huo mwaka jana jijini Dar es Salaam nje ya muda wa kujadili jambo hilo kwa mujibu wa Katiba ya CUF na kilichochagiza hoja hii ni baada ya Maalim Seif kupokea barua kutoka kwa Lipumba. Maalim aliitisha mkutano ule Prof Lipumba akiwa bado Mwenyekiti halali wa CUF.

Kilichotokea baadaye, Maalim Seif aliunda Kamati ya uongozi iliyoongozwa na Wakili Msomi Taslim Twaha na wakurugenzi wapya watano baada ya kuwang’oa waliokuwepo awali na baadaye aliunda Kamati nyingine iliyoongozwa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CUF Julius Mtatiro ambayo nayo kimsingi ilikuwa kinyume cha katiba ya CUF.

Na kuthibitisha haya, baada ya mkutano mkuu wa CUF uliofanyika kujadili kusudio la kujiuzulu la Prof Lipumba na kudaiwa kuwa mkutano huo ulikubaliana kwa zaidi ya kura 400 kuwa Lipumba alitakiwa kujiuzulu kati ya kura 14 zinazodaiwa kupinga uamuzi huo.

Lakini  bado mkutano ule ulishindwa kumchagua Mwenyekiti wa CUF, jambo linalothibitisha wanaomuunga Prof Lipumba ndani ya CUF kuwa mkutano ulivunjika kwa vurugu na ksababishwa kutofikiwa maamuzi yote kuwa halali.

Maana kama mkutano ungeendelea kwa kufanya maamuzi bila shaka nafasi ingetangazwa na Mwenyekiti angechaguliwa kwenye mkutano huo huo wa CUF. Nayasema haya ili kuthibitisha kwamba Prof Ibrahim Lipumba ndoye Mwenyekiti halali wa CUF kwa mujibu wa katiba ya CUF.

MSAJILI ASITOLEWE KAFARA

Ili kujiridhisha, Msajili wa vyama vya siasa alimuagiza Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif kumpelekea muhtasari wa kikao kilichokubaliana na kusudio la kujiuzulu kwa Prof Lipumba ikaonekana kulikuwa hakuna mjadala ama mjadala uliishia njiani bila kufikia maamuzi, isipokuwa uwezekano wa kughushiwa kwa idadi ya wajumbe wanaosemekana ndio waliokubaliana kwamba Prof Lipumba atekeleze kusudio lake la kujiuzulu.

Inadaiwa Maalim Seif alikuwa anacheza na katiba ya CUF kwa kuongeza wajumbe kutoka Visiwani Zanzibar ili wamsaidie kufanya maamuzi dhidi ya wajumbe wa bara ambao inaaminika kwamba wanamuunga mkono Prof Lipumba!

Kwa bahati mbaya ongezeko hilo la wajumbe kutoka Zanzibar halikuungwa mkono na toleo jipya la katiba ya CUF inayotumika kwa sasa. Mambo haya na mengine yanayohusiana na mahusiano ya mwenendo wa uongozi ndani ya chama, kati ya Mwenyekiti na Katibu Mkuu wa CUF.

Wakati wa maandalizi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi Nje ya Bunge (UKAWA), inadaiwa Maalim Seif alianza kuchukua nafasi ya Mwenyekiti wa CUF ndani ya vikao vya UKAWA kwa kufanya maamuzi bila kumshirikisha wala kutumwa kumwakilisha Mwenyekiti wake kwenye vikao hivyo, kutokana na kinachodaiwa ni hila za katibu wake.

Kwa mujibu wa baadhi ya taarifa za wajumbe, ambao ni viongozi wa  juu ndani ya CUF, ambazo hazijathibitishwa na RAI, zilienea tuhuma kwamba nia ya Maalim Seif ilikuwa kuwauzia Chadema nguvu ya wanachama wa CUF walioko bara ili apate kuungwa mkono Zanzibar.

Kwa mujibu wa tuhuma hizo, nia ya UKAWA ilikuwa ni kuiondoa kabisa CUF na kuifanya CUF Zanzibar na bara Chadema ili kuteng’eneza mizani ya kisiasa ndani ya UKAWA jambo ambalo Prof Lipumba alilipinga kwa nguvu zote.

Ushahidi wa haya unatokana na majimbo mengi ya uchaguzi waliyopewa CUF na UKAWA kuchukuliwa na Chadema kwa nguvu. Mfano wa majimbo hayo ni pamoja na jimbo la uchaguzi la Bukoba Vijijini mkoani Kagera, ambapo Chadema walilichukua na kusababisha jimbo hilo kutwaliwa na CCM.

Tuhuma ya kundi moja katika mgogoro huu dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ni mfano wa kile ninachokizungumza kwani kadri siku zinavyokwenda na mgogoro kuongezeka, tunaweza kushuhudia hujuma dhidi ya Msajili mwenyewe na vyombo vingine vya dola vinavyosimamia sheria nchini, katika hili Msajili asitolewe kafara.

Pili, kunaweza kujengeka imani kwa watu kwamba, Taasisi ya Msajili wa Vyama vya siasa nchini inaviruhusu baadhi ya vyama vya siasa au viongozi wa vyama hivyo kwa faida ya serikali jambo ambalo sio kweli.

Hatua hiyo inaweza kuondoa imani ya watu kwa taasisi hii muhimu na jukumu lake la kusimamia usajili wa vyama vya siasa, ambalo ndilo lengo la taasisi hiyo kwa mujibu wa Sheria Na.5 ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992.

Ninachofahamu, Msajili alisema Prof Lipumba bado ni Mwenyekiti halali wa CUF kwa sababu hakuna ibara ya katiba ya CUF inayomuondoa baada ya kuandika barua ya kufuta nia (kusudio) yake ya kujiuzulu baada ya CUF kushindwa kuitisha mkutano kwa wakati muafaka, ili kujadili kusudio la kujiuzulu la Prof Lipumba.

MADHARA YA VURUGU

Madhara ya vurugu hizi za kisiasa kwa nchi yenye watu maskini kama yetu, madhara yake ni makubwa. Kwanza ni kudhoofisha upinzani ambao ni muhimu kwa taifa letu na mataifa mengine duniani.

Pili ni kutengeneza uchochoro wa vurugu za kisiasa ambazo zina uwezekano mkubwa wa kuzalisha uhasama ambao unaweza kuhama kutoka kwenye vyama vya siasa na baadae kuathiri mtengamano na mshikamano wa wananchi katika taifa letu.

Wakati nchi inataka kujenga misingi katika mwelekeo wa uchumi wa viwanda, ni muhimu kwa wanasiasa na warasimu wakajifunza kuaminiana, kufuata katiba za vyama vyao na Katiba ya nchi kwa pamoja.

Jambo ambalo watu hawafahamu, likipatikana suluhisho la kudumu ndani ya CUF, litatoa fursa kwa watu kushiriki kwenye shughuli za maendeleo, kwa vyama vya siasa na wasio wanachama. Kwa sababu maendeleo hayana chama na yanafaidiwa na wanachama na wasio wanachama wa vyama vya siasa.

Kuwa na uvumilivu wa kisiasa (political tolerance) na kukubaliana na kutofautiana kwenye mambo yasiyo halifu sera na katiba za vyama vyao ni jambo la msingi sana, maana  upinzani sio uadui na wala uongozi sio dhuluma bali ni maafikiano! Mungu ibariki Tanzania!

Mwandishi wa makala haya anafanyia kazi zake jijini Mwanza na anapatikana kwa Simu Na. 0756 823 420/ 0784 822 407 au email nashon_kennedy@yahoo.com au nashonkennedy@ gmail.com