Home Habari VYETI FEKI VYATIKISA NCHI

VYETI FEKI VYATIKISA NCHI

1306
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU,

SASA ni dhahiri sekeseke la vyeti feki linatikisa nchi kutokana na moto wake kuunguza maeneo muhimu ya huduma  za jamii. RAI linachambua.

Zoezi la kuwaweka hadharani wenye vyeti feki, liliibuka mwishoni mwa mwezi uliopita kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki kumkabidhi Rais Dk. John Magufuli orodha ya watumishi wa umma wenye vyeti feki vya elimu ya kidato cha nne.

Orodha hiyo ambayo ilibeba zaidi ya  majina 9000 ilionekana kuwatikisa zaidi waalimu, madereva na wahudumu wengine wa ngazi ya chini ya kiuongozi.

Hata hivyo, kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo moto wa zoezi hilo unavyozidi kuunguza maofisa wa ngazi ya juu wa Idara na Taasisi za Serikali.

Katika siku za karibuni nchi imeshuhudia anguko kubwa la watumishi muhimu wa sekta ya afya zaidi ya 130 wakikumbwa na dhahama hilo la vyeti feki.

Uhakiki uliofanywa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) umebaini kuwa watumishi 134 wamebainika kughushi vyeti, huku wengine 38 wakibainika katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mshipa (MOI).

Tangazo lililotolewa mwanzoni mwa wiki hii hospitalini hapo na kusainiwa na Mkurugenzi Mtendaji, Profesa Lawrence Museru, lilitaja majina na idara zao ambao wamebainika kuwa na vyeti vya kughushi.

Profesa Museru alisema watumishi walioorodheshwa katika orodha hiyo wanapaswa kujiondoa  wenyewe kazini kabla ya Mei 15, mwaka huu.

Alisema watumishi ambao hawajaridhika na uamuzi huo, wametakiwa kukata rufaa kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kabla ya tarehe hiyo na kwamba barua hizo ni lazima zipitie kwa Mkurugenzi Mtendaji kwa ajili ya maoni yake.

“Wakuu wa Idara na Majengo mnatakiwa kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanaohusika hawaendelei kutoa huduma,” alisema Prof. Museru.

Idara ambazo zinaongoza kwa kuwa na watumishi ambao wamebainika kuwa na vyeti vya kughushi ni Kurugenzi ya Uuguzi ambapo watumishi 70 wamekumbwa na fagio hilo, ikifuatiwa na Kurugenzi ya Tiba ambao wapo watumishi 20.

Mbali na hizo Kurugenzi ya Tiba Shirikishi imebainika watumishi 14, Kurugenzi ya Tehama watumishi 11, Kurugenzi ya Upasuaji watumishi wanne, Kurugenzi ya Rasilimali Watu watumishi wawili.

Orodha hiyo inaonesha Kurugenzi ya Ufundi wapo watumishi watatu, Kurugenzi ya Fedha na Mipango watumishi watatu Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) watumishi watatu.

Inaonesha pia vitengo vinavyoripoti kwa Mkurugenzi Mtendaji wapo watumishi watatu na katika Taasisi ya Sayansi Shirikishi za Afya yupo mtumishi mmoja.

Aidha, katika Kurugenzi ya Tiba watumishi wote walikuwa kitengo cha magonjwa ya dharura.

Upande wa wauguzi wengi walikuwa wakifanya kazi Wodi ya Kibasila, jengo la wazazi namba moja na na namba mbili, Mwaisela, wodi ya wagonjwa wa nje na jengo jipya la wazazi.

Akifafanua zaidi kuhusu orodha hiyo Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),  Aminiel Eligaeshi alisema kwenye Kurugenzi ya Tiba Shirikishi watumishi hao walikuwa wakifanya kazi katika maabara kuu ya hospitali hiyo.

“Muhimbili tulikuwa jumla ya wafanyakazi 2,859 baada ya uhakiki wa vyeti vya taaluma 134 waligundulika kuwa wamegushi vyeti vyao, kwa hiyo tumebaki wafanyakazi 2,725, tumejipanga na tunaendelea kutoa huduma kama kawaida.

“Watumishi watatu waliopo katika vitengo vinavyoripoti kwa Mkurugenzi Mtendaji ni wale waliokuwa wakifanya utafiti na ushauri,” alisema.

Alisema wauguzi waliotajwa katika orodha hiyo wapo ambao walikuwa wakifanya kazi katika chumba cha upasuaji.

“Madaktari waliotajwa humo walikuwa wakifanya kazi katika Kurugenzi ya Tiba,” alisema Eligaeshi.

Naye, Ofisa Habari wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), Patrick Mvungi,  alisema wamebainika watumishi 38 wenye vyeti vya kughushi katika taasisi hiyo.

“Wapo wauguzi 16, wasaidizi wa wodini 16, mtaalamu mfumo wa IT mmoja, mtaalamu wa vipimo vya picha mmoja, fundi umeme mmoja, mtunza kumbukumbu mmoja, ofisa ugavi mmoja na mtaalamu wa maabara mmoja,” alisema.

MOTO KUWAKA ZAIDI

Mwenendo wa zoezi hili la kuwasaka wenye vyeti feki unadalili za kuwaka zaidi kwenye vitengo vingine muhimu ndani ya Serikali.

Hali hiyo inatajwa kuibua hofu kwa baadhi ya watumishi ambao wanadaiwa kufoji vyeti vya elimu ya kidato cha nne, ambayo iliwasaidia kuendelea na elimu ya juu.

RAI limedokezwa kuwa sakata hili kama litatekelezwa bila ubaguzi linaweza kuidhoofisha Serikali kutokana na idadi kubwa ya wataalamu wake wenye elimu za juu kuguswa moja kwa moja na tatizo la kukosa vyeti halali vya kidato cha nne.

Tayari baadhi ya mawaziri na wakuu wa mikoa wameshaanza kutajwa tajwa kwenye sakata hili la kukosa vyeti vya kidato cha nne hali inayoibua taharuki zaidi.