Home Habari VITABU FEKI KUZALISHA VILAZA ZAIDI  

VITABU FEKI KUZALISHA VILAZA ZAIDI  

4275
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU


IDADI kubwa ya Watanzania walioko katika elimu ya ngazi ya Msingi na Sekondari nchini wako katika hatari ya kupata elimu duni iwapo serikali haitachukua hatua za haraka za kuviondoa vitabu vya kiada vilivyo na makosa ya kiuandishi na kimaana.

Madai ya kuwapo kwa vitabu feki yaliibuka rasmi mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa uwasilishaji wa bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi ambayo ni Sh. 1,366,685,241,000.00, iliyowasilishwa na Waziri wa wizara hiyo, Profesa Joyce Ndalichako.

Bajeti hiyo ya mwaka wa fedha wa 2017/18 ni pungufu kwa asilimia 4.2 ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/17 unaoishia Juni 30 mwaka huu.

Wakati wa uwasilishaji wa bajeti hiyo, baadhi ya wabunge waliorodhesha madudu yanayoiandama wizara hiyo baadhi yake yakiwa ni ya kimfumo na kiutendaji.

Wabunge hao walibainisha kuwa moja ya sababu zinazoporomosha elimu nchini ni vitabu vya kiada kuwa na makosa pamoja na madeni ya waalimu yasiyokwisha.

Kutokana na kuibuka kwa madudu hayo ya kwenye vitabu ambayo yanagusa maslahi ya elimu moja kwa moja, RAI lilizungumza na baadhi ya wadau wa elimu nchini ili kujua madhara yaliyopatikana, yanayopatikana na yanayoweza kupatikana kutokana na madudu hayo ya kwenye vitabu.

Mwenyekiti wa Chama cha Wachapishaji Tanzania (PATA), Gabriel Kitua aliliambia RAI kuwa kumekuwa na makosa kwenye vitabu vya kiada kwa sababu serikali haikuchukua ushauri uliotolewa na wataalamu wa uchapishaji wa vitabu vya kiada.

Alisema Taasisi ya Elimu ama haikuwa na uwezo wa kitaalamu unaohitajika katika shughuli hiyo au ilipuuzia kupata wataalamu stahiki wa kufanya kazi hiyo.

“Utungaji vitabu vya shule unahitaji zaidi ya uelewa wa mitaala (carruculum) kitu ambacho Taasisi ya Elimu ina uzoefu nacho, lakini siyo katika utayarishaji wa miswada (manuscripts), michoro, mtiririko wa kufundisha somo na upangiliaji wa kurasa vitu ambavyo ni sawasawa na sanaa kwani vinahitaji vipaji zaidi na uzoefu,” alisema Kitua.

Alisema hatua ya vitabu vya kufundishia kuwa na makosa inaweza kuchangia kuwapo kwa mamilioni ya Watanzania mbumbumbu ambao kwa tafasiri sahihi ni kwamba ni watu wanaojua kusoma na kuandika, lakini hawajua mambo mengi kwa sababu vitabu viliwapotosha.

Akizungumzia suala hilo Mwalimu mmoja wa shule ya Msingi ya Mugabe iliyopo Sinza ambaye hakuwa tayari jina lake kuandikwa gazetini, aliliambia gazeti hili kwamba alishangazwa kuona mapungufu makubwa katika kitabu cha kufundishia hali iliyoonesha wazi kuwa mtunzi hakuwa na uwezo wa lugha aliyotumia kwani makosa ni mengi. Alitoa mfano wa mchoro wa mwalimu akiwa darasani anayaeandika ubaoni neno “taecher” badala ya “teacher.”

Akizungumza na gazeti hili mmiliki wa kampuni ya uchapishaji vitabu ya Mkuki na Nyota, Walter Bugoya alisema wachapishaji binafsi wamekuwa wakifanya kazi nzuri tofauti na inavyofikiriwa na Serikali.

Bugoya alisema utaratibu wa kuwatumia wachapishaji binafsi kuchapisha vitabu vya kiada unatumika katika nchi mbalimbali barani Afrika ikiwamo Zambia, Afrika Kusini, Kenya na hata Uganda.

“Kenya, kwa mfano iliwahi kutumia taasisi zao za elimu kuchapisha vitabu vya shule lakini kutokana na matatizo kama haya ndiyo ilikuwa ya kwanza kubadilisha mfumo huo ikifuatiwa na Uganda na baadaye Tanzania mwaka 1991.

“Mwaka 2010 Malawi ilituma ujumbe wa Taasisi yake ya Elimu kuja Tanzania kujifunza mfumo wa uchapishaji vitabu vya shule kupitia wachapishaji binafsi,” alisema Bugoya.

Mbali ya wachapishaji binafsi kudaiwa kuwa na umakini wa hali ya juu, lakini pia wanatajwa kuwa na bei rahisi tofauti na bei inayotumiwa na Tasisi ya Elimu nchini ambayo ndie mchapishaji mkuu.

Baadhi ya wadau wa masuala ya uchapishaji wameliambia RAI kuwa wastani wa vitabu vinavyochapishwa na Taasisi ya Elimu hufikishwaa Bohari Kuu jijini Dar es Salaam kwa wastani wa Sh 19/- kwa ukurasa mmoja na kusafirishwa hadi wilayani na hatimaye shuleni kwa wastani wa Sh 25/- kwa ukurasa mmoja, tofauiti na hali ilivyo kwa wachapishaji binafsi.

Wachapishaji binafsi, hadi kufikia mwaka 2014 walikadiriwa kugharimu wastani wa kiasi cha sh 10/- kwa ukurasa mmoja. Ambao ni wastani wa chini ya bei ya TIE.

Mkaguzi wa Shule za Msingi na Sekondari nchini, Educome Shirima, alikiri kuwapo kwa janga hilo, hata hivyo alisema hawezi kutolea ufafanuzi wa athari ya jambo hilo kwani vitabu hivyo viligawanya kwa shule za serikali pekee.

“Ni kweli wanaokagua wanabaini matatizo.  Vitabu vinavyolalamikiwa vilitengenezwa na serikali kwa kupitia TIE, vyote viligawiwa kwa shule za serikali ambazo ni za Msingi na Sekondari. Vile vitabu vya shule binafsi vilikuwa kwenye mchakato wa kuandaliwa.

“Kuhusu suala la ukubwa wa tatizo siwezi kulitolea ufafanuzi kwa sababu tayari Waziri ameunda Kamati huru ili kufuatilia hilo suala na itakapoleta taarifa ndipo itabainika kuwa ni kweli ama ni uongo, kwa sababu bila evidence (ushahidi) huwezi kujibu nini kinachoendelea,” alisema.

 

KIINI CHA MADUDU HAYA

Inadaiwa kuwa kiini cha kuwapo kwa suala hili la sera hasa baada ya Serikali ya Awamu ya Nne kuamua kusitisha kazi ya uchapishaji vitabu vya kiada kufanywa na wachapishaji binafsi na jukumu hilo kuachwa kwa Taasisi ya Elimu – TIE.

Miaka michache iliyopita, Rais wa awamu ya Nne alifanya mkutano na viongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ambapo alitoa kauli kuhusu suala la wingi wa aina za vitabu vya kiada katika shule na kuagiza kuwa hali hiyo itazamwe na idadi ya vitabu ipunguzwe ili viwe viwili au vitatu.

Agizo hilo lilikuwa na dhamira ya kuamsha mabadiliko makubwa ya sera iliyokuwapo juu ya matumizi ya vitabu vya kiada katika shule – sera ambayo ilikuwapo tangu mwaka 1991.

Agizo hilo liliisukuma Wizara ya Elimu katika Waraka wake Na. 4 wa 2014 kufuta sera ya awali ya uchapishaji na usambazaji vitabu kwa shule uliokuwa unafanywa na wachapishaji binafsi na kuwapa jukumu hilo TIE.

Mbali ya kuchapisha na kusambaza, lakini pia TIE ilitakiwa kutunga na kuhariri vitabu vya kiada kwa ajili ya shule za awali (pre-schools), shule za msingi, sekondari na vyuo vya Ualimu.

Waraka huo huo uliwaruhusu wachapishaji binafsi kuchapisha vitabu vya ziada tu (reference books).

Aidha, Waraka huo uliweka utaratibu wa utoaji ithibati ya miswada ya vitabu iliyothibitishwa na Taasisi ya Elimu ambao uliweka wazi kuwa miswada hiyo itapelekwa kwa Kamishna wa Elimu ambaye baada ya kupitia na kujiridhisha nayo kuhusu ubora na viwango, atawasilisha kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambaye kwa mujibu wa sheria ndiye atakayeidhinisha  matumizi ya vitabu hivyo mashuleni.

 

VIGOGO WASIMAMISHWA KAZI

Katika kuhakikisha jambo hilo la vitabu feki linapatiwa majibu ya kina tayari Prof. Ndalichako ameshawasimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania, Dk. Elia Kidga na Kaimu Kamishna wa Elimu, Nicolaus Buretta ili kupisha uchunguzi wa jambo hilo.

Mbali na hatua hiyo, lakini pia tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU)  imeshaanza kazi ya kuwachunguza vigogo hao waliosimamishwa kazi.