Home kitaifa KIVULI CHA BASHITE CHAMKOROGA KITWANGA

KIVULI CHA BASHITE CHAMKOROGA KITWANGA

373
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI


Kivuli cha mtu anayetajwa kwa jina la Bashite, ambaye  hajawahi kuelezwa rasmi kuwa ni nani na ana nafasi gani ndani ama nje ya Serikali kimeonekana dhahiri kumkoroga mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga.

Kitwanga, ambaye alishawahi kushikilia wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, anatajwa kukumbana na vizingiti kadhaa ndani ya safari yake ya kisiasa kwa sababu mbalimbali kubwa ikiwa ni baadhi ya makada wenzake kulimendea jimbo lake.

Miongoni mwa watu hao, ambaye hivi karibuni yeye mwenyewe alimtaja ndani ya ukumbi wa Bunge kwa jina moja la Bashite.

Akichangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji iliyowasilishwa na Waziri  wa wizara hiyo, Mhandisi Gerson Lwenge aliyeliomba Bunge kuidhinisha TZS bilioni 672.2 kwa ajili ya matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2017/18, Kitwanga alisema baadhi ya mambo yamekuwa yakikwama ndani ya jimbo lake kwa madai kuwa  Serikali imekuwa ikimuandaa Bashite kuwania jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Aliijia juu serikali na kusema kuwa inamhujumu ili apoteze jimbo katika uchaguzi ujao kwa kuamua kutokupeleka maji jimboni kwake.
Kauli hiyo ya Kitwanga inahalalisha taarifa iliyowahi kutolewa na RAI mwezi mmoja uliopita ikihusisha taarifa zilizoibua hoja ya Bashite na mbio za kuwania ubunge wa jimbo hilo mwaka 2020.

Akilalamikia hilo, Kitwanga alidai kuwa Serikali imeamua kutopeleka maji jimboni kwake kwa sababu inamuandaa Bashite kugombea kwenye jimbo hilo.

Akichangia hotuba hiyo, Kitwanga alieleza hali ngumu ya upatikanaji wa maji wanayopitia wakazi wa kijiji cha Kolomije ambapo ndipo alipozaliwa Bashite.

Alikwenda mbali zaidi kwa kuonyesha kukerwa na serikali kupuuza kupeleka mradi wa maji jimboni mwake na kwamba atahamasisha wananchi wa Misungwi kwenda kuzima mitambo ya maji ambayo ipo katika Kijiji cha Ihelele anachodai kuwa kimesahaulika katika miradi ya maji iliyopangwa kwenye bajeti ya 2017/28.

“Wakati nilipokuwa Waziri nilikuwa nashindwa kuibana serikali, lakini kwa vile sasa ni mbunge tu, basi patachimbika. Very unfair (si haki), nazungumza kutoka moyoni mwangu, haiwezekani mradi unakwenda Tabora unatumia 600 bilioni halafu watu wangu wanakosa maji hata ya bilioni 10,” alisema Kitwanga.

Hata hivyo, siku chache baada ya Charles Kitwanga kutishia kuhamasisha wananchi  kuzima mtambo wa kusukuma maji kutoka Ziwa Victoria kwenda mikoa ya Shiyanga na Tabora, Serikali ilimjibu kwa kumtaka ahame kwenye chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama anaona hatendewi haki.

Akihitimisha mjadala wa makadirio ya mjini Dodoma,  Mhandisi Lwenge alimjibu Mbunge huyo kwa kumtaka aihame CCM kama anaona hakitendi haki dhidi yake.

Dhamira ya jimbo la Misungwi kutazamwa na wengi pia ilipata kuelezwa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Joseph Gwajima, ambaye alidai kuwa moja ya sababu za kutajwa kwake kuhusika na dawa za kulevya ni vita ya kisiasa.

 

KITWANGA AMKARIBISHA KWA MAPAMBANO

Akizungumza na RAI Machi mwaka huu Kitwanga alisema hana hofu na jimbo lake na kwamba yuko tayari kupambana na anamkaribisha yeyote mwenye kulihitaji jimbo hilo.

Kitwanga ambaye anashikilia rekodi ya kuwa Waziri wa kwanza ndani ya Baraza la Mawaziri wa Serikali ya awamu ya Tano kutenguliwa, alikiri kusikia Bashite kulitaka jimbo lake, lakini bado yeye yupo kwenye mwaka wa pili wa uongozi wake hivyo hana hofu, badala yake anachokifanya sasa ni kuhakikisha anawapelekea maendeleo wapigakura wake.

“Kama kuna mtu anataka kugombea, utakapofika muda anakaribishwa, mimi sina matatizo na mtu yeyote, sasa hivi nafanya kazi ya ubunge kuhakikisha wananchi wangu wanapata maendeleo, hivyo siwezi kufikiria mtu anayeliwaza jimbo langu, siwezi kumzuia kunifikiria wala kumkataza, lakini muda utakapofika na duru ikianza wanakaribishwa tupambane, tena mimi nitafurahi kupambana na watu wazito wazito.

Maana yake mapambano ya watu wanyonge hayaleti ule uamsho wa uchaguzi, kwa hiyo kama kuna mtu anataka kama ni Gwajima aje na kama ni Bashite aje.

“Nashukuru kama wameonesha nia hiyo, waje kwani wanajua kama nitagombea 2020?, kwa sababu muda ukifika nitawaambia wananchi jamani bado nahitaji kuendelea ama lah! namkaribisha Bashite iwapo anataka kuwania jimbo hilo,” alisema.