Home kitaifa SAID MECKY SADICK: NIMECHOKA

SAID MECKY SADICK: NIMECHOKA

1284
0
SHARE

Na Safina Sarwatt ,Kilimanjaro,


ALIYEKUWA Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Said Mecky Sadick ameweka wazi kuwa ameamua kwa hiyari yake kuacha kazi kwa sababu amechoka na anahitaji kupumzika. RAI linaripoti.

Taarifa ya juzi kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi ilieleza kuwa mwanzoni mwa wiki hii Rais Dk. John Magufuli aliridhia maombi ya kuacha kazi kwa kiongozi huyo.

Mbali ya Mecky Sadick wengine walioridhiwa na Rais kuacha kazi ni aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya kurekebisha Sheria Tanzania Aloysius Kibuuka Mujulizi.

Mwingine ni aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania, Upendo Hillary Msuya Ikiwa ni siku chache mara bada ya Rais Magufuli kufanya ziara ya siku tatu mkoani Kilimanjaro, mkuu wa mkoa Kilimanjaro Saidi Meck Sadick amefanya maamuzi magumu ya kuachia kiti chake kwa hiari yake.

Katika mazungumzo ya ana kwa ana na RAI yaliyofanyika ofisini kwake, mkoani Kilimanjaro, Mecky Sadick alisema ameamua kupumzika kwa sababu anaona ameitumikia Serikali vya kutosha.

Alisema ameamua kupumzika kwa hiyari yake mwenyewe kwa sababu anaamini sasa ni muda sahihi wa kuwapisha vijana wamsaidie Rais kutimiza malengo.

“Ni kweli nimemwandikia barua Rais nikimuomba kupumzika, naamini nilikuwa na nafasi ya kuweza kulitumikia Taifa langu katika nafasi hii ya Mkuu wa mkoa, lakini najiona nimechoka.

“Nataka kupumzika, umri wangu umeenda, labda ieleweke tu, nilishaandika barua ya kupumzika muda mrefu sana na hata alipokuja Kilimanjaro nilimkumbusha na nashukuru ameridhia ombi langu,” alisema.

Kuhusu taarifa ya Ikulu kuwa ameacha kazi na si kama amestaafu kwa hiyari, alisema haoni tofauti, kwani ni kweli ameamua kujiweka pembeni.

“Hilo lisikupe shida. Siioni tofauti, kama ningeambiwa nimefukuzwa, hapo ningehamaki, lakini kuacha kazi, wala sioni tofauti, ni kweli nimeamua mwenyewe mwenyewe kwa hiyari yangu,”alisema .

Alisema pamoja na kutumikia nchi kwenye maeneo tofauti tofauti, lakini alianza rasmi kushikilia nyadhifa za uteuzi tangu mwaka 1999.

“Nilianzia kwenye Ukuu wa wilaya hadi mwaka 2005, baada ya serikali ya Awamu ya Nne kuingia madarakani, nikateuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa .

“Naishukuru sana serikali kwakuniamini na kufanya kazi na mimi, hii ni sifa kubwa sana kwangu.

“Hatua ya serikali zote kuniona nafaa hadi hivi sasa ni jambo la kumshukuru Mungu, nimechoka, ngoja nikapumzike,  nawaachia vijana waongoze pia, madaraka ni ya kila mtu,  mimi nimezeeka wacha nikapumzike naenda kuungana na raia wengine na nitaendelea kushirikiana na jamii,” alisema.

Akimzungumzia Rais Magufuli, alisema  ataendelea kumpongeza  kwa jitihada zake

za kupambana na vita dhidi ya ufisadi, dawa za kulevya, watumishi hewa na wale waliogushi vyeti na kwamba hayo yote anayafanya kwa maslahi ya Watanzania.

“Rais wetu ana nia njema kwa Watanzania, ni vema tukaendelea kumuunga mkono katika jitihada zake zote hasa hizi za Tanzania ya viwanda.

“Viwanda vinahitaji kilimo bora na ili kuendana na kasi hiyo kunahitajika vijana wenye nguvu.”

Alikwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa kila Rais amekuwa na mema yake na mabaya yake, lakini anaamini wote waliopitya na hata aliyepo wanafanya kazi kwa kufuata ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Nimefanya kazi na Serikali ya awamu ya Tatu, Nne na sasa Tano, kila aliyeingia madarakani alikuwa akitekeleza ilani ya CCM, walichotofautina ni namna ya utekelezaji wa Ilani tu.”

Amesema kuwa kila awamu ilikuwa na changamoto zake na mafaniko yake.

Nimeshiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo ya taifa hili kwa kushirikiana na viongozi wenzangu kwenye nyaja tofauti tofauti ya kielimu pamoja kiuchumi.