Home Makala TANZANIA YATIKISA UCHAGUZI MKUU KENYA

TANZANIA YATIKISA UCHAGUZI MKUU KENYA

282
0
SHARE
Kiongozi wa Wabunge wa Jubilee katika Bunge, Aden Duale.

NAIROBI, KENYA


SERIKALI ya Kenya imeanza kufuatilia fedha zote zinazotoka nje ya nchi kwa ajili ya kugharamia kampeni zao za uchaguzi.

Hatua hiyo imelalamikiwa na muungano wa vyama vya upinzani wa NASA unaodai kuwa walengwa wakuu wa angalizo hilo ni wao.

Vyanzo vya habari nchini humo vimeeleza kwamba, taasisi moja iliyoketi chini ya uenyekiti Mkuu wa Idara ya Utumishi wa Umma, Joseph Kinyua ilitoa maamuzi ya kufuatilia mahusiano baina ya vyama vya siasa na wafadhili kutoka nje, huku ikidaiwa kuwa walengwa wakuu ni muungano wa NASA.

Hata hivyo, kikao hicho kilikaa wakati mgombea wa urais wa NASA, Raila Odinga akitarajiwa kukutana na baadhi ya wanaosadikiwa kuwa wafadhili wakati wa ziara yake Jerusalem, Israel.

Kikao hicho, chini ya Kinyua, kilijumuisha maofisa kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Usalama wa Taifa(National Intelligence Service – NIS), Taasisi ya Kupambana na Rushwa (EACC), wawakilishi kutoka Mamlaka ya Mapato (KRA) na wawakilishi kutoka taasisi nyingine.

Baada ya ziara ya Israel, Raila alisafiri hadi Dubai na kurudi nchini mwake tayario kwa maandalizi ya mkutano wa hadhara wa NASA uliopangwa kufanyika Nakuru.

Vyanzo vya kuaminika vilivyofuatilia kikao hicho kilichofanyika katika jengo la Harambee (Harambee House) jijini Nairobi vilisema, Tanzania ni moja ya nchi zinazotajwa kuchunguzwa juu ya suala hili.

Katika mkutano wa chama tawala cha Jubilee kilichomthibitisha Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto kutetea nafasi zao kwenye uchaguyzi wa Agosti 8 mwaka huu, Kiongozi wa Wabunge wa Jubilee, Aden Duale, alidai kuwa Serikali ya Tanzania ilitoa kibali kwa NASA kuweka kituo cha ukusanyaji matokeo ya upigaji kura wakati wa uchaguzi.

Hata hivyo, NASA wamekana kuwapo kwa mpango huo na Duale mwenyewe hakuweza kutoa ushahidi wowote katika madai yake hayo.

Aidha, habari zinasema kwamba jitihada za NASA kupata fedha kutoka nje zitakazogharamia uchaguzi huo ni katika kuongezea kile walichokusanya nchini mwao,  inaelezwa kuwa, kwa ujumla uchaguzi huu utakuwa wa gharama kubwa katika historia ya Kenya.

Mweka Hazina wa Chama cha ODM cha Raila Odinga (katika muungano wa NASA), Kitutu Masaba na mbunge mmoja wa chama hicho, Timothy Bosire, ambao wamo katika kamati ya uchangishaji fedha, wamesema matumaini yao ni michango ya nje kufikia asilimia 30 ya bajeti ya kampeni, ambayo hata hivyo jumla yake kamili hawakuitaja.

Walisema watakuwa tayari kupokea misaada kutoka kwa marafiki kutoka nje kwa kufuata sheria. Wamesema iwapo misaada hii itakuja au la, wana uhakika wa kufanya kampeni itakayosimamiwa vyema na iliyokamilika kifedha katika eneo hili la dunia.

Utawala wa Uhuru Kenyatta unadaiwa kutoa maelekezo makali kwa taasisi zote za fedha, pamoja na mabenki nchini humo kuangalia iwapo kutakuwapo miamala ya fedha haramu ambazo zitaingia nchini mwao.

Inaelezwa kuwa, uwepo wa kituo hiki cha kuratibu fedha za kampeni (Financial Reporting Centre –FRC), ambacho ni taasisi ya serikali iliyoundwa kutokana na sheria ya kupambana na utakatishaji fedha (Crime and Anti-Money Laundering Act) kuna maana ya kwamba shughuli zote za muungano wa NASA zinaratibiwa wakati wote.

Jumamosi iliyopita msemaji wa serikali, Eric Kiraithe, aliliambia gazeti la Sunday Nation kwamba, wanafuatilia kwa karibu mawasiliano kati ya raia yeyote wa Kenya na mamlaka za mataifa ya nje na watu wengine katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.

Hata hivyo, alikataa kusema iwapo kuna chama kinacholengwa zaidi kuliko kingine katika uratibu huu, mbali na kusisitiza tu kwamba, wanataka kuhakikisha Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya 2017 inazingatiwa kikamilifu.