Home Makala WAZIRI WA BUSH ATETEA UAMUZI WA KUVAMIA IRAQ

WAZIRI WA BUSH ATETEA UAMUZI WA KUVAMIA IRAQ

193
0
SHARE
Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani, Condoleezza Rice.

WASHINGTON, USA


WAZIRI wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani, Condoleezza Rice, amesema uvamizi ulioongozwa na nchi yake dhidi ya nchi za Mashariki ya Kati na Asia ya Kati haukuwa na malengo ya kueneza demokrasia, bali ni kuimarisha usalama katika maeneo hayo ya dunia.

Rice, ambaye alifanya kazi chini ya utawala wa Rais George W Bush – awali kama mshauri mkuu wa masuala ya usalama kuanzia 2001 hadi 2005 na baadaye kama Waziri wa Mambo ya Nje (2005 – 2009), aliyaanika hayo katika mahojiano na taasisi ya Brooking Institute.

Rice alitoa mchango mkubwa katika Baraza la Mawaziri la Bush katika kipindi cha baada ya ulipuaji wa majengo mjini New York, Septemba 11 2001 – kipindi ambacho Marekani ilifanya uvamizi mara mbili wa kiwango kikubwa dhidi ya Afghanistan mwishoni mwa 2001 na baadaye Iraq mapema 2003.

Hata hivyo, pamoja na suala la tishio la kikundi cha kigaidi cha Alqaeda kilichokumbatiana na uliokuwa utawala wa Taliban nchini Afghanistan, na madai dhidi ya Rais Saddam Hussein wa Iraq kumiliki silaha za maangamizi, madai ambayo baadaye hayakuthibitishwa, Ikulu ya Marekani ilihalalisha uvamizi huo wa kijeshi kuwa ni kampeni ya kueneza demokrasia katika maeneo hayo.

Rice sasa alisema: “Hatukuvamia Iraq kusimika demokrasia, tulivamia Iraq kumng’oa Saddam Hussein, ambaye tulidhani alikuwa ana silaha za maangamizi alizokuwa anazitayarisha kuzitumia na hivyo kuwa tishio katika eneo hilo. Lilikuwa ni suala la usalama tu.”

Kuhusu Afghanistan, Rice anasema hawakuuondoa utawala wa Taliban kusimika demokrasia nchini humo, tuliwaondoa kwa sababu utawala ule ulikuwa unatoa hifadhi kwa kikundi cha Al Qaeda baada ya tukio la ulipuaji majengo la Septemba 11.

Rice alilinganisha malengo ya Marekani na yale ya wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, pale Marekani ilipoingilia kati kuyalinda mataifa rafiki dhidi ya kuenea kwa nguvu za Mataifa ya Kati (Axis Powers) – yaani Ujerumani chini ya utawala wa Kinazi na dola ya kibabe ya Japan.

Hata hivyo, alikiri kuwepo kwa dhana aliyoiita potofu iliyokuwapo kwamba vita ya kwanza iliyofanywa na Marekani katika Karne ya 21 ilichanganywa na “ajenda ya uhuru”.

Alisisitiza kwamba, uvamizi dhidi ya Iraq uliopewa jina la “Operation Iraqi Freedom” na ule ya Afghanistan kwa jina la “Operation Enduring Freedom” zililenga tu kuwaondoa aliowaita maadui wa Marekani.

Alidai katu asingemshauri Bush kusimika demokrasia Iraq na Afghanistan kwa kutumia nguvu za kijeshi, kitu ambacho kingekuwa mfano wa ajabu wa kukuza demokrasia.

Nchi zote mbili – Iraq na Afghanistan zimeteseka sana kutokana na mapigano yanayoendelea tangu uvamizi wa Marekani.

Nchini Iraq kwa mfano – kung’olewa kwa Saddam Hussein wa madhehebu ya Sunni walio wachache kuliongeza hali ya migongano ya kimadhehebu kati ya madhebu hayo na madhehebu ya Shia walio wengi.

Makundi ya kihafidhina ya Sunni, ambao baadhi yao walikuwa katika utawala wa Saddam Hussein na katika jeshi lake, ndiyo walichukulia vurugu za baada ya uvamizi kwa kuanza kuwashambulia askari wa Marekani na wafuasi wa Shia na hivyo kuanza kuhatarisha uimara wa serikali iliyosimikwa na Marekani.

Aidha, inadaiwa kwamba, makundi hayo na makundi mengine baadaye yaliungana na kuunda kikundi cha Dola ya Kiislamu — Islamic State of Iraq – mwaka 2006 na baadaye kujigeuza jina na kuwa ISIS.

Hata hivyo, baada ya Marekani kuyaondoa majeshi yake kutoka Iraq mwaka 2011, nchi hiyo ililazimika kuyarejesha tena mwaka 2014, ingawa kwa uchache, kusaidia mapambano ya majeshi ya Iraq dhidi ya ISIS.

Na kuhusu Afghanistan, tangu kuangushwa kwa utawala wa Taliban mwaka 2001, hadi sasa Marekani bado inaendelea kupambana na waasi ambao wamezidisha mashambulizi dhidi ya utawala wa Kabul na sasa hivi tayari wameteka maeneo makubwa ya nchi.