Home Habari MAUAJI KIBITI: MWIGULU NCHEMBA MAJARIBUNI

MAUAJI KIBITI: MWIGULU NCHEMBA MAJARIBUNI

428
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU


MAUAJI ya kutumia silaha za moto yanayowakumba viongozi wa kisiasa na Serikali yanayoendelea Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, yanaonekana kumwingiza kwenye majaribu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba. RAI linachambua.

Mwigulu, mwanasiasa aliyebeba sifa za uchapa kazi na uthubutu wa kuwa mstari wa mbele kwenye eneo linalomuhitaji, sasa anaweza kuingia kwenye orodha ya mawaziri waliopata kujiuzulu wenyewe au kutumbuliwa kutokana na kadhia ya mauaji ya Kibiti.

Dhana hii ya kuwajibika au kutumbuliwa kwa Mwigulu, inatokana na historia ya wizara yenyewe, ambayo hadi kufikia sasa imeshahudumiwa na mawaziri 25 tofauti ndani ya miaka 55 ya uhuru.

Kati ya mawaziri hao ni watatu tu ndio waliopata kuhudumu kwenye nafasi hiyo kwa muda mrefu, ambao ni Saidi Maswanya  (1967-73) Muhiddin Kimario (1983-89) ambao kila mmoja alihudumu kwa kipindi cha miaka sita mfululizo, huku Mwenyekiti wa sasa wa Bodi ya Parole Augustino Mrema akihudumu kwa miaka minne (1990-94) .

Nje ya mawaziri hao, waliosalia wote hadi kufikia kwa Nchemba ambaye alichukua kiti hicho kutoka kwa Charles Kitwanga aliyetumbuliwa kwa madai ya ulevi, wamehudumu kwa vipindi vifupi vya kati ya mwaka mmoja na miaka miwili.

Katika miaka ya karibuni Bunge ndio limekuwa kaa la moto kwa mawaziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani, kutokana na kuwa chanzo cha kutumbuliwa kwao kama ilivyokuwa kwa Balozi Emmanuel Nchimbi na baadae Kitwanga.

Dalili za Mwigulu kuanza kuingia kwenye majaribu zimeshaanza kuonekana baada ya mauaji hayo ya Kibiti kuvishwa sura mbalimbali ikiwamo ya ugaidi ambayo waziri huyo anaipinga na kuihusisha na ujambazi kama linavyosema Jeshi la Polisi.

Tayari Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeshaweka wazi kuwa mauaji hayo yana harufu ya kigaidi.

Hadi kufikia sasa majambazi hao wameshaua zaidi ya watu 30 wakiwamo askari polisi, viongozi wa Serikali na vyama vya siasa.

Askari polisi wanane waliuawa kwa kufyatuliwa risasi mapema Aprili wakitoka kwenye doria katika Kijiji cha Jaribu wilayani Kibiti na Ofisa Upelelezi wa Wilaya ya Kibiti (OC-CID), Peter Kubezya na wenzake watatu nao pia waliuawa kwa risasi Februari, mwaka huu.

KAULI YA MWIGULU

Mwigulu alipotembelea polisi wanaoendelea na operesheni wilayani Kibiti, aliibua maswali kadhaa yaliyoonyesha wasiwasi kama mauaji hayo yanasukumwa na wafanyabiashara wa mkaa, vitendo vya ujambazi, udini ama ugaidi.

“Kila nikitafakari naona kuna kamchezo kanachezwa, tusipoangalia kamchezo kanakochezwa tutatafuta adui ambaye hakuwapo na tutaacha adui ambaye anahusika.

“Mwanzoni watu tofauti tofauti kila mmoja alitoa tafsiri yake na wengine wakasema eti ni mkaa, tukawa tunatafuta uhusiano wa mkaa na viongozi wa CCM, yaani ugomvi wa mkaa na CCM wapi na wapi!

“Haya ni maswali yaliyoacha maswali mengi kuliko majibu, wengine wakasema misimamo mikali ya dini, tukahoji na CCM ni wapi na wapi kwa sababu CCM si dini hata viongozi wake wauawe?

“Likaja la ujambazi, hili nalo na CCM tofauti yake iko wapi hata watafute viongozi wa CCM waliostaafu miaka mitano iliyopita?

“Wengine wakasema tena ni ugaidi, sasa ugaidi na CCM ni wapi na wapi na yule anayeonyesha viongozi wa CCM ni nani na yuko wapi mpaka awaonyeshe waliostaafu,” alisema.

POLISI: HAKUNA UGAIDI

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, CP Nsato Marijani Msanzya, alisema askari waliuawa wakiwa njiani kuelekea kambini wakitokea lindoni eneo la Jaribu Mpakani, mara baada ya kuwekewa mtego na wanaodhaniwa kuwa ni majambazi.

Kamishna huyo alikataa kulihusisha tukio hilo na ugaidi, huku akisema hakuna haja ya kuanzisha kanda maalumu ya kipolisi katika Mkoa wa Pwani licha ya kutokea mashambulio ya kuwaua maofisa wa Jeshi la Polisi mara kwa mara katika eneo hilo.

“Hili si tukio la mara ya kwanza kwa mauaji ya aina hiyo yanayowalenga askari polisi kutokea katika maeneo ya Mkoa wa Pwani, wakiwemo viongozi wa Serikai na watendaji mbalimbali hali inayozidisha hofu kwa wananchi wa maeneo hayo kuhusu usalama wao na mali zao,” alieleza Kamanda Msanzya.

Aliongeza kwamba uonevu huo unaofanywa dhidi ya askari sasa umefika mwisho na kusema kuwa jeshi hilo linaingia katika operesheni maalumu ya kuwasaka wahalifu hao kwa lengo la kukomesha vitendo vya kikatili vya mauaji vinavyofanywa na makundi ya wahalifu.

Kuwapo kwa hali hii kunamlazimisha Mwigulu kupambana kwa nguvu zake zote akishirikiana na askari polisi ili kukabiliana na kadhia hii ambayo inampitisha kwenye majaribu ambayo yanaweza kumwondoa kwenye nafasi yake kama ilivyokuwa kwa watungulizi wake.

HISTORIA YA WIZARA

Wizara hii ina changamoto nyingi na imekuwa ikibebeshwa lawama mara kwa mara kutokana na mwenendo wake wa kiutendaji kazi, lawama ambazo zimekuwa zikiishia kwa kuwaangusha mawaziri wake.

Katika kipindi cha miaka 55, mawaziri 25 wamehudumu kwenye wizara hiyo, idadi inayofanya wastani wa kila waziri mmoja kuongoza kwa takribani miaka miwili tu.

Katika kipindi chote hicho wapo baadhi ya mawaziri walioondolewa kutokana na kashfa zilizoikumba wizara hiyo.

Balozi Nchimbi na Mbunge wa sasa wa Misungwi, Kitwanga ni miongoni mwa mawaziri wa miaka ya karibuni waliokutana na kashfa iliyowaondoa kwenye viti vyao.

Aidha, wapo mawaziri wawili ambao kutokana na kashfa zilizoikumba wizara yao kwa hiyari yao waliamua kujiuzulu.

Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi aliyeiongoza wizara hiyo kwa mwaka mmoja (1975-77) mwaka 1977 aliamua kujiuzulu baada ya kuibuka kwa kashfa ya mauaji ya watu katika mikoa ya kanda ya ziwa.

Waziri mwingine aliyejiuzulu kwa hiyari yake ni Abdallah Natepe aliyehudumu kwa maika mitatu (1980-1983).

Natepe alijiuzulu baada ya kutoroka kwa watuhumiwa wa kesi ya uhaini kutoka Gereza la Keko mwaka 1983.

Mwenyekiti wa sasa wa Bodi ya Parole anatajwa kuwa miongoni mwa mawaziri wachache wa wizara hiyo waliodumu kwa zaidi ya miaka mitatu (1990-94).

Hata hivyo kasi ya utendaji wake na ufuatiliaji wa mambo bila kuchoka ulimfanya kupunguzwa makali kinamna baada ya kuteuliwa kuwa Naibu Waziri Mkuu, cheo ambacho hakikupata kuwapo kikatiba  na hata sasa hakipo.

Baadae Mrema alikuja kuvuliwa uwaziri wa Mambo ya Ndani na kupewa wizara nyingine ndogo hatua iliyomfanya ajiuzulu uwaziri na kujiunga na chama cha upinzani cha NCCR-Mageuzi mapema mwaka 1995.

Pamoja na kazi nzuri ya kupunguza uhalifu kwa muda mfupi, Mrema pia alipata kukutana na kadhia ya kusigana na Waislamu mwaka 1993 baada ya kusimamia uhalali wa mabucha ya nyama ya nguruwe jijini Dar es Salaam.

Mawaziri wengine wa wizara hiyo waliokutana na kadhia mbalimbali ni pamoja na Ramadhani Mapuri (2003-05). Mapuri alijikuta akigombana na vyombo vya habari baada ya kugoma kuwachukulia hatua baadhi ya askari Magereza walipowapiga waandishi wa habari waliokwenda Ukonga kupata habari zilizohusu zoezi la bomoabomoa ya nyumba za jirani na Gereza la Ukonga.

Muhammed Seif Khatib (2000-03) yeye pamoja na wizara yake walikumbwa na kashfa ya vifo vya Mahabusi 35 waliokufa baada ya kukosa hewa katika Mahabusu  ya  kituo cha polisi cha Rujewa, mkoani Mbeya mwaka 2002.

ORODHA KAMILI

Hii ndio orodha ya Mawaziri wa Mambo ya Ndani tangu 1961.

 1. George Kahama – 1961
 2. Oscar Kambona – 1962
 3. Lawi Sijaona – 1962
 4. Job Lusinde – 1966
 5. Saidi Maswanya – 1967-73
 6. Omary Muhaji – 1973-74
 7. Ali Hassan Mwinyi – 1975-76
 8. Hassan N. Moyo – 1977-78
 9. Dr Salmin A. Juma – 1979-80
 10. Abdalla Natepe – 1980-83
 11. Muhidin Kimario – 1983-89
 12. Nalaila Kiula – 1990
 13. Augustino L. Mrema – 1990-94
 14. Ernest Nyanda – 1995
 15. Ali Ameir Mohammed – 1995-99
 16.  Muhammed S. Khatib – 2000-02
 17.  Omar R. Mapuri – 2003-05
 18. John Z. Chiligati – 2006
 19. Joseph J. Mungai – 2006-08
 20. Lawrence K. Masha – 2008 -2010
 21. Shamsi V. Nahodha – 2010-2012
 22. Dk Emanuel Nchimbi-2012
 23. George Mkuchika – 2012 – 2015
 24. Charles Kitwanga – 2016
 25. Mwigulu Nchemba – 2016 – hadi sasa.