Home Habari MFUNGO WA RAMADHAN KUWA MGUMU

MFUNGO WA RAMADHAN KUWA MGUMU

316
0
SHARE

NA WAANDISHI WETU


ZIKIWA zimesalia siku chache kabla ya kuanza kwa mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa waumini wa dini ya kiislam nchini na duniani kwa ujumla, bei za vyakula hususani nafaka kwenye baadhi ya masoko makubwa imeendelea kupaa licha ya msimu wa mavuno kukaribia.

Uchunguzi uliofanywa na RAI kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Iringa umeonyesha kupaa kwa bei kwenye maeneo mengi, huku baadhi ya masoko yakiwa na nafuu ya bei.

Mathalani soko la Manzese jijini Dar es Salaam, bei ya mahindi imeonekana kushuka kutoka 1,100 ya awali kwa kilo moja hadi kufikia Sh 750 hadi 900 kwa kilo moja.

Hata hivyo bidhaa kama Maharagwe, mchele, kunde, choroko na  mbaazi bei yake imeonekana kukwea kidogo.

Katibu wa Umoja wa madalali wa mahindi (UMA) kwenye soko hilo, Salum Abdalla alisema angalau kuna kumeanza kuwa na nafuu kwenye mahindi.

Alisema nafuu hiyo imesababishwa na kuongezeka kwa mavuno hali iliyochangia upatikanaji mkubwa wa bidhaa hiyo.

“Kwa sasa tunashukuru Mungu  mfumuko wa bei ya mahindi umepungua, awali tulifikia hatua ya kuuza kilo moja ya mahindi kwa Sh. 1,300, lakini sasa ni afadhali tumetoka kwenye bei hiyo sasa hivi tunauza kwa kati ya Sh. 100-750 kwa kilo,” alisema Abdalla.

Kuhusu bei ya unga wa mahindi kuendelea kuwa juu kwenye maduka ya kawaida alisema, hayo ni makudusi ya wafanyabiashara tu, lakini kwa sasa bei inapaswa kushuka.

“Mikoa mbalimbali kwasasa inatoa mahindi, hata madukani hawana budi kushusha bei za unga kwani wao wanachukua hapa kwa bei rahisi, lakini bado wanaendelea kuwakandamizi watanzania, tunategemea wauza unga wa mahindi watashusha bei hasa katika kipindi cha kuelekea mfungo wa Ramadhani,” alisema Abdala.

Hata hivyo uchunguzi wa Rai umebaini kuwa bei ya baadhi ya bidhaa muhimu zinazotumika sana kwenye mfungo wa Ramadhani bado ziko juu, huku nafuu ikipatikana kwenye mchele pekee.

Baadhi ya maduka jijini Dar es Salaam kilo moja ya unga imefikia kati ya Sh 2,000 hadi 2,300 hali inayopelekea kundi kubwa la familia hasa zisizokuwa na kipato cha uhakika kuhamia kwenye matumizi ya mchele.

 

IRINGA MCHELE BEI JUU

 

Wakati jijini Dar es Salaam, mchele ukionekana kuwa mwokozi wa wengi, mkoani Iringa hali ni tofauti kwani bei ya  unga  wa  sembe imeshuka huku bei ya mchele na viazi  mviringo ikipaa.

 

Kwa mujibu wa wasagishaji wa unga kutoka mashine ya  usagishaji  unga ya  DC iliyopo kata ya Makorongoni alisema,  kilo moja ya unga wa dona inauzwa kwa Sh. 1,40031,000 kutoka  Sh. 1,600 ya awali.

 

Mfanyabiashara  wa mchele   katika  soko la Mashine tatu Mathew Nyinge   alisema  kuwa  kwa  sasa bei ya mchele  kwa  kilo ni kati ya   Sh. 2,200 wakati  awali  mchele  kilo  moja  ulikuwa kati ya Sh.2000 hadi Sh.1970.

 

 

Juma Hassan anayejihusisha na biashara ya viazi mviringo, aliliambia RAI kuwa kwa sasa  ndoo ya viazi yenye ujazo wa lita 20  inauzwa  kwa Sh. 13,000 kutoka  bei ya wali  ya  Sh. 11,000.

 

Mbali na mfumuko wa bei za bidhaa, lakini pia mfungo wa mwaka huu unakuja huku baadhi ya wafungaji wake wakikabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo ukata uliosababishwa na hatua ya kupunguzwa kazi na wengine kuamua kuacha kazi kutokana na sakata la vyeti feki.

 

Mbali na hatua hiyo ya baadhi ya wafungaji kukosa kazi, lakini pia kunadaiwa kuwapo na kuyumba kwa biashara, hatua inayosukuma baadhi ya wafanyabiashara kufunga biashara.

Habari imeandaliwa na Faraja Masinde na Francis Godwin