Home Habari UFINYU WA BAJETI KUKWAMISHA TANZANIA YA VIWANDA

UFINYU WA BAJETI KUKWAMISHA TANZANIA YA VIWANDA

242
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI


WAKATI sekta ya kilimo na viwanda zikielezwa kutegemeana baadhi ya wachumi na wachambuzi wa masuala ya kilimo wamebainisha kuwa bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi haitoweza kutimiza ndoto ya Tanzania ya viwanda. RAI linaripoti.

Hatua hiyo imekuja baada ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti yake kwa mwaka 2017/18  ambayo badala ya kuongezeka sasa imepungua kwa Sh. bilioni 7.198.

Waziri Tizeba, ameliomba Bunge kumpitishia kiasi cha  Sh bilioni 267.865 tofauti na mwaka wa fedha unaoishia mwishoni mwa mwezi ujao, ambapo wizara hiyo ilitengewa Sh bilioni 275. 063.

Pamoja na pungufu hiyo, lakini pia bajeti inayoishia Juni 30, haikutekelezwa kwa asilimia mia kwani hadi kufikia Mei, serikali ilikuwa imetoa asilimia 3.31 pekee ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge la bajeti la mwaka jana.

Katika bajeti hiyo mpya waziri alibainisha kuwa sekta ya kilimo imetengewa Sh .bilioni 214.815. Alisema Sh bilioni 64.562 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh. bilioni 150.253 ni kwa matumizi ya maendeleo.

Itakumbukwa kuwa katika mwaka wa fedha wa 2016/17, Sekta ya kilimo ilitengewa Sh bilioni 210.359. Matumizi ya kawaida yalikuwa Sh bilioni 109.831 na  fedha za maendeleo Sh bilioni 100.527, lakini hadi kufikia mwezi huu ni Sh bilioni 3.369 (asilimia 3.31) ndizo zilizotolewa.

Licha ya Dk. Tizeba kubainisha kuwa Serikali imefuta kodi, tozo na ada 108 zilizokuwa kero kwa wakulima, wafugaji na wavuvi nchini baadhi ya wachumi wamesema kuwa kupunguza tozo na ada si dawa pekee ya kuboresha sekta ya kilimo nchini.

Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa Hadji Semboja, aliliambia RAI kuwa bajeti kuu ya Serikali inatakiwa kuelekeza nguvu katika kuiboresha sekta ya kilimo.

“Ninachoona hapa, makosa yapo kwa watoa taarifa na watoa elimu, hasa wanapotaka kutoa taarifa kuhusu bajeti kwa ujumla. Bajeti ni utaratibu ambao upo kisheria wa mapato na matumizi ya kisheria, bajeti inatumika kuiwezesha serikali kutumia rasilimali zake vizuri kwa wananchi.

“Uwezo wa serikali kutotoa huduma nzuri kwa sekta ya kilimo si suala geni, halijawahi kutekelezwa kwa kiwango kinachotakikana ingawa Mwalimu Nyerere naye alihusika sana katika kusisitiza kilimo.

“Si Tanzania pekee, nafikiri nchi nyingi za kimasikini zina mkazo wa kilimo ila bajeti zake hazijaweza kuwezesha utekelezaji wa nguvu katika kuboresha sekta ya kilimo. Tangu kipindi cha Mwalimu alikuwa akipiga kelele kuhusu suala hilo.

“Hata hivyo watoa taarifa wanapaswa kuweka mchanganuo vizuri kwamba fedha za miundombinu kama vile barabara, maji na mingine pia zinasaidia ukuaji wa sekta ya kilimo,” alisema.

Aidha, alisema sekta ya viwanda inaihitaji sana sekta ya kilimo hivyo Serikali ilitakiwa kutilia mkazo sekta ya kilimo ili kutimiza ndoto ya Tanzania ya viwanda.

“Hizi sekta mbili zinategemeana, lakini tukiangalia viwanda vilivyopo sasa hakuna vinavyomilikiwa na watanzania ambavyo vinaunga mkono masuala ya kilimo kwa asilimia 100, tukiangalia katika asilimia 100 karibu asilimia 85 ni shughuli ambazo zinatekelezwa na mtu mmoja hadi wanne, wanatumika kupanga au kuboresha shughuli za uzalishaji.

“Viwanda vya kisasa ni asilimia mbili tu, kwa hiyo matatizo ya kilimo si kwenye bajeti tu ni mfumo wa maendeleo ya sekta ya viwanda ambayo hayatoshi kuvutia sekta ya kilimo.

“Na hata fedha zilizoelekezwa viwandani hazitoshelezi, hivyo hata kilimo hakiwezi kuendelea kwani haivutii maendeleo ya sekta hiyo. Kwanza kilimo chetu hakikopesheki kwa sababu si cha kibiashara, pili kinategemea mvua, si cha umwagiliaji, nguvu kazi inadorora kadiri siku zinavyozidi kwenda, vijana wenye nguvu wanakimbilia mijini na vijijini kunabaki familia dhoofu ambazo haziwezi kuzalisha kilimo cha kibiashara, ni vijiji vichache ambavyo vinazalisha kibiashara kwa mfano Kahe – Moshi, vijana wanalima mpunga, hivyo hawakimbilii mijini kwa kuwa wanapata kipato kikubwa kuliko hata walioajiriwa.

“Suala la viwanda kukua sidhani kama litawezekana kwa sababu hata vilivyopo si vya Watanzania ambao ni wazalendo, kwa maana kundi la watu weusi halipo hata katika orodha  ya Watanzania matajiri.

“Tukiangalia bei za mahindi bado zipo juu, kwa hiyo kipato cha Watanzania asilimia 70 kinategemea kiimo na huko ndiko hali ni duni. Inabidi kutengenezwe utaratibu utakaosaidia  kuvutia Watanzania kujikita kwenye kilimo.” Alisema mfumo mzima wa bajeti unatakiwa kutengeneza mazingira wezeshi kwa wakulima kuhamasika kuendelea kuzalisha. Pia Serikali isiweke ugumu kwa Watanzania kuuza mazao yao ndani na nje ya nchi.

“Mkulima mmoja mmoja akilima mazao yake anatakiwa apate fursa ya kutafuta masoko,” alisema.

Hoja ya Profesa Semboja iliungwa mkono na  aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti ya Kuondoa Umaskini Tanzania (REPOA), Profesa Samuel Wangwe ambaye alisema serikali imeonesha dhahiri kutokuwa na nia ya dhati katika kuendeleza sekta ya viwanda.

“Kilimo na viwanda ni vitu viwili vinavyotegemeana pakubwa, hivyo kama wameibana kiasi hicho sekta ya kilimo hakika suala la kukua kwa sekta ya viwanda itakuwa ngumu sana kwa sababu wakulima wanahitaji viwanda kuuza mazao yao,” alisema.

Akichangia bajeti ya Wizara hiyo Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo), alisema changamoto kubwa ya Tanzania ni kutokubadilika kimaendeleo kwa sekta ya kilimo wakati bado inaajiri watu wengi  nchini.

“Asilimia  65.5 ya watanzania wote kama alivyotueleza Waziri hapa inategemea kilimo. Hiki ndicho kiini cha umasikini wa Tanzania. Tatizo kuu la msingi ni uwekezaji mdogo kwenye Kilimo, tumeona wenyewe hapa bungeni, kati ya bilioni 100.53 za bajeti ya Maendeleo ya Wizara hii, Waziri amelieleza Bunge kuwa mpaka Mei 4, 2017 Wizara imepokea Sh. bilioni 3.34, sawa 3.31%. Hii ndiyo changamoto ya msingi ya sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi, uwekezaji hafifu.

“Ni dhahiri kuwa Serikali haina fedha, hata hayo makadirio ya bajeti ya maendeleo ya bilioni 150 yanayoletwa na Wizara hii ili tupitishe kwenye bajeti hii ya mwaka ujao wa fedha (2017/18) ni ni makadirio hewa, uwezo wa utekelezaji ni mdogo kwa kuwa hakuna fedha na Waziri hajatuonyesha miujiza mipya anayoweza kufanya ili kuhakikisha upatikanaji wa fedha zaidi za miradi hii ya maendeleo.

“Mwaka jana wakati wa mjadala wa bajeti ya wizara hii, nilielekeza mchango wangu katika kufungamanisha sekta ya Viwanda na sekta ya Kilimo. Bado nasisitiza umuhimu wa kuweka nguvu kubwa kwenye uanzishwaji wa viwanda vya bidhaa za kilimo (agro – processing industries) ili kuongeza thamani ya mazao ya wakulima wetu, kutumia malighafi ya ndani, na hivyo kuzalisha ajira za kutosha nchini. Hata hivyo, mwaka huu nitajielekeza kwenye kufungamanisha sekta ya Kilimo na Hifadhi ya Jamii nchini.

“Ushauri wangu kwa Wizara ni kutafuta chanzo kipya cha ndani cha Uwekezaji mkubwa kwenye Kilimo, chanzo hicho ni Mifuko ya hifadhi ya Jamii. Ili kupata fedha za kutosha kuwekeza kwenye Kilimo hatuna budi kuongeza uwekaji akiba nchini, njia sahihi ya kufanya hilo ni kuzifungamanisha sekta za Kilimo, Uvuvi na Ufugaji na hifadhi ya jamii.

“Uwekaji akiba nchini hivi sasa ni mdogo kwa kiwango cha 16% tu ya Pato la Taifa wakati nchi kama China wananchi wao huweka akiba mpaka 50% ya Pato la Taifa.

Hivyo basi, Hifadhi ya Jamii kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wote walio katika sekta isiyo rasmi inaweza kuwa moja ya njia imara za kuongeza uwekaji akiba nchini na kuwalinda watu kwenye makundi hayo dhidi ya majanga ya kiuchumi na kijamii,” alisema.