Home Makala ETI, CHRYSOSTOM UMEFARIKI

ETI, CHRYSOSTOM UMEFARIKI

138
0
SHARE

HIVI ni kweli! Eti mwandishi nguli wa safu hii ya ‘Nilonge Nisilonge’ ambaye pia ni Mwalimu wa wengi kwenye tasnia ya Habari, Chrysostom Rweyemamu amekufa!

Mmmhh…!!! Napata hofu juu ya hili, kuna uthibitisho wowote wa taarifa hizi? Isije ikawa ni uzushi tu wa mitaani, maana siku hizi suala la kuzushiana kifo limekuwa la kawaida sana.

Hapana hizi ni taarifa za kweli, ni taarifa sahihi zisizo na chembe ya shaka, zimethibitishwa na familia yake na hata viongozi wenzake wa ofisini kwake alikokuwa akifanya kazi hadi alipokutwa na mauti.

Eti, wanadai huenda leo hii mwili wake ukahifadhiwa kwenye nyumba yake ya milele huko kijijini kwao Muleba mkoani Kagera.

Kwani ilikuwaje mpaka nguli huyu akatutoka!! Aaaah… ni habari ndefu, lakini watu wake wa karibu eti, wanadai alikuwa mgonjwa, lakini Nilonge Nisilonge inashangazwa na taarifa hizi za kifo chake kwa sababu hakupata kuonesha kuwa ni mgonjwa wa kufa leo wala kesho, maana hakuwa dhaifu wa mwili wala akili.

Narudia Chrysostom, maarufu kama Mwalimu nguli na gwiji la Habari nchini, hakuwa mgonjwa wa kumfikiria kuwa atakufa leo au kesho, alikuwa na afya yake, alionekana kuwa imara nyakati zote hata pale alipokuwa akilalamika kusumbuliwa na maradhi ya sukari.

Hakuonesha kuishiwa matumaini ya kuishi, bali alisononeshwa na namna ugonjwa wa sukari ulivyomlazimisha kuondoka kwenye maisha yake ya kawaida na kuhamia kwenye maisha yasiyo na ka bilauri ka bia, ka nyama ka kuchoma na vipochopocho vingine alivyokuwa akivipenda kama vile ndizi Bukoba na mahindi ya kuchoma aliyokuwa akiyafuata kwa miguu yake nje ya geti la ofisini kwake.

Hayo ndiyo yalikuwa masononeko yake makubwa,lakini pia alishaamua kukabiliana nayo na tayari alishayamudu, maana alipunguza na baadae kuacha kabisa ka bia, ka nyama ka kuchoma na hata chai yake haikuwa yenye sukari tena, badala yake alikuwa akitembea na mfuko wake uliokuwa na kikopo cha asali.

Eti, leo Chris ni marehemu na hatutamwona tena, hatutamwona tena akiwa amevalia pama lake ambalo alikuwa akilitumia zaidi nyakati za jua kali.Nimefurahi kuona familia yake imemsindikiza kwenda Kagera akiwa na pama lake kichwani, sina hakika kama lile ndilo pama alilokuwa akilipenda zaidi, lakini angalau linamfanano na lile nililowahi kumuona akilivaa mara kwa mara.

Hatutamwona tena Mwalimu, hatutamwona akiwa ndani ya mashati yake ya vitenge na suruwali zake pana zilizomkaa mwilini barabara, hatutamwona Mwlaimu akiwa anapanda na kushuka ngazi za kuelekea ofisini kwake huku akitembea kwa mwendo wa pole uliokuwa ukimlazimisha kuinua miguu yake taratibu mithili ya mtu aliyekuwa akiiburuza.Eti, Chrysostom amekufa, amekufa bila hata kusema ni nani aanamwachia jukumu la kuiandika safu yake ya Nilonge Nisilonge. Hajaacha wosia kwa kweli.

Ingawa niliwahi kujaribu kuiandika safu hii kama nilivyojaribu leo, sikuweza sawa sawa, maana alinieleza kuwa nimejitahidi, lakini bado. Pamoja na kuniambia kauli hiyo, lakini hakuwahi kuniambia niongezee bidii kwenye eneo gani ili niweze kutosha kwenye viatu vyake.

Huenda hakuniambia kwa sababu aliamini bado ana muda mrefu wa kuiendeleza safu yake ambayo binafsi natamani iendelee, kwa sababu kwangu ndio itakuwa njia pekee nay a kweli ya kumkumbuka, lakini sina hakika kama nitatosha kwenye viatu vyake hivi vikubwa.

Mwalimu hataonekana tena akiwa ndani ya gari yake aina ya Prado, ambayo katika kipindi chake cha mwisho alilazimika kuiacha nyumbani kwake Mbweni, jijini Dar es Salaam na kutembea kwa miguu kwa sababu alitakiwa kufanya hivyo ili kuupa mwili wake mazoezi.

Awali hatua hiyo ilimsononesha, lakini baadae aliizoea na kuifurahi na hakuona tabu kutembea kwa umbali hata wa kilomita tatu mpaka tano.

Chris, amekufa katika kipindi ambacho chumba cha Habari cha New Habari (2006) Ltd kikimuhitaji sana kuliko yeye alivyokihitaji.

Amekufa akiwa na umuhimu mkubwa kwa waandishi wa habari wa NHL kutokana na uwezo wake wa kusimamia maudhui bora na sahihi ya habari.

Hakuwa mtu wa kupenda kuona mwenzie anaangamia, alikuwa ni mtu mwenye kupenda kuona kila mtu ndani ya Tasnia ya Habari, anafikia kiwango cha kuwa Mwandishi au Mhariri bora.

Pamoja na ukongwe, uzoefu na umri wake wa miaka 63, Mwalimu aliendelea kuandika na kuhariri pale alipopata nafasi ya kufanya hivyo, tofauti na ilivyo kwa baadhi ya wakongwe ambao kwao jambo muhimu ni kukosoa maandiko ya wenzao bila wao kuonesha mfano kwenye maandiko wanayopaswa kuyaandika kwa mikono yao.

Katika kuhakikisha kuwa haachio kuandika, Mwalimu alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha safu hii ya Nilonge Nisilonge, inatoka katika kila toleo na ilipoacha kutoka bila sababu za msingi aliumia maumivu yaliyomsukuma kuhoji ili kupata majibu toshelezi.

Hakupenda kuona magazeti ya RAI, MTANZANIA, BINGWA na DIMBA yanachezewa, yanabeba makosa aliyoyaita ya kipuuzi, alipenda kuona magazeti yote ya NHL yanabeba habari nzuri na zenye maudhui yanayokidhi haja ya msomaji.

Mwalimu alikuwa mjuzi wa lugha, alikijua Kiswahili kwa ufasaha na alikijua Kiingereza kwa uzuri kabisa, uwezo huo wa kujua lugha ulimfanya kuwa kamusi ya wengi ndani na nje ya New Habari.

Kwa sababu ya hulka yake ya kupenda vitu vizuri, alijitahidi kuhakikisha anachokijua yeye basi kinawaingia wengi – iwe ni kwa wakati mmoja au kwa nyakati tofauti.

Inastaajabisha kuambiwa eti, leo hii Chrysostom ni marehemu na hatainuka tena kuja kusimamia postmortem ya magazeti yanayozalishwa na NHL.

Mwalimu, hataonekana tena kwenye vikao vya mpango kazi vya kila siku vilivyokuwa vikiwahusisha wahariri pekee, vikao ambavyo ni Mwalimu pekee, aliyekuwa mstari wa mbele kuandika kila habari iliyokuwa ikijadiliwa kwa siku hiyo.

Hakuona ugumu hata kidogo kubeba ka ‘notebook’ kake kadogo na kalamu yake katika kila kikao hata kama kingekuwa kikao kifupi cha namna gani, alijitahidi kuhakikisha ananukuu masuala muhimu ya siku hiyo.

Mwalimu alikuwa akiuishi ualimu, alikuwa akifurahia kufundisha, alijitahidi kutoa maelekezo popote pale alipoona kuna kasoro na alipongeza pale alipoona panastahili pongezi.

Leo, Mwalimu amelala kimya, kimya kabisa, hapumui, hatikisiki wala hasemi chochote. Chrysostom,bahati mbaya amekufa akiwa na ndoto moja tu, ambayo nadiriki kuisema kuwa naijua na alishapata kunieleza yeye mwenyewe mara kadhaa.

Ndoto yake kubwa ilikuwa ni kuona darasa la Maarifa Media Trust (MAMET) linarejea, alitamani hivyo kwa sababu alinieleza wazi wazi kuwa darasa hilo lilikufa kifo cha kulazimishwa na walioliua anawajua na alikuwa akiwachukia kwa sababu waliliua kwa sababu ya chuki zao kwake.

Siri kubwa ambayo hii sitaisema popote ni kutaja majina ya watu walioshiriki moja kwa moja kuiua MAMET.

Pamoja na MAMET kuuawa kwa hila kamwe hakukata tamaa, badala yake aliamini iko siku darasa lake hilo lingerejea na angezalisha tena waandishi wa Habari bora kabisa.

Pamoja na madhaifu yake ya kibinadamu, ukweli ni kwamba Mwalimu anabaki kuwa alama ya ushujaa kwenye tasnia ya Habari nchini, amezalisha waandishi wengi ambao leo hii ni bora kwenye maeneo yao ya kazi.

Katika kuhakikishi kipawa alichopewa na Mungu wake anakigawa kwa wengine, alifanikiwa kushiriki moja kwa moja au kwa mawazo, matendo na hata wakati mwingine kutumia fedha zake kuanzisha vyama vya kitaaluma, kikiwemo Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET).

Bahati mbaya Mwalimu amemaliza safari yake ya hapa duniani, ameimaliza kwa kuacha nyayo ambazo ni jukumu letu tuliofanikiwa kupitia mikononi mwake kwa kutufundisha darasani au nje ya darasa, kuzifuata nyayo hizo.

Ni jukumu letu kuhakikisha tunayaenzi mema yake kwa vitendo, pengine kifo cha Chrysostom kiwe darasa kwa wanahabari wote kutambua kuwa kifo kipo na tunachotakiwa kufanya ni kutenda mema ili kuacha alama ya ushindi duniani.

Leo hii Chrysostom analiliwa na wengi kwa sababu aliwatendea mema watu wengi, haimaanishi kama hakuna aliowaumiza, lakini ukweli unabaki kuwa waliotendewa mema ni wengi kuliko walioumizwa nae.

ROHO YA MAREHEMU ILAZWE MAHALA PEMA PEPONI AMIN.