Home kitaifa RAIS MAGUFULI APONGEZWA

RAIS MAGUFULI APONGEZWA

180
0
SHARE

NA   FRANCIS  GODWIN, IRINGA


UAMUZI wa Rais John Magufuli kumteua Mwenyekiti  wa Taifa  wa  chama  cha  ACT – Wazalendo, Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, umeonekana  kuwagusa viongozi wa dini na wanasiasa mbalimbali nchini.

Wanasiasa na viongozi hao wa dini wameenda mbali zaidi na kusema kuwa uteuzi huo umeunganisha Watanzania  kwani ameonyesha kuvuka mipaka ya Demokrasia  iliyozoeleka  ndani ya  Chama  Cha Mapinduzi (CCM)  kwa  kuifanya  Serikali yake  kuwa ya  Watanzania  wote.

Wengi  wanadai kuwa demokrasia  iliyokuwa  ikisubiriwa kwa shauku  kubwa ya kuona Serikali inakuwa ya wote na si ya chama kimoja imeanza kuonekana kwa Rais  Magufuli  kavunja  mwiko .

Naibu  katibu  mkuu wa CCM -Tanzania  Bara,  Rodrick Mpogolo akiwa  mkoani  Iringa katika mazungumzo yake na wanachuo wa  vyuo mbalimbali alisema bado Rais Magufuli anauwezo mkubwa wa  kushinda  kwa  kishindo kwenye uchaguzi mkuu  mwaka 2020 kutokana na kuonekana kuwa kiongozi wa wote.

Mpogolo alisema nguvu ya  vyama  vya  upinzani kwa  sasa  haipo na ambae amekifanya chama kuwa na heshima  kubwa ni Rais Magufuli ambae  kupitia  utawala  wake  hivi  sasa  kila mmoja anaipenda  serikali ya  CCM .

Alisema njia  pekee ya  kuendelea  kumsaidia rais Dkt Magufuli ambae ni Mwenyekiti wa CCM Taifa  ni  vijana na Watanzania  wote  kufanya kazi kwa  juhudi na kusimama  kwenye  uzalendo  zaidi  badala ya kuwaza  vurugu na maandamano yanayohamasishwa na baadhi ya  wapinzani.

Aidha, aliyekuwa Katibu wa  Chadema- Kanda ya  Nyasa, Frank  Mwaisumbi, anasema  kuwa  wanaomchukia Rais wana yao ila  teuzi   alizozifanya zinaungwa mkono na kila Mtanzania  mpenda  Demokrasia.

” Uteuzi  wa Anna Mghwira    ni uteuzi  ulioonyesha  kiwango cha  juu  cha  Demokrasia  na uzalendo  ambacho rais  wetu  ameonyesha  kuwa  kila Mtanzania   mwenye sifa  anaweza  kutumikia jamii inayomzunguka ….kweli mimi si mnafiki  nampongeza  sana  Rais kwa   uteuzi  alioufanya.”

Alisema  mwenendo  wa  teuzi zinazoendelea ndani ya serikali ya  awamu ya tano  ni zenye  tija  kubwa kwa maendeleo ya  taifa  letu na  zenye  kuleta maana  sahihi ya  siasa ndani ya Tanzania na Afrika  .

” Kinachofanyika  ndicho  tulikuwa tunahitaji  japo  wengi  wetu  tulichelewa  kumuelewa JPM ila  sasa  kila mmoja anamuelewa  vizuri  zaidi kuwa alichokisema anakifanyia kazi, “alisema.

Kiongozi wa kanisa la  Orthodox mkoa  wa Iringa  Fr. Cleopas Bachuba alisema   kuwa akiwa kama  kiongozi  wa kanisa  hilo  anapongeza hali ya amani iliyopo nchini na kwamba  katika  kipindi  cha  serikali ya awamu ya tano  hakuna maandamano  yaliyofanywa na vyama.
Alisema kitendo cha Rais  kuchanganya  watendaji kazi wake mfano kwa  kumteua mkuu wa mkoa wa  Kilimanjaro  kutoka chama cha  ACT Wazalendo ni hatua  nzuri ya  kuelekea  katika  Demokrasia  ya  kimaendeleo ambayo kila mmoja alikuwa akiisubiria kwa hamu kubwa .

” Sisi kama  viongozi wa  dini  mimi na wenzangu  kazi yetu  kubwa ni kuendelea  kumuombea  Rais wetu na  serikali yake  ili  umoja na mshikamano na amani  izidi  kutawala  na kwa  kufanya hivyo matunda ya nchi  hii  yatakuwa  faida kwa  watanzania  wote na  vizazi vijavyo”

Kiongozi huyo  alisema  pamoja na  kuwa  chama  chake ni Biblia na kanisa kwa maana ya  kuwaombea  watu  wote  ila iwapo  serikali iliyopo madarakani  haitakuwa na  demokrasia  nzuri kama  hii ya  sasa  bado  hata  waliopo makanisani  hawatakaa kwa amani  hivyo  wajibu  wa  viongozi  wote ni  kuongoza jamii kwa amani  zaidi .

Kada wa Chadema  mkoa wa Iringa, Wito  Msafiri alisema uteuzi huo anaupongeza  sana kwani kwa  kufanya  hivyo hata maendeleo katika nchi yataendelea  kuwepo  iwapo   watu  wazuri  ambao  wanaweza  kuongoza jamii bila kujali itikadi za  vyama  vyao wataendelea  kupewa nafasi .

” Unapokuwa  mkuu  wa nchi  lazima  uzingatie Katiba ya  nchi  inasema  nini  hivyo anapoamua kuteua  watu  kutoka nje ya  mfumo  wa CCM uliozoeleka  si kosa, yupo  sahihi.

Hata hivyo, Msafiri  alisema  ni  vema  walioteuliwa  wote  kutangaza  kujiuzulu  nafasi  zao  za  siasa  ili  kubaki kuwa viongozi  huru  kuliko  kuwa  makada  wa  vyama kwa  kuifanyakazi ya  umma  huku  wakiwa ni viongozi wa  vyama  hivyo  japo haiwazuii  kuwa  viongozi  wa vyama vya  siasa na  serikali .

“Mwaka  2012 ndani ya  CCM kulikuwa na wazo la  kutenganisha  Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais ila  tumekuwa  tukishuhudia  Rais  wetu akiwa majukwaani akitamka  wazi  kuwa  Watanzania  wana bahati ya kuwa na Rais ambae sio mwana siasa ni  mtendaji  zaidi “

Wito alisema  kuendelea  kuteuliwa kwa makada  wa vyama vya upinzani bado si tatizo kwa  uhai wa vyama  vya upinzani kwani  wapo  wanachama wa upinzani ambao wanafanya kazi ya  siasa katika vyama  vyao  ila  wanafanya  hivyo kwa ajili ya kujionyesha  ili  kuweza  kutafuta nafasi  za kuteuliwa katika serikali na  kuwa japo kuteuliwa kwa wapinzani  ndani ya  serikali ya  CCM ni anguko  jingine kwa  wana CCM ambao  walikuwa  wakisubiri kuteuliwa  katikanafasi  hizo .

Hilda Maungu ni  mmoja kati  ya  wasomaji  wa  gazeti hili la RAI kutoka wilaya ya Tanga mjini  mkoa  wa Tanga akitoa  maoni  yake  juu ya   teuzi  mbali mbali  zinazofanywa na  Rais alisema  kuwa wao  kama  wananchi  wa  kawaida  wanachokiona ni  kuwa rais  amejitofautisha  kwa  kiasi  kikubwa na  watangulizi  wake  na yupo kwa ajili ya kuona taifa  linasonga  mbele  na  ndio maana anateua hata waliopo  upinzani ila  wenye  moyo  wa kuwatumikia  watanzania .

Aliyewahi kuwa kada  wa  vyama vya CCM , NCCR  Mageuzi  na  Chadema Mzee  David  Butinini  alisema  kwanza wajibu  wa Rais  chini ya  ibara  ya  38  anapaswa kufanya  uteuzi  mbali mbali  ikiwa ni pamoja na kuteua  wakuu wa mikoa na wabunge wa kuteuliwa .

Katibu  wa  UVCCM mkoa  wa Iringa  James Mgego  alisema  kuwa  uteuzi  huo umepokelewa  kwa shangwe  na  vijana  wa mkoa wa Iringa  na  kuwa  wale  wanaobeza wanashindwa  kutambua  kuwa  Rais  ni  wa  Watanzania  wote  na hapangiwi nani  wa  kufanya nae  kazi  ya kuwatumikia Watanzania .