Home kitaifa UJUMBE MZITO WA NDESAMBURO KWA SERIKALI

UJUMBE MZITO WA NDESAMBURO KWA SERIKALI

186
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU


MWANZONI mwa wiki iliyopita, Taifa lilizizima baada ya kupokea taarifa ya kifo cha mwanasiasa na mwanamageuzi wa kweli wa siasa za upinzani, Dk. Philemon Ndesamburo.

Ndesamburo ambaye mpaka mauti yanamkuta alikuwa ni mfanyabiashara na Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia ya Maendeleo (Chadema), pia aliwahi kuwa mbunge wa jimbo la Moshi mjini kwa vipindi vitatu mfululizo.

Siku moja kabla ya mauti kumkuta mwanasiasa huyo alituma makala yake kwenye gazeti hili iliyobeba ujumbe mzito kwa Serikali, akishauri njia za kupita ili kukinusuru Kilimo na kuifikia Tanzania ya viwanda.

Ujumbe huo aliuandika kwa mkono wake, huku akitoa rai ya kumvumilia kwani wakati mwingine uzee unamfanya kushindwa kuandika kwa utulivu.

“Naomba mnivumilie, nyakati nyingine nashindwa kuandika kwa sababu ya uzee, ila nitajitahidi kuhakikisha naandika kila ninapoiona haja hiyo,”huu ni ujumbe alioutuma mwenyewe.

UJUMBE WAKE

Serikali ya Rais John Magufuli inataka kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Ina maana kwa sasa Tanzania si nchi ya viwanda? Pengine  kwa sababu kuna viwanda vichache vilivyohoi au havipo kabisa?

Viwanda vilikuwepo enzi za utawala wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Watawala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliomrithi Nyerere, ndio walioua viwanda vyetu.

Vile viwanda alivyotuachia mwalimu, vingalikuwepo, kama nchi tungekuwa mbali sana kwenye sekta hii. Leo, tunalalamika kuanza upya kutokana na watawala wa CCM  kutoendeleza sera  ya viwanda. Viwanda vyetu vimefia mikononi mwa watawala wanaotokana na CCM.

Nilikuwa najaribu kukumbusha wasomi kuwa tulikuwa na viwanda vilivyofia kwa walewale wanaotaka kuvifufua leo. Hili nitalijadili kwenye makala nyingine nikipata nafasi wiki lijalo.(angelijadili wiki hii kama angekuwa hai)

Leo, ninachotaka kujadili  kwa faida ya wasomaji wangu ni  mambo mawili. Moja, ni njia  tunayopaswa kupitia ili kuelekea kwenye Tanzania ya viwanda na Pili, ni aina ya viwanda tunavyofikiria kuvianzisha na faida yake kwa wazalendo wa nchi hii.

Nikianza na jambo la kwanza, ninaona ni lazima tupitie njia ya kuboresha kilimo ili tufike kwenye Tanzania ya viwanda.

Ni muhimu  viwanda hivi,vikawa na uhusiano wa moja kwa moja na sekta ya kilimo inayoajiri Watanzania wengi.

Nimetembelea nchi nyingi duniani, ikiwemo Uingereza. Nimejifunza juu ya historia ya Mapinduzi ya viwanda ya uingereza karne ya 18. Uingereza ndio nchi ya kwanza duniani kuwa na mapinduzi ya viwanda.

Msingi wa mapinduzi ya viwanda nchini Uingereza ulikuwa ni mapinduzi ya kilimo (Agrarian Revolution.) Mapinduzi ya kilimo nchini uingereza yalichochewa na teknolojia, mitaji na miundombinu bora.

Kabla ya kutokea kwa mapinduzi ya kilimo, waingereza walipitia kwenye kipindi cha kujikusanyia mitaji na kuboresha huduma za kibenki kwa ajili ya kuwajengea uwezo wakulima.

Ukusanyaji wa mitaji, ulisabisha Uingereza kuwekeza kwenye ugunduzi wa teknolojia. Ugunduzi wa teknolojia ulikuwa muhimu kwa ajili ya viwanda na kilimo.Waingereza,walikuwa wamejikusanyia mitaji ya kutosha kuwekeza kwenye kilimo.

Nchi ya Uingereza, haikuwa na  ardhi kubwa, kwa hiyo wakulima mabepari wakubwa waliendesha uporaji dhidi ya wakulima wadogo ambao baadaye waligeuka nguvu kazi ya mabepari. Hakuna sababu ya uporaji kutokea Tanzania kwa sababu tuna ardhi ya kutosha.

Kilimo cha kutumia teknolojia ya kisasa nchini Uingereza kilileta tija kubwa katika uzalishaji wa malighafi wenye tija kwa ajili ya viwanda.Wakulima walitumia mbegu bora. Walitumia mbinu za kisasa kuzalisha,kuandaa na kutunza mazao.

Kwa sababu ya uwezo mkubwa wa kiteknolojia wakulima walikuwa hawategemei mvua pekee, bali walitumia rasilimali maji kuhakikisha mazao yao yanastawi.

Serikali ya Uingereza iliboresha vizuri miundo mbinu ya  usafiri kwa ajili ya kusafirisha mazao ya Wakulima kwenda kwenye masoko, viwandani.

Tanzania inafaa tupitie njia hii kama kweli tunataka kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda.Utashi wa serikali pekee hautoshi.

Ni lazima tutumie njia sahihi na mikakati sahihi.Tusiishi kwa kauli tu, bali tuangalie namna ya kuiendea njia na mikakati sahihi ili kutengeneza Tanzania ya viwanda. Matangazo na kauli ya Tanzania visiwe na nguvu kuliko mikakati na matendo.

Serikali ya Tanzania chini ya  Rais John  Magufuli iweke mazingira ya mapinduzi ya kilimo.Kama nchi, tunapaswa kuwa na mitaji ya kuwekeza kwenye kilimo cha teknolojia ya kisasa.

Wenzetu Waingereza,walijikusanyia mitaji na kuboresha mifumo ya kibenki kwa ajili ya wakulima. Tanzania ya Viwanda inahitaji mitaji kwa wakulima. Tuhakikishe mitaji hii inakuwa kwa wazawa kwa asilimia kubwa. Kuruhusu kiasi kikubwa kutoka nje itakuwa sawa na ukoloni mamboleo.

Sisi Watanzania tumshukuru Mungu daima, ametubariki kwa kutupa ardhi kubwa yenye rutuba na tunazungukwa na vyanzo vingi vya maji.

Lakini  rasilimali hizi hatujazitumia ipasavyo kutokana na ukosefu wa mitaji na teknolojia.

Napenda kusisitiza tena; ili  kufanikisha mapinduzi ya kilimo, tunahitaj mtaji  na kuwekeza kwenye kilimo cha kiteknolojia  sambamba na kuboresha miundombinu. Kuwaza Tanzania ya viwanda huku wakulima wengi wanaendelea kutumia zana duni ni mzaha mkubwa sana.

Wakulima wetu walio wengi wanatumia kilimo duni, wanaishi vijijini mahali ambako hakuna miundombinu bora.Wanategemea kilimo cha mvua za msimu. Mazingira haya hayawezi kuchochea mapinduzi ya kilimo.

Kama tunapitia njia ya kuboresha kilimo ili kuleta mapinduzi ya viwanda, basi mazao ya kilimo yatazalishwa kwa ajili ya viwanda vya hapahapa nchini. Hakutakuwa na haja ya nchi kuuza malighafi nchi za nje kwa hasara kama tulivyozoea kufanya hivyo toka enzi la ukoloni.

Viwanda vitakavyoanzishwa vikitegemea mapinduzi ya kilimo basi kutakuwepo uhusiano mkubwa wa viwanda vyetu na wananchi ambao wengi ni wakulima. Wananchi watamiliki uchumi wa taifa lao.

Jambo laPili, ninataka kushauri juu  ya aina ya viwanda tunavyotaka kuvianzisha. Serikali ijiepushe kuaanzisha viwanda vinatakavyohodhi uzalishaji wa kila kitu; kuanzia malighafi na bidhaa yenyewe.

Nina maanisha kuwa kuanzishwe viwanda vinavyozalisha bidha tu lakini viwanda hivyo vizungukwe na viwanda vidogo vinavyotengeneza vitu kwa ajili kuviuzia viwanda vikubwa. Kwa kimombo viwanda vinavyozunguka viwanda vikubwa vinaitwa backyard industries.

Kwa mfano, kama kutaanzishwa kiwanda cha kutengeneza nguo nchini.Kiwanda hicho kisihodhi uzalishaji wa kila kitu kinachotakiwa ni kutengeneza nguo tu.

Kiwanda kikubwa dhima yake iwe ni kutengeneza nguo iliyokamilika. Vitu vya lazima kwa ajili ya utengenezaji wa nguo vizalishwe na backyard industries.

Serikali  inaweza kuruhusu kuanzishwa kwa backyard industries ambazo zitazalisha vifungo vya nguo, nyuzi, au vitambaa kwa ajili ya kukiuzia  kiwanda kikubwa.Serikali isitoze ushuru kwa hizi backyard industries.

Kazi ya viwanda vikubwa ni kununua malighafi kwa viwanda vidogo na kutengeneza bidhaa.

Serikali ikianzisha viwanda vya aina hii, watu wengi watapata ajira nchini, viwanda vitakuwa chini ya miliki ya Watanzania wenyewe.Wananchi watamiliki uchumi wa viwanda wa taifa lao.

Kwa mfano, ilivyo hivi sasa kwenye kiwanda cha kuzalisha sukari cha TPC hapa Kilimanjaro, wakulima wamenyimwa ajira.

Kiwanda cha TPC kimehodhi mashamba na kinazalisha miwa chenyewe kwa ajili ya kuzalisha sukari. Watu wanaozunguka kiwanda hiki wanayatazama tu mashamba ya miwa inayotumika kuzalisha sukari.

Sasa kiwanda kama hiki ni mfano mbaya sana kwa viwanda kwa sababu kinapoka nafasi ya wananchi kujiajiri katika uzalishaji wa miwa na kukiuzia kiwanda.

Buriani Dk. Ndesamburo, RAI tunaamini ujumbe wako huu utafungua fikra mpya juu ya Tanzania ya viwanda.