Home Habari EAC ITAWEZA KUGUSA MAISHA YA WACHOVU?

EAC ITAWEZA KUGUSA MAISHA YA WACHOVU?

365
0
SHARE

Na Deus M Kibamba,

YAMEZUNGUMZWA mengi kuhusu Mkutano wa 18 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo Mwenyekiti anayemaliza muda wake, Rais, Dk. John Pombe Magufuli alikabidhi kijiti kwa Mwenyekiti anayefuata, Rais Yoweri Kagutta Museveni wa Uganda.

Wakuu wengine waliohudhuria ni pamoja na Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Burundi, Gaston Sindimwo, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masuala ya Afrika Mashariki wa Rwanda, Francois Kanimba na Mshauri wa Uchumi wa Rais wa Sudan Kusini, Aggrey Tisa Sabuni. Mkutano ulifanyika  Mei 20 mwaka huu.

Ukiacha suala la ushiriki usioridhisha kwa maana ya wakuu wa nchi wawili tu kushiriki Mkutano huo, huku nchi nne zikituma wawakilishi kwa ngazi ya Makamu wa Rais, Waziri hadi Mshauri wa Rais; Watu wengi wamezungumzia na kukosoa jinsi mkutano ulivyoshughulikia suala la Mkataba wa ushirikiano kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya, maarufu kama EPA uliozigawa nchi za ukanda huu hadi kufikia Rwanda na Kenya zikiukubali na kusaini wakati kundi la pili la Tanzania, Uganda na Burundi likikataa kutia saini, nao kwa sababu mbalimbali. Kama ilivyodhihirika, Umoja wa Ulaya ulikuwa umefanikiwa na kushindwa kwa wakati mmoja. Kufanikiwa, kwa sababu Rwanda na Kenya waliweza kulainika baada ya kufikiria maslahi ya Nchi zao zaidi badala ya maslahi ya kikanda ya Jumuiya nzima ya Afrika Mashariki.

Mpaka mkutano unakaa Dar es Salaam, Kenya ilikuwa imeshasaini Mkataba huo na kupelekea lengo la kujadiliana mkataba huo kwa pamoja ambalo EAC ilijiwekea miaka 10 iliyopita kuvurugika kabisa. Kwa upande mwingine, EU ilikuwa imeshindwa kuzishawishi nchi za Uganda na Tanzania kuweza kusaini Mkataba huo kwa jinsi ulivyo na vipengele vyake vyote.

Kwa upande wa Burundi, Umoja wa Ulaya ulichangia kuweka ugumu wa kusainiwa kwa mkataba huo baada ya kupitisha uamuzi kwa umoja huo kuwawekea vikwazo maofisa wakuu kadhaa wa serikali ya Nchi hiyo kufuatia kuzidi kuzorota kwa hali ya haki za Binadamu tangu Rais Pierre Nkurunziza alazimishe kuogombea urais kwa muhula wa tatu mapema mwaka 2015 jambo ambalo limezua mgogoro wa Kisiasa katika Mitaa ya Bujumbura. Sudan ya Kusini, kwa upande wake haikuwa na la kuzungumza katika hili kwa kuwa wakati mazungumzo ya EPA yanaanza hata ilikuwa haijawa Nchi kwa kuwa uhuru wake ulipatikana mwaka 2011 baada ya kujitenga na Sudan. Ni dhahiri kuwa itaichukua muda mrefu Juba kabla ya kuanza kuelewa na kuingia katika mazungumzo ya EPA!

Kwa upande wa Kenya, na kiasi fulani Rwanda, hofu ya kupoteza fursa na maslahi ya Kibiashara na Umoja wa Ulaya ilipelekea nchi hizo kuamua kukubaliana na Mkataba huo kama ulivyo huku Kenya ikiusaini ili kuwahi kuendana na tarehe ya ukomo ya Oktoba, 2016. Pia, kumekuwa na mjadala miongoni mwa wachambuzi wengi juu ya matumizi ya Ikulu ya Magogoni kama ukumbi wa Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi za Afrika Mashariki.

Katika hili, waliofurahishwa na uamuzi huo walionekana kuegemea zaidi upande wa uokoaji gharama za uendeshaji wa Mkutano huku wakosoaji wakihoji endapo kufanyia Mkutano kama huo ikulu kunaendana na dhana na lengo ya  EAC kugusa Maisha ya Wananchi wa Kawaida wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa maoni yangu, mjadala uliofuatia Mkutano huu umekosa umakini katika kuzungumzia suala la Jinsi wananchi wa hali mbalimbali wanavyoweza kushiriki na kuongeza tija katika vikao, mikutano na uendeshaji mzima wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuepuka kuifanya EAC kuwa mradi wa Marais na Mawaziri, tena wa Mambo ya Nje pekee.

Katika kukumbushana, Mkataba unaoanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki unaweka bayana katika ibara zake kadhaa kwamba Jumuiya itapaswa kuwa ya Wananchi na kuwashirikisha ipasavyo. Hata hivyo, hilo linamaanisha nini? Je kumekuwa na maendeleo kiasi gani katika kufikia au hata kuelekea lengo hilo? Na Je, hatua zipi zinaweza kuchukuliwa ili Wananchi wa Kawaida, wake kwa waume katika nchi zote sita wanachama wa EAC yaani Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudan ya Kusini waweze kushiriki ipasavyo na kufikia kujiona kama sehemu muhimu ya shughuli za kila siku za Ushirikiano huo?

Hivi kwa mfano, kufanyika kwa Mkutano kama huo wa 18 wa Wakuu nje ya ukumbi wa ikulu kusingewezesha Wananchi wafanyabiashara kutoka Mbagala, Chamazi na Bunju kushiriki, kufuatilia na kuuliza maswali yanayowakera katika shughuli zao za kila siku? Nafahamu kuwa Waandishi walialikwa kuomba vibali kushiriki Mkutano kwa lengo la kuandika na kutangaza habari zake, lakini Je, kulikuwa na ulazima gani kwao kuhitaji kupata vibali ndipo waweze kuingia Mkutanoni? Na kwa wananchi wa Kawaida ambao si wanahabari au hata wachambuzi na waandishi wasiotambulika rasmi kama wanahabari kama mimi, ingewezekana vipi kuweza kushiriki na kuchangia katika Mjadala wa Mkutano huo muhimu?

Na tukizungumzia kwa msingi wa wadau wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivi wadau wakuu wa EAC ni nani? Niliwahi kuuliza swali hili kuhusu Mpango wa Umoja wa Afrika wa Kujitathmini kuhusu masuala ya Uwazi, Utawala bora na demokrasia (APRM) na sikupatiwa majibu ya kuridhisha. Inavyoonekana, wabia wa michakato kama hii ya utangamano hasa barani Afrika wamebaki kuwa Marais na Mawaziri, basi. Na kama hili ni la kweli, Je tutafika tuendako?

Na kwa nini hata Mawaziri wanaokutana mara kwa mara wawe ni wa Mambo ya Nje au Biashara pekee? Hivu hatuna cha kushirikiana kuhusu Kilimo, Sanaa au Michezo?  Hivi katika hali ya kawaida, nini kinatangulia kwa umuhimu katika ushirikiano wa kikanda na mtangamano kama huu wa Afrika Mashariki kati ya Mambo ya Nje au Biashara? Tuna umakini wa kiasi gani katika hili? Endapo, mathalani wanawake wafanyabishara na wachuuzi kutoka mitaa ya Kabalagala (Uganda) au Charambe na Tandale (Tanzania) au hata Kibera na River Road (Kenya) wangekuwa na masuala ya kuhoji na kuuliza serikali zao kuhusu utangamano, hivi wizara sahihi ingekuwa ni Mambo ya Nje? Wanaanzaje kufika katika wizara ambayo wataalam wake ni watu waliobobea katika masuala ya Kichina, Ulaya, Kifaransa na kihispania au Kireno?

Mkutano wa 18 pia ulimpitisha na kumwapisha naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Tanzania ili kuchukua nafasi ya Dkt. Enos Bukuku ambaye amemaliza muda wake. Kwa mujibu wa ibara ya 68 ya Mkataba wa EAC wa mwaka 1999, Manaibu katibu Mkuu pia hupitishwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi wanachama wa EAC baada ya uteuzi wa Kikao cha Mawaziri kutokana na  pendekezo la Nchi anakotokea. Kisheria, Naibu Katibu Mkuu huhudumu kwa muda usiozidi vipindi viwili vya miaka mitatu. Safari hii, Wakuu wa Nchi wamemteua Mhandisi Steven Mlote, ambaye hadi hivi karibuni alikuwa Msajili wa Bodi ya Wahandisi nchini na Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Pia, Mlote aliwahi kuwa Mwenyeiti wa Jumuiya ya Wahandisi katika EAC jambo linalomweka katika nafasi nzuri kuweza kufanya kazi ya Naibu katibu Mkuu au hata Katibu Mkuu wa EAC kwa ufanisi mkubwa.

Kwa maoni yangu, Mhandisi Mlote ana uwezo wa kuwakilisha mawazo na maslahi, japo finyu, ya wasomi wa taaluma yake pamoja na wafanya biashara, wakandarasi na wadau wengine wa sekta za ujenzi, miundombinu na uchukuzi kutokana na ujuzi na uzoefu alionao. Kikubwa anachohitaji ni uwezo wa kusikiliza vilio vya wataalam na watumiaji wa huduma za kihandisi na miundombinu itokanayo na taaluma hiyo katika Afrika Mashariki. Pia, atakutaji kuweza kujielimisha juu ya masuala mengine mapana ya utangamano ambayo akiwa kama Naibu Katibu Mkuu atalazimika kuyafahamu hata kama ni nje kidogo ya taaluma yake ya uhandisi. Namwona akiwa kuingo mkubwa katika EAC kwa wataalamu, watoa huduma na watumiaji wa uhandisi na mazao yake.

Akiwa mtu aliyetokea sekta binafsi na ya kiraia, anayo nafasi nzuri zaidi kushauri namna bora ya kushusha EAC kutoka juu iliko sasa na kuwahusisha wananchi zaidi kuliko Katibu Mkuu wake, Balozi Leberat Mfumukeko ambaye uanadiplomasia wake na kwamba alikuwa kigogo mzito katika serikali ya Burundi kunamweka mbali sana na maisha ya kawaida ya wana- EAC kiasi cha kupata shida juu ya namna ya kuipeleka Jumuiya mashinani kwa wafanyabiashara na wananchi wengi. Namwona akiwa msaada mkubwa katika kuimarisha fursa za mikutano ya Katibu Mkuu na sekta binafsi na AZAKI iitwayo SG Forum ambayo hadi sasa inaendelea kwa kusuasua kutokana na kukosa maono ya namna ya kutekeleza fursa hiyo inayoanzishwa na Ibara ya 127 (4). Mpaka sasa, fursa hii ya Mkutano wa Mwaka kati ya Katibu Mkuu wa Jumuiya na wadau wa Sekta binafsi na Asasi za Kiraia haijatumika vizuri.

Ukweli ni kwamba kumekuwa na maendeleo katika kuimarisha utangamano wa Afrika Mashariki tangu Marais wa Uganda, Tanzania and Kenya walipokubaliana kuunda Kamisheni ya uanzishaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1993, ikifuatiwa na kutiwa saini kwa Mkataba wa uanzishaji wa Jumuiya hiyo mwaka 1999 chini ya uongozi wa Marais Daniel Arap Moi, Benjamin William Mkapa na Yoweri Kagutta Museveni wa Kenya, Tanzania na Uganda. Aidha, kuanzishwana kwa ukanda wa kibiashara mwaka 2001 na umoja wa Forodha baadaye mwaka 2005 kwa mujibu wa ibara ya 75 ya Mkataba, kumechagiza malengo ya kuijenga Afrika Mashariki kama soko huria linalotegemea sana sekta binafsi na ufunguaji biashara huria kama misingi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ni faraja kwamba hatua kubwa zilipigwa wakati wa Katibu Mkuu mtanzania, Juma Volter Mwapachu kuanzia mwaka 2005 hadi 2011.

Kwa kuanzisha umoja wa Forodha, nchi za Afrika Mashariki zilikuwa zimekubaliana kufuta ushuru wote wa forodha ndani ya Jumuiya kwa bidhaa zinazovuka mipaka ya Uganda, Tanzania na Kenya.  Baadaye kidogo, Nchi za Burundi na Rwanda ziliamua kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 2007 na kupanua zaidi uwanda wa ushirikiano wa forodha kufikia nchi tano. Na ilipofika mwaka 2008, Marais Jakaya Mrisho Kikwete, Pierre Nkurunziza, Mwai Kibaki, Paul Kagame na Yoweri Museveni walisaini itifaki ya soko la pamoja la Afrika Mashariki katika ghafla iliyofanyika Arusha. Kwa kufanya hivyo, Wakuu wa EAC walikuwa wmekubaliana kupanua ushirikiano na kuhusisha masuala mengine mengi zaidi ikiwemo uhuru wa watu kwenda kokote katika Jumuiya; Kuhamishwa kwa mitaji na fedha kwenda popote ndani ya Jumuiya; pamoja na uhuru wa kutoa huduma popote katika mipaka ya Jumuiya.

Kiukweli, biashara miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki imeongezeka kwa zaidi ya mara mbili kutoka dola bilioni 2.2 hadi bilioni 5 kufikia mwaka 2012. Wakati huo huo soko la Afrika Mashariki sasa limefikia idadi ya watu milioni 150 ambayo si haba kwa namna yoyote ile. Aidha, kumekuwa na hamu kwa nchi zingine majirani kutaka kujiunga na Jumuiya ili kuendelea kujenga udugu, kushirikiana na kufanya biashara kwa pamoja. Mpaka mwaka 2016, kulikuwa na maombi matatu ya kutaka kujiunga na EAC kutoka nchi za Sudan ya Kusini, Somalia na Sudan. Baada ya kukubaliwa na kujiunga rasmi kwa Sudan ya Kusini mwaka 2016, Mkutano wa 18 ulijadili maendeleo katika kuhakiki maombi na utayari wa Somalia.

Pamoja na yote hayo, Changamoto hazikosekani. Itifaki ya Soko la pamoja bado haijulikani kwa wananchi wa Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na maudhui na malengo yake makuu. Aidha, suala la kuruhusu uhuru kamili wa wananchi kwenda na kuishi popote katika Jumuiya bado linaleta Mushkeli, sambamba na lile la wana-EAC kuruhusiwa kufanya kazi katika nchi yoyote. Muhimu zaidi, suala la umilikishaji wa Ardhi kwa wanajumuiya lina utata na ukakasi mwingi hasa kutokana na historia pamoja na hali halisi ya Nchi wanachama wa Afrika Mashariki. Maeneo ambayo yangewagusa wananchi moja kwa moja yanaonekana kuwa na ugumu kuyatekeleza. Nionavyo, EAC inapaswa kuwa Jumuiya ya wananchi walalahoi kabisa wa Jumuiya yetu.

Kwa bahati mbaya, uzoefu unapingana vikali na ukweli huo. Kwa mfano, nani anajua kuwa miaka michache iliyopita, Tanzania iliwatimua wananchi wenye asili ya Rwanda wapatao 1,000 kutoka nchini? Pia, Kenya, Kinara mwingine wa ushirikiano wa EAC ilianzisha mchakato wa mchakato wa marekebisho ya sheria za uhamiaji kuanzia mnamo Julai, 2012 kwa lengo la kuzuia utoaji wa vibali vya kuishi na kufanya kazi kwa wageni ambao ni vijana wa umri chini ya miaka 35 pamoja na wale ambao kipato chao ni chini ya dola za Marekani 2,000 kwa mwezi. Yote haya, na mengineyo kwa bahati mbaya yanakinzana na dhana ya ujenzi wa EAC kama Jumuiya ya forodha na hasa soko moja, pamoja na malengo ya utangamano wetu. Swali muhimu hapa ni Je tunapiga hatua kwenda mbele au kurudi nyuma?

Binafsi, nilitaraji kuona makubwa kutokana na Mkutano wa 18 wa Wakuu wa Nchi. Nilitamani kuona maamuzi makubwa yakifikiwa kuelekea kutatua changamoto zinazokwaza ushirikiano katika EAC katika hatua hizi za umoja wa forodha na Soko la pamoja kabla ya kuanza kuzungumzia ushirikiano wa kiuchumi/kifedha na baadaye Shirikisho la Kisiasa.  Nilidhani ingekubalika kuwa kuanzia mkutano huu, wananchi wote wanaruhusiwa kushiriki na kuchangia mikutano ya EAC katika ngazi zote. Hilo lingefuatiwa na hoja kuwa mikutano yote iwe inafanyika katika kumbi zenye nafasi ya kutosha na zinazoweza kufikiwa na wananchi wote. Nilitaraji maelekezo kuwa mkutano ujao ufanyike uwanja wa Taifa ili ushiri uwe mpana inavyowezekana na kwamba hakutakuwa na ulazima kwa mtu yeyote kuhitaji kibali kushiriki mikutano ya EAC, hata kama ni ule wa wakuu wa Nchi za Jumuiya.

Hivi kwani tunaficha nini? Kama suala ni usalama, ningetaraji kuwa kuwa na ulinzi, ukaguzi na uhakiki wa kutosha kuhakikisha usalama wa kila anayehudhuria na kushiriki Mikutano hiyo. Zaidi ya yote, nilitaraji wakuu wakubaliane kuwa ni kitambulisho cha taifa pekee kitahitajika kwa mwananchi wan chi moja kuingia nchi nyingine za Jumuiya. Kwa wazanzibari, nilifikiri kuwa hata kadi ya Mkaazi yaani Zan ID ingetosha kumruhusu mpemba kuingia Mombasa kama anavyoingia Tanga. Kwani mbona mtu anaruhusiwa kupanda ndege kwa kadi ya NIDA kutoka Kisongo, Arusha hadi Unguja? Kwa nini isiwe hivyo kwa safari Kigali au Bujumbura? Inanisononesha kuwa utaratibu huu ulianza kutumika kwa ubaguzi kwa wananchi wa Kenya, Uganda na Rwanda katika kile kilichokuja kujulikana kama Muungano wa walio tayari. Kwa nini siyo kwa Jumuiya nzima ya Afrika Mashariki?

Tuendako, naiona haja kwa EAC kujifunza kutoka Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS. Huko, ushirikiano umefikia mahali ambapo wananchi wananchi wanachama wanaweza kusafiri, kwenda na kuishi popote katika eneo la Jumuiya yao bila vikwazo vyovyote. Hapa kwetu, Nadhani kumekuwa na maneno mengi kuliko vitendo, ikiwemo katika suala la pasi ya Africa Mashariki ambayo haijapiga hatua zozote za maana. Ndiyo maana, tayari wana-EAC tumesharukia wazo jingine la pasi ya Afrika ambayo ilizinduliwa na kutolewa kwa washiriki wa Mkutano wa 27 wa kawaida wa wakuu wa Nchi wa Umoja wa Africa (AU), Kigali, Rwanda mapema mwaka 2016. Kutolewa kwa pasi ya Afrika kulikuja miezi sita tu baada ya maamuzi kufanyika mwezi Januari mwaka huo huo wa 2016 hali inayoonesha umakini na mwitikio wa hali ya juu. Lakini kwa nini pasi ya Afrika Mashariki inachukua miaka au muongo mzima?

Kwa ujumla, EAC ni lazima ifanywe kuwa na ishirikishe wananchi kuliko hali ilivyo sasa.

Sawa, inanipa faraja kwamba viongozi wetu wakuu wanashirikiana lakini je ushirikiano wao unatosha? Tutaishia kushangilia vicheko na makubaliano ya wakuu wa Nchi na serikali zao pasipo ushirikiano kushuka na kuwahusisha wananchi, watafiti, wafanya biashara, mabenki, wana-muziki na wengineo? Nayaona makampuni makubwa yakijitahidi kuvuka mipaka kama inavyotokea sasa kwa Kampuni ya Bia ya Afrika Mashariki; Benki ya CRDB; Makampuni ya Bakhresa; IPP na Nation Media; pamoja na Chandaria, Bidco na Nakumatt. Lakini hawa ni tembo wa Afrika Mashariki. Sisimizi watashirikiana lini? Tatizo liko wapi? Juhudi za ziada na za makusudi zinahitajika kuwezesha ushirikiano miongoni mwa makundi ya Wanawake, wanafunzi, wafugaji wa asili, wakusanya matunda na mizizi maporini, wachimbaji wadogo madini, wavuvi, pamoj na MVIWATA na VIBINDO. Ni kwa namna hiyo ndipo tutaifanya EAC kuwa ya watu wa kawaida na wa hali zote na siyo kubaki ya vigogo, wanasiasa na wakuu wa Nchi pekee kama Mkutano wa 18 ulivyothibitisha.

Deus Kibamba ni Msomi, Mtafiti, Mchambuzi na Mhadhiri wa Masuala ya Demokrasia ya Katiba, Sayansi ya Siasa, uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia. Ameongoza Taasisi mbalimbali kama Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo Cha Taarifa kwa Wananchi, Mwenyekiti wa JUKWAA LA KATIBA TANZANIA na Mhadhiri katika Chuo Cha Diplomasia, Kurasini, Dar es Salaam. Anaptikana kwa email – dkibamba1@gmail.com au Simu. +255 788 758581.