Home Makala KUZIPOKA HALMASHAURI VYANZO VYA MAPATO NI KUZIUA

KUZIPOKA HALMASHAURI VYANZO VYA MAPATO NI KUZIUA

241
0
SHARE

HILAL K. SUED,

Hakuna kitu kisichotozwa kodi hapa duniani – labda hewa tunayopumua, ingawa sina hakika sana katika hili pia. Aidha sheria za kodi zimetengeneza wahalifu wengi kuliko sheria nyingine yoyote ile serikali mbali mbali inazotunga ingawa si wote wanashughulikiwa kisheria.

Kodi ndiyo imekuwa suala ambalo serikali zote duniani zinalifukuzia tangu dunia ilipoumbwa, na ni suala ambalo ndilo hulisimamia vyema pengine kuliko masuala mengine yote katika nchi.

Na kwa serikali yetu ya Tanzania, huenda inazipiku nyingine nyingi duniani katika hilo kwa sababu katika miaka ya hivi karibuni tumekuwa tukitangaziwa ukusanyaji kodi umekuwa ukivunja rekodi mwaka hadi mwaka na umekuwa kama wimbo kwa kuutangazia umma ‘uvunjaji rekodi’ katika kuboresha maisha ya wananchi wake.

Lakini pia tunaweza kusema kwamba serikali inafanya hivyo kwa sauti mbili: Moja kama mkusanyaji mkubwa wa kodi na pili kama mfujaji mkubwa wa kodi hizo. Lakini hilo la pili ndilo linaonekana kero kubwa sana kwa wananchi ingwa si mada ya makala hii.

Kwa ujumla hakuna shughuli yoyote ya binadamu katika dunia hii ambayo serikali haiitozi kodi, kuiwekea liseni, kuisimamia na kuidhibiti. Daima serikali huhakikisha raia wake wote waitumikie, ama kwa kuwamo katika orodha yake ya waajiriwa, au katika orodha ya walipa kodi wake.

Kuna baadhi ya watu wanaona ulipaji kodi kwa lazima ni kitu haramu (immoral) na hufananishwa na uporaji wa mali za watu unaofanywa na serikali. Lakini serikali huhalalisha uporaji huo kwa kuuwekea sheria.

Wanasema kwa kuwa serikali hukusanya kodi kwa njia za kulazimisha na kutumia nguvu, ikisaidiwa na vyombo vyake vya dola kama polisi na mahakama, basi hii ni sawasawa na ujambazi uliojikita ndani ya serikali (institutionalized banditry) – kwa maneno mengine ni wizi mtupu.

Aidha pia tunashuhudia mamlaka za serikali zinavyosukumana, au tuseme zinavyoshindana katika utozaji na ukusanyaji wa kodi. Hili zaidi linajitokeza katika utawala wa Awamu hii ya Nne.

Wiki iliyopita Mameya wa halmashauri kadhaa nchini walitoa duku duku lao kupinga mapendekezo ya Serikali kuendelea kuwapunguzia vyanzo vya mapato.

Wamesema hivyo baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango katika Bajeti ya Serikali ya mwaka 2017/18 kupendekeza kuondoa tozo nyingine zilizokuwa zinachukuliwa na mamlaka za halmashauri.

Lakini hatua hizi zilianza kuchukuliwa katika bajeti iliyopita ya 2016/17 ambapo Serikali iliondoa mamlaka ya kukusanya kodi ya majengo kutoka halmashauri na kulikabidhi jukumu hilo Mamlaka ya Mapato (TRA). Safari hii serikali imekwenda mbele zaidi – imeziondolea halmashauri jukumu la kukusanya kodi ya ushuru wa mabango na huku ikipunguza ushuru wa mazao kutoka asilimia tano hadi tatu.

Dk Mpango alisema serikali imelipa TRA jukumu hilo kutokana na kuwa na ufanisi na mtandao mpana wa ukusanyaji wa mapato ulioenea nchi nzima. Alissema uamuzi huo haukuwa na lengo la kuchukua chanzo hicho cha mapato cha halmashauri, bali kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa kodi.

Kuzinyang’anya halmashauri vyanzo vya kodi si jambo jipya, ingawa safari hii limekuja kivingine – yaani kwa njia ya moja kwa moja.

Historia ya serikali za mitaa katika nchi hii baada ya uhuru inashabihiana sana na hali ilivyo katika halmashauri hizo aliyoirithi Rais Magufuli. Mwanzoni mwa miaka ya 70 halmashauri zote zilifutwa ili kupisha kile kilichoitwa ‘madaraka mikoani’ – programmu ambayo haikuwa imeeleweka sawasawa. Unafuta serikali za mitaa halafu unaita madaraka mikoani?

Wadadisi wa mambo wanasema hapo ndipo palikuwa mwisho wa muda mfupi, tangu uhuru, wa utawala bora na wa uwajibikaji katika utendaji kazi wa serikali uliokuwapo – na kuwa mwanzo wa uchafu wote ambao serikali za awamu zilizofuatia zilisema zilidhamiria kuuondoa – zikashindikana – na sasa Magufuli naye anajaribu kwa namna yake.

Programu hiyo ilishindwa vibaya kwani kuendesha utawala katika wilaya na sehemu za miji – hasa katika utoaji wa huduma za jamii na mambo yalikuwa hovyo kweli hasa katika miji. Makusanyo ya kodi yalikuwa yanafanywa na serikali kuu na hivyo kila wilaya/miji ilikuwa inagawiwa fedha za kujiendesha na utoaji wa huduma za jamii.

Badala ya halmashauri ziliundwa zilizoitwa “kamati za maendeleo za wilaya” zikijumuisha wakuu wa idara mbali mbali chini ya Wakurugenzi wa Maendeleo wa Wilaya (DDDs) pamoja na viongozi wengine wa chama – wakati ule – TANU ambao wote walikuwa “madiwani” wa halmashauri hizo.

Lakini hakukuwepo mpango wa namna hiyo katika miji, isipokuwa jiji la Dar es Salaam ambalo lilikuwa na Meya na Mkurugenzi wake ambao wote walikuwa wanateuliwa na rais. Kwa ujumla huduma za jamii zilizorota, kwani kulikuwa hakuna uwajibikaji au uwajibishaji.

Hali ilivyozidi kuwa mbaya mapema miaka ya 80 chaguo lililobakia lilikuwa ni kuurejea utaratibu wa zamani ambao hutumika katika asilimia 95 ya nchi duniani – yaani kuwapo kwa halmashauri.

Hata hivyo inawezekana kauli ya Dk Mpango kuzipora halmashauri vyanzo vya kodi ni sahihi kwenye suala la ufanisi katika ukusanyaji kodi, ingawa sijui katika matumizi ya kodi.

Na hata kama tukikubali ni makosa kuamini kwamba serikali inaweza kutoa vitu/huduma bure bila ya kwanza serikali hiyo hiyo kuwanyang’anya wengine – sote tunakubali wazo la kuwatoza watu kodi – iwapo tu itatumia fedha hizo kugharamia shughuli za manufaa kwa wananchi walio wengi.

Kwa maneno mengine hoja zote zinazojengwa dhidi ya utozaji kodi zinatokana na namna serikali inavyotumia kodi hizo, na siyo kodi yenyewe.

Kwa mfano kama serikali inajigamba kuvunja rekodi katika ukusanyaji wa kodi, kwa nini tena inapitisha bakuli kuomba fedha za kujenga vyumba vya madarasa?

Sawa, serikali yasema hailazimishi mtu kulipa hiyo michango. Kama ni hivyo, basi ni vyema ikabakia hivyo – yaani iwe hiari ya mtu.