Home Habari MASHISHANGA: RAIS MAGUFULI SI MALAIKA

MASHISHANGA: RAIS MAGUFULI SI MALAIKA

548
0
SHARE

NA VICTOR MAKINDA,

KADA wa siku nyingi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwamo ukuu wa Mkoa, Steven Mashishanga, amesema Rais Dk. John Magufuli ni binidamu kama binidamu wengine na asichukuliwe kama malaika licha ya kwamba ana madaraka makubwa ya urais.

Alisema moja ya mambo muhimu ambayo kiongozi anapaswa kukubaliana nayo ni ukosoaji kutoka kwa jamii anayoiongoza.

Akizungumza na  RAI nyumbani kwake mjini Morogoro, Mashishanga alisema kuwa Rais Magufuli kama kiongozi mkuu wa nchi hawezi kukwepa kukosolewa pamoja na matendo mengine ya kibiadamu kama walivyo biniadamu wengine.

Alisema katika utendaji wa kiongozi huyo wa nchi wapo  watakaoumia na wapo watakaonufaika.

Akifafanua kauli hiyo, Mashishanga alisema kuwa hakuna kiongozi mkuu wa nchi duniani kote ambaye anaweza  kufanya kazi kama malaika pasipo kulaumiwa na wananchi anaowaongoza, hata kama anatenda mazuri kiasi gani.

“Magufuli ni kiongozi mzuri sana, lakini sio malaika. Anayo mapungufu madogo madogo  ukilingalinisha na mazuri yake hata hivyo njia nzuri ya kupima utendeji wake ni mwaka 2020, huo ndio utakuwa wakati muafaka wa kupima nini amefanya na nini hajafanya  katika kutekeleza ilani ya CCM aliyonadi kweye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.”

Mashishanga aliongeza kuwa  Rais Magufuli ameipokea nchi hii ikiwa imejaa uvundo wa rushwa, ufisadi, utendaji  wa mazoea wa viongozi wa Serikali na watumishi wa umma, kutowajibika kikamilifu kwa viongozi, urasimu katika utekelezaji  wa huduma za wananchi, mishahara hewa, mikataba mibovu pamoja na deni kubwa la Taifa.

Alisema Rais Magufuli ameonesha njia ya wapi  anataka Tanzania ifike . Kwa kuwa anakabiliwa na masuala mengi kwa wakati mmoja na kwa kuwa ameonesha dhamira ya kutatua kero sugu ambazo zimekwaza maendeleo kwa muda mrefu, ni lazima atalaumiwa na wananchi hususan wale waliozoea kuishi kwa mazoea.

“Huyu si malaika kusema kwamba atafanya mazuri tu ambayo yatampendeza kila mmoja. Wanaomlaumu sasa Rais Magufuli hawakosei, kama wasingemlaumu leo, ni  lazima wangelijitokeza tu.

“Kwa kuwa Rais Magufuli ameonesha dhamira ya dhati ya kupambana na madudu, wale waliozoea kuvuna vipato vyao kupitia rushwa, kughushi nyaraka na wavivu kazini lazima watamlaumu na kumuona kuwa hafai, lakini mimi nasema utendaji  wa   Magufuli  zaidi ya asilimia 90 ni mzuri,’’ alisema.

Juu ya maoni yake kuhusu utendaji wa Rais Magufuli, Mashishanga alisema kuwa upungufu anaouona yeye katika awamu hii ni kutowajibika kikamilifu kwa baraza la Mawaziri.

“Watakao na wanaomwangusha Rais Magufuli ni watendaji wake, hususan baadhi ya Mawaziri ambao wanaonesha dhahiri kutokwenda na kasi yake.  Rais lazima awe mkali sana kwa kuwa Watanzania wengi, wananchi na viongozi walitawaliwa na mazoe mabaya.

“Hawa ni lazima wanyooshwe kikamilifu ili kuacha kuishi kimazoea na kubadilisha mtindo wa maisha yao ili kwenda na kasi ya Rais kwa lengo la kuifikisha Tanzania kwenye maendeleo yatakayoleta ustawi wa maisha ya wananchi.

“Mawaziri wanatakiwa kumshauri vizuri Rais. Wanatakiwa kumsaidia katika utekelezaji wa ilani ya chama. Hawa  wanatakiwa kuwa wabunifu sana na wasikae maofisi kusubiri ripoti, washuke kwa viongozi wa chini yao na wananchi.

“Wakahamisishe na kusukuma maendeleo ili wananchi waondokane na kero mbali mbali. Kujifungia maofisini na kusubiri ripoti au kusubiri mpaka Rais aseme ndio watekeleze  ni mapungufu makubwa ya kiutendaji.”

DHANA YA CCM KUISIMAMIA SERIKALI

Akielezea dhana ya  CCM kuisimamia Serikali, Mashishanga alisema kuwa  ni vema CCM ikarejea  mwongozo wa Chama wa mwaka 1981 ambao unakitaka chama kuisimamia serikali kikamilifu.

“CCM ndiyo iliyoshinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, baada ya kunadi sera zake na kukubalika kwa wananchi na kuchaguliwa. Serikali iliyopo madarakani ni Serilkai inayotokana na Chama cha Mapinduzi, hivyo ni lazima chama kiufuate mwongozo wa mwaka 1981 unaotamka wazi wazi kuwa chama kupitia vikao vyake, kinatakiwa kuielekeza serikali pale penye mapungufu ya utendezi na utekelezaji wa sera.

“Ninayaona mapungufu kwa chama changu CCM kwa sasa,  chama kinaiogopa Serikali ikiwa ni kinyume chake. Ilitakiwa serikali ikiogope chama sio  chama kuiogopa Serikali. Malengo ya chama chochote cha siasa ni kushika dola.

“Chama kinapoaminiwa na wananchi na kuchagulia kuunda serikali,  viongozi wa chama wanapaswa kuwa wakali kwa viongozi wa Serikali pale ambao  Serikali imeonesha mapungufu ya utekelezaji wa sera za chama.

“Vikao vya juu vya chama vina nguvu ya kumkemea hata Rais wa nchi pindi anapoonesha kwenda kinyume na utekezaji wa ilani ya chama.

“Kwa kuwa ikiwa Serikali itashindwa ku ‘deliver’ kuzalisha kile ambacho wananchi kiliwavutia kukichagua chama kilichounda serikali, chama hicho kitakataliwa na wananchi. Chama kikikataliwa na wananchi, chama hicho hufa kifo cha asili.”

Aliongeza kuwa ameiona hatari kwa baadhi ya viongozi wa serikali ambao kimsingi wametokana na chama wanakipuuza chama.

“Hii ni hatari sana. Viongozi wa Serikali wanatakiwa kukiogopa chama. Wanajitahidi kukijenga na kuteleza sera za CCM pasipo chama hakuna viongozi. Viongozi wa chama wasiache kuyatafuta na kuyaibua matatizo ya wananchi na kuyafikisha Serikalini ili yatatuliwe.

“Serikali ikayapuuzia basi kamati kuu na NEC iwawajibishe viongozi na watendaji wa serikali, hapa lazima chama kiwe cha Serikali ni lazima chama kiisimamie Serikali,” alisema.

MAUWAJI YA KIBITI

Kuhusu hali mbaya ya usalama inayokabili mkoa wa Pwani maeneo ya Rufiji, Kibiti, na Mkuranga, Mashinga alisema kuwa, anakishangaa chama kupitia NEC na Kamati Kuu ya chama kutotoa tamko lolote juu ya mauaji yanayoendelea kutokea katika mkoa wa Pwani.

“Nilihitaji CCM ingetoa tamko kupitia Mikutano yake Mikuu, lakini nimeshangaa kwa ukimya wa chama changu juu ya  madhira wanayoyapata wananchi wa Pwani.

“Huu sio utamaduni wa chama. Chama lazima kiendeleze utamaduni wa kuyazungumzia kwa kutoa matamko juu ya matatizo makubwa yanayoikumba jamii.”

Aidha, ameishauri Serikali, kutotumia nguvu kubwa katika kulikabili tatizo hili la mauwaji, bali itumie mbinu za kisayansi kukabiliana nao.

“Serikali isitumie nguvu kubwa ya vyombo vyake vya ulinzi na usalama katika meaeneo yanapotokea mauwaji. Isiufanye mkoa wa Pwani kuwa eneo la kivita, mbinu hii inaweza isifanye vizuri sana. “Nionavyo Serikali iwatafute washauri nasaha, wanasaikolojia, viongozi wa madhehebu mbali mbali wa dini na wazee waliobobea katika usuluhishi wa migogoro waende Pwani kuzungumza na wananchi wa makundi na rika mbali mbali, kubaini chanzo hasa cha mauaji hayo. Kama ni kulipiza kisasai basi waseme kwa nini wanalipiza kisasi nini kikifanyika wataacha kufanya hivyo. Matumizi ya nguvu hayawezi kuleta suluhu ya haraka na pengine inaweza kusababisha mgogoro huu kuwa mkubwa zaidi

“Kwa upande wa  wananchi wa Pwani ninawaomba wasiikubali hali hiyo. Wasiruhusu mioyo yao kutawaliwa na jabza , hasira na roho ya visasi, wakatae kuuwawa na kuuwa watu wasio na hatia, waitafute amani kuanzia mioyoni mwao, waipende na kuitunza tunu ya Taifa letu tuliyoachiwa na viongozi wetu waasisi.”

MAISHA YAKE

Akielezea kuhusu maisha yake baada ya kustaafu anasema kwamba kwa sasa anaishi kwa kudra za mwenyezi  Mungu.

“Nimefanya kazi CCM  tangu mwaka 1982 nikiwa nimeteuliwa kama Katibu wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga. Niliendelea kukitumika chama mpaka mwaka 1995 nilipoteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga. “Nimefanya kazi katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza na Morogoro mpaka mwa 2006 nilipostaafu. Nilipostaafu CCM, nakumbuka nilipata Sh. 400,000 tu na nilipostaafu ukuu wa Mkoa nililipwa malipo ya mkupuo pesa kidogo ambazo  hazikutosha kufanya shughuli yoyote endelevu.

“Serikali ifanye marekebisho ya sheria ya malipo kwa wakuu wa mikoa wastaafu. Tuwe tunalipwa pensheni, kutotulipa pensheni inatuletea shida sana kwa sisi viongozi  ambao tumetumikia chama na Serikali kwa muda mrefu na baadae tunaishi pasipo kulipwa chochote jambo linalotuletea adha kubwa sana katika maisha ya uzeeni.

“Sijutii utumishi wangu ndani ya chama na Serikalini. Nilifanya kazi kwa  kusukumwa na uzalendo wangu kwa nchi yangu. Isipokuwa ni vema Bunge libadili sheria kuhusu malipo ya wakuu wa mikoa. Nimejaribu kuwasiliana moja kwa moja na viongozi wakuu wa nchi, Rais wa awamu ya tatu Benjamini Mkapa na wa awamu ya nne Jakaya Kikwete, kuhusu malipo ya pensheni, lakini sijafanikiwa kupata chochote.

“Ninamshukuru Mungu, ninaishi vizuri kwa kudra  zake, nina afya njema, ninao watoto nimewasomesha, wananisadia,  lakini pia  ninaishi vizuri na viongozi wa CCM na Serikali wa mkoani na Taifa kwa ujumla.”

Mashishanga anatoa wito kwa serikali kuwatunza na kuwaenzi wastaafu kwa kuwapatia matatibu na kuwaongezea pensheni. Wakati mishahara ya watumishi wa sasa inapanda na pensheni ya watumishi waliostaafu ni vema pia zikawa zinapanda ili kutufanya tumudu maisha ya uzeeni na changamoto zake.