Home Habari kuu RIPOTI YA MAKINIKIA: YAIBUA VITA MPYA YA KISIASA

RIPOTI YA MAKINIKIA: YAIBUA VITA MPYA YA KISIASA

870
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI,

RIPOTI ya Kamati ya pili ya kuchunguza usafirishaji wa makinikia nje ya nchi  iliyokabidhiwa mwanzoni mwa wiki hii na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Profesa Nehemiah Osoro kwa Rais Dk. John Magufuli, imeibua vita mpya ya kisiasa nchini. RAI linaripoti.

Vita mpya ya kisiasa iliyoibuka sasa ambayo inapiganwa kwa maneno nje na ndani ya Bunge ni ile ya ni upande gani unaostahili kubebeshwa zigo hili la ubadhirifu wa madini.

Zinazosigana hapa ni pande mbili za kisiasa, upande mmoja ukiongozwa na makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) huku upande wa pili ukiongozwa na makada wa vyama vya upinzani hasa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Makada wa Chadema pamoja na baadhi ya viongozi wao wanaamini kuwa CCM na serikali zake inastahili kubeba lawama hizi kwa sababu wao ndio wameifikisha nchi hapa ilipo na kwamba wao upinzani walikuwa wa kwanza kulipigania suala hili la kutaka uwazi kwenye mikataba yote ya madini kama ambavyo Kamati ya Profesa Osoro imependekeza.

Wakati Chadema wakiibeba hoja hiyo na kujiita wao ndio waasisi wake, kwa upande wa CCM ambao baadhi ya wabunge wake walikuwapo kwenye mabunge yaliyotangulia na baadhi yao kuwamo ndani ya Bunge hili kutajwa kushangilia upitishaji wa mikataba ya hovyo kwa shangwe na vigelegele wao wanaamini hatua iliyopigwa sasa na Rais Magufuli ni ya chama na wanapaswa kujipongeza.

Mnyukano huu wa nani anastahili kusifiwa juu ya kilichobainika kwenye uchimbaji na usafirishaji wa madini, sasa umeonekana kuibua joto la kisiasa kwa vyama hivyo viwili, tofauti na ilivyokuwa awali, ambapo hakukuwa na hoja nzito yenye kuweza kuviingiza vyama hivyo kwenye vita ya maneno.

Mbali ya Chadema na CCM, lakini pia sasa chama kipya cha ACT-Wazalendo nacho kinaonekana kupata nafasi ya kupenya kwenye mnyukano huu baada ya Kiongozi wake Mkuu, Zitto Kabwe kuwa miongoni mwa wanasiasa waliopata kulipigia kelele suala hili la ubadhirifu wa madini akiwa ndani ya Chadema.

Katika Bunge la tisa Zitto alijikuta akiadhibiwa kukaa nje ya Bunge kwa miezi minne baada ya kuwasilisha hoja binafsi iliyohusu mgodi wa Buzwagi.

Uamuzi huo wa Zitto unatajwa kuwa moja ya kazi nzuri alizopata kuzifanya mbunge huyo ambaye anatajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko katika sekta ya madini nyakati ambayo hakuna mwanasiasa aliyethubutu kukosoa sera za uwekezaji kwa namna alivyofanya.

Zitto alipata kumkalia kooni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi ambaye ametajwa kwenye kamati ya Prof. Osoro kama Waziri aliyeshiriki kulihujumu Taifa. Akiwa ndani ya Bunge la tisa Zitto alimtaka Karamagi kujieleza ndani ya Bunge kuhusu mkataba mpya wa madini na mashariti yake ya kodi kwani alipata taarifa kuwa amesaini mkataba huo  akiwa hotelini nchini Uingereza.

Karamagi alishindwa kufanya hivyo na ndipo Zitto aliwasilisha Hoja Binafsi Bungeni (akiwa mbunge wa kwanza kufanya hivyo katika Bunge la Tisa na la Nane kwa pamoja). Hoja ya Buzwagi ilisababisha Zitto kusimamishwa ubunge kwa miezi minne hata hivyo Septemba 10, 2007 alitangaza Azimio la Songea lililomshinikiza Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kuunda Kamati ya Bomani iliyopewa kazi ya  kupitia mikataba yote ya madini nchini.

Baada ya Kamati hiyo iliyoundwa Aprili 10, mwaka huu kukabidhi ripoti  iliyoibua madudu mengi yanayofanyika kwenye biashara ya uchimbaji wa madini tangu mwaka 1998, Zitto aliibuka na kusema kuwa mwisho wa siku historia inaandikwa tu!

ZITTO NA UZALENDO

“Uzalendo ni kufanya jambo ambalo wengi hawakuelewi lakini wewe unajua ni jambo sahihi na unakubali kutukanwa, kususubikwa, kusimangwa, kuzushiwa, nk. Unapambana tu. Mwisho wa siku waliokuita msaliti watakuita shujaa.

“Waliokuzomea wanashangilia. Wewe unafanya nini? Unakaa kimya kwani kwenye kukaa kimya pia kuna kusema kukubwa zaidi. Muhimu nchi ifaidike.
Huko nyuma nilipata kusema, hata Mungu akinichukua sasa unakwenda ukiwa umetabasamu kwani unakuwa umetimiza wajibu wako duniani. Kina Josina Umm Kulthum wataishi kwa heshima inshallah.”alihitimisha.

LISSU: TUMETISHWA SANA

Wakati Zitto akiyasema hayo kwa upande wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliomba kuweka rekodi sawa sawa juu ya suala hilo la makinikia.

Alisema naomba niweke rekodi ya masuala haya sawasawa, For the Record: What Goes Around Comes Around!!! Leo wapinzani wa Serikali ya Magufuli tumesemwa sana na kutishiwa kushughulikiwa bungeni na nje ya Bunge.

Kwa sababu hiyo, naomba niweke rekodi ya masuala haya sawa sawa.

“Mwezi Machi ’97 Bunge lilipitisha Sheria 2 kwa siku moja kwa kutumia Hati ya Dharura.

1) Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbali mbali za Fedha ya ’97 ilifuta au kupunguza kodi nyingi kwa ajili ya makampuni ya kigeni ya madini.

2) Sheria ya Uwekezaji Tanzania ’97 iliwapa wawekezaji wa kigeni ulinzi mkubwa na manufaa mengi kama vile kuondosha nje fedha na faida yote wanayopata kwa uwekezaji wao nchini.

Mwaka ’98 Bunge lilipitisha Sheria ya Madini ’98 ambayo ilitamka kwamba mwenye milki ya madini na fedha yote itokanayo na mauzo ya madini ni mwenye leseni ya kuchimba madini hayo.

Sheria hizo tatu nimeziita ‘Utatu Usio Mtakatifu’ (Unholy Trinity) katika maandiko yangu mbali mbali, na nimezichambua sana tangu mwaka ’99 nilipoanza harakati dhidi ya sekta ya madini ya aina hii.

Kwa miaka yote hii hadi leo, Sheria hizi za madini zimeungwa mkono na kupigiwa debe na kila kiongozi na mbunge wa CCM, Magufuli included.

Watu hawa, with very few and minor exceptions, ndio wamekuwa washangiliaji wakubwa wa unyonyaji wa makampuni ya kigeni ya madini katika nchi yetu.

Na ukweli ni kwamba watu hawa na Chama chao ndio wamefaidika sana na utaratibu huu katika sekta ya madini.

Wachache tuliopinga utaratibu huu tuliitwa kila aina ya majina mabaya na uzalendo wetu ulihojiwa kama unavyohojiwa leo na Magufuli.

Kwa mfano, Rais Mkapa alidai, wakati anazindua Mgodi wa Bulyanhulu, kwamba upinzani wetu ulikuwa ni ‘ujinga uliofichama katika kivuli cha taaluma.’

Baadhi yetu, kama mimi na Dk. Rugemeleza Nshala, tulikamatwa na kushitakiwa mahakamani kwa uchochezi. Tulikabiliwa na kesi hiyo kuanzia Mei ’01 hadi ’08 ilipofutwa kwa kukosekana ushahidi.

Kama ilivyokuwa wakati wa Mkapa mwaka ’01, leo pia Rais Magufuli ametukebehi na kuahidi kutushughulikia ‘tukiropoka’ nje ya Bunge.

Tunaambiwa ni lazima tumuunge mkono Rais wetu katika hii ‘vita ya uchumi.’ Ni sheria ipi ya Tanzania inayotulazimu kumuunga mkono Rais wetu hata kama tunaona amekosea?

Hebu naomba tuitafakari hii ‘vita ya uchumi’ kidogo. Je, nani hasa ni maadui zetu katika ‘vita’ hii? Ni makampuni ya madini ya kigeni? Kama ni hivyo, fikiria yafuatayo:

1) Wakati tuko vitani, Rais Magufuli na serikali yake wameiruhusu Acacia Mining (tunayoambiwa hata haijasajiliwa!!!) kuendelea kuchimba, kusafisha na kusafirisha nje ya nchi dhahabu kutoka Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara Tarime.

Amezuia magwangala yasisafirishwe nje kwenye makontena lakini dhahabu yenyewe hamna shida ikisafirishwa na wezi hawa!

2) Wakati mapambano ya ‘vita ya uchumi’ yakiendelea, dhahabu yote inayochimbwa Geita Gold Mine (Mgodi mkubwa kuliko yote nchini) inaendelea kuchimbwa, kusafishwa na kusafirishwa nje ya nchi.

3) Wakati tuko vitani, Rais Magufuli na serikali yake ameruhusu kila mgodi wa dhahabu nchini kuwa na kiwanja chake binafsi cha ndege ili wezi hawa waweze kutorosha ‘dhahabu yetu’ kwa urahisi zaidi.

4) Wakati tungali vitani, ‘Utatu Usio Mtakatifu’ wa sheria zetu za kodi, uwekezaji na madini uko pale pale ulipokuwa mwaka ’97-’98, cosmetic changes excepted.

Aidha, licha ya kuwa vitani, sisi bado ni signatories wa MIGA Convention na bilateral investment treaties (BITs) zinazowalinda hawa tunaoaminishwa kuwa ni wezi na maswahiba wao wa miaka yote.

5) Wakati tuko kwenye hii vita kubwa ya uchumi, jemedari wetu mkuu na serikali yake hawajatengua mkataba hata mmoja wa uendelezaji madini (Mineral Development Agreements – MDAs) walizosaini hawa anaowaita wanyonyaji na serikali za watangulizi wake Jakaya Kikwete na Ben Mkapa.

6) Wakati tunahamasishwa kumuunga mkono jemedari huyu shupavu, bado hatujaonyeshwa mkataba hata mmoja waliosaini na wanyonyaji hawa tangu miaka ya mwanzo ya ’90.

Leo Jemedari Mkuu ameahidi kwamba mikataba hiyo italetwa bungeni. Safi sana.

Lakini je, hii ni mara ya kwanza tunaahidiwa hayo?

Mwaka ’08 Jemedari Mkuu wa kabla yake alituahidi hivyo hivyo. Tuwe na subira kabla ya kuanza kushangilia prematurely.

7) Nimemsikia Magufuli akielekeza wahusika wote wa uchafu huu washughulikiwe. Kweli?

(a) Je, Jakaya Kikwete aliyesaini leseni za Bulyanhulu na Nzega mwaka ’94 anaponaje?

(b) Je, Ben Mkapa aliyekuwa Rais na Mwenyekiti wa Cabinet wakati haya yanafanyika anaachwaje?

(c) Je, waliokuwa mawaziri na manaibu wao wote wakati haya yanatokea wanasalimikaje?

(d) Je, wale washangiliaji na wapiga meza wa bungeni, ambao waliunga mkono kila walicholetewa bungeni na kukipitisha kilivyo wanakosaje lawama?

8) Nimesikia Acacia Mining hawana hata leseni/usajili wa kuendeshea shughuli zao hapa nchini. Labda. Hata hivyo, jiulize yafuatayo:

(a) Hivi wamekuwa wanalipa kodi kama PAYE, SDL, income tax, withholding tax, mrahaba, n.k., kwa kutumia jina gani miaka yote hii?

(b) Je, wana akaunti yoyote katika benki za Tanzania? Kama ndio, wamezifungua kwa jina gani?

Kama hapana, wanalipaje mishahara ya wafanyakazi wao wa Kitanzania au watoa huduma mbali mbali wa Kitanzania?

(c) Je, wanalipa bili za umeme kwa TANESCO au za simu kwa Vodacom, Tigo, Airtel, n.k. kwa kutumia jina gani?

(d) Je, wamesajiliwaje katika Soko la Hisa la Dar kama Acacia kama wanaendesha shughuli zao kihuni hivi?

(e) Kuna kitu kinaitwa ‘estoppel’ katika Sheria yetu ya Mikataba (the Law of Contract Act, Cap. 345) na katika Sheria yetu ya Ushahidi (the Law of Evidence, Cap. 6). Je, estoppel haituhusu kwenye suala hili la leseni au usajili ya Acacia?  Kama estoppel inahusika, je, hoja hii ya ukosefu wa usajili ina uzito gani, kama upo, kisheria?

9) Nimesikia Sheria za Madini zinatakiwa kufanyiwa marekebisho makubwa. Sawa kabisa.

Lakini je, kwanini Rais Magufuli hajasema chochote juu ya Sheria za Gesi Asilia na Mafuta ambazo zilipitishwa haraka haraka kwa Hati ya Dharura baada ya sisi ‘waropokaji’ kutimuliwa bungeni na Spika Anna Makinda mwaka ’15?

Au Rais wetu anaamini kwamba Sheria za Gesi Asilia na Mafuta hazina matatizo licha ya kupitishwa kwa utaratibu ule ule uliotumika kwa Sheria za Madini?

10) Wakati tunaingojea kwa hamu mikataba ya madini iletwe bungeni, hebu na tujiulize yafuatayo:

(a) Mikataba ya uchimbaji gesi asilia na mafuta nayo iko wapi?

(b) Mikataba ya manunuzi ya Bombardier na Dreamliner za Magufuli nayo italetwa bungeni au itabidi tusubiri aondoke madarakani kwanza kama ilivyokuwa kwa JK na BM?

(c) Mikataba ya ujenzi wa airport Chato na Reli ya Standard Geji ya Waturuki au Wachina na mabarabara kibao nayo italetwa bungeni au ndio basi tena tusubiri Bwana mkubwa atakapoondoka madarakani?

Wakati tukisubiri kufukuzwa bungeni na Spika Ndugai kwa maelekezo ya bosi wake, na wakati tukisubiri dhahama ya Bwana Mkubwa nje ya Bunge, hebu na tujiulize hivi nani hasa ndiye mzalendo wa kweli wa nchi hii?

Hebu na atutajie majina na namba za simu za wale wote ambao amedai wamekuwa wanawasiliana na Acacia na lini walifanya mawasiliano hayo na yalihusu kitu gani. Kutoa hukumu kwa innuendo peke yake haitoshi, tunahitaji ushahidi thabiti kutoka kwa Rais Magufuli.

Sijazungumzia bado plagiarism ya taarifa mbali mbali za kiserikali na zisizo za kiserikali katika Taarifa ya Kamati ya Prof. Osoro. Hili ni la baadae.”

MTATIRO: HAKUNA WA KUZIMA MJADALA

Kada wa Chama Cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro alisema wajibu uko palepale na uongozi wa nchi siyo hisani na sisi ni Taifa masikini sana hadi sasa.

“Ni mwendawazimu tu ndiye anaweza kufunga mjadala wa Madini. Huu ni mjadala utakaokuwepo siku zote, hakuna wa kuuua. Marekani wana kila kitu, Ulaya wana kila kitu, wana fedha za kutosha mifukoni, na hawajaridhika, wanahoji hadi mke wa Rais wao anatembeaje, anavaaje n.k. Sembuse sisi! Tutahoji tu na kila jibu moja likitolewa tutahoji lingine, na likitolewa tutahoji lingine. Maana, sisi tunaona miaka 20 mbele yenu. Come On!”

PROF. KITILA ATOA NENO

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Prof. Kitila Mkumbo alionekana kuwananga wapinzani kwa kusema kuwa: Kuna ugonjwa unaitwa opposition defiamt disorder (ODD). Dalili kubwa ni kupinga kwa lengo la kupinga hadi unajipinga mwenyewe. Tuuepuke.”

MAHANGA NAE ASEMA

Naibu waziri wa zamani wa Serikali ya awamu ya nne Dk. Milton Mahanga alisema: Ushindi mkubwa umepatikana kwa wale wote ambao kwa miaka mingi walikuwa wakilalamikia mikataba mibovu ya uchimbaji madini na gesi na mafuta, kwamba ipitiwe upya na Bunge. Rais Magufuli leo ameagiza mikataba hiyo irudishwe Bungeni kupitiwa upya. Hongera JPM. Hongera wapinzani na wanaharakati mliopiga kelele sana miaka mingi.

Wakati upande wa upinzani wakiyasema hayo kwa upande wa CCM, wao wamepongeza hatua ya Rais Magufuli na kudai kuwa ni vema watu wote waliotajwa kwenye ripoti hiyo wakawajibishwa ipasavyo.

SPIKA NDUGAI ALIA NA MIKATABA

Spika wa Bunge, Job Ndugai alipongeza hatua ya Rais na kuahidi kuunda timu ya Spika itakayokuwa na jukumu la kufuatilia suala la uchimbaji wa madini ya almasi nchini.

“Hii mikataba ya kijinga hata kama ilifungwa mwaka gani ni mikataba ya ovyo hii…Mimi na wabunge wenzangu tutazitendea haki sheria za mabadiliko kuhusu gesi na madini, nitaunda timu ya Spika kufuatilia uchimbaji wa almasi,”alisema.

WASOMI WASHANGAA

Wasomi na wachambuzi wa siasa nchini wanalitazama jambo hili kama moja ya maeneo ambayo wanasiasa wanataka kujitafutia umaarufu juu ya suala hili badala ya kuweka maslahi ya Taifa mbele.

PROF. BAREGU: CCM INASAKA MTAJI WA KISIASA

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino, Profesa Mwesiga Baregu alisema Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndio wanachukulia suala hilo la makinikia kisiasa.

“Zoezi lote la makinikia nadhani linaficha mambo mengi, sasa tunahangaika na makinikia lakini hatuhangaiki na dhahabu yenyewe, kwa maana kuwa makinikia ni mabaki ya dhahabu, lakini misingi ya kudhulumiwa ipo kwenye migodi yenyewe.

“Hata kuijenga hoja ya makinikia kuwa kubwa kiasi hiki imefanywa kisiasa, kwa sababu mbili, kwanza katika rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba ambayo nilishiriki kuiandaa, mambo haya yaliwekwa wazi katika vifungu vitatu, kuwa ni wajibu wa kila mtu kulinda, kuendeleza na kutumia rasilimali za nchi kwa manufaa ya watanzania. Lakini cha ajabu hivyo vifungu viliondolewa baada ya wabunge wa CCM kubaki peke yao katika Bunge Maalumu la Katiba. Pia kelele nyingi sana zimepigwa na kina Mnyika, Lissu, Zitto na wengine kuwa tuangalie undani wa hili jambo ila walipuuzwa.

“Ukisoma sera ya mwaka 1997 ya madini ambayo ilikuwa ya kwanza kuna mambo matatu, moja ni kwamba ile sera ya Nyerere kwamba tusivune madini mpaka tukiwa tayari, haikuzungumzwa kabisa. Lakini kwanini ilitupwa na tuna malengo gani ya kimsingi, kwamba labda tumevuna lakini tuna sera endelevu kwa kuweka akiba kwa vizazi vijavyo haya yote hayakuzungumzwa wala kuwekwa, ile sera inaonesha kama ilitungwa na wawekezaji wenyewe hivyo kwa sera ile ni lazima sheria isingeweza kutulinda,” alisema.

Alisema ni lazima kuwepo na umakini katika kushughulikia suala hilo ikiwa ni pamoja na kupitia upya sera, sheria, mikataba iliyoingiwa kuhusu rasilimali zote.

“Rais amesema sheria zote za madini zipelekwe kuangaliwa bungeni je, gesi, maliasili vitaangaliwa lini, hivyo lazima tuwe na fikra pana kuhusu usimamizi wa rasilimali zetu, hakuna mtu anayetaka siasa za rahisirahisi, wapinzani hatuangalia tumepiga goli au tumepigwa… ni kutumia akili, kwa sababu ni sawa na kutibu dalili za ugonjwa wakati ugonjwa wenyewe umebaki palepale,” alisema.

Nakumbuka mwaka 2002, nilitembelewa na Profesa mmoja, mshauri wa Mkurugenzi Mkuu wa Anglo Gold, alikuwa anafanya utafiti kwamba watumie njia gani kurudisha faida kwa jamii (CSR), kwamba wafanyie nini ili na wao washiriki katika uvunaji wa dhahabu, nikawaambia wasifanye hisani watupe bei inayofaa kwa madini yetu, akanijibu kuwa tungependa kufanya hivyo ila watanzania wakija kusaini mikataba, wanasaini tu hawafanyi mazungumzo yoyote wakati sisi tupo kwa ajili ya kutengeneza fedha. Sasa hayo ya viongozi wetu kuanguka na kusaini ndio yamezaa haya ya sasa.

PROF. SHUMBUSHO: NI MCHEZO WA KISIASA

Kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho, alisema kinachoendelea sasa ni mchezo wa kisiasa.

“Kila mtu anataka kuonesha umwamba wake, kuwa wapinzani hawakuwa kwenye serikali kwa hiyo mikataba hiyo imesababishwa na CCM.

“Lakini sioni cha maana katika vita hii kwa sababu wote tunakubaliana na Rais kuwa tuliumizwa sana kwenye mikataba ya madini, nani ameshinda sio suala la msingi, kubwa tumegundua kuwa kumbe tulikuwa tunaibiwa miaka yote hiyo, waliohusika wanatakiwa kuchukuliwa hatua, ila sasa Taifa ndio limeshinda.

PROF. MPANGALA: AZIMIO LA ARUSHA LINATUTAFUNA

Aidha, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala, alisema ripoti za kamati zote mbili zimeshughulikia machimbo matatu tu yaliyopo chini ya kampuni ya Acacia ili hali kuna machimbo 11 makubwa ya madini nchini.

“Ila imeonesha kwa jinsi gani tunaibiwa, sasa tunaibiwa hayo matatu kwa kiwango hicho, na sasa tuna machimbo makubwa 11, je itakuwa ni kiasi gani tumeibiwa? kwa kiwango tulichoibiwa inabidi kuweka matanga.

“Ni kilio na sababu yake ni sera na mikataba mibovu ambayo nimezaa sheria iliyosababisha tuibiwe kwa hali ya juu. Sasa mhusika ni nani ingawa wapo waliotajwa na wamenufaika ila hao walikuwa watekekelzaji tu wa sera iliyopo.

“Nimekuwa nikisema mara nyingi hawanielewa, kwamba dhambi kubwa ya Tanzania ni kulitupa Azimio la Arusha. Azimio lilizungumza mambo yote haya, kulinda rasilimali, madini yasichimbwe mapaka tuwe na uwezo, miiko ya uongozi, rushwa na ufisadi. Katika kipindi cha azimio hili hapakuwa na mambo makubwa kama hayo, sasa tukalitupa ingawa yale masharti ya Benki ya dunia na Shirika la Fedha duniani (IMF) tusingewewa kuacha kuyapokea ila wengi walioyapokea kwa kulinda misingi yao.

“Kuhusu ubinafsishaji walihakikisha vitu vya msingi hawabinafsishi, hata nchi za kibepari zilizoendelea njia kuu za uchumi zinamilikiwa na serikali lakini hapa kwetu hadi reli ilibinafisishwa kwa wahindi.  Sera ubinafsishaji ilikuwa ya hovyo, utalii umekufa… tembo wanauawa hovyo, kisa tumetupa azimio la Arusha.

“Ni kweli tumeibiwa pa kubwa, ila sasa ili tuweze kutatua tatizo tuangalie chimbuko ni nini. Lakini pia namshauri Rais aangalie sera ya nchi, hatuna sera wala dira, angeweka kwanza dira kwa kushirikiana na watanzania, namna gani tuendeshe kilimo, viwanda, kwa sababu tusifungue viwanda wakati wawekezaji wenyewe hatuwajui nao wataiba kama wa madini.

“Hatuna sera ya taifa, kujua mali tunayozalisha tunagawana vipi ni jambo la msingi, kwa sabbau ukianga Afrika kusini madini yameitajirisha sana nchi hiyo ila watu wake ni maskini wa kutupwa, hivyo lazima kuangalia mali za nchi ili ziwanufaishe.”