Home Habari TAIFA STARS DONDA SUGU

TAIFA STARS DONDA SUGU

301
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU,

MSEMA kweli ni mpenzi wa Mungu., vilevile mficha ugonjwa kilio kitamuumbua. Hakuna haja tena ya kuoneana aibu na kuendeleza itikadi za kuongoza timu kwa dhana ya bora liende.

Muungwana yoyote ni wazi hupenda kuambiwa ukweli kisha akaupokea na kuufanyia kazi. Hivyo ndivyo inavyoweza kuwa sehemu ya kuelekea mafanikio.

Mwenendo wa timu ya soka ya taifa ‘Taifa Stars’ bado siyo wa kuridhisha na hasa baada ya matokeo ya hivi karibuni kati yake na Lesotho ni dhahiri imeonesha wazi safari yake kuelekea kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani ‘CHAN’ ndio inaelekea ukingoni.

Katika mchezo huo Taifa Stars ilishindwa kabisa kutumia vema nafasi ya kucheza nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 katika Uwanja wa Azam Complex, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Inaweza kuwa ajabu kuitafsiria hayo timu ya taifa ilihali ndio kwanza ikiwa imecheza mechi moja tu kati ya sita inazotakiwa kucheza katika kundi lake la H kutafuta nafasi moja sambamba na timu za Uganda, Lesotho na Cape Verde lakini ukweli ni kwamba aina ya mchezo iliyocheza ndiyo inayozima ndoto za timu hiyo kufuzu.

Si ajabu kutamka wazi kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Salum Mayanga amevalishwa viatu vikubwa visivyolingana naye. Majukumu aliyopewa kuinoa timu hiyo ni makubwa mno kulinganisha na matokeo yanayosubiriwa  na watanzania wengi.

Taifa Stars ilicheza mpira mbovu mno pengine kuliko zama zingine zozote zilizowahi kutokea. Kocha Mayanga alitumia mfumo wa 4:4:2 ‘flat’ambao hakuna kocha anayeutumia duniani hivyo kumlazimu kuwatumia mawinga wawili wenye mbio Simon Msuva na Shiza Kichuya kupeleka mashambulizi mbele hali iliyopoozesha mchezo na kuwafanya Stars wasiwe tishio.

Ukiangalia uhalisia wa bao ililofungwa ni dhahiri ilikosekana nidhamu ya kimchezo kutokana na wachezaji wa safu ya ulinzi kushindwa kujipanga na kufanya ‘marking’ hasa katika eneo la hatari huku pia walinzi wa kati Bakari Mbonde na Abdi Banda wakipishana na  kumpa nafasi adui ya kufunga kirahisi na kusababisha matokeo kuwa sare.

Kifupi kocha Mayanga aliishiwa mbinu na wala hakuwa na ‘plan’ b ya kuweza kupindua hivyo matokeo yakabaki kama yalivyo. Dalili za kushindwa kimbinu zilianza toka aliposhindwwa kimkakati baada ya kupeleka kambi nchini Misri katika nchi ambayo hali ya hewa ni tofauti sana na alipocheza mechi yake.

Hii inadhihirishwa na kelele alizopigiwa kocha huyo toka alipotangaza kikosi miezi kadhaa iliyopita ambapo maoni ya wcahambuzi wengi wa soka hapa nchini waliweka wazi kuwa kikosi kilichaguliwa kwa mazoea kwa kuangalia majina fulani fulani na kusahau kuzingatia uwezo halisi wa mchezaji sambamba na aina ya mashindano inayokwenda kushiriki.

Kwa mfano wengi walilalamikia uteuzi wa mchezaji Thomas Ulimwengu ambaye toka atue nchini Sweden katika timu ya Fc Eskilstuna hajapata nafasi ya kucheza kutokana na kuwa majeruhi kwa muda mrefu lakini alichaguliwa katika kikosi hicho na hata katika ya hivi karibuni amedhihirisha wazi uwezo wake umeshuka.

Pamoja na kupangwa kama mshambuliaji wa mwisho katika mchezo huo tofauti na ilivyozoeleka akitokea pembeni hapo awali bado alishindwa kwenda na kasi tena hafifu ya Stars katika pambano hilo.

Lakini pia uteuzi wa Banda kama beki wa kati nao umetia shaka katika upangaji wa kikosi katika mchezo huo kwani ukweli ni kwamba mchezaji huyo ambaye ni kiraka ndani ya timu yake ya Simba lakini hajafanikiwa kucheza mechi nyingi akiwa kama mlinzi wa kati.

Kifupi ndani ya Simba, Banda ni chaguo la pili kama siyo la tatu kutokana na ukweli kuwa kupata kwake namba ni mpaka baada ya wale wa kikosi cha kwanza wanapokuwa na tatizo.

Lakini pamoja na kushindwa kwa kocha huyo, swali linaweza kuwa je nini asili ya soka la Tanzania?

Ukienda Brazili haitakuchukua muda mara moja utabaini asili ya soka la nchi hiyo ni samba. Ukienda Hispania halikadhalika utabaini asili yao ni lile soka la Barcelona yaani kutandaza chini mpira ‘total football’, hali kadhalika England, Ujerumani na nyinginezo kila moja ina asili yake.

Nchi zote hizo zimefanikiwa katika hilo kutokana na kuongozwa na falsafa ya ligi bora za nchi zao.

Wakati Kocha Mayanga analaumiwa kwa kushindwa kuonesha njia kwa timu hiyo,  ikumbukwe hakuna falsafa halisi ya soka la Tanzania. Kila kocha anayekuja anakuja na aina yake na kuondoka nayo sawa na mvurugano ambao mwisho wa siku wachezaji ndiyo wanaochanganywa.

Nakumbuka wakati kocha Mbrazil Marcio Maximo akitua kwa mara ya kwanza nchini kuifundisha Taifa Stars alikiri hilo kwa kuweka wazi kuwa soka la Tanzania halieleweki na ili kufanikiwa lazima ujengwe mfumo utakaoonesha aina yake halisi ya soka.

Ni kweli Kocha Mayanga hana jipya atakalolifanya kwa timu hiyo lakini pia wka mazingira yalivyo ni wazi kocha yoyote atakayekuja naye atakutana na changamoto nyingi lakini kwanza akitakiwa kutengeneza mfumo mpya utakaobaki kuwa nembo ya soka la Tanzania.

Kwa dhana hii ni wazi Taifa Stars ya sasa ina nafasi finyu na kamwe haiwezi kuifusu fainali za Chan achilia mbali zile za Afcon na hata Kombe la Dunia.

Nini hasara ya matokeo mabaya ya Taifa Stars wka mashabiki na wadau wengine? Kuna uwezekano mkubwa timu hiyoi ikakosa mashabiki pale itakapokuwa inacheza nyumbani.

Kwa hali hii kuna uwezekano mkubwa hamasa na ushabiki wa soka ukabaki zaidi kwa timu za wakongwe hapa nchini Simba na Yanga hususani lile pambano la watani wa hadi.
Mashabiki wa soka siku zote wao hupenda matokeo basi. Lakini pia huwa na uvumilivu kwa timu inayocheza kwa mipango na kuonesha matumaini.

Si ujinga kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kujitafakari na kuamua kuanza upya hasa kwa kumuangalia na kumpa jukumu hilo mshauri wa ufundi wa timu za vijana, Kocha Kim Paulsen.

Mafanikio yanayoonekana kwa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ yametokana kwa kiasi kikubwa na Kim ambaye alianza misingi imara ya ujenzi wa timu hiyo na zingine za vijana kabla ya kutimuliwa kazi na TFF.