Home Makala Kimataifa USHIRIKIANO WA UPINZANI UNAPOSHINDWA KUTWAA MADARAKA!

USHIRIKIANO WA UPINZANI UNAPOSHINDWA KUTWAA MADARAKA!

247
0
SHARE

NA HILAL k. SUED,

Katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja uliopita hali ya ushirikiano wa vyama vya upinzani Barani Afrika umekuwa ukikua, kupata nguvu na hata kufurahiwa na wengi.

Huko Senegal mwaka 2000 kikundi cha vyama vya upinzani kiliunganisha nguvu chini ya mwavuli wa “Sopi” – yaani “mabadiliko” na kufanikiwa kuung’oa utawala wa chama kimoja ulioduma kwa miaka 40.

Na mwaka 2002, upinzani nchini Kenya ulifanya vivyo hivyo. Katika uchaguzi wa 1992 na 1997 vyama vya upinzani vilishindwa na chama tawala – KANU ingawa vilikuwa vikipata zaidi ya asilimia 60 ya kura zote.

Lakini mwaka huo (2002) viliunganisha nguvu chini ya mwavuli wa National Rainbow Coalition – NARC na hivyo kukiondoa chama cha KANU kilichokuwa madarakani tangu 1963.

Na kuanzia 2000 ushirikiano wa vyama kabla ya uchaguzi umezibadilisha serikali katika nchi za Senegal (kwa mara ya pili), Liberia, Madagascar, Malawi, Mali, Mauritius, Nigeria na Gambia.

Na inasadikiwa kwamba katika uchaguzi wake wa 2018 Zimbabwe itajiunga katika orodha hii inayozidi kukua. Chama cha Morgan Tsvangirai cha Movement for Democratic Change (MDC) na kile cha Joice Mujuru cha National People’s Party (NPP) vimekubaliana kimsingi kuungana katika kumkabili Robert Mugabe na chama chake cha ZANU-PF.

Aidha vyama vingine ambayo vimeonyesha nia katika umoja huo ni chama cha Movement for Democratic Change-Ncube (MDC-N) cha Welshman Ncube, People’s Democratic Party (PDP) cha Tendai Biti, Zimbabwe African People’s Union (ZAPU) cha Dumiso Dabengwa’s na kile cha Simba Makoni cha Mavambo/Kusile/Dawn (MKD).

Iwapo utasimama huu utakuwa muungano mpana kwani umejumuisha wanasiasa maarufu nchini humo ambao wana wafuasi nje ya maeneo yanayojulikana ya upinzani.

Lakini katika kila muungano mmoja wa upinzani unaofanikiwa katika uchaguzi Barani Afrika, kuna mingine kadha inayoshindwa baada ya matumaini makubwa ya awali. Hivyo suala la kujiuliza ni kwa nini miungano mingine hufanikiwa na mingine hushindwa?

Wachunguzi wa masuala ya demokrasia Barani Afrika wanasema ishara moja iwapo umoja wa upinzani utashinda katika uchaguzi unatokana na hali ya siasa ya nchi ilivyo na namna sheria na kanuni za kuendesha siasa zilivyo. Hali ya namna hii inawezesha vyama kuunganisha nguvu katika mshikamano ambao hauwezi kuathiri hadhi yao na misimamo yao ya kisiasa.

Mwanasayansi wa kisiasa Nicolas Van de Walle anasema muungano wa vyama hufanya kazi vizuri pale unapoonekana kuwa na uwezekano mkubwa wa kushinda na hivyo kuwashawishi viongozi wengine wa chama tawala kuhama na kujiunga.

Hawa wanaohama si kwamba tu wanaongeza nguvu katika upinzani, lakini pia huwavuta wafuasi wengine wa chama tawala na hivyo kuweza kuvutia zile kura za wapigakura ambao hawajafanya maamuzi.

Kwa mfano kabla ya uchaguzi wa Nigeria wa mwaka 2015, chama cha All Progressives Congress (APC) cha Muhammadu Buhari kiliongezewa nguvu na viongozi waliohama kutoka chama tawala cha People’s Democratic Party (PDP) cha Goodluck Jonathan.

Hali kadhalika Zambia kwenye uchaguzi wa 2016, makumi ya viongozi walihama kutoka chama tawala cha Patriotic Front (PF) na kile cha Movement for Multi-party Democracy (MMD) na hivyo kuongeza kwa kiasi kikubwa matumaini ya kushinda kwa chama cha United Party for National Development (UPND) cha Hakainde Hichilema.

Hata hivyo hakikushinda. Kwa kiasi kikubwa hali ilivyokuwa katika uchaguzi huo wa Zambia inafanana na ilivyokuiwa kwenye uchaguzi wa hapa Tanzania mwaka mmoja nyuma – matumaini makubwa ya kushinda kwa umoja wa vyama vya upinzani chini ya mwavuli wa UKAWA yaliyeyuka.

Inaelezwa mkakati kama huu si wa kutegemea sana. Kwanza kabisa huwa vigumu sana kwa viongozi wa chama tawala kuhama. Na iwapo watafanya hivyo huwa ni kazi kubwa kwa wafuasi wa upinzani kuwapigia kura watu ambao hadi karibuni tu walikuwa sehemu ya serikali wanayotaka iondolewe madarakani.

Uganda ni mfano unaokinzana sana na ule wa Nigeria au Zambia ambapo kuhama vyama kwa viongozi si suala la gharama kubwa. Chama kikuu cha upinzani cha Forum for Democratic Change (FDC) cha Dr Kizza Besigye siku zote kimekuwa kinajitambulisha kama chama kinachoandamwa na kuonewa na utawala, kitu ambacho hudai si halali na kinyume cha katiba na sheria.

Katika hali ya namna hii huwa ni vigumu kuwashawishi viongozi wa chama tawala cha NRM kuhama na kujiunga na FDC. Isitoshe, iwapo viongozi wa chama tawala watahama inaweza kuwa kazi kubwa kuwakumbatia bila ya kuathiri hadhi ya FDC yenyewe.

Katika uchaguzi wa Uganda wa 2016 FDC ilijikuta katika wakati mgumu ambapo kikiwa kama sehemu ya muungano wa vyama vya upinzani (ambao FDC kilikuwa sehemu yake) uliamua kumuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani aliyefukuzwa, Amama Mbabazi kuwa mgombea wa urais wa muungano huo.

FDC ilijikuta ichague ama kumuunga mkono mtu ambaye siku zote alikuwa akipambana ndani ya serikali ya Yoweri Museveni, au kijitoe katika muungano huo. Kiliamua kujitoa muungano huo.

Wachunguzi wa mambo wanasema kilichotokea Uganda 2016 kiliathiri sana matumaini ya kungo’olewa kwa utawala wa miaka 31 wa Yoweri Museveni na kilitokana na kutokukubaliana nani awe mgombea wa upinzani baina ya Dk Besigye na Mbabazi.

Dk Besigye ana ufuasi karibu maeneo yote ya nchi ingawa hajawahi kupata zaidi ya asilimia 37 ya kura katika chaguzi tatu zilizopita.

Kwa upande wake waziri mkuu wa zamani Amama Mbabazi alikuwa hajulikani katika medani ya upinzani, lakini alikuwa maarufu sana kitaifa na alikuwa anafazifahamu njama zote za serikali kihusu masuala ya uchaguzi.

Lakini FDC ilikataa kumuunga mkono, ikajitoa na hivyo muungano wa upinzani ukaanguka.