Home Habari MAMILIONI YAYEYUKA KILIMANJARO

MAMILIONI YAYEYUKA KILIMANJARO

332
0
SHARE

NA SAFINA SARWATT, MOSHI

MADAI ya ufisadi ndani ya vyama vya Ushirika nchini yameendelea kuibuka baada ya hivi karibuni wanachama wa Chama cha  msingi cha Uru Shimbwe kuwatuhumu viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika Kilimanjaro (KNCU) kuchukua mamilioni ya fedha zao kinyume na taratibu. RAI linaripoti.

Tayari wanachama hao wameazimia kuwaburuza Mahakamani viongozi wa KNCU baada ya kushindwa kulipa deni la zaidi ya Sh. 113 milioni.

Tuhuma hizo zimekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuonya kuwa Serikali haitamsamehe mtu yeyote atakayejihusisha na ubadhirifu wa mali na fedha za Ushirika nchini.

Majaliwa alitoa kauli hiyo katika Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika mkoani Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine alisema Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali ikiwemo kuwapeleka katika vyombo vya dola wezi wa mali na fedha za ushirika kwani wamekuwa wakirudisha nyuma maendeleo ya vyama hivyo.

Wanachama wa vyama vya msingi wanadai kuwa KNCU  imekaa na malipo ya ushuru wa kahawa kwa miaka mitano mfululizo.

Mbali na kukaa na kuzuia ushuru, lakini pia KNCU imejikuta ikizongwa na deni hilo baada ya kuchukua mkopo kwa chama hicho kwa ajili ya kukusanya  kahawa katika msimu  wa mwaka 2015/2016.

Kufuatia deni hilo mkutano mkuu wa wanachama wa chama cha Uru shimbwe wameazimia kwenda kukamata mali za KNCU na kuiburuza mahakamani.

Wanachama hao tayari wamemwagiza Mwenyekiti wao kuchukua hatua za makusudi ili kurejesha fedha hizo mara moja na endapo fedha hizo hazitarejeshwa kama walivyokubaliana wataifikisha KNCU mahakamani kwa

matumizi mabaya ya mali za wanachama, ambapo fedha hizo zilichukuliwa bila kufuata taratibu zinazotakiwa.

Mwenyekiti wa chama msingi Uru Shimbwe, Deudatus Temba, alikiri KNCU kuchukua fedha kwao kwa ahadi ya kuzirejesha.

Temba alisema KNCU waliiandika barua kwa  chama chao wakitaka kupewa mkopo wa  Sh.75 milioni,  ambapo waliahidi kurejesha kwa riba ya asilimia 15 pamoja na kuwalipa fedha za malipo ya ushuru ambazo ni zaidi ya milioni 28.3.

“Deni hilo ni la muda mrefu sasa, KNCU walikosa fedha za kukusanyia Kahawa  katika msimu uliopita ya mwaka 2015/2016 kutoka kwa wakulima na kutoa mwongozo wa barua ya kutaka chama msingi Uru Shimbwe kutoa milioni 75 kwa makubaliano ya kuirejesha kwa riba ya asilimia 15 kwa mwaka, lakini mpaka sasa bado hawajarejesha fedha hizo,”  alisema.

Mmoja wa wanachama hao, Bertin Mkani alisema suala ambalo limejitokeza ni la aibu kwa sababu hatua ya KNCU kuchukua fedha za chama cha msingi  bila kurejesha ni sawa na baba kulaghai mwanae.

“Tupo tayari kwenda kwa Waziri mwenye dhamana  kuishitaki KNCU kwani fedha hizo zilikuwa zimepangiwa matumizi na wanachama kwenye mkutano ulipita kuwa zikanunulie gari kwa ajili ya kuanzisha mradi wa usafirishaji wa abiria.

“Mbaya zaidi kinachotushangaza bodi imehusika kutoa fedha za wanachama bila kufuata taratibu zinazotakiwa ambazo ni kuitisha mkutano wa wanachama ili wakubali kutoa fedha,” alisema.

“Azimio la kwanza tunalifikisha suala hilo kwa mrajisi wa vyama vya ushirika pamoja na Waziri wa Kilimo kuishitaki KNCU, baada hatua hizo tutakwenda kuiburuza mahakamani,  alisema.

Afisa ushirika wa Halmashauri ya Wilaya Moshi, Eliyona Omar, alikiri kulijua suala hilo, hata hivyo alisema fedha hizo zilichukuliwa bila ofisi yake kushirikishwa jambo ambalo ni kinyume na taratibu.

“Nimeagiza uongozi wa KNCU warejeshe mara moja fedha hizo, kwani hakukuwa na ridhaa ya Mrajisi Mkuu.

“Kutokana na mkopo huo kukiuka taratibu zinazotakiwa nimeagiza kwamba barua iandikwe kwa uongozi wa KNCU kurejesha fedha hizo na pamoja na riba zake, kwani ofisi yangu haijashirikishwa hivyo walikiuka taratibu na hakuna maazimio ya wanachama kwa hiyo mkopo huo haupo kisheria,” alisema.

“Cha msingi bodi ifuatilie suala la malipo ya ushuru wanayodai kwa zaidi ya miaka mitano mfululizo kwani KNCU walidai biashara ilienda vibaya lakini fedha ya mkopo ya million 75 lazima zirejeshwe pamoja na riba zake,” alisema.

Akizungumzia madai hayo Mwenyekiti wa KNCU , Aloyce Kittau, aliliambia RAI kuwa madai hayo hayajui, lakini atayafatilia kwa Meneja Mkuu wa Ushirika huo, Honest Temba.

“Haya mambo huenda yamefanyika kabla ya uongozi wangu, lakini pia kwa sasa siko ofisini, naomba muda nilifuatilie suala hili,” alisema.