Home Latest News MMILIKI VICHWA VYA TRENI HUYU HAPA

MMILIKI VICHWA VYA TRENI HUYU HAPA

1698
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI,

WAKATI Taasisi na Idara za Serikali zikikana kuhusika na vichwa 15 vya treni vilivyoingia nchini bila mkataba wowote, RAI limebaini kuwa mmiliki halali wa vichwa hivyo ni Shirika la Reli Tanzania (TRL).

Ukweli wa suala hilo unathibitishwa na kauli aliyopata kuitoa Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Masanja Kadogosa alipofanya mahojiano yaliyochapishwa kwenye kurasa za katikati za gazeti hili toleo namba 1281 la Desemba 15,2016.

Katika mahojiano hayo  yaliyobebwa na kichwa cha habari ‘TRL: Mageuzi makubwa usafiri wa reli yaja’ pamoja na mambo mengine, Kadogosa aliweka wazi kuwa katika kuboresha usafiri huo Shirika hilo limeagiza vichwa 13 vya treni kutoka Afrika Kusini.

Kauli hiyo ya Kadogosa ilikuja baada ya kuulizwa swali lililotaka kujua ulipofikia mpango wa kununua vichwa 11 (hatukuwa na uhakika na namba) vya treni kutoka Afrika kusini.

Akilijibu swali hilo, Kadogosa alisema: Bado mpango huo upo, tunaendelea na taratibu, ila pia tayari tumeshanunua kutoka huko Afrika kusini vichwa 13.

Hata hivyo Kadogosa hakuweka wazi kuwa vichwa hivyo viligharimu kiasi gani na ni kampuni gani ya Afrika Kusini iliyouza vichwa hivyo kwa TRL.

Ukweli wa TRL kuwa mmiliki wa vichwa hivyo unathibitishwa pia na vichwa vyenyewe kuwa na nembo ya Shirika hilo, lakini pia kauli aliyoitoa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko inatosha kuujulisha umma mmiliki wa vichwa hivyo ni nani.

Kakoko aliweka bayana kuwa vichwa hivyo vina nembo ya TRL na kwamba kilichopo ni kutokea kwa mgogoro kati ya shirika hilo na kampuni iliyotengeneza vichwa hivyo baada ya kubainika kuwa mchakato wake wa ununuzi haukuwa sahihi.

Pamoja na ukweli huo kuwa wazi, TRL ilivikana  vichwa hivyo mara baada ya Rais Dk. John Magufuli kufichua hadharani  uwapo wa vichwa hivyo Bandarini.

TRL ilidai kuwa haihusiki kwa namna yoyote na vichwa hivyo kwa kuwa hakuna taarifa zozote zinahusu uagizwaji wake.

Alisema TRL haivitambui vichwa hivyo kwa kuwa si mali yake. “Hivi ni vichwa vikubwa sasa kwanini tuvikatae kama ni vyetu, ila ukweli ni kwamba hatuvitambui kabisa,” alieleza.

VICHWA VIWILI VILISHATANGULIA

Kwa mujibu wa taarifa iliyowahi kutolewa kwa vyombo vya habari na TRL Machi 23, 2015 ilibainisha kuwa vichwa viwili kati ya 15 vya treni vilivyonunuliwa na shirika hilo vilipokelewa katika Bandari ya Dar es Salaam Machi 21, 2015.

Taarifa hiyo ilisema vichwa hivyo vimetengenezwa nchini Afrika Kusini na kwamba ununuzi huo umegharimu kiasi cha Sh70.9 bilioni ambazo zote zilishalipwa.

“Vichwa hivi vilivyopokelewa na TRL vimetengenezwa  kupitia mkataba kati ya TRL na kampuni ya EMD ya Marekani, huku utengenezaji wa ukifanywa na kampuni ya DCD ya nchini Afrika kusini,ambapo vichwa vyote vimeghalimu kiasi cha shilingi bilioni 70.9 pesa za kitanzania na tayari zimeshalipwa.

“Aidha, vichwa hivi vinatarajiwa kupokelewa na TRL kwa awamu tatu, ambapo katika awamu ya kwanza tayari vichwa viwili vimeshapokelewa, awamu ya pili itafanyika Aprili mwaka huu (2015) ambapo vitapokelewa vichwa vitano, huku awamu ya tatu itafanyika juni (2015) kwa vichwa sita.

“Tofauti na vichwa vya zamani, kichwa kimoja kinaweza kubeba tani 32,500 kwa mwaka tofauti na tani 25,00 kwa vichwa vya sasa vinavyotumika ambapo mbali na vichwa hivyo TRL imepokea vitendea kazi vingine vikiwamo, Mabehewa  214 pamoja na mtambo wa kunyanyulia mabehewa (Breakdown crane).

“Mradi huu ni moja kati ya mpango wa serikali kuifufua  TRL chini ya mpango Tekeleza kwa matokeo makubwa sasa BRN, mpango ambao utawezesha kusafirisha tani  milioni 3 kwa mwaka kuanzia mwaka 2016 kutoka tani 200000 kwa mwaka 2014, mbali na hili kupatikana kwa mabehewa itasaidia TRL kusafirisha  abiria mara tatu kwa wiki tofauti na mara mbili kwa sasa hali ambayo itasaidi kukuza ufanisi wa shirika hili,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari.

MCHAKATO

Pamoja na mambo mengine taarifa zinaonesha kuwa mchakato wa ununuzi wa vichwa hivyo vya treni ulianza mwaka 2012 baada ya aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe kupokea mapendekezo ya  Kamati Ndogo ya Ushauri na Kutengeneza Sera za Reli.

Dk. Mwakyembe alisisitiza kuwa serikali itaagiza vichwa vipya 13 vya treni kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kutoa huduma bora za reli

Alisema vichwa vya kukodi vinakuwa ni mzigo mkubwa kwa serikali hali inayofanya kutumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kuviendesha huku baadhi vikiwa ni chakavu.

Kamati hiyo ndogo ya Ushauri na kutengeneza Sera ya Reli iliundwa ikiwa na majukumu mbalimbali chini ya Mwenyekiti wake, Mhandisi Dk. Malima Bundara.

Mhandisi Dk. Bundara alikuwa mjumbe wa Bodi ya TRL kabla ya kung’olewa na Rais Magufuli, Desemba 2015, pia alikuwa Rais wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET).

Katika kipindi hicho kamati hiyo ilibaini changamoto nyingi ikiwemo ya udhaifu wa usafiri wa reli.

RAI lilizungumza na Dk. Bundara ili kutolea ufafanuzi suala hilo,  ambapo pamoja na mambo mengine alitaka kupatiwa maswali kwa njia ya maandishi.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Rais Dk. Magufuli ndio aliyeliibua sakata hilo baada ya kusema kuwa kuna vichwa 15 vya treni vilishushwa katika bandari ya Dar es Salaam lakini havina mwenyewe.

“Inawezekana vipi vichwa vya treni vinafika hapa bandarini, vinashushwa lakini mwenyewe hajulikani! Ni kwa sababu hakuna coordination, huo ni mchezo mchafu. Vyombo vya dola vianze kuwachunguza hao”

“Vichwa 15… wamefanya mission yao na havihitajiki, TRL wanasema hawajaagiza wala hakuna document (nyaraka) yoyote waliyosaini ya kusema wanahitaji lakini vimekuja vikateremshwa hapa wala hamuulizi vimetoka wapi, walivyomaliza kuteremsha TPA ndio mkaanza kuuliza wakati meli ilishaondoka na vichwa vyenyewe inasemekana ni vibovu.

“Ni lazima hapa kulikuwa na mchezo na inawezekana rushwa ilikuwa inatembea. Nina hakika wizara mtakaa, inawezekanaje vichwa vinateremshwa bila kujua vinaenda wapi,” alisema.

Wakati Rais Magufuli akitoa kauli hiyo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani naye alimuunga mkono na kusema kuwa wizara haikuwa na taarifa juu ya ujio wa vichwa hivyo na kwamba taarifa ya Rais ni sahihi.

VIGOGO KUTUMBULIWA

Kubainika ukweli wa sakata hili kunatajwa kuwa na nafasi kubwa ya kung’oka na vigogo wa wizara, TRA na TRL kutokana na manunuzi yake kutia shaka.

Mbali ya kuwepo kwa shaka kwenye manunuzi, lakini pia hatua ya wahusika wa vichwa hivyo kuvikana kwa nia ya kujisafisha mbele ya Rais nako kunaweza kuwa hatua nyingine itakayomlazimisha Rais kutumbua baadhi ya vigogo wa Idara na Taasisi hizo zilizohusika.

Ukweli huo wa baadhi ya vigogo kuwa mtegoni hasa kwa kumdanganya Rais unabebwa na ukweli kuwa kiongozi huyo wa nchi hapendi uongo kwani alishawahi kumtumbua mteule wake Anne Kilango Malecela wakati huo akiwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Kilango alitumbuliwa kwa madai ya kutoa taarifa potofu juu ya wafanyakazi hewa, ambapo yeye alisema hakuna mfanyakazi hewa kwenye mkoa wake huku taarifa ya uchunguzi uliofanywa na Ikulu ukibaini kuwapo kwa wafanyakazi hewa 45.