Home Makala BUSARA YA MWALIMU NYERERE KURUDISHA VYAMA VINGI BADO HAIKUBALIKI  

BUSARA YA MWALIMU NYERERE KURUDISHA VYAMA VINGI BADO HAIKUBALIKI  

234
0
SHARE

 NA SHERMARX NGAHEMERA


KWA Watanzania wadadisi, wameshaanza kuona shida iliyoletwa na kudharau maoni ya wengi ambayo ilitumiwa na Mwalimu Nyerere katika kurudisha vyama vingi katika Katiba na mwenendo wa siasa nchini unavyotikisa taifa.

Bila shaka kila Mtanzania makini na mwenye mapenzi mema na taifa hili atakuwa analo jibu sahihi la namna mchakato wa Katiba ulivyokuwa katika Awamu ya Nne na kuanzishwa Ukawa. Ni mwendelezo wa kile kile alichokidharau Mwalimu Nyerere.

Wajuzi wa mambo wanasema siasa ni kila kitu katika maisha ya binadamu, haikwepeki kwa maisha ya binadamu ya kileo, kwani kazi na matokeo yake yamesheheni kila upande upitao na kila uchao.

Ukiwa mwanasiasa au siyo utaguswa na maisha ya kila siku, kwani maisha siku hizi ni siasa na hivyo utazikuta semi kama hizi ni siasa za familia na hata mke na mume. Kwa maana kuwa kile ukionacho au kukiamini sio halisi, yaani ‘si-hasa’ au siasa.

Unaguswa na siasa katika kila pembe ya maisha, kwani mchezo wa wanasiasa una athari kwa mengi, kwani wameshikilia rasilimali za nchi, mkoa, wilaya, kata na familia, kwani maisha ni zao la siasa.

Utakwenda hospitali ukikuta au kutokuta dawa au daktari ni matokeo ya matendo ya wanasiasa, dukani ukikosa sukari au bei yake haishikiki ni tokeo la wanasiasa na una haki kulalamikia wao.

Wangapi tunalalamikia hali mbaya ya kupanda gharama za maisha kwa ujumla wake; wanasiasa wanahusika hapo, kwani rasilimali zetu wameshikilia wao na wanafanya maamuzi mbalimbali ambayo yanatufikia sisi katika muundo mzima wa uwakilishi.

Demokrasia inajali sana uwakilishi na hivyo tujali sana wale ambao tunawachagua kutuwakilisha, kwani si hoja wakajijali wao zaidi yetu na kutuhujumu. Hujuma hufanyika kwa kujali sana siasa kuliko ukweli wa mambo na hivyo huvunga kufa.

Ni kawaida enzi hizi kuwa na wanasiasa wasio na upeo wa kutenda, bali kuitanguliza siasa mbele kama chombo kikuu cha utendaji wao. Ni wajasiriamali wa siasa!

Ni ukweli ambao unatusuta sasa na kuleta sintofahamu kwa wote wanasiasa, yaani chama tawala (CCM) na vyama mbadala vya upinzani kuwa wakati wa mchakato wa kurudisha mfumo wa vyama vingi mwanzoni mwa miaka ya tisini, ni Watanzania asilimia 80 kati ya 100 ndio waliopiga kura zao za kuukataa mfumo huo na asilimia 20 zilizobaki ndio walioukubali mfumo wa vyama vingi na kadiri tunavyokwenda tunathibitisha kuwa ni hali halisi kile ambacho tulikipuuza awali.

Chakushangaza Mwalimu Nyerere, Baba wa Taifa, alibeza mawazo ya wengi na kuweka yake kuwa ni bora, nchi ikawa na vyama vingi na kweli ikawa akidai kuwa anatunusuru na majanga ya utawala wa chama kimoja, huku akisisitiza kuendelea na muundo (structures) wa chama kimoja kwa kudai kuwa mabadiliko yatakuja polepole na watu watabadilika nayo. Alikataa mabadiliko, lakini alipenda mtazamao mpya unafanyaje na upacha huu?

Tumebadili nini idadi ya vyama, sura za watawala au muundo wa maisha au misingi ya taifa? Hiyo ndiyo vurugu ya nchi kama inavyojiashiria katika vyombo vyake na hasa kile kinachoitwa mhimili wa Bunge, ambapo ni mkusanyiko wa watu wenye itikadi tofauti, wanaotaka kucheza shere kwa kisingizio kuwa wanawakilisha Watanzania wakati hawana cha Utanzania. Ni mkusanyiko wa watu wasiochangamana (strange bedfellows) na hivyo ni vurugu tupu.

Si rahisi kukubali, lakini kinachoendelea bungeni hakina maudhui ya siasa ya vyama vingi, bali inadhihirisha wazi kuwa tuko kutekeleza kile ambacho hakiko kwenye ajenda na wabunge, si wenyewe, ila wanawakilisha watu na si majimbo yao na hawana la kwao, ila kuambiwa nini cha kufanya. Hivi basi hawa ni wachezaji wa kulipwa na si walio na utashi kwa yale wanayofanya. Sina maana ya kudharau au kukebehi, bali ninaeleza hali halisi ya kile kilichopo ili kufanya tafakari na kujirudi. Hakuna mkosaji hapa.

Kila mtu Bungeni analalamika, yaani Spika, Naibu Spika, wabunge, wenyeviti wa kamati na wengineo kwa nafasi zao wanalalamika na hakuna wa kumlaumu. Kwa nini?

Kwa kifupi hatukuwa tayari kwa vyama vingi na umma haukutayarishwa kwa ujaji huo kwa maana ya kulazimishwa tu na umaarufu wa Mwalimu Nyerere na si mahitaji halisi ya umma.

Hali hii ni doa kwa taaluma ya takwimu na siasa za nchi, kwani kulikuwa na maana gani kuzunguka nchi nzima wakati Nyerere alikuwa na jibu mfukoni? Sioni namna ya kuzungumza bila kumtaja Baba wa Taifa, kwani kila ninapotazama ninamkuta yupo na anahusika.

Ingawa sasa yeye hayupo na si vizuri kuongelea watu waliokwenda mbele ya haki, historia iliwapendelea na hivyo wachwe na wapumzike kwa raha ya milele.

Haitoshi kukubali na kufikiri kuwa watu wenye busara zao na wenye upeo wa kuona mbali waliojiona wameshindwa kufikisha kura za kutimiza azima yao walisaidiwa na Marehemu Baba wa Taifa kwa kauli yake maridhawa ya uamuzi wa asilimia 20 ya wanaokubali mfumo wa vyama vingi uheshimiwe. Huko ni kuona mbali kwa karibu, kama vile kuona mbali mwezi na kuwa karibu wakati wa usiku kama vile umebadilisha umbali, kumbe ni mtazamo na hali tu. Umbali wetu na mwezi uko palepale. Sasa tuko sabini kwa thelathini, imesogea kidogo kueleka upinzani baada ya miaka zaidi ya 30.

Bila shaka Mwalimu Nyerere aliona mbali ya mbali, kwani aliona siku moja Tanzania yasije yakatokea kama yaliyowakuta madikteta suriama (benevolent dictators) na hivyo ikawa kwa CCM na watawala wake kugeukwa na kulalamikiwa kuwa madikteta kwa kuzika upinzani. Aliona afuate mawimbi na sio maporomoko au upepo.

Kiutawala uwepo wa upinzani  kimsingi ndio chachu ya mabadiliko ya taifa lolote lile linaloheshimu mfumo huu, utawala unaotokana na mfumo huu lakini pia unaosimamiwa na utawala wa haki na sheria kwa vitendo na kutumia matokeo ya tafiti sahihi na sio kauli za wanasiasa majukwaani zinazominya mifumo na mwenendo mzima wa taifa.

Tulikuwa na haraka gani badala ya kukubali matokeo ya Tume halafu tungejipanga na kuelimishana na baada ya miaka mitano au kumi kupiga kura tena ya vyama vingi au vitatu ili kupata ushindani pevu, badala ya hali iliyopo ya vyama 23 wakati vyama 18 ni vya kifamilia, koo au kikabila?

Tunapata faida gani ya utitiri huu wa vyama vya siasa?

Je, demokrasia imeongezeka wakati ni vyama vitano tu au sita kwa sasa vina wabunge na madiwani? Hivi tunamdanganya nani na kwa faida ya nani? Kwa nini tumejenga dhana ya kuwa kila kitu kiwe cha kitaifa na wala si kuwa cha jimbo, mkoa au wilaya na kulazimisha kuwa tuko wamoja, wakati tuko vipande vipande na sisi wengine tunaburuzwa tu katika mfumo usiojali uwepo na utofauti wetu? Ninaomba tubadilike na kuwa wakweli na nafsi zetu badala ya kujaza ripoti zenye kubeba dhambi ya kusema uongo kwa maslahi ya wachache ili wawe watawala.

Mwalimu aligundua CCM ilikuwa imara wakati wa enzi za utawala wake, kwani alitembea kwa kile alichokisema na kuishi kwa urefu wa kamba yake, bila kujilimbikizia mali na aliyemfuata alikuwa muungwana aliyefikiri kila mtu yuko kama yeye  kuwa  hewala sio utumwa na sio kuwa wajasiriamali wa siasa!

Urahimu wa Rais Ali Hssan Mwinyi ulifanana na ule ukata wa Mwalimu Nyerere, lakini baada ya hapo nchi ilianza kumiliki sifa nyingine na kuachana  na maisha ya wachamungu hao kwa kuliongoza taifa na kuingiza  umagharibi  uliosheheni uleo na hivyo kwa maono  yao lazima tunukie waridi, ingawa sisi tuna  nanasi, embe, ndizi,  vyote vina harufu nzuri, lakini hatukuviendeleza kuvuna rehe yake wala rujuwa, ili nasi tuwe na cha kwetu mbele ya watu. Tukaifuata waridi kwa gharama kubwa bila sababu ya msingi.

Sitaki kumsema Nyerere, lakini yeye alishaonesha kuwa ni mtu wa mabadiliko, kwani alikwenda China akiwa Mmagharibi, akivaa suti ya pande tatu, lakini alirudi China akiwa mtu mpya aliyevaa Kimao na hakuvaa tena suti ya pande tatu, ila ya jirani yake inayoitwa suti ya Kaunda.

Nyerere kwa kweli maono yake ya mbali aliwasaidia asilimia 80 ya Watanzania ambao kama alivyo yeye mwanafalsafa, alishitushwa sana na ukweli wa mambo na moyoni mwake aliamini kuwa wananchi wake  walikuwa ni wajinga wa ufahamu wa mwenendo wa dunia.  Alijutia hali hiyo, kwani aliwanyima kuiona dunia katika hali yake halisi kwa kuzuia runinga kuwako nchini na wanamtegemea yeye aone mambo halafu awaeleze nini kinaendelea.

Ndivyo  ilivyokuwa na hivyo ilikuwa mwafaka kwake na nia nzuri  yake ilikuwa kuwawezesha hawa wajinga wa asilimia 80 wapate msisimko wa mfumo huu wa vyama vingi ili hatimaye waungane na asilimia 20 ambao tayari walikuwa wameukubali mfumo huu na kuutumia kuiondoa CCM. Ni kosa kubwa sana.

Nyerere alishindwa kuelewa athari ya utawala wake kwa watu na uwanja wa siasa; hakujua kuwa yeye ni kila kitu kwao na watamsikiliza na kumfuata, lakini mantiki itamshushua, kwani Watanzania wana mtazamo na imani tofauti na si rahisi na kuwa alifanikiwa kutengeneza taifa na sio utawala. Ndiyo! Mambo hayakuwa mabaya kwa kuwa na upinzani na damu haikumwagika, lakini mantiki inadai kuwa, haki ya wengi iliminywa na matokeo yake ni zile vurugu, kutoleana na kusemana mabaya Bungeni.

CCM hakikuwa chama cha Nyerere pekee, bali chama cha Watanzania wote, kwa hiyo kuna watu wanaona walionewa kwa kulazimishwa kuwepo vyama vingi na hivyo kuwachukulia wapinzani wote kama hawastahili kuwepo Bungeni hapo (impositors).

Ni dhambi ya asili ya siasa za Tanzania ya leo na hivyo Bunge halitatulia mpaka maelezo ya kuridhisha yapatikane kumnusuru Mwalimu au elimu ya vyama vingi iingizwe kwenye mitaala. Ndiyo kila kitu kwa kupitia shule, hata madawa ya kulevya kwa nini isiwe demokrasia kama demokrasia?

Wapinzani wanawaona wenzao kuwa ni mbumbumbu kwa sababu hawakuona mapema ujio wa vyama vingi na hivyo watolewe na ikibidi hata kwa nguvu, kwani ni zamadamu.

Nguvu ya ziada inatakiwa ili tuwe kawaida kisiasa, kwani yale yanayoelezwa na kufanywa na wabunge wetu ni njiapanda tuliyonayo katika uwanja wa siasa. Tubadilike kwa kuwa na mitazamo sahihi na ukweli kwetu wenyewe.