Home Latest News CHADEMA WANAMPENDA SANA LOWASSA!

CHADEMA WANAMPENDA SANA LOWASSA!

589
0
SHARE

NA MARKUS MPANAGALA,

MARA nne nimemsikia Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, akibainisha kuwa atagombea urais ifikapo mwaka 2020. Lowassa ni mwanachama wa Chadema na Mjumbe wa chama hicho tangu mwaka 2015 alipohamia akitokea CCM.

Matamshi yake ya kusema atagombea urais mwaka 2020, huwa yanaifikirisha sana na kuhitimisha labda Chadema wanampenda sana Lowassa ndiyo maana anao uhakika wa kugombea urais awamu ya pili kupitia chama hicho.

Lowassa aligombea urais kwa tiketi ya Chadema mwaka 2015 ikiwa ni mara yake ya kwanza kuwania urais kupitia chama cha upinzani nchini.

Uamuzi wa kugombea urais kupitia Chadema, ulikuja baada ya kukatwa ndani ya CCM chini ya uenyekiti wa Jakaya Kikwete. Kukatwa kwa mwanachama kwenye chama chochote ni jambo la kawaida, licha ya kwamba wapo wanaodhani chama kikitenda haki dhidi yake ni uasi. Lakini chama hicho hicho kikitenda haki kwa ajili yake kinaonekana kuwa kizuri sana na atakimwagia sifa lukuki.

Hata hivyo, kwa mwanasiasa suala la kukatwa linakuwa na tafsiri nyingi na sababu zinakuwa pomoni zikiambatanishwa na manung’uniko ya kuonewa.

Mathalani, kukatwa kwa Lowassa ndani ya CCM hakukunishangaza hata kidogo, kwa kuwa nilifahamu hatokuja kuvuka kikwazo hicho chini ya Mwenyekiti Jakaya Kikwete.

Sina uhakika kama Lowassa mwenyewe alifahamu kuwa atakatwa, lakini alichelewa sana kujitenga na CCM toka mwaka 2008 baada ya kujiuzulu uwaziri mkuu.

Wataalamu wa masuala ya ulinzi na usalama wanasema urafiki wa wanasiasa au mtu yeyote (binafsi nimetokewa haya mara nne kwa ngazi za chini), huwa unakoma pale mmoja anapokuwa mkuu wa dola au kukitumikia chombo cha dola katika nafasi yoyote ile.

Hiki ndicho kilichotokea mara baada ya Jakaya Kikwete kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakukuwa na urafiki tena kati ya mkuu wa dola na rafiki yake wa zamani. Tukiambiwa kuwa bado ni marafiki tunachezwa shere tu. Labda baada ya kustaafu.

Ndiyo kusema mkuu wa dola akiwa rafiki yako usitegemee hata siku moja akaja kufanya mambo kwa kigezo cha urafiki wenu. Haitakuja kutokea. Ukibisha hilo muulize kilichomtokea Charles Kitwanga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Muungano.

Sasa basi, tukirudi kwenye hoja kuu ya Lowassa na uchaguzi wa mwaka 2020, kuna swali moja linanisumbua; mwanasiasa huyo nguli atawania urais kupitia tiketi ya chama gani?

Tunanfahamu yeye ni mwanachama wa Chadema, lakini utamaduni wa chama hicho haumpatii nafasi ya pili Lowassa kuwa mgombea wao wa urais mwaka 2020.

Uchaguzi wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi ulipofanyika mwaka 1995, Chadema hakikusimamisha mgombea wa urais. Mwaka 2000 pia Chadema hakikusimamisha mgombea wa urais.

Mwaka 2005 Chadema kikamsimamisha Freeman Mbowe kuwa mgombea urais. Baada ya kinyang’anyiro hicho,  Mbowe alitajwa kushika nafasi ya tatu nyuma ya Jakaya Kikwete na Profesa Ibrahim Lipumba.

Katika uchaguzi wa mwaka 2010, Freeman Mbowe hakugombea urais, badala yake Chadema kilimteua Dk. Wilbroad Slaa ambaye alikuwa Mbunge wa Karatu kupeperusha bendera ya chama hicho.

Mwaka 2015, Dk. Slaa hakugombea urais, badala yake Chadema kilimteua Edward Lowassa, kupeperusha bendera ya chama hicho kwa kushirikiana na baadhi ya vyama vya upinzani kama vile NLD, NCCR-Mageuzi na CUF kuunda umoja wao ulioitwa Ukawa.

Sasa sikiliza!

Kutoka mwaka 2005 hadi mwaka 2015, utaona kuna kikwazo kikubwa kwa Lowassa kugombea tena urais kwa tiketi ya Chadema. Labda itokee kwamba Chadema wanampenda sana Lowassa kiasi kwamba hawana kauli nyingine zaidi ya kusema “Ndiyo Mzee.”

Mwaka 2005 Chadema ilikuja na mgombea mpya, Freeman Mbowe. Mwaka 2010 hakugombea, ikiwa na maana mwaka huo Chadema ilikuja na mgombea mpya, Dk. Wilbroad Slaa aliyepambana na Jakaya Kikwete.

Mwaka 2015, Chadema ilikuja na mgombea mpya wa urais, Edward Lowassa. Ndiyo kusema Dk. Slaa hakupewa nafasi ya pili kugombea urais kwa tiketi ya Chadema.

Katika muktadha huo utaona kuwa Chadema ina utamaduni wa kipekee kwenye suala la uteuzi wa wagombea wa urais nchini tangu kilipoanza kusimamisha wagombea wake.

Litakuwa jambo la ajabu kuona Chadema wakisaliti utamaduni waliojijengea kwa kumpa nafasi ya pili Lowassa. Ndiyo maana nabaki na swali, Lowassa atagombea urais kwa tiketi ya chama gani?

Kama kusema atagombea bila kuitaja Chadema labda tukubaliane na manazi wa Chadema kuwa Lowassa atagombea urais mwaka 2020 kwa tiketi ya chama kingine. Kwamba anaweza kugombea kwa tiketi ya CUF, NCCR, NLD, TLP, UDP, Chauma au kingine chochote atakachochagua.

Vinginevyo utamaduni wa Chama cha Chadema ni kikwazo kwa Lowassa, sababu kila mwaka wa uchaguzi kwenye nafasi ya urais wanakuja na mgombea mpya.

Kusema hivyo si kwamba Chadema hawawezi kubadilisha utaratibu huo, bali namna walivyojenga taswira ya chama chao inatuwia vigumu kuamini kuwa Lowassa atapewa nafasi ya pili.

Jambo la mwisho la kukumbushana kwamba kile kilichomtokea Dk. Slaa kwenye mbio za kuelekea uchaguzi wa mwaka 2015 na ndicho kitakachompata Lowassa. Yaani kukatwa au kutupwa nje ya kinyang’anyiro.

Namna alivyokatwa Dk. Slaa ndivyo ambavyo Lowassa atakakatwa na Chadema. Sioni uwezekano wa yeye kuwa mgombea urais mbele ya mwenyekiti wa sasa Freeman Mbowe.

Na labda mgombea atakuwa mtu mwingine kabisa ambaye ataibuliwa kwa staili ile ya Dk. Slaa au ya Lowassa. Labda Frederick Sumaye. Labda Josephat Gwajima. Yote yanawezekana.

Baruapepe; mawaazoni15@gmail.com