Home Makala MAGARI YANAPOKUWA MATESO KWA BINADAMU

MAGARI YANAPOKUWA MATESO KWA BINADAMU

116
0
SHARE
Moja ya ajali katika barabara zetu

NA HILAL K. SUED,

WAKATI barabara zetu katika maeneo ya mikoani bado zinaendelea kuwanyemelea wanazozitumia, wasafiri na watembea kwa miguu kutokana na vifo na ulemavu, zile za mijini hasa katika Jiji la Dar es Salaam, zinasababisha mateso ya aina yake katika misongamano ya magari.

Tofauti kubwa baina ya hayo mawili ni katika spidi. Katika barabara za mikoani ni mwendo wa kasi ambao ndio umekuwa ukiathiri maisha ya wananchi, lakini jijini Dar ni ‘mwendo wa konokono’ ambao umekuwa ukiwakasirisha na kuathiri watumiaji wa vyombo hivyo.

Na katika hali zote hizo mbili mamlaka husika, pamoja na jitihada wanazofanya, bado wanashindwa kudhibiti hali hiyo. Sababu kubwa ya kushindwa huku mi kwamba suala zima linahusu magari, vyombo vya barabarani ambavyo vinatoa tafsiri muhimu kuhusu tabia ya binadamu.

Katika kitabu chake ‘The Magnificent Ambersons’ mtunzi wa riwaya Mmarekani, Booth Turkington, aliandika hivi: “Pamoja na mionekano yao ya daima ya kuangalia mbele, magari ni hatua moja nyuma katika ustaarabu wa binadamu, kwani bado haiaminiki iwapo yanaongeza ubora wa ulimwengu na anasa katika maisha ya binadamu, isipokuwa vifo na kuvunjika kwa mifupa. Kusema kweli, magari hayakutakiwa kuvumbuliwa hapa duniani.”

Hayo aliyaandika mwaka 1918 – miaka kumi kabla ya Henry Ford kuanza kuunda magari kwa wingi.

Pamoja na ukweli kwamba Watanzania ni wageni katika matumizi ya magari, ukilinganisha na Wamarekani au watu wa Ulaya, lakini kama walivyo mamilioni wenzao kwingine duniani wako tayari kupingana na sehemu ya mwisho ya nukuu ya Tarkington. Yaani dunia pasipo magari? Huo ni utani!

Lakini wananchi wa nchi nyingi katika Ulimwengu ya Tatu, ikiwemo Tanzania, wameweza kumiliki magari kwa sababu ya kuwepo kwa nchi moja inayoitwa Japan. Wamarekani na Wazungu wa Ulaya wenye asili ya uchoyo mkubwa, wasingeweza kuusambazia ulimwengu magari, tena kwa bei rahisi tu.

Lakini tangu yalipovumbuliwa, magari yamekuwa yakihusishwa na mwendo kasi, yaani mbio za magari. Ilikuwa mwaka 1895 pale mashindano ya kwanza ya mbio za magari yalifanyika, wakati magari yalikuwa katika hatua za mwanzo tu ya kuendelezwa na kuboreshwa.

Hivyo basi kuanzia mwaka huo, magari na mwendo kasi imekuwa vitu ambavyo haviwezi kutenganishwa kama vile lugha ya mitaani isemavyo ni “spidi tu kwa kwenda mbele.” Matokeo yake ni athari kubwa kwa maisha ya binadamu na mali.

Hii ni kwa sababu binadamu wanaabudu sana kwenda kasi wakiwa ndani ya magari. Ni kitu bado hakijaeleweka kwanini ikawa hivyo, pamoja na tafiti nyingi kufanyika. Muitaliani Enzo Ferrari, bingwa wa zamani wa mbio za magari (Formula 1” aliwahi kunena: “Mbio za magari ni ulevi mkubwa ambao mtu anajitolea kila kitu, bila kujali bila kusita.”

Aidha, angalia ukweli huu pia: Kwanini siku zote dereva aliye nyuma yako anaonekana kama vile yuko kwenye mashindano ya mbio za magari na yule aliye mbele yako anaonekana kama vile anatalii tu?

Kwa mtu yeyote mwenye akili timamu, ajali nyingi za barabarani zinazotokea siku hizi na kusababisha vifo lazima zinaibua swali: Kunani katika sekta ya uchukuzi? Kwanini ajali hizi zinaongezeka kwa idadi na vifo na kwamba inaonekana hakuna hatua zozote zinachukuliwa kwa dhati kutatua kadhia hiyo?

Kikubwa tunachokiona kutoka viongozi wa juu kabisa wa nchi ni kutuma rambirambi kwa wafiwa. Lakini atatuma rambirambi ngapi? Hata hivyo, huwa hawafanyi hivyo kwa ajali ndogondogo iwapo vifo ni watu watatu au wanne.

Kama nilivyotaja hapo mbele mamlaka zetu zimekuwa zinajitahidi kudhibiti hali hii, lakini kama ilivyo kwa changamoto nyingine nyingi zinazowakabili wananchi, ama kunakuwa hakuna utashi wa dhati wa kisiasa nyuma ya jitihada hizo au nazo hufunikwa na mambo ya ufisadi.

Katikati ya miaka ya 90, Serikali ya Awamu ya Tatu ya Benjamin Mkapa ilianzisha ulazima kwa magari yote ya abiria (yaani mabasi) kufungwa vifaa maalumu vya kudhibiti kasi ya mabasi hayo yaani ‘vidhibiti mwendo” (speed governors).

Ulazima huu ambao ulilenga kupunguza ajali za barabarani kuhusu mabasi ya abiria, pia ulihusu mabasi ya ‘daladala.’ Kwa kifupi ni kwamba, kwa mabasi ya kwenda mikoani kifaa kilitakiwa kudhibiti spidi kutozidi kilomita 80 kwa saa yaani hata dereva akikanyaga kiongeza-mwendo (accelerator) hadi mwisho.

Na kwa daladala spidi isizidi kilomita 50 kwa saa. Ili zoezi hili kuwa na baraka za kisheria, Sheria ya Usalama Barabarani (Road Traffic Act) ya mwaka 1973 ilirekebishwa.

Zoezi hilo lililotajwa kuwa la nia njema kwa masilahi ya taifa na watu wake, lilianzishwa kwa kishindo lakini hatimaye lilipotea kimya kimya kwa sababu mbali mbali kubwa iliyotajwa ni kwamba hakukuwepo na utafiti wa kutosha na kukumbwa na harufu ya ufisadi.

Ufisadi ulitajwa kwani wamiliki wa mabasi hayo ndiyo walilazimika kugharamia vifaa hivyo kwa kuvinunua kwa bei kubwa hadi Sh 500,000 kwa kila kifaa (wakati ule) na kwamba kwa kuwa vilikuwa vinatengenezwa nje ya nchi, awali aliteuliwa muagizaji mmoja tu wa kuvileta nchini na kuvisambaza kwa bei aliyopanga yeye.

Hivyo kulikuwa na madai ya watu fulani ‘wapiga dili’ walioiuzia Serikali wazo hilo na watendaji serikalini wenye maamuzi wakaingia kichwa kichwa. Kuna baadhi wanataja kwamba zoezi lile halina tofauti sana na hili la sasa la mashine za EFD (electronic fiscal devices) ambazo wafanyabiashara walilazimishwa kununua kwa bei kubwa.

Hata hivyo, baadaye ilikuja kugundulika kwamba vidhibiti mwendo vile ambavyo ‘ubora’ wake ulikuwa umethibitishwa na Shirika la Viwango nchini (TBS) havikuwa na ubora wowote kwa lengo lililokusudiwa. Ingawa viliweza kudhibiti spidi zinazotakiwa, lakini vifaa hivyo havikuwa na kinga ya kutochokonolewa (tamper proof) na madereva/wamiliki wa mabasi walikuwa wakivichokonoa kuharibu lengo zima la vifaa.

Hali hii ya uchokonoaji wa vidhibiti mwendo ilisambaa sana kwani baadaye mamia ya polisi wa usalama barabarani (traffic police) walikuwa na kazi moja kubwa – ya kukamata mabasi ambayo vidhibiti mwendo vyake vilikuwa vimechokonolewa. Hili nalo likazalisha mwanya mwingine wa rushwa kwa polisi wa usalama barabarani na matokeo yake ni kwamba ajali za mabasi ziliongezeka badala ya kupungua.

Hata hivyo, wengi walihoji busara iliyotumika ya kulazimisha vidhibiti mwendo kwa mabasi ya abiria tu na si kwa magari ya aina nyingine ambayo pia hutumia barabara hizo hizo. Walisema hata kama basi litakuwa limedhibitiwa spidi na kifaa hicho, je, magari mengine yanayotumia barabara hiyo hiyo kama vile malori na magari mengine madogo madogo?