Home Habari AFRIKA SASA ISIMAME KWA MIGUU YAKE

AFRIKA SASA ISIMAME KWA MIGUU YAKE

128
0
SHARE

 

Rais Paul Kagame

 

NA RAMADHANI MASENGA

BAADA ya kuchaguliwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama chake cha Rwanda Patriotic Front (RPF), moja ya mambo aliyosema Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ni kwamba Afrika inatakiwa kuamua mambo yake kutokana na hali yake.

Kagame, shupavu kama jiwe; hataki tafsiri ya Ulaya juu ya mambo yao ifanane na tafsiri ya Afrika. Anapinga kwa nguvu zote namna demokrasia inavyotafsirika Marekani na Ulaya, pia itafsiriwe hivyo Afrika. Hataki. Anataka kila mmoja kutokana na mazingira yake na uelewa wake, atafsiri hali yake.

Ndiyo, kuna mantiki kubwa katika kauli ya Kagame. Acha kufikiria kuwa eti kasema aliyosema kwa sababu anatuhumiwa kuminya demokrasia. Kuwa na tafsiri pana zaidi, ili upate maana pana.

Ni ujinga kulazimisha usawa wa tafsiri wa hali ya Afrika na nchi zinazojiita dunia ya kwanza. Kwa kuwa kila mmoja ana tamaduni, maadili na mila na desturi zake, basi ni lazima pia itafsiri zifuate hali yake, mtazamo na uelewa wake. Siyo tulazimishane tafsiri zao za demokrasia na maadili zifanane na zetu, hali tuko tofauti mno, kimaadili, uelewa na kiuchumi.

 

Si vibaya kwa Ulaya na Marekani, binti kuvaa nguo ya ndani mbele ya wazee wake. Ila ni haramu na laana kubwa katika jamii zetu.

 

Kulazimisha kulinganisha tafsiri katika hali ya mambo katika mataifa yetu, imefanya hata hao watu wa Ulaya na Marekani kujiona wana haki ya kutushangaa, pale tunapokataa ushoga, usagaji na sasa mimba kwa wanafunzi. Kwao ushoga na usagaji ni kitu cha uhuru wa kila mtu. Kitu ambacho serikali wala mamlaka zake hazitakiwi kuingilia kati. Ila kwetu hali hii ikoje?

 

Afrika na baadhi ya nchi za Asia, kwa miaka mingi imekumbwa na ujinga wa  kuamini katika mawazo na tamaduni za Marekani na Ulaya, ndiyo maana hata mambo yao yamedumaa. Kagame anaamini taifa lake lina demokrasia. Hataki kujilinganisha na Ulaya au Marekani. Kwake Ulaya na Marekani si mfano. Wao wana mazingira yao, tamaduni zao na maadili yao. Kwao demokrasia yao ni kitu sahihi sana kwao. Ila sio kwa Rwanda wala Afrika kwajumla.

 

Katika kauli ya Kagame, kuna mengi ya kujifunza na kuangalia kwa jicho pana zaidi. Wakati Ulaya na Marekani wakiwa bize kutushupalia katika kile wakiitacho demokrasia na utawala bora, yapi ya maana wameweza kutusaidia?

 

Je, kwa kushirikiana na watu wao kisha kumuua Gaddafi, ni kuwasaidia Walibya? Baada ya kumwua Gaddafi, Libya na wananchi wake wamefaidika na kitu gani? Demokarasia imepatikana? Katika nyanja ya maendeleo kuna mambo ya kujivunia?

 

Baada ya kuuawa Gaddafi, Marekani na Ulaya wako bize na mambo yao. Sasa wana mipango mipya juu ya Libya. Kwa kuwa jinamizi lililokuwa likiwazuia kuchukua mafuta kijinga jinga limeondoka, sasa wanatumia makampuni yao ya kinyonyaji, kwenda kuwekeza. Hivi ndivyo Libya ilivyoboreka sasa katika upande wa demokrasia baada ya kifo cha Gaddafi.

 

Viongozi wa Afrika bado wameendelea kudumazwa kiakili na msaada wa vyandarua na ujenzi wa vyoo katika shule za msingi kutoka Marekani na kuona Marekani na Ulaya ni marafiki.

 

Juzi Marekani imejitoa katika kongamano la mazingira. Marekani ni taifa la pili kwa kuchangia uharibifu wa mazingira duniani, kwa sababu ya utitiri wa viwanda vyake.

 

Ila katika kongamano la kujadili athari na njia ya kudhibiti hali ya uchafuzi wa mazingira imejitoa. Imeona ujinga. Katika hili hata baadhi ya Wamarekani wanaishangaa serikali yao.

 

Tujiulize, ni nani hasa mhanga wa mabadiliko ya tabia nchi duniani? Ni Afrika, Ulaya Mashariki pamoja na Asia. Siyo Marekani, Ulaya wala China. Ila katika kongamano muhimu sana kwa mustakabali wa Afrika na hali ya hewa duniani, Marekani imejitoa—inashangaza. Ila viongozi wa Kiafrika ni kama wamepigwa ganzi. Wako bize na mambo mengine. Hata kutoa matamko tu la kuilaani Marekani, wameogopa.

 

Wakati Marekani akifanya hivyo, bado kuna viongozi Afrika wanaamini suluhisho la matatizo yao yatamalizwa na ‘urafiki’ wao na Marekani. Ujinga.

 

Kujitoa kwa Marekani katika kongamano hilo ni ishara kuwa kila mmoja afe na lake. Na huu siyo ukweli mpya. Ukweli huu umekuwapo kwa miaka mingi duniani, ila umekuwa ukifichwa kwa misaada ya kilaghai na mikopo ya kuifukarisha Afrika.

 

Tangu Afrika ianze kupokea  hiyo misaada kutoka kwa wanaojiita wahisani, imepiga hatua gani za kimaendeleo? Misaada yao inaambatana na masharti ya kipuuzi na mikataba ya ovyo. Ukijaribu kuwa makali kama Robwert Mugabe wa Zimbabwe, wanajipanga kukuwekea vikwazo, ili kuwatisha na wengine.

 

Sasa ugonjwa huo wa kutishika umeingia hadi katika vichwa vya wasomi wetu. Ukijaribu kutetea rasilimali za nchi, wananchi wako wenyewe, tena wasomi hasa, wanaibuka na kukupigia kelele uache, kwamba yasije kutukuta kama ya Zimbabwe. Sijui tunawaza na akili za kiwango gani!

 

Ni muda sasa wa Afrika wabadilike. Wajue kuwa kama sio wao wenyewe kuwa na mikakati na mipango madhubuti, hakuna mwingine wa kuja kubadilisha hali yao kiuchumi.

 

Kwa pamoja wajiulize, baada ya kelele za Marekani kwa mataifa waliyosema yana demokrasia hafifu na kufanikiwa kuwaondoa viongozi wao madarakani, wamekuwa msaada gani kwa wahusika?

Baadhi ya majarida yenye mrengo wa kimagharibi, yamekuwa yakimkosoa sana Kagame na utawala wake. Ila je, hali ya maisha ya Wanyarwanda ikoje? Je, Wanyarwanda hawafaidiki na matunda ya Kagame? Uchumi wa Rwanda upo katika hali gani?

 

Kama Waafrika inabidi kwa pamoja, tuwe na tafsiri ya mambo yetu bila kuingiliwa. Na ndiyo maana katika hilo Kagame ameahidi ndani ya miaka kumi ijayo Rwanda inabidi iwe na uwezo wa kujitegemea katika bajeti yake kwa asilimia mia, ili kuachana na kelele za mataifa ya Magharibi na washenga wao.

 

Afrika inabidi kwa pamoja, ijipange na kujua kuendesha mambo yao. Hali ya kutegemea mawazo na mtazamo wa kimagharibi ni kujidanganya na kujichimbia kaburi la ustawi wao. Matokeo ya haya yote ni kukosewa heshima na kutukanwa kuhusu ushoga na usagaji. Kukataa ushoga na usagaji eti ni ujinga. Ni kushindwa kutoa haki za kibinadamu.