Home Habari MABADILIKO YA MAWAZIRI YAJA

MABADILIKO YA MAWAZIRI YAJA

217
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU
Magufulipwani KAULI za hivi karibuni za dhidi ya baadhi ya mawaziri pamoja na ukimya wake katika kujaza nafasi mbili za Waziri na Naibu waziri, zinadhihirisha wazi ujio wa mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri. RAI linachambua.

Kwa zaidi ya miezi miwili sasa tangu Mei, 24 mwaka huu Rais Magufuli hajaijaza nafasi ya Waziri wa Nishati na Madini iliyokuwa ikishikiliwa na Profesa Sospeter Muhongo.

Wakati nafasi ya Waziri wa Nishati na Madini ikiwa wazi kwa zaidi ya miezi miwili, nafasi ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu iliyokuwa ikishikiliwa na Dk. Abdallah Possi aliyekuwa akishughulikia walemavu iko wazi tangu Januari 19, mwaka huu.

Kitendo cha nafasi hizi mbili kuwa wazi kwa muda mrefu, kinatajwa kuwa ni mkakati wa Rais Magufuli na wasaidizi wake kujipanga ili kufanya mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri yenye lengo la kuteta ufanisi anaouhitaji.

Duru za habari kutoka Serikalini zimebainisha kuwa mabadiliko hayo yatafanyika kabla ya mwaka huu kufikia ukingoni, lengo likiwa kutekeleza bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/18 kwa ufanikisi na kiwango cha hali ya juu.

Uamuzi huo wa kufanya mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri pia unatajwa kusukumwa zaidi na namna mawaziri wengi wanavyofanya kazi kwa mazoea huku baadhi yao wakisubiri kuagizwa au  kuelekezwa mambo ya kufanya na Rais, Makamu wa Rais  au na Waziri Mkuu.

Ukweli wa hili umethibitishwa na Rais mwenyewe alipokuwa jijini Tanga hivi karibuni  katika uzinduzi wa kiwanda kipya cha Saruji cha Kilimanjaro.

Akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tano jijini Tanga ambayo pamoja na mambo mengine pia iliambatana na uzinduzi wa ujenzi wa mradi mkubwa wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania, Rais Magufuli alionesha wazi kuchoshwa na utendaji kazi wa baadhi ya mawaziri.

Rais alimkosoa waziwazi Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage; Waziri wa Kilimo, Chakula na Mifugo, Dk. Charles Tizeba; Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa; Wizara ya Nishati na Madini na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango.

Alisema mawaziri hao wamekuwa wakimkera  huku akionekana kumkalia zaidi Mwijage ambaye alisema anakerwa na kigugumizi cha waziri huyo katika kuwanyang’anya wamiliki wa viwanda ambavyo havijaendelezwa.

“Hivi Waziri Mwijage unapata kigugumizi gani mpaka sasa hujafuta kiwanda  chochote licha ya kuwapo wawekezaji walionunua, lakini hawajaviendeleza, nasema katika hili unanikwaza. Viwanda visivyofanya kazi vipo tu kwanini havifutwi, waziri unamwogopa nani wakati mimi ndie niliyekuteua.

“Nikuombe waziri fumba macho usiangalie sura za marafiki zako, viwanda vingi tuliwapa marafiki. Nimekueleza tukiwa ofisini kwenye cabinet (Baraza la Mawaziri) nilikuita wawili ofisini na hadharani, kote hujanisikia, unataka nikueleze nikiwa kaburini. Waziri nakuagiza fungia viwanda vyote visivyoendelezwa, wengine ikibidi wakamatwe, wapelekwe lokapu kidogo, wakitupeleka mahakamani tutajua namna ya kupambana nao…”alisema Rais Magufuli.

Mbali ya Mwijage waziri mwingine anaetajwa kuchochea ujio wa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri ni Dk. Tizeba ambaye ameshindwa kutatua matatizo yanayokikabili kiwanda cha Maziwa cha Tanga Fresh.

Rais alimtaka Dk. Tizeba kutumia siku saba za kutatua changamoto zote zinazokwamisha maendeleo ya kiwanda hicho.

Aidha, alizigusa wizara kadhaa hasa baada ya kushindwa kufunga mashine maalumu ya kupima wingi wa mafuta yanatoka nje ya nchi (Flow meter).

Rais alisema ni mwaka sasa tangu Waziri Mkuu aagize kutangazwa kwa zabuni ya kufungwa kwa mashine hiyo, lakini ajabu hata kandarasi hajapatikana badala yake anatafutwa kwa ujanja ujanja.

“Matatizo mengine yanashindwa kutatuliwa kutokana na visheria vya ovyoovyo na vya kijinga, mawaziri mlioko hapa mpelekeeni salamu Waziri Mbarawa, suala hili likitaka kutatua inabidi uhusishe Wizara ya Fedha na Mipango, Nishati na Madini na Maji, Viwanda na Biashara, ni bahati mbaya hawa watu mara nyingi hawawasiliani hali inayosababisha mambo mengi kukwama”.

MWIJAGE KUCHUKUA MAAMUZI MAGUMU

Katika mazungumzo yake na RAI yaliyofanyika kwa njia ya simu, Mwijage alisema hayuko tayari kuendelea kumkwaza Rais na badala yake ameamua kufanya maamuzi magumu kwani anataka kikombe hicho kimuepuke.

Alisema ukisoma mpango wa pili wa miaka mitano na ukisikiliza hotuba ya Rais wakati anahutubia Bunge kwa mara ya kwanza, imeelezwa wazi kwamba tunataka kuhakikisha viwanda tulivyo navyo vinafanya kazi na kuongeza uwezo wa uzalishaji.

“Viwanda vyetu vilikuwa vinazalisha kwa asilimia 30/40 sasa tunataka vizalishe zaidi, lakini pia Rais ametaka  tuanzishe viwanda vipya na kuhakikisha  viwanda vilivyobinafiishwa ambavyo havifanyi kazi na vyenyewe vifanye kazi ili vitengeneze ajira kwa sababu vijana wengi hawana ajira, vizalishe bidhaa za kuuza nchini na nje ya nchi na mwishowe viongeze wigo wa kulipa kodi, ndivyo alivyosema Rais na ndivyo maandiko yanavyosema.

“Juni 22, mwaka huu, aliniagiza nisimamie hiyo shughuli ya kurejesha viwanda vilivyobinafsishwa na kwa hakika kazi inafanyika, lakini Rais anaonekana kutoridhishwa na kasi tunayokwenda nayo.

“ Tayari nimeshatengeneza mpango na tukiwa katika kiwanda cha matunda Bagamoyo baada ya kuridhishwa na uanzishwaji wa viwanda vipya alinitaka nimalizie hili la viwanda vya zamani.

“Ni kweli amesema namkwaza na ni kweli namkwaza kwa sababu alishaniambia hivi vipya navimudu, mbona vile vya zamani siviwezi na anavitaka.

“Anavitaka kwa sababu ni rahisi kumpa mwekezaji na kuvifanyia kazi kwa haraka kuliko kwenda kuanza upya kwa kuvunja msitu na kujenga majengo, inachukua muda mrefu.

“ Sasa ili kwenda na kasi ya Rais mimetengeneza mpango ambao unatofauti kubwa na ule wa zamani, nimeamua kuwahusisha wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya katika kuchukua viwanda hivi, nimefanya hivyo kwa sababu wao ndio wako kwenye maeneo husika.

“Iko orodha ya viwanda vyote vilivyobinafsishwa, kwakuwa sitaki kupigwa changa la macho kwa kupewa orodha ya uongo nimeliacha jukumu hilo kwa wataalamu mikoani ili wao waridhie nao watashirikiana na wakuu wa mikoa, ndio wataleta ripoti kwa Katibu wa Wizara na yeye ndio atanikabidhi ili kuifanyia kazi.

“ Lakini pia nimeamua kukaa kikao na Mawaziri mwenye sekta husika, watu lazima wajue mimi ni Waziri wa viwanda, lakini hivi viwanda vina sekta.

“ Nitakutana nao Agosti 10, leo na nafanya hivyo ili kuepuka kuparamia viwanda ambavyo huenda mawaziri husika wameshaongea na wahusika.

“Nitakachokifanya ni kupiga pigo takatifu, hilo pigo nikikupiga hunyanyuki, utaratibu wa pigo hili ni kukutana na mawaziri wanaohusika, na nasema wazi mawaziri waje ama wasije mimi nitafanya maamuzi magumu.

MABADILIKO MAKUBWA

Mwijage alisema tangu Rais azungumzie suala la kupokonya viwanda, mambo mengi yametokea ikiwa ni pamoja na baadhi ya wamiliki wa viwanda kuanza kufunga mitambo.

“Tayari yupo mwekezaji mmoja ameshashusha mitambo kwa ndege. Siku ya Alhamisi (leo) nitafanya maamuzi magumu, nimeshamwomba Rais asinikumbushe ananiumiza, nitampa furaha, amesema niwashughulikie, nitawashughulikia.

“Amini wapo watakaokwenda Segerea, nimeshaambiwa niwapeleke, nitawapeleka tu. Tatizo tulilonalo ni kuwa vijana wengi hawana ajira, huyu mzee anauchungu na wananchi wake, sisi hatunyang’anyi mtu kiwanda, tunachotaka viwanda vifanye kazi, hata kama atawekeza shetani sisi tuko tayari.

“Watanzania tunashida ya kutaka kuwekeza wenyewe, hatutaki kushirikiana na wenzetu wengine, hali hii ndio inafanya viwanda vingi kukwama, nawaomba Watanzania watafute washirika wafanye kazi nao ili viwanda vifanye kazi. Naomba kikombe hiki kiniepuke,”alisema.

MAWAZIRI WANAJENGEWE HOFU

Mhadhiri wa kitivo cha elimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. George Kahangwa alisema ni dhahiri sasa mawaziri na watumishi wote wa serikali wanajengewa hofu jambo linaloweza kuwafanya kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Licha ya mawaziri hao kushauriwa kujiuzulu pia Dk. Kahangwa alisema wanapaswa kutambua kuwa Rais aliyepo madarakani sasa ni mkali.

Alisema aliyozungumza Rais Magufuli ni mwendelezo wa kudhihirisha tabia yake ya ukali kwani hata akitoa hotuba mahali popote huzungumza maneno ya ukali.

“Kwa hiyo rais tuliye naye ni mkali. Kwa maana hiyo hata wale baraza la mawaziri nadhani mpaka sasa wanapaswa kufahamu kuwa kiongozi wao aliyewateua ni mtu wa namna gani, bila shaka hata lugha za namna hiyo ni kitu wanachokitegemea.

“Ni kitu ambacho kwa watendaji wote watumishi wa kada za chini na hata hao mawaziri amekwisha kuwajengea uoga kwa hiyo hata aliyosema kwamba mawaziri wapumbavu nafananisha na aliyoyasema Nabii Issaau Bwana Yesu alipowaambia mitume wake kwamba kuna mmoja wenu atanisaliti, kila mmoja alitetemeka alihofu kwamba ni yeye lakini hawakuweza kujua ni nani mpaka alipomsema mwenyewe. Hivyo basi hata hawa mawaziri waliomo katika baraza lake watakuwa wanaendelea na hiyo hofu, wataishia kusema labda ni fulani au Yule.

“Pengine ni utaratibu wa kuwafanya wale ambao walikuwa wanatenda chini ya kiwango waamke. Ila kustahiiana ni jambo muhimu sana hata kama mtu ana udhaifu wake, nakumbuka  Mwalimu Nyerere alikwepa sana kutumia neno makali, alisema watu ni wajinga na kusema anachagua neno kwa umakini. “sisemi wapumbavu nasema wajinga”.

“Kwa hiyo tunaona style ya uongozi uliopita na wa sasa ni tofauti. Kwa kweli haipendezi masikioni kwa watanzania waliozoea lugha ya staha na ustaarabu. Sasa mawaziri watambue kiongozi aliyepo ni wa namna gani ili wajiepushe na maneno ya namna hiyo kwa utendaji wao uliotofauti lakini rais atambue kuwa watu wakimwogopa kupitiliza huenda utendaji vilevile ukawa utendaji wa kutojiamini na wakatenda kwa hofu na watu wakitenda kwa kutojiamini wanaweza kuharibu kazi,” alisema.

Aidha, aliongeza kuwa “mawaziri ambao wanajijua si wapumbavu kama wanaona katika sentesi hii wametajwa mtu ukiambiwa mpumbavu na wewe unajua si mpumbavu basi unaachia hiyo nafasi. Sidhani kama wanafungwa kwamba wasiweze kujiuzulu na wale ambao wanajua wamesemwa ni wapumbavu na upumbavu huo hawakubali wakiendelea kukaa basi watu watawatazama kwamba ni wapumbavu,” alisema Dk. Kahangwa.

Aidha, Mhadhiri mwandamizi wa kitivo cha siasa kutoka Chuo Kikuu cha Mt. Agustino (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu alisema Rais Magufuli alipaswa kuwakemea Mawaziri wake katika Baraza lake la Mawaziri, vikao vya baraza la mawaziri kwa sababu katika hali ta utendaji wa kazi, tunaongozwa na dhana ya kuwajibika kwa pamoja.

“Kwa hiyo pale wanapofeli, mawaziri wote wanahusika na rais humohumo. Nashangaa kuona kauli ile kwa sababu  lengo la baraza la mawaziri ni kupeana mawaidha na kusemana humohumo kwenye vikao na ili muweze kupeana nguvu wakati huo huo kuambizana ukweli. Ila alichokifanya pale ni kuwaaibisha ndio maana hata mimi nilishasema siwezi kufanya kazi na huyu bwana pamoja na kwamba hashauriki lakini pia anapenda kudhalilisha wenzake.

“Na nina uhakika kuwa hilo haliwezi kuleta ufanisi au tija katika lile linalotakiwa kufanyika. Hawa ni binadamu na kwa kawaida kunatakiwa heshima kidogo ili muweze kusahihishana na kwenda mbele, lakini hili la kuwatolea lugha kali si sahihi.

“Tatu hao walioambiwa hayo maneno nashangaa bado hawajajiuzulu kwa sababu kama mteuzi wako rais ameshaonesha hana imani na wewe unasubiri nini! Kama ni watu wanajiheshimu na kujiamini ukishaambiwa hivyo na kutukanwa kama mtoto, sasa wanataka awaambieje kuwa hawataki! nilitegemea kama ni watu wanaojiheshimu, wangesema tunakaa pembeni… cha ajabu Mwijage anasema ‘usinikumbushe tena’ maana yake nini?

“Nadhani pia marais wetu wana tabia moja ya kutaka kufurahisha hadhara za watu pamoja na ile ya kutumbua, haya ni mambo ambayo yana taratibu zake na miiko yake. Haya ni mambo ya serikali ambayo yanaongozwa kwa utaratibu kwa sababu mwisho wa siku watanzania wanazidi kupoteza imani na uongozi wake,” alisema Profesa Baregu.

Hoja hiyo ya Profesa Baregu pia iliungwa mkono na Mhadhiri wa Chuo kikuu kishiriki cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala ambaye alisema licha ya Rais kuelewana na mawaziri wake pia kila awamu ina ya uongozi huja na style yake.

“Ingawa kiutaratibu asingesema hadharani angerudi Ikulu akawaita na kuwapa maneno, lakini hadharani mbele ya umma na vyombo vya habari ni kama vile kuwadhalilisha watendaji wako wa chini. Lakini ndio hiyo style bila shaka mawaziri wenyewe wanaielewa ni ya utawala mpya.

“Kiutaratibu ni unatakiwa kulinda heshima ya watendaji wako, unajua heshima ya mawaziri lazima ilindwe mbele ya wale wanaowahudumia sasa kuwasema hadharani kidogo inashusha hadhi yao ingawa ndio style yake kwa sababu sasa hivi kuna kauli mbiu ya ‘msema kweli ni mpezi wa Mungu’ yupo tayari kusema ukweli wakati wowote na mahali popote. Lakini kiutaratibu alitakiwa kuwaita na kuwaambia bana hapa mbona hivi… hili haliendi, ndio uongozi unavyotaka,” alisema Profesa Mpangala.