Home Habari kuu LIPUMBA ATAKA JPM ABADILIKE

LIPUMBA ATAKA JPM ABADILIKE

279
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa Profesa Ibrahim Lipumba ameitaka Serikali kutekeleza kwa vitendo kauli aliyoitoa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kwa kuruhusu mikutano ya hadhara na mazungumzo baina ya viongozi wa upinzani na chama tawala.

Profesa Lipumba ametoa kauli hiyo baada ya Rais Kikwete kusema vyama vya siasa vilivyopo madarakani havitakiwi kuvichukulia vyama vya upinzani kama maadui, bali wabia katika kuendeleza misingi ya demokrasia kwa kuzingatia utawala wa sheria.

Kikwete alitoa kauli hiyo wiki iliyopita Afrika Kusini wakati katika kongamano liilojadili mada kuhusu utawala bora na sheria iliyowasilishwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afrika Kusini Barney Pityana.

Kikwete pia alishauri wabunge wa vyama tawala Barani Afrika kuzikosoa serikali zao pindi wanapoona zinakwenda kinyume na ilani za uchaguzi.

“Kama kuna kitu chochote ambacho mkutano huu unaweza kutoa maoni ni kuhimiza kuwa vyama tawala vione kuwa vyama vya upinzani si kama adui ila ni washindani wa kisiasa na washirika wa serikali,” alisema Kikwete.

Akizungumza na RAI juzi, Profesa Lipumba aliunga mkono kauli hizo za Kikwete na kueleza kuwa jambo alilolizungumza ni jambo la msingi kwa kuwa vyama vya upinzani vipo kwa mujibu wa sheria hivyo ni vyama halali.

Lipumba alisema ni vyema vyama vilivyopo madarakani (CCM) vikaheshimu sheria na kutoa fursa kwa vyama vya upinzani kufanya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Viruhusu kuwepo kwa mikutano ya hadhara ili vyama vya upinzani viweze kukutana na wananchi ilimradi vifanye kazi kwa mujibu wa sheria za nchi,” alisema.

Alisema vyama vya upinzani vinatoa changamoto nzuri kwa kuikosoa serikali ili mwisho wake iweze kufanya vizuri, pia  vinasaidia nchi kurejesha mambo mazuri ambayo yalipendwa na wananchi.

“Kwa mfano hapa Tanzania tulikuwa tukipiga kelele sana kuhusu kodi za kichwa ambazo zilikuwa zinatumika kuwanyanyasa wananchi hatimaye ndani ya chama tawala wakaona ni kweli na kubadilisha mfumo.

“Sisi tulikuwa tunapiga kelele sana kuhusu masuala ya rushwa na ufisadi tena ilikuwa ni ajenda yetu kubwa, baadaye hata watu waliopo ndani ya madaraka nao wakaichukua hiyo ajenda.

“Tulikuwa tunapiga kelele sana kuhusu maliasili kwamba tunaibiwa kwenye dhahabu na madini, wenzetu baadhi yao wakaona hiyo hoja ina ukweli.

“Kwa hiyo ukivipa vyama vya upinzani fursa ya kuweza kujadili na kutoa hoja kuhusu masuala ya maendeleo hata chama tawala kinajifunza. Kuviachia uhuru na vifanye kazi yake inaisaidia jamii kwa ujumla wake,” alisema.

Profesa Lipumba aliungana pia na Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe kwa kusema kuwa kutokana na hali iliyopo sasa kauli ya Rais Kikwete ni kauli muafaka ila kwa kuwa ameizungumzia Afrika kusini anapaswa kuja kuizungumza pia hapa Tanzania.

Mwishoni mwa wiki Zitto katika ukurasa wake wa Twitter aliamtaka Rais Kikwete kuja kuirudia kauli hiyo hapa nchini.

“Lakini ingekuwa vizuri pia angeizungumzia hapa nchini. Maana alipohojiwa hapa nchini alisema yeye ni mkulima tu wa mahindi na mfugaji hazungumzii mambo ya kisiasa sasa ameenda Afrika kusini anatoa kauli nzito, wakati humu ndani ya nchi anasema anashughulikia maziwa ya ng’ombe,” alisema Prof. Lipumba.

Aidha, alisema kauli hiyo ni nzuri na ni vema hata viongozi wa vyama vya upinzani na vyama tawala kuwa na fursa ya kukutana katika vikao na kuzungumza mambo mbalimbali kwa faida ya nchi.

“Sio vikao rasmi kama vya kibunge hapana, lakini kuzungumza na kubadilishana mawazo kwa sababu mnapokuwa mnazungumza hata ukienda kwenye jukwaa la kisiasa ukimzungumzia mtu ambaye unakutana naye mara kwa mara hata kauli zako kidogo zinamzingatia kuwa huyu naye ni binadamu nakutana naye… lakini kama tulipeana uhasama hata watu wakienda kwenye majukwaa wanaenda na hasira mwishowe kauli zenyewe zinakuwa za kushutumiana kupita kiasi. Hivyo utaratibu wa kuweka mfumo wa viongozi kukutana ni utaratibu mzuri,” alisema.

Alitolea mfano mwaka 2001 kuwa baada ya muafaka Rais wa wakati huo, Benjamini Mkapa aliweka utaratibu wa kukutana na upinzani.

“Mzee Kingunge alikuwa waziri anayeshughulikia mambo ya mahusiano na umma. Mkikutana kuna masuala kama haya ya viwanda vilivyobinafsishwa ambapo tulipendekeza kufanywe utafiti tena kwa kina viwanda ambavyo havitimizi malengo yake kama ilivyokuwapo kwenye mkutano virudishwe serikalini, tukatoa mawazo kama hayo, alisema.

“Pia Rais Mkapa akawa anatukaribisha Ikulu pindi walipokuja viongozi wa nchi za nje anatupa nafasi na sisi kama viongozi wa upinzani kuzungumzia masuala ya nchi,” aliongeza.

Serikali iwe na uwazi

Aidha, Prof. lipumba pia alitolea mfano suala la ndege ya Tanzania aina ya Bombardier ambayo imezuiliwa nchini Canada kuwa kutokana na madai mbalimbali kuwa ni mojawapo ya mambo ambayo yanapaswa kuwekwa wazi ili mjadala ufungwe.

“Tukiangalia hili suala la madai ya ndege yetu kuzuiliwa kule Canada nayo pia ni muendelezo wa serikali kutoweka wazi mambo yake, kama kuna tatizo ni vizuri lijulikane limezungumzwa kwa sababu gani.

“Ni jambo jema sana hasa wapinzani wanapotoa hoja ni vema serikali kuueleza ule ukweli kwani kama pana hoja itafahamika tulikosea hapa au pale na suala litakwisha. Lakini usipoeleza ukweli suala hilo linaweza likawa linaendelea kwa sababu tu kauli uliyoitoa si sahihi. Msemaji wa serikali anatakiwa kuelezea ukweli kwa umma na si kusingizia wapinzani. Kwa hiyo kauli ya Rais Kikwete ni kauli nzuri lakini pia aweze kuisemea akiwa hapa nchini,” alisema Prof. Lipumba.

DOVUTWA: NI KAULI HAI

Aidha, Mwenyekiti wa kitaifa wa Chama cha United Peoples Democratic Party (UPDP), Fahmi Dovutwa aliungana na Profesa Lipumba kwa kubainisha kuwa kauli ya Kikwete ni kauli hai kwa sababu anaiona Tanzania ilivyo sasa, anazijua na ana uzoefu na nchi za Afrika.

Alisema mambo haya ya upinzani kughasiwa kila mara katika nchi za Afrika imekuwa kama chakula na mboga au utamaduni wa vyama tawala.

“Lakini kurudishwa kwa demokrasia kumepunguza sana msukosuko wa mapinduzi katika nchi zetu kwa sababu watu wamepata mahali pa kutolea lile joto lao walilokuwa nalo.

“Kuruhusiwa kwa mfumo wa vya vingi na uvumilivu wa kisiasa ni moja ya mambo ambayo yameleta utulivu katika Bara la Afrika ni maeneo machache sana tangu mwaka 1990 kuwapo kwa mapinduzi. Kwa hiyo kauli ya Kikwete ni hai kwamba kuwepo na muingiliano kati ya upinzani na vyama tawala kwani hii inapunguza misukosuko hata uchaguzi ukishafanyika hakutokuwa na mapinduzi.

“Kama ilivyokuwa Angola mwaka 1975 walifanya uchaguzi MPLA Angola – Savimbi aliposhindwa akaingia msituni. Hali kadhalika Msumbiji – Renamo iliposhindwa wakakataa na kuingia msituni. Lakini sasa hivi tangu kuanze mikutano hilo suala halipo.

“Tukiangalia hapa kwetu kipindi cha Kikwete kulikuwa na msukosuko lakini haukuwa mkubwa kama wa sasa. Kwa sababu Kikwete alifanya juhudi sana kupoza joto la vyama kwa kuwaita kuzungumza nao hata wakati mwengine joto lililotokana na viongozi wa mikoani huko rais alikuwa anakubali kuzungumza na viongozi wa vyama na kuyamaliza,” alisema Dovutwa.

Vivyo hivyo, aliyekuwa Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), Balozi Khamis Kaghasheki aliizungumzia kauli hiyo ya Kikwete katika ukurasa wake wa Twitter kwa kuandika: “Nimetafakari kauli ya JK kuhusu vyama Afrika, nakiri kiongozi aliyebobea katika uongozi hukabiliana na muziki hata kama hapendi mdundo wake.”

MWISHO