Home Habari WABUNGE CUF WAIANGUKIA MAHAKAMA KUU KUWALINDA

WABUNGE CUF WAIANGUKIA MAHAKAMA KUU KUWALINDA

301
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

MGOGORO unaoendelea kufukuta ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) umechukua sura mpya baada ya wabunge 19 kufungua shauri Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam kuzuia kiongozi yeyote wa chama hicho kutowachukulia hatua za kinidhamu wabunge, madiwani na viongozi wengine hadi mashauri yaliyopo Mahakamani juu ya uhalali wa uongozi wa chama yatakaposikilizwa na kutolewa maamuzi.

Hatua hivyo imekuja ikiwa ni wiki chache zimepita baada ya Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kutangaza kuwavua uanachama wabunge wanane na madiwani wawili wa viti maalumu wa chama hicho kwa madai ya utovu wa nidhamu na usaliti.

Prof. Lipumba alisema Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama cha Wananchi (CUF) limewavua uanachama wabunge na madiwani hao miongoni mwao ni wale waliosusia wito wa kwenda kujieleza juu ya tuhuma zinazowakabili za kula njama na Chadema ili kuweza kumuondoa yeye madarakani.

Wabunge hao 19 wanaodaiwa kuwa upande wa Katibu Mkuu Maalim Seif Shariff Hamad, waliiomba mahakama itoe nafuu kwa kuwalinda na kuwaacha watekeleze majukumu yao kwa mujibu wa sheria za nchi mpaka hapo mgogoro huo utakapopatiwa ufumbuzi na kumalizika.

Akizungumza na RAI juzi, Msemaji wa CUF upande wa Maalim Seif, Mbarala Maharagande alisema shauri hilo namba 69/2017 limetajwa jana mbele ya Jaji Wilfred Ndyansobera.

Aidha, alikana kuwapo kwa taarifa za baadhi ya wabunge wa upande wa Maalim Seif kufungua shauri la kuiomba mahakama hiyo iwakutanishe Profesa Lipumba na Maalim Seif.

“Zipo taarifa kwenye mitandao pia eti Maalim Seif ameomba msamaha kwa Prof. Lipumba kwa kutumia Mahakama! Huyo labda atakuwa Seif Balozi lakini sio Maalim Seif Sharif Hamad- Mwamba wa Kisiasa nchini.

“Maalim Seif anaongozwa na misimamo na maazimio ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa. Hawezi kupewa shinikino na yeyote.

“Tunazo taarifa za wabunge watatu waliotishwa kutaka kuvuliwa uanachama na kupoteza majimbo, ambao wamejiyumbisha kutokana na mazonge waliyokuwa nayo na hofu ya maisha. Hakuna wabunge wanaoweza kufanya vile inavyodaiwa.

“Kwa sababu hakuna kifungu cha sheria ndani ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano ya Tanzania au sheria za mwenendo wa mashauri ya madai inayolazimisha watu waliotofautiana wapatane kwa lazima. Hakuna amri ya Mahakama ya namna hiyo. Hata hizo kanuni za usuluhishi (Arbitration procedures) haziko hivyo,” alisema.

Hata hivyo, alisema hakuna sababu za Maalim Seif kumuomba radhi Profesa Lipumba.

“Lipumba hakufukuzwa wala kulazimishwa ajiuzulu. Katiba ya CUF Ibara ya 117(2) haitoi nafasi tena ya kuwa Mwenyekiti wa Chama Taifa baada ya kujiuzulu kwake.

“Uenyekiti wake unatokana na maamuzi ya swahiba wake wa karibu, mshirika wa mambo yote si mwingine ni Msajili wa Vyama vya siasa nchini,” alisema.

Alisema Profesa Lipumba amekuwa akimtaka Katibu Mkuu aende ofisini Buguruni, na amefanya juhudi za kuwatafuta watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini kufanikisha hilo.

“Lipumba hakumkosea Maalm Seif au kinyume chake. Lipumba ana mgogoro na Taasisi ya CUF ambapo wajumbe 47 wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa  kati ya 60 (kama ukiwajumuisha wote na waliofukuzwa uanachama) hawamuungi mkono. Huwezi kuwa Mwenyekiti wa Baraza ambalo halikukubali kabisa,” alisema.

Aidha, akizungumzia taarifa za baadhi ya Wabunge kufungua shauri la kumzuia kwachukulia hatua za kinidhamu, Profesa Lipumba alisema bado hajapata taarifa hizo hivyo anasubiri mwanasheria wake ampatie.

“Hizo taarifa watendaji wangu wanaweza kuwa nazo, kwa sababu pia wale waliovuliwa uanachama wamelalamika haikuwa sahihi ila haya mambo yapo kwenye kamati za maadili ambayo inafanyia kazi ndipo tutoe mapendekezo kwenye baraza kuu.

“Wakili wangu hajanieletea hiyo kesi, sijapata maudhui ya kesi hiyo hivyo siwezi kuizungumzia kwa sasa,” alisema Prof. Lipumba alipozungumza na RAI.

Aidha Msemaji wa CUF upande wa Lipumba, Abdul Kambaya alisema hajakutana na Wabunge waliodaiwa kujisalimisha mbele ya Lipumba.

“Sijakutana nao, labda wamekutana na viongozi wengine hivyo siwezi kukanusha wala kukubali uwapo wa kitu hicho. Labda wenyewe wanaweza kuzungumzia hasa ukizingatia kesi waliyofungua jana (Jumanne) Mahakama Kuu kuwaomba Mwenyekiti na Maalim wakutanishwe,” alisema.