Home KIMATAIFA ANGEL MERKEL NA CHANGAMOTO ZA KUUNDA MUUNGANO

ANGEL MERKEL NA CHANGAMOTO ZA KUUNDA MUUNGANO

52
0
SHARE

NA Abbas Abdul Mwalimu

SEPTEMBA 24, Mwaka huu, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alishinda tena uchaguzi na hivyo kuendelea kuliongoza taifa hilo kubwa barani Ulaya kwa muhula wa nne.

Akiongea katika Makao Makuu ya Chama chake cha Christian Democratic Union (CDU) huko Berlin, Kansela Angela Merkel aliyaita matokeo ya uchuguzi huu kuwa ni ya ‘kushangaza’ lakini alikiri kuanguka kwa uungwaji mkono wa chama chake na kuongeza kuwa wana kazi ya kufanya kidogo.

Chama cha CDU cha Merkel na ushirika wake wa Christian Social Union (CSU) cha Bavaria kwa jumla vilipata asilimia 33 ya kura zote ukilinganisha na asilimia 41 vilivyopata mwaka 2013. Hii ikiwa ni sawa na anguko la asilimia 8.5 na kufanya kuwa matokeo mabaya kwa chama hicho tangu mwaka 1949.

Chama mshirika cha CDU cha muda mrefu, Social Democrats kimeanguka kwa asilimia 5 na kupata asimilia 20.5 ya kura zote ukilinganisha na mwaka 2013.

Merkel alikiri kutaka kuendelea na muungano wa kuunda serikali na chama hicho cha mlengo wa kati kushoto ingawa kiongozi wake Martin Schulz ameonesha kukataa. Merkel anatarajiwa pia kuvijumuisha vyama vya Free Democratic Party (FDP) na Environmentalist Green.

UCHUMI, USALAMA NA WAHAMIAJI

Changamoto kubwa katika muungano huo ni tofauti zao katika mambo ya msingi.

Green wakisimama kwenye Mazingira, FDP Kodi wakati CDU kikijikita kwenye Uhamiaji.

FDP wao wanataka kuona ile dhana ya uchumi wa soko hurua ikisimamiwa ipasavyo sambamba na kutoingiliwa kwa uhuru wa maisha ya mtu mmoja mmoja.

Mbali na hayo, FDP pia wamekuwa kinyume na kile kinachodaiwa kuwa ni kodi kandamizi kwa wafanya biashara na kuhitaji mabadiliko katika mfumo wa kodi na kuleta muunganiko wa tozo za kodi barani Ulaya.

FDP kinarejea tena katika siasa za Ujerumani baada ya kukosekana kwa miaka minne katika Bunge la Bundestag.

The Green kilichojinasibu kwa sera yao ya ‘ten-point plant’ wao wamejikita zaidi katika kuangalia masuala ya mazingira na usalama wa tabia nchi.

Walienda mbali zaidi na kumtaka Kansela Angela Merkel kukubaliana na masharti ya Mkataba wa Paris ili kupunguza uzalishwaji wa hewa ya ukaa ambayo huchangia kuondoka kwa tabaka la ozoni (ozone layer) hali ambayo inachangia kuongezeka kwa joto na kusababisha maisha ya viumbe kuwa hatarini.

CDU bado imesimama kwenye Sera yake ya ‘Mlango wazi’ yaani ‘Open Door’ kwa lugha ya kigeni. Sera hii kwa kiasi kikubwa imeonekana kutoungwa mkono na baadhi ya washirika wake kama chama dada cha CSU. Wengi wa wanaokosoa sera hii wamehusisha uingiaji wa wakimbizi ndani ya Ujerumani na matukio ya kigaidi jambo ambalo wanaamini linatia hofu katika usalama wa Ujerumani.

Hofu nyingine iliyojitokeza miongoni mwa baadhi wa wanachama wa vyama pinzani ni suala la uislamu katika Ujerumani (Islamization) hii ikichangiwa hasa na idadi ya wakimbizi zaidi ya laki sita kutoka nchi za Syria na Afghanistan.

Changamoto nyingine ni  Wajerumani wa Mashariki kuona wametengwa kiuchumi ukilinganisha na Magharibi hali inayodaiwa kuwashawishi wengi kukipigia kura chama cha Alternative fur Deutschland (AfD) ambapo kilipata siti 94 za Bunge la Ujerumani sawa na asilimia 13.

AfD walipata kura hizi kutokana na Sera yao ya kupinga uingiaji wa wakimbizi nchini Ujerumani ambao inadaiwa wanahudumiwa vizuri kuliko raia wengi wa Mashariki jambo lililopelekea kupata uungwaji mkono mkubwa toka upande huo.

Changamoto nyingine inaletwa na chama cha CSU ambacho kinamtaka Merkel aungane na mlengo wa kulia ili kurejesha uungwaji mkono toka kwa raia zaidi ya milioni moja.

Suala la uwepo wa ukomo wa wakimbizi ni hoja nyingine ya CSU ambayo  wanaamini wakiisimamia ipasavyo watapata uungwaji mkono kutoka upende wa Mashariki jambo amabalo Kansela Merkel amelipinga.

Muungano wa chama cha Social Democrats na CDU/CSU unatarajiwa kudumu kwa kipindi cha miezi kadhaa kutoka sasa, wakati Kansela Angela Merkel akiendelea na mchakato wa kutafuta chama ama vyama vya kuungana navyo kuunda serikali ya Bundesregierung.

Labda kujitoa kwa kiongozi mwenza wa chama cha AfD Frauke Perry na kuamua kutokiunga mkono chama chake katika Bunge la Bundestag kunaweza kuwa na faida kwa Kansela Angela Merkel katika kupunguza ugumu wa kuunda serikali ya mseto.

Ni jambo la kusubiri kuona.