Home Makala Kimataifa HII NDIO SABABU  YA LUNGU KUMWACHIA HICHILEMA

HII NDIO SABABU  YA LUNGU KUMWACHIA HICHILEMA

165
0
SHARE

NA HILAL K SUED

MWEZI uliopita Agosti 16, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Zambia, Hakainde Hichilema, aliachiwa huru baada ya kuwekwa mahabusu kwa miezi minne.

Tukio hili ambalo lilikuja muda mfupi baada kuingilia kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, lilishangiliwa na watu wengi duniani hususan makundi ya wanaharakati wa haki za binadamu.

Wengi pia waliona kuachiwa kwake kulikuwa ishara iliyoonyesha kwamba, Rais Edgar Lungu, alikuwa ni mtu wa kutumia busara. Na wengine walisema Jumuiya ya Madola angalau bado ina nguvu ya ushawishi kwa wanachama wake. Hata hivyo, ukweli halisi ni tofauti na hayo.

Hichilema, kiongozi wa chama cha United Party for National Development (UPND), alikamatwa Aprili 11 na kufikishwa mahakamani kwa kosa la uhaini, kwamba msafara wake wa magari ulishindwa kutoa njia kwa msafara wa Rais Lungu ambao ulikuwa unaelekea sehemu moja na ule wa Hichilema.

Baadaye shtaka jingine liliongezwa, kwamba Hichilema na wengine walikula njama kuhamasisha kikundi kimoja kilichopachikwa mamlaka ya “Rais wa Jamhuri ya watu wa Zambia” katika sherehe iliyokuwa inafanyika eneo la Kuomboka ambalo wawili hao walikuwa wakienda kushiriki.

Katika kile mtu wa kawaida angeliona kama ni tukio tu la kosa la trafiki barabarani au kuingilia masuala ya itifaki kuhusu rais, badala yake likakuzwa na kuwa kosa la uhaini.

Polisi walimkamata Hichilema kwa kutumia nguvu kubwa kwa kile walichoita “kosa ambalo lingeweza kusababisha kifo kwa Rais wa Jamhuri ya Zambia kwa lengo la kupora mamlaka ya nchi.”

Wengi waliona matukio haya yanatokana na chama cha UPND kukataa kukubali ushindi wa Lungu, katika uchaguzi wa 2016. Kutiwa mbaroni kwa Hichilema, kulikuja mara baada ya mkutano na waandishi wa habari ulioitishwa na chama tawala cha Patriotic Front (PF) ambapo Naibu Katibu Mkuu wake, Mumbi Phiri, alidai Hichilema akamatwe na ashtakiwe kwa kosa la uhaini la kutokubali ushindi wa Lungu.

Na katika kipindi cha miezi minne kilichofuatia sauti nyingi zilipazwa ndani na nje ya Zambia zikitaka kesi dhidi ya Hichilema ianze kusikilizwa mara moja au aachiwe. Mamlaka zilitumia kila mbinu za kisheria kuchelewesha kesi ili tu kuendelea kumuweka gerezani kiongozi huyo wa upinzani na hivyo kupandisha joto la kisiasa nchini.

Jitihada kadhaa za kufanya mazungumzo kati ya Lungu na Hichilema hazikuwahi zinazaa matunda. Hivyo ilikuwa mpaka pale Patricia Scotland, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth), katika ziara yake ya siku nne nchini Zambia mapema mwezi uliopita ulipopokelewa kwa zulia jekundu ndipo Serikali ikaanza kutikisika.

Baada ya mikutano kadhaa baina yake na viongozi hao wawili (kila mmoja wakati wake) msuluishi huyo aliondoka siku nne kabla ya Hichilema kufikishwa mahakamani. Kesi ilikuwa ianze Agosti 16, lakini siku hiyo ilipofika, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) aliiondoa kesi hiyo mahakamani na hivyo kiongozi huyo wa upinzani kuwa huru.

Kuna baadhi wanasema msuluhishi huyo alitoa vitisho vya kuwawekea vikwazo vya usafiri viongozi na maofisa wa Zambia. Lakini kuna hoja nyingine ya mshiko, kwamba mivutano ya kisiasa ya ndani baada ya uchaguzi wa mwaka jana ilikuwa inapandisha joto na kumfanya Lungu kutumia mguvu kubwa za kibabe kuwashughulikia wapinzani hivyo kuanza kuonekana anaanzisha utawala wa kiimla.

Wachunguzi wa mambo wanasema hujuma dhidi ya Hichilema zilianza hata kabla ya uchaguzi wa Agosti 2016. Katika mkutano wake mmoja wa kampeni Juni 2016 Lungu, akijibu tuhuma za upinzani kwamba utawala wake ulikuwa unapanga kupora ushindi kupitia wizi wa kura, alijibu: “Kama Hichilema akikataa matokeo, ataona jinsi nitakavyomshughulikia.”

Kauli hii ilionyesha kwamba, Lungu alikuwa anapanga ushindi wake katika uchaguzi na kwamba mpinzani wake angeupinga ushindi huo. Aidha, ilionyesha kwamba Lungu alikuwa anatafuta sababu ya kumtia mbaroni Hichilema na kumfungulia mashtaka kama njia ya kumtisha akubali matokeo.

Wachunguzi wa mambo wanasema katika mpango huo shtaka la uhaini lilifaa zaidi kwa sababu halina dhamana, na hivyo likatafutwa ‘kosa’ kutokana na mwanya wa lile tukio la msafara wake wa magari.

Wanasema lengo kuu hasa halikuwa kumpata Hichilema na hatia, kwani mwenendo wa kesi nzima ungeibua mapungufu mengi tu kwa upande wa mashtaka. Lengo lilikuwa ni kumlazimisha ayakubali matokeo ya uchaguzi.

Kitu ambacho Lungu hakukitarajia ni nguvu kubwa iliyojitokeza ya kupinga kukamatwa kwa Hichilema. Kukamatwa kwake kulilaaniwa na viongozi mbali mbali barani Afrika – kutoka Kenya, Zimbabwe, Afrika ya Kusini na Nigeria ambao walidai kuachiliwa kwake mara moja.

Lakini upinzani mkubwa ulitoka Baraza la Maaskofu wa Katoliki la nchi hiyo (Zambia Conference of Catholic Bishops -ZCCB) ukiongozwa na Askofu Telesphore Mpundu. Wiki moja baada ya kukamatwa kwa Hichilema, Mpundu alitoa kauli iliyolaani tukio hilo na kumshutumu Lungu kwa kutaka kuanzisha utawala wa kidikteta.

Aidha, jitihada za watawala kuipuuza kauli hiyo zilikuwa na matokeo hasi – kwani taasisi mbili nyingine za dini – Council of Churches in Zambia na Evangelical Fellowship of Zambia nazo ziliunga mkono kauli ya Askofu Mpundu katika mkutano wao wa pamoja na waandishi wa habari.

Na Mei 25, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Afrika ya Kusini – Democratic Alliance (DA), Mmusi Maimane, alifukuzwa kutoka Zambia. Alikuwa amewasili kuhudhuria kesi dhidi ya Hichilema.