Home Makala Kimataifa VIONGOZI AFRIKA WAMESAHAU MISINGI YA UMOJA WAMEKUMBATIA UKOLONI

VIONGOZI AFRIKA WAMESAHAU MISINGI YA UMOJA WAMEKUMBATIA UKOLONI

144
0
SHARE

NA MPOKI BUYA

NINAPOLITAFAKARI Bara la Afrika naikumbuka hotuba ya karne ya Kwame Nkrumah aliyoitoa mwaka 1963 huko Addis Ababa – Ethiopia, ambayo hakuna kiongozi yeyote aliyewahi kutoa hotuba nzito yenye kugusa kila moyo wa mtu mweusi popote duniani.

Mwasisi huyu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (AU), alijua fika Afrika bado ina safari ndefu katika kujikomboa kutoka katika mikono ya wazungu (mabepari). Alijua kwamba Afrika ina safari ndefu katika kuumaliza umasikini, magonjwa, ujinga na vita ya wenyewe kwa wenyewe, hivyo katika hotuba yake maarufu na ya mwisho kabla hajapinduliwa ilikuwa ni hotuba ambayo itadumu daima katika mioyo ya watu weusi vizazi na vizazi.

Katika hotuba hiyo ngumu iliyopewa jina la “AFRICA MUST UNITE NOW “na kuwaambia kwamba Afrika haitafika popote pale kama hatutaungana, akiongea kwa uchungu aliwaambiaa wenzake wakina Julius Nyerere, Agustino Neto, Sokou Toure, Haile Selasie, Kenneth Kaunda na wengine wengi kwamba kabla hawajaondoka Afrika iwe tayari imeungana, lakini cha kushangaza hakuna kiongozi hata moja aliyemwelewa Nkrumah. Miaka 30 baadaye ndio wanatambua kwamba wangejua wangemsikiliza.

Afrika miti imebadilika lakini nyani ni wale wale, shida zimeliandama bara la Afrika na watu wake kama mwanga wa tochi unavyosafiri gizani, vita ya huko Congo, Burundi, Somalia, Afrika ya Kati na Mali, vyote vinatokana na kugombania madaraka.

Vita hivyo vinasababisha umasikini, magonjwa yasiyokwisha, ubaguzi wa rangi, ukiritimba na ukabila, ukandamizaji wa haki za binadamu, ukosefu wa chakula, udini kwa mfano huko Afrika ya kati na Nigeria, kuongezeka kwa makundi ya kigaidi kama Seleka, Ant-baraka, Janjaweed uko Sudan. Boko haramu kaskazini mwa Nigeria, ISIS – Libya na kaskazini mwa Afrika na kugombania mipaka. Viongozi  wabaya wanapoingia madarakani na mabaya huongezeka, viongozi wababe wanapotwaa madaraka watu wazuri wanakaa kimyaa, viongozi wazuri wanapoingia madarakani watu wazuri huibuka tena, wako wapi watetezi wa haki za binadamu Afrika?

Imefikia wakati Afrika hatuwezi kukemeana wenyewe mpaka tukemewe na Marekani au Uingereza. Wako wapi viongozi wa dini wa kukemea maovu Congo, Afrika ya Kati, Burundi, Zimbabwe, Rwanda, Angola, Sudani? Hakuna kabisa, wote wapo kimya wanaacha kizazi kiendelee kuangamiaa.

Ukisoma historia ya Afrika kuanzia miaka ya 1954 mpaka mwaka 2017 inafurahisha na kusikitisha sana, lakini ukisoma historia ya bara la Afrika kuanzia mwaka 1995 mpaka 2017 ndipo utagundu hali ilivyo mbaya.

Leo kijana ukienda Sudani Kusini makabila ya Nuela na Dinka wanachinjana mwaka wa sita sasa huu, Sudani Kusini ndio taifa changa na masikini kuliko yote  duniani. Umoja wa Afrika joka la kibisa halijui kukamata panya tena.

Afrika utakwenda wapi ukatalii zaidi ya Tanzania? Mataifa yaliyokuwa yanaitwa visiwa vya amani leo vimekuwa visiwa vya damu za wakina mama na watoto na dunia imetuacha tuendelee kumalizana. Hotuba ya Nkuruma imepuuzwaa; alisema Afrika inatakiwa iwe na jeshi moja ili iweze kutatua matatizo yake kwa wakati, lakini pengine leo Afrika ingekuwa ndio taifa pekee ambalo kuna amani na utulivu.

Afrika yetu ilikuwa na viongozi makini kama akina Thomas Isidore, Noel Sankara, haikuwa ya hovyohovyo kama ilivyo ya sasa katika baadhi ya nchi, wakina Sankara waliamini maendeleo ya Afrika huletwa na Waafrika wenyewe kwa kujituma na kudumisha umoja wa bara letu. Viongozi wa sasa hawaamini kama maendeleo yanaweza kuletwa na Waafrika, wanaamini maendeleo ya Afrika huletwa na wazungu. Thomas Sankara ndani ya muda mfupi alifanya makubwa Burkinabe, Afrika ya kina Odimba Toivo, Muhammad Sekou Toure na wakina Steven Biko, Nelson Mandela ilikuwa inathamini ngozi nyeusi.

Walitumia muda wao kuwatetea Waafrika, lilikuwa bara lililosimama vyema, si Afrika hii ya kina Jacob Zuma ambaye anatuhumiwa rushwa na kesi zisizo na msingi. Licha ya kuwa madarakani, Zuma ameshindwa kuzuia wenyeji kuwaua wageni (Xenophobia).

Mwaka 2015 Zuma alituhumiwa na Julius Malema kwa kutumia kodi za wananchi katika kukarabati jumba lake huko Kwa Zulu-Natal. Zuma ambaye mwaka 2010 alituhumiwa katika kesi ya ubakaji, bado serikali yake imetuhumiwa kuhusika na mauji ya waandamanaji wa migodini. Pamoja na hayo yote, sasa ameteuliwa kuwa mwenyekiti mpya wa SADC.

Afrika ya kina Kwame Nkrumah ilikuwa Afrika yenye malengo, ilikuwa inasonga mbele kwa kasi. Afrika ya sasa kiongozi akitoa hotuba inakuta imejaa vituko na vitisho kwa raia wake mwenyewe, viongozi wa sasa wakitoa hotuba zao muda mwingi anazungumzia chama chake na kutoa vitisho kwa chama pinzani badala kuzungumza kwamba baada ya miaka kadhaa Afrika itakuwa wapi, wao wanajadili namna ya kudhibiti upinzani. Tunaka kusikia baada ya miaka 15 ijayo tutakuwa tunazalisha tani milioni 20 za sukari au mahindi, tunataka kusikia ifikapo 2025 tutakuwa tumemaliza suala la umasikini na ujinga.

Katika bara letu la Afrika kiongozi akipanda jukwaani unatetemeka kwamba sijui ataongea nini! Wakina Kwame Nkrumah wakisimama walikuwa wanatoa hotuba zenye maono, wakina Nyerere wakitoa hotuba unafarijika, lakini sasa Afrika imebadilika, viongozi wetu hawasikilizi tena hotuba za kina Nkrumah, Sankara au Patrice Lumumba, wanasikiliza hotuba za kina Donald Trump na Putin.

Afrika ya kina Muamar Gaddafi wa Libya ambaye alikuwa anachangia asilimia 50 ya pato la mfuko wa Umoja wa Afrika ulioanzishwa na Nkrumah mwaka 1963, viongozi hawa hawakutaka mabepari waendelee kutufadhili, kwani walijua fika kwamba hakuna mzungu mwenye uchungu na Bara la Afrika zaidi ya kuja kuchota dhahabu na almasi.

Robert Mugabe kwenye kikao kilichofanyika mwaka huu Ethiopia alichangia ng’ombe 300 na wafuasi wake walichangia ng’ombe 300 ambao jumla walikuwa na thamani ya dola za Marekani milioni moja. Angekuwa na uwezo angechangia zaidi, nampa pongezi Mugabe. Tungepata viongozi wenye msimamo kama Mugabe Umoja wa Afrika usingelia njaa, umoja huo unashindwa kusimamia mambo yake ipasavyo, kwani unategemea msaada kutoka mataifa ya Ulaya na Marekani.

Leo AU hawana maana tena, kwani wanashindwa kutatua matatizo ya njaa, ugaidi, magonjwa na mazingira mpaka wapate msaada kutoka nje. Nkrumah alisema lazima Afrika ijitegemee, tusipojitegemea tutaendelea kutumiwa na kunyanyaswa na mabepari. Umoja umeshindwa kusimamia maamuzi yake wenyewe mpaka usikilize Marekani, Ujerumani, Ufaransa wamesema nini.

AU ambayo inafadhiliwa na wazungu kwa asilimia 60 ni ngumu sana kujitegemea. Umoja huo umeshindwa kuzuia vita inayoendelea Afrika ya Kati ya Waislamu na Wakristo, wanaochinjwa bila hatia. Kundi la Seleka wameshindikana mwaka wa saba sasa, wazungu wameshatuona wapuuzi wanatuangalia Afrika jinsi tunavyomalizana kwa mambo yasiyo na msingi.

Congo hakujawahi kuwa salama, mwaka wa 40 sasa bado hawajawahi kupumzika, kila siku ni vita, ni mauaji tu. Thomas Sankara walisisitiza umoja na mshikamano, walisisitiza upendo na ushirikiano, lakini baada ya waasisi wa bara hili kupinduliwa na wengine kufia gerezani hakuna kinachoendelea zaidi ya matukio ya kutisha kila kona ya Afrika.

Tumeshindwa kukemeana, kushikamana, wageni wanakuja kuchota madini na kutumia ardhi yetu. Tangu waondoke waasisi wameingia viongozi ambao wanajali matumbo yao wenyewe na marafiki zao, naishangaa Congo jinsi ilivyo masikini, achilia mbali madini na ardhi yenye rutuba waliyonayo. Afrika itajitambua lini? Wanaojiita wanaharakati wapo kwenye mitandao ya kijamii, ni nani atalitetea bara la Afrika?

Historia inaniambia walikuwapo watu wagumu sana miaka ya 1950 kama vile Herman Ondimba Toivo, viongozi ambao hawakuwa na kitu, lakini walikuwa na uchungu wa nchi zao na Afrika kwa ujumla wake, Toivo alikuwa mstari wa mbele katika kupambana na ubaguzi wa rangi huko Afrika Kusini, alifungwa na serikali ya kikoloni mwaka 1966 na kuachiwa mwaka 1984 akiwa ametumikia miaka 16 gereza moja na Nelson Mandela. Herman alikuwa mwanachama wa ANC, ingawa yeye alikuwa raia wa Namibia.

Leo viongozi wetu wamesahau misingi ya Afrika wamekumbatia misingi ya kikoloni.

Agustino Neto wa Angola aliamini katika umoja ili kuifikisha Afrika mbali, Lakini tunaona licha ya Congo kubarikiwa ardhi yenye rutuba, mito mikubwa, madini, ndio Taifa masikini la kutupwa duniani.

Licha ya Joseph Kabila kukaa madarakani miaka 16 mpaka sasa, hakuna anachojivuniaa hata kimoja kwa kuwa Wakongo wanakufa na kuteseka na umasikini. Hapo napata picha na akili kwamba kumbe kukaa madarakani muda mrefu siyo tija wala sifa, unaweza ukakaa madarakani muda mrefu lakini usifanye chochote.

Bali ni kuacha majonzi na maumivu kwa wananchi wako mwenyewe. Tangu aingiee madarakani mwaka 2001, Wacongo walimwamini sana, walimuunga mkono, lakini leo watu wanakufa kwa kuandamana na kutaka kumwondoaa madarakani. Alitakiwa kuondoka madarakani Desemba mwaka 2016, lakini mpaka sasa yupo, tena ametangaza kuondoka madarakani mwaka 2018.

Viongozi wengi wa Afrika wanaifanya Katiba kama mchezo wa kamari, wanapenda kamari lakini wanaliwa. Tunahitaji viongozi kama wakina Herman Ondimba, ambaye alipambana na wazungu Afrika Kusini, alipambana na wazungu Namibia, alipambana na wazungu Zambia, alikuwa  na roho ngumu kwa ajili ya Bara la Afrika. Hakupenda kuona Afrika ikiangamia na kupoteza heshima yake.

Mwandishi wa makala haya ni msomaji wa RAI, anapatikana kwa simu namba 0762155025 au barua pepe; mpokibuyahgmail.com