Home Makala MUBUTU SESESEKO ALIIFANYA DRC DAMPO LA WALANGUZI (1)

MUBUTU SESESEKO ALIIFANYA DRC DAMPO LA WALANGUZI (1)

178
0
SHARE

Na Mbwana Allyamtu


NIMEKUWA nikitoa makala kadhaa katika hizo nchi ambazo nilizitembelea, ikiwa ni pamoja na nchi hii ya Kongo-DRC ambayo nitaanza kuifanyia upembuzi sasa.

Nitaanza kwa kuchambua namna Rais wa pili wa nchi hiyo, Mobutu Seseseko, alivyochangia mauaji ya Waziri Mkuu wa kwanza wa Kongo–DRC, Patrice Lumumba.

Pia jinsi alivyoigeuza Kongo kuwa jalala la mabepari. Pamoja na hilo nimeona ni vyema kuuendeleza waraka huu kwa sababu historia ya Kongo imekuwa kivutio tosha kwa wasomaji wengi.

Kimsingi Kongo-DRC kumekuwepo na machafuko ya kisiasa ya wenyewe kwa wenyewe kwa karibu miaka 55 sasa toka Taifa hilo lijinyakulie uhuru wake Juni 30, mwaka 1960 kutoka kwa Ubelgiji (Belgium). Hali ya kisiasa ni ngumu mno hasa mashariki mwa nchi hiyo. Machafuko yamekuwa katika sura kuu mbili, yani vita mashariki ya Kongo-DRC vikiongozwa na makundi ya waasi na pili  mivutano ya kisiasa.

Hata hivyo, mantiki hizo mbili ndio mijadala mikubwa duniani juu ya Kongo-DRC kwani pande zote za dunia hujadili mustakabali wa Kongo-DRC kwa kutazama nyanja hizo mbili nilizozitaja hapo juu.

Hivyo basi leo tutatazama kwa undani juu ya namna Mobutu alivyoifanya Kongo kuwa Taifa linalonuka damu ikiwa ni pamoja na kifo cha Mwasisi wa Taifa hilo, Patrice Lumumba na namna gani Mobutu alichagiza kifo hicho.

Nasema hivyo kwa sababu yapo mengi niliyoyaona na kujifumza nilipokuwa nchini humo. Kabla ya kubobea katika uchambuzi huu si vibaya tukaifahamu Kongo-DRC kijiografia, kiutamaduni, kihistoria na kiutawala.

Kijeografia, Kongo-DRC ni nchi ya pili kwa ukubwa barani Afrika yenye ukubwa wa karibu hekta milioni 2.24 na eneo ambalo ndio msitu mkubwa barani Afrika unapatikana msitu wa Kongo. Pia Mto Kongo ni mto wa pili kwa ukubwa Afrika ukipakana idadi ya wakazi wake ni milioni 72 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2013. Mji mkuu wake ni Kinshasa.

Kiutawala

Rais Joseph Kabila ndiye mkuu wa nchi hiyo kwa sasa, ni rais wa nne na kiongozi mkuu wa tano toka nchi hiyo kupata uhuru mwaka 1960. Kiutawala nchi hiyo imegawanyika katika majimbo 11 ambayo ni Jimbo la Katanga, Jimbo la Bandundu, Jimbo la Orientale, Jimbo la West Kasai, Jimbo la East Kasai, Jimbo la North Kivu, Jimbo la South Kivu, Jimbo la Bakongo, Jimbo la Equator, Jimbo la Kinshasa na Jimbo la Maniema. Hata hivyo, zipo taarifa kuwa kumeongezwa majimbo mengine.

 

Kiutamaduni

Kongo kuna makabila makubwa manne na madogo madogo zaidi ya 500. Kati ya makabila hayo makubwa ni kabila la Luba, Wakongomani, Wakasai na Washinwa (Wangala); wanazungumza Lingala.

 

Kihistoria

Kongo-DRC ni miongoni mwa nchi zenye historia kubwa barani Afrika toka mwaka 500 BC, lakini huwezi kuzungumza historia ya jamii ya Wabantu kuanzia migawanyiko ya makabila ya Wabantu toka mwaka 100 BC ukaacha kuitaja Kongo.

 

CHIMBUKO NA HISTORIA YA KONGO-DRC

 

Wakazi wa kwanza huaminiwa kuwa walikuwa ni wawindaji wa jamii ya Wasani pamoja na Wambilikimo (Wambute) walioishi Kongo katika karne ya 4BC, badaye walifika wahamiaji Wabantu wenye ujuzi wa kilimo na uhunzi katika karne ya 2 BC.

Jina la Kongo linahusiana na Mto Kongo unaopitia nchi yote na pia Ufalme wa Kongo uliopatikana zamani katika sehemu za magharibi za Angola na Kongo ya leo. Upande wa kusini, kuanzia karne ya 17, kulikuwa na ufalme ulioitwa Dola la Kazembe ambalo lilikuwa koloni binafsi.

Na baada ya mkutano wa Berlin mwaka 1884-1885, Kongo ilianza kutawaliwa na Ubelgiji ambayo iliwekeza kiuchumi Kongo na kuanzisha makampuni makubwa ya migodi kama vile ‘Société Générale’ na ‘Union Minière du Haut Katanga’ yalichimba madini hasa katika Jimbo la Katanga. Makampuni haya yalikuwa na athari  kubwa.

Jimboni Katanga ilikuwa maarufu kwa shaba iliyochimbwa huko. Pia kwa uranium iliyotumiwa kwa mabomu ya kwanza ya kinyuklia ya Marekani mwaka 1945. Kutokana na ukoloni na unyonyaji kukithiri uliofanywa na wakoloni wa ubelgiji kwa muda, ndipo vuguvugu la ukombozi lilipoanza.

Kuanzia miaka ya 1920, Wakongo wengi walionyesha upinzani huo katika mahudhurio katika makanisa ya Wazungu na kuanza kujiunga na madhehebu mapya ya wafuasi wa dini ya Kiafrika ya Simon Kimbangu yaliyopigwa marufuku na Wabelgiji kuanzia mwaka 1926. Tangu mwaka 1950 upinzani uliongezeka na kuonyesha pia uso wa kisiasa.

Hata hivyo, nchi hiyo ilipata uhuru wake mwaka 1960 chini ya Serikali ya umma iliyoongozwa na Patrice Lumumba na Joseph Kasavubu, baada ya uhuru huo nchi iliingia katika mgogoro mkubwa wa kiutawala ambao baadaye uliigharimu Taifa, jambo ambalo aliyekuwa Rais Joseph Kasavubu alimfukuza kazi Lumumba Septemba 5, mwaka 1960, lakini naye Lumumba alitumia bunge kupiga kura ya kutokuwa na imani na Rais Kasavubu, hivyo Lumumba akatangaza rasmi kumfukuza kazi Kasavubu.

Katika mtifuano huo ndipo yakatokea mapinduzi ya kipandikizi yaliyoongozwa na  kiongozi wa jeshi mwenye cheo cha ukanali ‘Mobutu Sese Seko (Joseph Mubutu)’ aliuchukua uongozi na kutangaza kuitawala Zaire (Kongo ya sasa) akishirikiana na Kasavubu Septemba 14, 1960, ambapo aliunda Serikali ya mpito mpaka pale alipomtimua kazi Kasavubu na kuikalia Kongo-DRC kijeshi Septemba 2, 1964.

 

MOBUTU SESE SEKO NI NANI?

Kwakuwa makala haya maudhui yake ni kumwsangazia Rais Mobutu aliyeitwa rais wa enzi wa zama zile Kongo ikiitwa Zaire ambaye ndiye aliyeifanya Kongo-DRC ionekana Taifa lililopoteza dira na kuwa sehemu isiyo salama kabisa katika Afrika kuishi. Sasa tuianze kwa kumwangazia Mobutu kama ifuatavyo;

Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu wa Za Banga alikuwa kiongozi wa kijeshi dikteta huko Zaire (sasa Kongo-DRC). Mke wake wa kwanza, Marie-Antoinette Mobutu, alifariki kwa ugonjwa wa moyo Oktoba 22, mwaka 1977 Genolier- Switzerland akiwa na umri wa miaka 36. Na hatimaye Mei mosi mwaka 1980 alimuoa Bobi Ladawa pamoja na pacha mwenzake Kosia, Bobi na Kosia ni pacha wanaofanana na mzee aliamua kuoa wote wawili.

Mobutu alitoka kabila la Ngbandi na alizaliwa Lisala Congo, mama yake Mobutu Marie Madeleine Yemo, alikuwa mhudumu wa hoteli aliyekimbia kijijini kwao Lisala kwa vitisho vya chifu wa kijiji.

Alikutana na baba yake Mobutu Alberic Gvemani ambaye alikuwa mpishi wa jaji wa Kibelgiji. Jina la Mobutu alipewa na mjomba wake, baba yake Mobutu alifariki akimwacha na umri wa miaka nane. Mke wa jaji alihuzunishwa sana na kifo hicho na alijenga mapenzi makubwa kwa kijana Mobutu, alianza kumfundisha kuongea, kusoma na kuandika Kifaransa hatimaye Mobutu alikuwa na uwezo mzuri sana wa lugha hiyo.

Mama yake aliyeitwa Yemo, aliishi kwa kutegemea msaada wa ndugu na jamaa, hali iliyomlazimu kuhama kila mara ili kukidhi mahitaji ya watoto wanne alioachiwa. Elimu ya kwanza ya Mobutu ilikuwa Leopoldville, lakini mama yake alimhamishia kwa mjomba Coguilhaville, ambako alijiunga na Shule ya Christian Brothers School, hii ilikuwa shule bora chini ya kanisa katoliki. Kutokana na umbo lake, alikuwa maarufu katika michezo, alikuwa na uwezo mzuri kimasomo pia. Pamoja na haya alikuwa mhariri wa gazeti la darasa.

Mobutu pia alijulikana kwa kuiga kwa kubeza, wanafunzi wenzake wanakumbuka alivyokuwa anambeza padre wa Kibelgiji ambaye lugha yake ya kwanza ilikuwa Kiholanzi alipoongea Kifaransa kwa makosa. Mwaka 1949 Mobutu alitoroka shule kwenda Leopoldville kukutana na rafiki zake wa kike. Mapadre waligundua hilo, walimkamata wiki chache baadaye. Mwaka wa shule ulipokwisha Mobutu alipewa adhabu ya kutumikia jeshi kwa kosa la kutoroka shule hii ilikuwa adhabu wa wanafunzi watukutu.

Mwandishi wa makala haya ni msomaji wa RAI na mchambuzi wa masuala ya kidiplomasia. Anapatikana kwa simu namba +255679555526 na DRC