Home Habari CCM YATAMBA KUCHUKUA KATA ZOTE ARUSHA

CCM YATAMBA KUCHUKUA KATA ZOTE ARUSHA

365
0
SHARE

Na ABRAHAM GWANDU, ARUSHA

VYAMA vya siasa vyenye ushindani katika medani za siasa nchini, Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema ) vimeanza majigambo ya kushinda uchaguzi wa marudio katika Kata nane za mkoa wa Arusha.

Pamoja na mkoa huo kujulikana kama ngome imara ya kisiasa kwa vyama vya upinzani hususan Chadema, safari hii viongozi wa CCM wamejiapiza kwa gharama yoyote kuisambaratisha ngome hiyo kwa kushinda kata zote katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Novemba 26, mwaka huu.

Aidha, wakati CCM ikishindwa kuweka wazi viongozi wa kitaifa watakaoshiriki uzinduzi rasmi wa kampeni zao, kwa upande wa Chadema kimeweka wazi baadhi ya viongozi wake watakaoshiriki.

Viongozi hao ni pamoja na wabunge mashuhuri, viongozi wa kitaifa akiwamo Mwenyekiti Freeman Mbowe, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Edward Lowassa naye ametajwa kushiriki kikamilifu kunadi wagombea katika Kata mbalimbali.

Akizungumza na RAI jana kwa njia ya simu akiwa eneo la Usa River wilayani Arumeru, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Arusha Shabani Mdoe alisema pamoja na kwamba hawajaanza kampeni, lakini Chama chao kina uhakika wa kushinda Kata zote.

Katika mahojiano hayo, Mdoe alizifananisha kampeni za Chadema ambazo hazijazinduliwa rasmi kuwa ni sawa na baiskeli ya mbao ambayo hata ikitangulia kuanza safari haitafika mbali itakuwa imeachwa na chombo chenye kasi (CCM) na kufika mwisho wa safari ya ushindi.

“Hapa ninapozungumza na wewe tupo kwenye vikao vya mkakati wa kufanikisha ushindi katika Kata zote,wenzetu Chadema tayari wameanza kampeni sisi bado lakini nikuhakikishie tumewatanguliza kama baiskeli ya mbao ambayo tutaipita wakati haijafika kokote,”

Aidha alipoulizwa sababu za kujiamini wakati Kata zote hizo zilikuwa mikononi mwa Chadema kabla ya madiwani waliochaguliwa kujiuzulu kwa kile kilichodaiwa na Mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari na yule wa Arusha Mjini Godbless Lema ni kununuliwa na CCM ,Mdoe alisema washindani wao hawana sera.

“Washindani wetu hawana sera wala ajenda mahususi ambayo wataitumia kuwashawishi wapiga kura ambao kwa mujibu wa utafiti mdogo niliofanya  tayari wameng’amua kuwa Chadema hawawezi kuwaletea maendeleo zaidi ya kuwatukana majukwaani viongozi wakuu wa kitaifa akiwemo Dk. John Magufuli.

“Hivi jiulize ni mpiga kura gani atakuwa tayari kumchagua kiongozi ambaye ni lazima baadaye atakwenda kuomba hela za kujenga miundombinu ya barabara, maji ,afya na elimu huku akifahamu ilani inayotekelezwa ni ya chama kilichoshika dola ambayo kwa sasa ni CCM?” alihoji Mdoe.

Kuhusu uwezekano wa nafasi finyu ya  ushindi wa chama chake bila kusaidiwa na vyombo vya dola ,Mdoe aling’aka na kushangazwa na madai hayo kwa kile alichosema kuwa ni jambo lisilowezekana katika ulimwengu wa teknolojia.

“Vyama vyote vinao mawakala katika vituo huku kura zikijumlishwa na matokeo kusambazwa katika mitandao hata kabla ya majumuisho,hizi ni dalili za kushindwa hata kabla kura hazijapigwa ,sisi tutashinda kihalali kwa vile serikali inayoongoza inatimiza wajibu wake na wananchi hasa wapiga kura wanaona kwa macho yao ,watatuchagua kwa hayo sio vinginevyo “ alisema Mdoe.

Kwa upande wake  Chadema kupitia kwa Katibu wa Kanda ya Kaskazini Amani Golugwa alisema kauli na majigambo ya CCM ni ishara kuwa huenda chama hicho kimejipanga kuiba kura jambo ambalo ameonya kuwa wasithubutu kwani chama chake kimejipanga kuwashghulikia watakaoiba kura mithili ya mwizi.

“Kazi yetu imerahisishwa na viongozi wa kitaifa wa CCM, tunayo masuala mengi ya kuwaelimisha na kuyafafanua kwa wapiga kura, ila hatubezi majigambo yao huenda wamejipanga kuiba kura nawaonya wasithubutu kwasababu tutawashughulikia kama mwizi”

“Chadema inakumbuka kauli ya aliyekuwa DC wa Arumeru ambaye sasa ni RC wa Manyara kuwa mkurugenzi asithubutu kumtangaza mgombea wa Chadema hata kama atashinda bali amtangaze wa CCM.”alisema na kuongeza.

“Iwapo hayo ni maagizo na yatatekelezwa itakuwa kosa la jinai kwa mujibu wa sheria ,sisi tutakabiliana na huyo muhalifu kama mwizi kabla ya kumkabidhi Polisi ,wewe unajua mwizi anavyofanywa kabla hajafikishwa kwenye vyombo vya sharia” alionya Golugwa.

Golugwa alisema kuwa chama chake kimejipanga kushinda Kata zote sio tu za Mkoa wa Arusha bali Kanda nzima ya Kaskazini ili kuimarisha ngome yake katika Mikoa ya Arusha , Manyara, Kilimanjaro na Tanga na kwamba ili kufanikisha mkakati huo viongozi wote wa kitaifa wakiwemo Mwenyekiti Freeman Mbowe, Mawaziri Wakuu wastaafu Edward Lowassa na Frederick Sumaye wanatarajiwa kushiriki kampeni za kuwanadi wagombea  .

Pia alizungumzia uamuzi wa Chadema kukata rufaa tume ya taifa ya uchaguzi mara baada ya kuenguliwa kwa wagombea wa chama hicho katika Kata mbili za Ngabobo na Makiba wilayani Arumeru na kwamba tayari wamejaza fomu namba 12.