Home Latest News CHANGAMOTO ZA ‘WAMACHINGA’ ZAHITAJI UFUMBUZI WA HARAKA

CHANGAMOTO ZA ‘WAMACHINGA’ ZAHITAJI UFUMBUZI WA HARAKA

222
0
SHARE

NA HILAL K. SUED

MWAKA uliopita Rais Dk. John Magufuli, alitoa agizo kwa mamlaka za Mkoa wa Dar es Salaam kutowabughudhi wafanyabiashara wadogo wadogo wa mitaani maarufu wamachinga, kwani wengi wao ndio waliompigia kura.

Lakini hata hivyo alitoa kauli ya ziada kwa kusema wafanyabiashara hao wanaweza kuhamishwa iwapo tu watatengewa maeneo mengine ambayo yatakuwa rafiki kwa shughuli zao.

Tangu wakati huo mandhari ya Jiji la Dar es Salaam, hususan maeneo ya katikati ya Jiji yamebadilika, pembezoni mwa barabara kadhaa ambazo hapo awali zilikuwa tupu sasa zimejaa wafanyabiashara hao wakiwa wametandika bidhaa zao kusubiri wateja. Hii inaonyesha agizo moja la Rais Magufuli limetimizwa kikamilifu, la kutowabughudhi wafanyabiashara hao.

Lakini lile la pili la kuwahamisha endapo tu watatengewa maeneo rafiki, bado halijapatiwa ufumbuzi na bila shaka linashindikana kutokana na changamoto kadhaa, kubwa ni ile ya kuwapatia maeneo rafiki. Kuna baadhi pia wanataja sababu nyingine ya mgongano ni mamlaka ipi inayohusika katika suala hilo, ile ya Serikali ya mkoa au Halmashauri ya Jiji.

Itakumbukwa kwamba miaka miwili tu baada ya kuingia madarakani, utawala wa Awamu ya Nne ya Jakaya Kikwete ulianzisha kampeni kabambe ya kulisafisha Jiji la Dar es Salaam kwa kuwaondoa wafanyabiashara hao wa barabarani kutoka katikati ya Jiji pamoja na kuviondoa vibanda vya biashara “vioski” vilivyokuwa vimezagaa mji mzima na kupoteza kabisa mandhari nzuri ya Jiji.

Na hapo hapo Serikali ya Kikwete ilitangaza kuwajengea wafanyabiashara hao eneo lao la biashara Ilala lilikuja kujulikana kama “Machinga Complex” kwa msamiati usio rasmi.

Hata hivyo, uamuzi wa kujenga makazi haya rasmi, ambayo pia ilitangazwa yangejengwa katika wilaya nyingine za Jiji sasa unaonekana ulikuwa wa kisiasa zaidi kuliko wa kihalisia katika kuwahudumia wafanyabiashara ndogo ndogo wa jijini Dar es Salaam ambao wengi wao ni vijana walioshindwa kuendelea na elimu ya juu kwa sababu mbalimbali.

Hadi sasa hivi majengo hayo hayajakidhi malengo yaliyokusudiwa na badala yake baadhi ya sehemu za majengo hayo polepole yamekuwa yakibadilishwa na kuwa matumizi ya ofisi mbalimbali.

Wadadisi wa mambo wanasema huwezi kuwajengea makazi ya ghorofa wachuuzi wa barabarani. Wanasema bora lingetafutwa eneo kubwa tambarare na kuwajengea vibanda tu au sana sana yawe na ghorofa moja tu.

Na kutokana na hali hii, Halmashauri ya Jiji ambao ni mmiliki wa majengo hayo imeshindwa kulipa mkopo wa kujengea uliotolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii – NSSF hadi kupendekezwa kwamba majengo hayo yakabidhiwe Mfuko huo kuyaendesha ili ijaribu kurejesha fedha zake.

Agizo la Rais Magufuli la kutaka wamachinga wasibughudhiwe bila shaka linatokana na kuwaona vijana ni kundi katika jamii lenye changamoto nyingi pamoja na kuwa na elimu duni, ukosefu wa ajira na kadhalika.

Katika kipindi chake chote cha miaka 10, Jakaya Kikwete, mtangulizi wa Dk. Magufuli, hakulipa tatizo la vijana kipaumbele kinachostahili. Kwa mfano hakuwahi hata siku moja kukutana nao ana kwa ana kuwasikiliza. Lakini katika kipindi hicho hicho, kwa nyakati tofauti amekutana na wazee, hususani wa Dar es Salaam takribani mara tano.

Na karibu mara zote hizi amekutana na wazee hao si kwa ajili ya kupata ushauri kuhusu mustakabali na maendeleo ya taifa, bali ni katika kujitetea au kuutetea utawala wake kuhusu dosari na/au kashfa ndani ya utawala, kwa mfano kashfa ya Akaunti ya Escrow.

Mikutano hiyo iligeuzwa kuwa ni jukwaa la yeye kutoa hotuba kwa wazee hao na si kujadiliana nao kwa njia ya usawa kama ilivyokuwa enzi za Mwalimu Nyerere.

Kwa ujumla mikutano hii ya Kikwete na wanaodaiwa kuwa wazee wa Dar es Salaam, imegeuzwa kuwa mahali pa kulishtaki kundi fulani katika jamii linaloonekana kwenda kinyume cha utaratibu na kuashiria tishio kwa chama tawala.

Aliwahi kukutana na wazee hao, pia kwa njia ya kuwahutubia, kuwashtaki kwao madaktari waliogoma na wanaharakati waliowaunga mkono. Wazee ilikuwa ni mahala pa kujipa ahueni (solace) kutoka kwa wazee hao.

Kuna baadhi wanasema kwamba, laiti Kikwete angekutana na vijana wa biashara ya ‘kimachinga’ kabla ya kuwajengea majengo yale ya ‘Machinga Complex’ jijini Dar es Salaam kwa kupata ushauri wao kwanza, majengo yale yasingejengwa, hasa kwa namna yalivyojengwa.

Hivyo basi kuna wito kwamba ingefaa Magufuli apange kukutana ana kwa ana na vijana na kutaka mawazo yao kuhusu mustakabali wao katika jamii.

Maagizo ya kusema tu wasibughudhiwe hayatoshi katika kutatua changamoto zao ambazo ni lukuki. Halafu isitoshe hadi lini wataendelea kuzagaa pembezoni mwa barabara za Jiji la Dar es Salaam? Sifikirii hata yeye anaridhika kwa vijana hawa kuwa barabarani daima dumu.

Kuna siku Serikali inaweza kusema imepata ufumbuzi lakini itajikuta inapata wakati mgumu kuwaondoa kutokana na wingi wao.