Home Habari KAULI ZA JPM ZAIBUA MJADALA BUNGENI

KAULI ZA JPM ZAIBUA MJADALA BUNGENI

387
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI

KAULI za Rais John Magufuli alipokuwa ziarani hivi karibuni zimeonekana kuligawa Bunge baada ya baadhi ya Wabunge wa upinzani kulalamikia kauli hizo kuwa zina upendeleo huku Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mawaziri wakihaha kuzitetea.RAI linaripoti.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku chache zimepita baada ya Rais Magufuli, ambaye alifanya ziara mkoani Mwanza na kuwataka mawaziri husika na viongozi wa chama na mkoa, kutowabomolea wakazi wa eneo la Kigoto Mwanza, kwa sababu walimpa urais na pia wanatakiwa waangaliwe na jicho la huruma.

Aidha Novemba 7, mwaka huu, Rais Magufuli alipiga marufuku viongozi wanaozuia wananchi wanaolima kando ya mito baada ya kupokea kero ya kijana aliyejulikana kwa jina la Rosh Omary, ambaye alilamika kuwa mazao yake yalifyekwa kando ya Mto Nkenge, Kyaka mkoani Kagera.

Kufuatia kauli hizo, mjadala mkali umeibuka katika vikao vya Bunge ambavyo vilianza Jumanne wiki hii. Baadhi ya Wabunge wa upinzani waliochangia mjadala kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2018/2019, walizilalamikia kauli hizo.

Mjadala huo uliibuliwa na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa juzi jioni, wakati akichangia mapendekezo hayo ambapo pamoja na mambo mengine, alisema kauli ya Rais Magufuli kuwa wakazi wa Kigoto, wasibomolewe nyumba zao kwa kuwa walimpa kura nyingi za urais. Alisema hicho ni moja ya kiashiria cha kutokuwapo kwa utawala bora nchini.

“Katika awamu hii, ili tujue tabia za utawala bora, unaweza kuona lazima kuwepo na ushirikishwaji, lazima kuwe na utawala wa sheria, watu wakitaka kuhoji wanakataliwa tunaweza kutekeleza huu mpango?

“Utawala bora ni kwa serikali zote. Wanasema hakuna upendeleo wakati maeneo mengine wanaambiwa kwa sababu ninyi mlinipa kura hamtabomolewa, maeneo mengine wanabomolewa. Hapo kuna utawala bora?” Alihoji Msigwa na kumuibua Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenister Mhagama ambaye alisema si kweli kuwa Serikali ina upendeleo.

“Kwa mujibu wa kanuni ya 68, 64 1(a) anachosema Mbunge jambo hili si la kweli kwa kuwa Serikali haijawahi kuvunja mahali popote kwa sababu eneo hilo halikutoa kura kwa Serikali yetu.

Waziri alisema uvunjaji wa majengo utazingatia sheria na kanuni, Mbunge asipandikize maneno ambayo si kauli za Serikali ndani ya Bunge letu,” alisema.

Hata hivyo, Msigwa alikataa kauli hiyo na kusema ananukuu maneno aliyosema Rais alipokuwa Kanda ya Ziwa.

“Alisema ninyi hamtabomolewa kwa sababu nyinyi mlinipa kura. Na nimesema kwenye tabia za utawala bora lazima kusiwepo na upendeleo, ukienda Kimara, Tabora ni mabuldoza tu, hamkusikia haya mambo,” alisema Msigwa.

Aidha, Mhagama alitetea tena kwa kuomba utaratibu, ambapo alisema Msigwa amevunja kanuani 68 (1) na 64 (1) na 64 1 (d) anataka kutumia jina la Rais katika kushawishi Bunge litoe maana ya kazi za kitaasisi ambazo si sehemu ya majadala huo.

Pia Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula, aliomba taarifa na kusema kuwa katika eneo hilo, tayari kumebomolewa nyumba nne.

Hata hivyo, Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), naye aliomba taarifa na kusema kuwa Rais yuko Kagera na kasema wale waliojenga pembeni ya mito wasibughudhiwe kabisa.

Aidha, mjadala huo ukaibuka upya tena jana katika kipindi cha maswali na majibu wakati Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Kangi Lugola, akijibu swali la Mbunge wa Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwanko (CCM), aliyetaka kujua mkakati wa Serikali katika kukabiliana na athari za mazingira katika vyanzo vya mito.

Wakati akijibu swali hilo, Lugola alisisitiza kuwa Rais Magufuli alitumia kifungu cha 57 cha Sheria ya Mazingira kuruhusu vijana wa eneo la Kyaka kulima kando ya mito.

Hata hivyo, Msigwa aliibuka tena na kutaka kujua wananchi wamsikilize Rais, au waziri na ni sheria gani inatoa huo upendeleo.

“Rais anatoa vibali kwa mujibu wa sheria, na akaagiza wizara kuandaa utaratibu wa kutoa vibali hivyo vya kulima ndani ya mita 60, Rais hajavunja sheria, ninyi mtakapochochea mtapambana na sheria,“ alisema Lugola.

Aidha, waziri mwenye dhamana, Januari Makamba, alisimama na kutoa maelekezo kuwa Serikali iliziagiza serikali za mitaa kuorodhesha vyanzo vyote vya maji na kupeleka taarifa wizarani.

“Kifungu cha 57 (1) kinaweka zuio, kifungu cha pili kinaruhusu waziri kuweka muongozo katika maeneo mahususi. Na tutaandaa mwongozo wa namna ya kufanya shughuli hiyo,” alisema Makamba.

Kauli za Rais Magufuli

Oktoba 30, mwaka huu, Rais Magufuli aliagiza wakazi wa eneo la Kigoto, Mwanza kutobomolewa numba zao kwa sababu walimpa urais na pia wanatakiwa waangaliwe na jicho la huruma.

“Tusiwafukuze tusubiri kwanza, kwa sababu ardhi yote ya nchi hii kwa mujibu wa Sheria Namba Nne ya mwaka 199, Sheria Vijiji Namba Tano ya mwaka 1999, Sheria ya Mipango Miji ya mwaka 20017, ardhi yote msimamizi wake ni Rais. Na mimi hawa wa Kigoto na wa Muze, ndio walinipa urais, inawezekana walifanya  makosa, lakini kwa sababu serikali yangu ina huruma, ndio maana ninasema ndugu zangu    msiwabomolee.

“Waziri wa ardhi na mawaziri wanaohusika na maeneo hayo,  Waziri wa Mambo ya Ndani, Uchukuzi na Ulinzi, wakae kwa pamoja waangalie ramani zote zilivyo ni mahali gani ambapo tunaweza  kuwa na human face, human face ya CCM, ni sura ubinadamu, na chama chenye sura ya ubinadamu ni CCM tu. Kwa hiyo wakae angalau ndani ya wiki tatu na mkuu wa mkoa na viongozi wa chama mtoe mapendekezo mapya.

Yapo maeneo ambayo kwa kweli itabidi lazima wahame. Kwa mfano yaliyopo ndani ya airpot, ndege kubwa zikija zitapeprusha nyumba zenu. Kama umejenga karibu na kifaru, siku kikilipuka utakuwa umelipukiwa,” alisema.