Home Latest News KIGODA CHA MWALIMU NYERERE KISAIDIE KUKEMEA MAOVU YANAYOTUSIBU

KIGODA CHA MWALIMU NYERERE KISAIDIE KUKEMEA MAOVU YANAYOTUSIBU

188
0
SHARE

NA BRYCESON MATHIAS

INGAWA maandiko matakatifu kwenye vitabu vya dini yanaonya kwamba, ‘amwagaye damu ya binadamu, damu yake itamwagwa na binadamu’ (mwanzo 9:6), naona kuna haja ya wadau wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere wakemee umwagaji damu, kwa kuwa huo si usia aliotuachia Baba wa Taifa.

Binafsi naumizwa sana moyo na kutokwa machozi nikiwashangaa baadhi ya Watanzania, walio wachafu wa mwili na roho waliofanya tuadhimishe kumbukumbu ya kumuenzi mwanzilishi wa Taifa hili Mwalimu, Julius Kambarage Nyerere, mwaka huu nchi ikiwa imeghubikwa na umwagaji wa damu tofauti na nia yake.

Nikisema hayo, nakumbuka maandiko matakatifu ya vitabu vya Mungu ‘yasemayo ‘Amwagaye damu ya binadamu, damu yake itamwagwa na binadamu; maana binadamu aliumbwa kwa mfano wa Mungu’ (Mwanzo 9:6). Najiuliza wanaofanya hivyo Mungu atawaacha?

Huu ni mwaka wa 18 hadi tulipofikia siku ya kuadhimisha kumbukumbu tangu kufariki kwake Oktoba 14, 1999, akiwa nchini Uingereza alipokuwa amelazwa akisumbuliwa na maradhi ya kansa ya damu.

Ni bahati mbaya kwa Watanzania,  ijapokuwa tunasifika kuwa kisiwa cha amani, kwa miaka ya hivi karibuni ardhi, kauli na matendo ya baadhi ya watu wetu, yameuuza ustaarabu wa nchi hii kwa shetani na kuifanya iwe kama dimbwi la kumwaga damu za watu wasio na hatia, kwa wanaosikika au kuonekana wanatetea haki!

Laana hii kubwa, hakuna kiongozi wa dini, Serikali, jamii, mila au ukoo atakayeikwepa kwa sababu vinywa vyao vimekaa kimya badala ya kukemea kwa nguvu uovu huu ambao kwa sasa hapa nchini, umekithiri na kuwa kama bidhaa rahisi ya kuku wao wakiwepo.

Mwalimu Nyerere ni Kiongozi pekee asiyeigwa ambaye alikuwa na kitambi na misuli ya uadilifu, ambaye nguvu zake kila nukta zilifikiria jinsi ya kuwafanya Watanzania wawe wamoja, wasiwe na udini, ukabila, ukanda, urafiki ukoo au uchama, tofauti na wenye uroho wa madaraka, ambao kwa sasa hung’angania vyeo hadi kuamua kumwaga damu za watu.

Tumeona na kushuhudia umwagaji damu huu maeneo mengi, ambayo hata nikiorodhesha kwenye makala hii nafasi haitatosha, lakini itoshe kukumbusha damu ya watoto wa ‘Lucky Vicent Arusha, damu ya Mbunge wa Singida Mashariki, Antipas Mughwai Lissu, mauaji ya Rufiji na Kibiti, maiti za kwenye viroba, mauaji ya Padre Zanzibar, mauaji ya Alphonce Mawazo, yawe kama kiwakilishi cha mengine yote.

Umwagaji mwingi wa damu uliofanyika nchini mwetu sasa umekuwa laana ambayo haiwezi kuoshwa kwa kujisafisha kwenye majukwaa ya siasa au visingizio vya ‘Watu wasiojulikana,’ isipokuwa  ni kwa viongozi wa dini, Jukwaa la Kigoda cha Mwalimu Nyerere’ kukemea umwagaji damu namna hiyo na ikibidi wahusika kutubu dhambi hiyo wakimaanisha ili Taifa hili lisafishike!.

Yawezekana kukemea kwa sauti za watu wengine maarufu kulikofanywa hakusikiki, kwa nafasi hii niombe Jukwaa la Kigoda cha Mwalimu Nyerere lichukue hatua ya kukemea umwagaji damu huo ikiwemo kuona maiti kwenye viroba, iwe kama sauti yetu Watanzania kumlilia Mungu na Baba wa Taifa, ikipita kwenye Kigoda hicho ili kukomesha ukatili huo.

Wakati wa uhai wake, Mwalimu Nyerere alichukia na kukemea vikali aibu na mambo yasiyofaa kwa ustawi na mustakabali wa maendeleo ya Tanzania, Afrika na dunia kwa ujumla, tofauti na leo ambavyo viongozi wengi na hata wa dini ambao baadhi yao wamekuwa kimya hawathubutu hata kupinga umwagaji damu huo, isipokuwa kutoa matamko yasiyo na matendo.

Katika uhai wake, Mwalimu Nyerere alichukia na kukemea vikali takribani mambo 11 ikiwa ni pamoja na:

UJINGA

Mwalimu Nyerere alikuwa ni miongoni mwa wasomi na waumini wachache na ni Mtanzania wa kwanza kupata nafasi ya kusoma masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Edinburg, Uingereza na kuhitimu mwaka 1952 akiwa ni gwiji wa uchumi na historia, lakini leo hii hatuoni magwiji wa kukemea umwagaji damu hadharani labda Askofu Dk. Josephat Gwajima wa ufufuo na uzima ambaye amethubutu bila woga.

Mwalimu hakupenda ujinga na hivyo alipigana vita kali dhidi ya ujinga na alifanikiwa kwa nafasi yake kuwaondolea ujinga Watanzania wengi, wakiwamo viongozi wetu wa sasa ambao walisomeshwa bure katika mazingira mazuri ya kuridhisha kwa manufaa ya nchi yetu.

Ndiyo maana Rais Kikwete Februari 3, mwaka 2007 alisema: “Sisi tuliwekezwa na ni lazima tuwekeze kwenu ili miaka 30 ijayo rais atoke miongoni mwenu”. Kama Nyerere asingechukia ujinga kwa kuboresha mazingira ya elimu, ikiwemo elimu ya watu wazima, basi leo hii tungekuwa na vingozi zezeta’.

Vita ya ujinga sasa si yakuridhisha. Watanzania wengi hasa waishio vijijini hawajui kusoma na kuandika pamoja na kutoa elimu ya msingi bure na kupunguzwa ada ya sekondari na kuongeza idadi ya madarasa, bado shule hizi zinakosa waalimu na vifaa vya kutosha.

Pia idadi kubwa ya Watanzania pamoja na kufaulu hawapati nafasi ya elimu ya juu kutokana na sera chakavu na mifumo kandamizi iliyopo nchini, kama ya kuangalia madaraja katika utoaji wa mikopo na asilimia za uchangiaji gharama za elimu ya juu. Inasikitisha kwa Watanzania badala ya kukuza maendeleo ya elimu tunakuza umwagaji damu.

Kwanini hatujifunzi kwenye usemi huu? “If education is Expensive try ignorance as your option” (Kama elimu ni ghali, jaribu ujinga). Serikali yetu ni wazi kabisa kuwa inaona elimu ni gharama, hivyo imeamua kujaribu ujinga kwa kile inachokiita kuchangia elimu ya juu eti Serikali haina uwezo. Je, kumwaga damu ndiko kuzienzi fikra za Mwalimu Nyerere?

UBINAFSI NA UFISADI

Katika mambo aliyoyaamini sana na kuyapa mkazo wa aina yake, ni pamoja na masuala ya haki na usawa. Mwalimu siku zote alijenga imani katika misingi ya utu, haki na usawa kwa kila raia wa dunia hii.

Aidha, Mwalimu alipinga sana mianya ya unyonyaji aliyoiita ‘mirija’. Mwalimu alipinga sera za kuleta matabaka katika Taifa, iwe ni matabaka ya kiuchumi kwa kuwa na kundi la walionacho na wasionacho, udini, ukabila, uswahiba na urafiki katika uongozi wake.

Mwalimu hakuruhusu ubinafsi na ufisadi ambao leo hii umekithiri miongoni mwa viongozi wengi hapa nchini ambao umeganda kama kupe hata kwenye taasisi za dini nchini bila woga wala hofu ya Mungu.

Mwalimu aliwahi kusema: “Hakuna mtu yeyote katika jamii atakayekuwa na mahitaji yote muhimu wakati wengine katika jamii hiyo hiyo hawana chochote”. Na huu ni ukweli usiofichika, Mwalimu Nyerere asingekuwa mzalendo wa kweli basi leo hii familia yake ingekuwa ndio mabilionea wa nchi hii.

Mwalimu alijikita katika siasa ya ujamaa na kujitegemea na hatimaye Azimio la Arusha mwaka 1967 ili kahakikisha keki ya Taifa  inakuwa na mgawanyo sawa kwa wote. Lakini leo hii Azimio la Arusha limesahauika kabisa, hali ya viongozi wa Serikali wanatanguliza mbele masilahi binafsi, hali ambayo baba wa Taifa aliipinga tabia hiyo chafu inayozidi kuchukua sura mpya kila kukicha.

 UBEPARI

Mwalimu alikuwa ni nuru ing’aayo gizani, si giza ling’aalo nuruni. Alipinga mfumo wa ubepari kwa kuuita mfumo wa ufukarishaji’. Hivyo aliimarisha misingi imara katika itikadi yake ya ujamaa na kujitegemea, ikiwa ndiyo itikadi pekee yenye misingi ya utu, haki na usawa.

Mwalimu alichukizwa sana na mfumo mpya wa kibepari uliozuka baada ya yeye kung’atuka madarakani aliouita ‘ ubepari wa pembezoni’ yaani ni ubepari wa kishenzi unaotoa mianya kwa wachache kutumia mirija kuwanyonya wanyonge.

Tanzania yetu leo hii bila hata aibu katiba ya Jamhuri ya Muungano katika ibara yake ya (3) inasema, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa. Hili linaleta utata na mkanganyiko kwani kimaandishi ni wajamaa lakini kimatendo ni zaidi ya ubepari.

Unaweza kuangalia uuzwaji holela wa nyumba za Serikali zilizojengwa kwa jasho la Mzee Nyerere na akina Rashid Kawawa, ubinafsishaji holela wa viwanda pamoja na mikataba mibovu inayotanguliza masilahi ya wachache! Mwalimu hakusita kukemea mambo ya kihuni kama haya.

Katika kitabu chake cha Ungozi wetu na hatima ya Tanzania ukurasa wa 28, Mwalimu alisema: “Halmashauri kuu ya Taifa iliketi Unguja, ikabadili Azimio la Arusha bila kwanza kutafuta maoni ya wananchi na walikuwa na haki ya kufanya hivyo maana sera ni yao. Ubaya wao ni kwamba, jambo lenyewe walilifanya kwa hila na ujanjajanja na mpaka sasa wanaendelea kuwadanganya wananchi kwamba sera ya CCM ni ya Ujamaa na Kujitegemea.”

UKABILA NA USEHEMU

Wakati Mwalimu Nyerere alipokuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alifanikiwa kuwaunganisha wanafunzi katika jumuiya moja iitwayo USARF ikijumuisha wanafunzi kutoka nchi zote za Afrika. Aliona kuwa ni vema kwani Afrrika ni moja.

Leo hii wanafunzi wetu wanajitambulisha na kujitanabaisha kwa makabila na sehemu watokazo. USARF imekufa kabisa na imebezwa na vikundi vya makabila yao. Hali hii ya ukabila na usehemu inatawala kona zote za nchi yetu na ndiyo maana watu wengi wakienda kuomba kazi au hata huduma katika sehemu fulani, utasikia anaulizwa wewe ni kabila, dini gani au unatoka mkoa gani? Hapa tulipofikia nchi yetu imepotea kisiasa, kijamii na hata kiuchumi.

Naamini roho ya Mwalimu Nyerere inahuzunika sana kuona wanafunzi wanavyomkumbuka wakidai haki zao hasa katika vipindi vya migomo, wakati hili ambalo aliasisi hawalienzi.

UBINAFSISHAJI HOLELA WA MALI  ZA UMMA

Wakati wa uhai wake Mwalimu alilaani vikali ubinafsishaji holela wa mashirika ya umma. Alwakataa Mabeberu waliojiita ‘ wawekezaji walionuia kufilisi utajiri wa nchi yetu huku wakishibisha matumbo yao.

Leo hii vigogo wa Serikali wanajichukulia majumba ya Serikali, viwanda, mashamba bila kujali wao wenyewe wakitoka madarakani au kwenye utumishi wa umma hapo baadaye wataishi wapi. Je, huku ndiko kumuenzi Mwalimu aliyekataa kuishi kwenye nyumba kubwa kule Butiama, akisema yeye si tembo?  Uko wapi uzalendo aliotuachia Nyerere?

KUONGOZWA KWA RIMOTI  NA NCHI MATAJIRI

Nakumbuka siku moja Mwalimu Nyerere akiwa katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, nikiwa katika Wizara ya Ulinzi aliwahi kusema: “Tangu lini IMF ikawa International Ministry of Finance?” (Wizara ya Fedha ya Kimataifa).

Leo hii viwanja hivyo hivyo vinatumika kuusifu ubeberu wa IMF na wawekezaji wake, huku tukiwekewa masharti magumu ya kuongoza nchi yetu kwa masilahi ya mabeberu.

Mwalimu aliwaonya mataifa tajiri wasiingilie mambo yetu ya ndani, pale walipoona masilahi yao hayazingatiwi, mara kwa mara walimhoji Mwalimu ambapo yeye aliwaamuru waondoke haraka na misaada yao yote. Mwalimu hakupenda misaada ya kinafiki iliyolenga kuwaangamiza wananchi wake, alipinga amri na maagizo ya taasisi za fedha kama Benki ya Dunia (WB) na IMF. Hivyo, aliheshimu maamuzi yake sahihi katika kulinda heshima ya nchi yetu na watu wake.

Kipindi chote cha uhai wake Mwalimu alisisitiza haja ya mataifa ya Afrika kujitawala na kuwa huru katika kujiamulia mambo yake.

“Inapotokea taifa kuuza uhuru wake kwa ajili ya misaada ya kiuchumi au kukubali kukaliwa na majeshi ya nje, taifa hilo linakuwa limepotea na litanyonywa na watu wake watakuwa wanakandamizwa popote pale,” alisema Mwalimu.

Kama tungekuwa na misimamo kama Nyerere, tungeheshimika. Lakini leo hii Mwalimu angefufuka na kuona watu wanavyong’ang’ania madaraka kiasi hata cha kumwaga damu kwa visa na visasi, angefadhaika sana na kuona jinsi tunavyomuenzi kwa kumdhihaki, huku tukiwa na kauli za nyoka ndumila kuwili.

UBABE NA VITISHO KATIKA UONGOZI

Mwalimu aliamini kuwa kiongozi bora hapaswi kuwa na jazba na asiyetumia ubabe wala vitisho katika maamuzi au katika kutatua tatizo ambalo jamii inataka litatuliwe kwa masilahi na manufaa ya Taifa. Aliamini kuwa kiongozi bora ni yule anayeruhusu mianya ya majadiliano baina yake na wale anaowaongoza. Asiyetumia lugha chafu au kashfa na kejeli kwa watu wake.

Leo hii tawala mbalimbali zikiwemo taasisi za elimu ya juu na hata chombo cha juu kabisa cha maamuzi (Bunge) vinatumia ubabe na vitisho katika maamuzi.

Hivi karibuni na sasa tumeshuhudia migomo ya wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi, hasa sekta binafsi na umma, vyuo vikuu kila kukicha huku maamuzi ya kibabe yakitumika na watawala wa vyuo katika kukandamiza haki za wanafunzi na wafanyakazi hata kwa kuwatishia kwa FFU na maji ya washawasha.

Masikini wanafunzi hawa wanabaki wanalia huku wakiimba kama si juhudi zako Nyerere na …angesoma wapi au kufanya kazi wapi?”

Tunaona pia Bunge linavyopitisha maamuzi ya kibabe yasiyo na masilahi kwa wananchi na hata kuadhibu wale wanaojaribu kutetea masilahi ya wanyonge. Bunge hilo hilo linatumia pia lugha za kejeli na dharau kuwatisha wananchi, ubabe na vitisho si misingi ya demokrasia na utawala bora.

UMANGIMEZA NA UKIRITIMBA

Wakati wa uhai wake Mwalimu aliheshimu mipaka, taasisi za utawala na mali za umma. Alichukia matumizi mabaya ya rasilimali za umma, pia aliheshimu mawazo yake mwenyewe na ya wenzake.

Mwalimu aliamini kwamba, kiongozi asiyependa ukiritimba na umangimeza ni lazima awe mfuasi mzuri wa maadili anayoyasimamia, mwaminifu na mwadilifu kwa manufaa ya Taifa lake. Mwalimu hakupenda kutetea uovu wa viongozi eti kwa kutunza heshima zao au kulinda vyama vyao bila kujali uhusiano wao wala majina yao.

Hivyo, katika Serikali yake Mwalimu hakuwa na ubia na mtu yeyote duniani!
Leo hii ni viongozi wangapi ambao wanadumisha fikra na misimamo ya Mwalimu nyerere kwa vitendo kama si matamko tu?

USIRI WA MIKATABA NA MAKAMPUNI YA KIGENI

Mwalimu alisisitiza uwazi katika mikataba mbalimbali ambayo Serikali iliingia na makampuni ya kigeni. Katika kitabu chake cha Uhuru na Maendeleo, Mwalimu anasema: “Viongozi wa Kiserikali wana wajibu mkubwa wa kuwafahamisha wananchi nini Serikali inafanya na kwa sababu gani”.

Lakini ni tofauti kabisa na hali ilivyo sasa, hali inayopelekea manung’uniko na malumbano yanayohusisha hata ugawaji wa zabuni za Serikali, hasa labda tuangalie mfano mmoja tu wa Mkataba wa Buzwagi ambao ulikuwa ni maarufu kama Mkataba wa Karamagi kati ya Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na Kampuni ya Barrik Gold Mine.

Mkataba huu ulikuwa ni siri kubwa baina ya Barrik na Waziri tu, hali iliyopelekea Mbunge Zitto Kabwe kusimamishwa shughuli za bunge kwa miezi minne, baada ya kuhoji uhalali na uharaka wa utiaji saini mkataba huo unaodaiwa kusainiwa hotelini (Churchil Hotel) mjini London, Uingereza.

Hivi nchi yetu itakuwa kituko mpaka lini? Kimichezo tuwe kichwa cha mwendawazimu, mbona hatuoni viongozi wanaoleta tija na maendeleo, isipokuwa nchi inatota na kulowa umwagaji wa damu?

Nakumbuka Rais Thabo Mbeki wa Afika Kusini alitudharau sana alipokuwa katika moja ya ziara zake hapa nchini, alisema wakati biashara ya Tanzanite inatoa dola milioni 500 kwa mwaka duniani, Tanzania nchi pekee duniani yenye madini hayo inapata dola 80 tu.

Rais Mbeki alitukejeli kwa kusema hakuna sababu ya kumtafuta mchawi wakati sheria ya uchimbaji madini tumeitunga wenyewe inayoruhusu wageni waondoke na asilimia kubwa ya madini hayo na sisi kuambulia mashimo.

Hali hii inanipa shaka hasa nikichunguza upeo wa kufikiri wa baadhi ya viongozi wetu, ndipo ninapokumbuka usemi wa waziri mstaafu, Arcado Mtagazwa (CCM), alioutoa bungeni 1993, alisema:

“Tutakapokufa vizazi vijavyo vitafukua makaburi yetu ili vione vichwa vyetu viongozi vilikuwa na ubongo wa aina gani kwa sababu yaelekea hatufikiri sawasawa”. Kauli hii alilazimika kuitoa baada ya kuona kwamba baadhi ya maamuzi yanayofikiwa na Serikali yetu hayana masilahi kwa Taifa na ni ubinafsi.

RUSHWA

Katiba ya CCM katika ahadi yake ya nne inasema: “Rushwa ni adui wa haki, sitatoa rushwa wala kupokea rushwa”. Jambo la rushwa mzee wetu mpendwa Mwalimu Nyerere pia alilikemea vikali enzi za uhai wake kwani alijua wazi kuwa rushwa ni kikwazo cha maendeleo ya umma katika kila Taifa.

Leo hii nchi yetu imegubikwa na rushwa na hata kuhalalishwa na kuitwa; Takrima’ ili tu kukidhi matakwa na mahitaji ya mahafidhina’. Viongozi wa Serikali, baadhi ya viongozi katika taasisi mbalimbali wameweka mbele rushwa kama msingi wa kushibisha matumbo yao.

Baya zaidi hata viongozi wa CCM chama pekee kilichoasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere wamezisahau kabisa falsafa zake na chuki yake dhidi ya rushwa na hata katika chaguzi mbalimbali za Chama Cha mapinduzi zilizofanyika.

Siku chache zilizopita tumeweza kusikia kama si kushuhudia vitendo vya rushwa vikifanyika waziwazi katika chaguzi hizo, jambo ambalo licha ya kushindwa kutumia mamlaka waliyonayo katika kuvisaidia vyombo husika kuchukua hatua za kisheria, viongozi wamebaki wakilalamika na kushtaki kwa wananchi kuhusiana na vitendo hivyo vichafu vinavyotendeka ndani ya CCM, Serikali na hata katika sekta nyinginezo nyingi nchini.

Nakumbuka Kabuye (Mb-TLP) aliwahi kuwashutumu bungeni viongozi kuwa, ana uhakika wabunge wote waliingia kwa rushwa, wabunge hao walioshutumiwa walimtaka Kabuye afute kauli naye alisema: “Kwa kulazimishwa nafuta kauli”. Walimlazimisha lakini hoja yake ilibaki kuwa ni ya msingi.

 UCHU WA MADARAKA

Mwalimu Nyerere ni miongoni mwa viongozi wachache sana duniani waliokosa kuwa na uchu wa madaraka. Ni miaka 24 sasa tangu Mwalimu ang’atuke madarakani kwa hiari yake akiwa kama rais wa awamu ya kwanza wa nchi yetu na ni miaka 22 tangu aachie uongozi wa CCM kama Mwenyekiti wa chama. Ndipo alipoamua kwa hiari yake kurejea Butiama na kuendeleza kilimo.

Uroho wa madaraka leo hii umekithiri, viongozi wengi wanaendelea kung’ang’ania madaraka bila kujali uzee walionao. Mahafidhina hawa wamezoea kusema vijana ni Taifa la kesho’ ili wao wazee waendelee kuhujumu mali za nchi yetu.

Na unafiki wao ni pale wanaposema vijana ni nguvu kazi ya taifa, sentensi hizi mbili kimantiki zinakinzana. Mbaya zaidi na kinachouma ni pale unapoona watoto wa vigogo au viongozi wa Serikali wakiwa ndio kama warithi wa nafasi za wazazi wao ndani ya CCM na hata Serikali ya CCM.