Home Latest News KWANINI SEKRETARIETI YA AJIRA ISIWE NA MATAWI YAKE?

KWANINI SEKRETARIETI YA AJIRA ISIWE NA MATAWI YAKE?

225
0
SHARE

NA MARKUS MPANGALA

MIAKA kadhaa iliyopita nilishindwa kuwaelewa kabisa watendaji wa Wakala  wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) hapa nchini. Nilikuwa siwaelewi kwa sababu siku moja niliwahushudia wafanyabiashara fulani kutoka Songea mkoani Ruvuma, wakizunguka vyumba vya ofisi vya taasisi hiyo kwenye jengo la Ushirika liliko Barabara ya Lumumba, Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam kwa madhumuni ya kusajili kampuni yao.

Pili, niliwahi kumsaidia rafiki yangu, Albert Nyaluke Sanga, ambaye ni mfanyabiashara mkubwa mkoani Iringa, ili apate leseni ya biashara. Haikuwa leseni yake binafsi, bali aliamua kumsaidia kijana mmoja aliyekuwa na ndoto za kuwa mfanyabiashara, lakini alikosa pa kunzia.

Rafiki yangu huyo anapenda kuwasaidia vijana wanaojishughulisha na ujasiriamali kwa sababu anaamini hiyo ndiyo njia pekee ya kuwakomboa, badala ya elimu yao na kuondokana na matembezi ya kusambaza bahasha za kuomba nafasi za kazi.

Tangu kuzaliwa kwake hadi leo, akiwa kwenye umri wa utu uzima, hajawahi kuajiriwa kokote, kwahiyo anahimiza vijana wamtumie kuwasaidia ushauri.

Wakati tukishughulikia hilo, ndipo nilijiuliza swali ni kwa vipi taasisi kubwa kama BRELA inaendesha mambo katika njia za kizamani ambazo zinasababisha gharama kubwa na kutoharakisha upatiakaji wa huduma?

Kwamba mfanyabiashara alilazimika kufunga safari kutoka Songea hadi Dar es salaam kushughulikia usajili wa kampuni. Baada ya miaka hiyo, angalau sasa utendaji wa mamlaka hiyo umebadilika licha ya kasoro za hapa pale ambazo ninaamini zitabadilika siku za usoni.

Angalau sasa unaweza kujisajili kupitia ofisi zao zilizoko mikoani, kwa njia ya mtandao au kufanya huduma za malipo ya usajili kwa maelekezo yaliyoko katika tovuti yake.

Kitu kimoja ambacho ninapenda kuyaambia mashirika ya umma, ni kwamba bado yana mwendo wa kobe katika matumizi ya tovuti, pamoja na mitandao ya kijamii. Mara kadhaa nimekuwa nikijiuliza hilo bila majibu.

Angalau nimewahi kuwasilisha na mashirika kadhaa yenye kurasa zao kwenye mitandao ya kijamii, lakini nilichowaambia ni kusisitiza matumizi sahihi ya kurasa hizo kwa madhumuni ya kutoa taarifa, sio kuanzisha kama fasheni.

Kama tunatoa takwimu, basi tuhakikishe tunawafikia wengi kwa kuwa kundi kubwa linahamia kwenye ulimwengu wa digitali. Hilo ni lazima, tutake, tusitake  zama zimebadilika na waendeshaji wa mashirika hayo watalazimishwa na wakati.

Hivyo basi, kwa kuwa BRELA wamefanya mabadiliko hakika ninawapongeza. Hatuanzishi mashirika ya umma ili yawe kikwazo kwa Watanzania badala yake yatoe mwongozo, ushirikiano na huduma madhubuti kwa watanzania.

Baada ya hayo, tugeukie upande wa Sekretarieti ya Ajira hapa nchini. Hapo ndipo palipojaa mambo ya kushangaza. Bado Sekretarieti inaendesha mambo yake kizamani sana.

Pengine naweza kusema zile zama za kutumia kompyuta zilizokuwa kubwa kama makabati ya nguo, wakati tunaishi kwenye zama za kasi za mitandao na kusogeza huduma kwa wahitaji.

Nimeona kasoro nyingi kwa Sekretarieti ya Ajira inapowaita kwa usaili waombaji wa nafasi za kazi. Kwa mfano ni jambo la kushangaza Sekretarieti ya Ajira inapowatangazia vijana wa Kitanzania nafasi za kazi, kisha inataka wote waje Dar es salaam kufanya usaili na mitihani.

Mtanzania aliyeko wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara, au aliyeko wilayani Karagwe, mkoani Kagera analazimishwa kusafiri kutoka huko hadi Dar es salaam kuhudhuria usaili wa Sekretarieti ya Ajira.

Huu ni utaratibu wa kizamani sana, nadhani ulifanyika katika zama za kati za awe (Middle Stone Age) yaani miaka 25,000 iliyopita, enzi za Homo Sapiens.

Sekretarieti ya Ajira inao uwezo wa kuwa na matawi yake katika mikoa yote. Serikali inayo majengo mengi ambayo yangeweza kutumika kuendesha shughuli za sekretarieti hiyo, kuliko kuwakamua vijana wa Kitanzania kiasi kikubwa cha fedha huku wakikosa kazi hiyo huambulia hasara tu.

Mathalani, wangeweza kuwa na matawi katika Kanda ili kurahisisha utoaji wao wa huduma. Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati, Kanda ya Kusini, Kanda ya Mashariki na Zanzibar.

Uwezekano wa kuendesha zoezi la usaili na mitihani kwa ajili ya kuchuja waombaji wa ajira, linafanyika katika Kanda husika. Hatua hiyo itapunguza umaskini na kuwapa ahueni vijana tunaotafuta ajira serikalini.

Kwa mfano, waombaji ambao ni vijana na hawajapata ajira, wanatakiwa kupanda mabasi kutoka Bukoba hadi Dar es Salaam kwa gharama ya shilingi 62,000 kwa safari moja. Anatakiwa alale Dodoma ndipo afike eneo la usaili kufanya mitihani yake. Ukiongeza ghamara ya safari ya kurudi alikotoka, ina maana analipia 62,000 tena, ikiwa na maana 124,000 bila kula, kunywa wala kulala!

Vijana hao hao wanatakiwa kurudi tena Bukoba au Nanyumbu kwa gharama kubwa zaidi wakati Sekretarieti ya Ajira ingeweza kuepusha gharama na usumbufu kama huo. Tumeona watu takribani 56,000 wanagombea nafasi 400 za kazi zilizotangazwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA). Wametoka kila upande wa nchi hii, na kwa gharama kubwa, lakini mwisho wa siku wameambulia dhiki na shida tu.

Mtu anatumia shilingi 46,000 kwa safari moja kutoka Songea hadi Dar es salaam. Akimaliza kufanya usaili, anatakiwa kulipia tena shilingi 46,000 kurejea Songea. Hapo hatujahesabu gharama za chakula na malazi, ambayo kwa hesabu ya haraka haraka ni shilingi 200,000. Hivi Sekretarieti ya Ajira haiwezi kuepusha umasikini zaidi unaowakaba waombaji hawa?

Nafikiri wakuu wa Sekretarieti ya Ajira wanapaswa kukubaliana nami kuwa wanaendesha mambo kizamani sana. Jambo ambalo linachangia vikwazo visivyo na sababu, pamoja na ukosefu wa ufanisi. Tatizo letu tunapenda sana kuona watu wanashindwa, badala ya kufanikiwa. Hizi ni fikra zilikuwapo enzi za Ujima na ukabaila (Primitive Communalism na Feudalism) na sio nyakati hizi za maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Kusema hivyo sina maana ya kuwatetea waombaji pekee, bali hata watendaji wa Sekretarieti wanatakiwa kufahamu majukumu yao yamebaki Dar es salaam pekee, kwani ukiritimba na utendaji wa zama za mawe ambazo zinarudisha nyuma ufanisi wao.

Nafikiri katika karne ya 21, hatupaswi kujenga taifa la kutegemea huduma kutoka makao makuu pekee. Ni lazima tutoe huduma zetu karibu na wananchi. Tunahitaji kusogeza huduma kwa wananchi, sio kila kitu hadi kifanyike Dar es salaam tu.

Ni lazima Sekretarieti ya Ajira wamsaidie Rais John Magufuli katika kupambana na umaskini, pamoja na ukosefu wa ajira. Haiwezekani Serikali ikatangaza nafasi za kazi 50,000, halafu ikataka waombaji wote wafunge safari kwenda kufanya usaili Dar es salaam.

Siamini kuwa Sekretarieti ya Ajira haiwezi kuwa na wasimamizi watatu wa usaili na mitihani katika mkoa wa Mwanza kuliko watu 40 maskini wasio na ajira kusafiri hadi Dar es Salaam kufanya mitihani.